![]() |
SEHEMU YA NNE |
FUNGA YA RAMADHANI, HUKUMU,
FADHILA NA ADABU ZAKE.
Ibrahim A. H. Ghulaam
(SEHEMU YA NNE)
BAADHI YANAYOTAKIWA AYAKITHIRISHE MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI
1- Kisimamo cha usiku (Swalah ya tarawehe), amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (سبحانه وتعالى ) husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake}. (Al Bukhariy na Muslim).
*Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia), amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {Msivizuilie vijakazi vya Mwenyezi Mungu (wanawake) (kuhudhuria ibada) katika misikiti ya Mungu}. (Al Bukhariy na Muslim).
Na haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu za kimsingi zinazo kubalika kisheria, amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {wakiwaombeni ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni}. (Muslim).
2- Kuzidisha kusoma Quran.
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Quran na ndio mwezi ulioteremshwa ndani yake Quran, Amesema Allah (سبحانه وتعالى ):
{{Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani).}} (97:1). Na {{(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani…}} (2:185).
3- Sadaka. Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Amesema Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):
Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم ) mkarimu (mtoaji) na alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhani wakati anapokutana na Jibriyl (عليه السلام ) (Al Bukhariy na Muslim).
*Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga, amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {Mwenye kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu chochote}. (Ahmad na Annasaiy).
4- Kufanya Umrah, amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ):
{Umrah katika mwezi wa Ramadhani una malipo sawa na Hijjah}. (Muslim).
5- Itikafu (nako ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha na ibada mbalimbali), inasuniwa kufanya itikafu na hasa katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) amesema: Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وسلم ) akifanya itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).
6- Kuutafuta usiku wa cheo (laylatul-qadr), na zaidi katika kumi la mwisho la Ramadhani, imepokewa hadithi kutoka kwa Mama ‘Aishah (رضي الله عنها) amesema:
Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ):
{Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho za Ramadhani} (Al Bukhariy na Muslim)
Na amepokea Abu Hurayrah (رضي الله عنه ) kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم ) amesema: {Mwenye kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (سبحانه وتعالى ) husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo)}. (AlBukhariy na Muslim).
7- Toba. Nako ni kurudi kwa Allah (سبحانه وتعالى ) kutokana na makosa aliyoyatenda mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia tena makosa hayo).
*Tukumbuke ya kwamba Mwanaadamu si mkamilifu daima yupo katika hatari ya kufanya makosa, sawa makosa hayo ikiwa ni makosa ambayo ameyahisi au hakuyahisi wakati wa kuyafanya kwake, toba ndio njia ya kujikosha na madhambi ya makosa hayo, na kipindi cha mwezi wa Ramadhani ni fursa muhimu ya kutubia.
* Ikiwa katika makosa yake kuna haki za wanaadamu inamlazimu kuzirejesha kwa wenyewe haki hizo.
FADHILA ZA FUNGA
Zimepokewa Hadithi nyingi sana zinazoelezea fadhila za funga ya Ramadhani, miongoni mwa hadithi hizo ni hadithi zifuatazo:
1- Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ):
{Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo (toka kwa Allah (صلى الله عليه وسلم )) husamehewa madhambi aliyoyatanguliza}. (Al Bukhariy na Muslim).
2- Na amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {amesema Allah (سبحانه وتعالى ):
Kila amali ya mwanaadamu (aifanyayo) ni yake, wema (mmoja) hulipwa kwa mfano wake mara kumi mpaka mara mia saba, isipokuwa funga, hakika ya funga ni Yangu mimi, na Mimi najua namna gani Nimlipe kwa funga hiyo, ameacha matamanio yake na chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu, mfungaji ana furaha mbili, furaha wakati wa kufutari kwake na furaha nyengine pale atapokukutana na Mola wake. Harufu yakinywa cha mfungaji inapendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko harufu ya miski}. (Al Bukhariy na Muslim).
Itaendelea inshaAllah ...