4/25/2020


SEHEMU YA TANO

FUNGA YA  RAMADHANI,  HUKUMU,
FADHILA NA ADABU ZAKE.
                           
Ibrahim A. H. Ghulaam

(SEHEMU YA TANO)

YANAYOPASWA KUJIEPUSHA NAYO MFUNGAJI.

1-  Tabia chafu na maneno maovu, kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika.

2- Kuzidisha usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.

3- Kupoteza wakati mwingi katika michezo na maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada mbali mbali.

4- Kuacha kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa kwa jua.

5- Kufanya israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari.

6- Kufutari kwa vyakula vyenye harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu thaumu, vitunguu maji, doriani, na kadhalika kwa kuhofia kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika kwa Swalah.

7- Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na unyenyekevu.

YANAYOTAKIWA KWA KUMALIZIKA RAMADHANI.

1- Kutoa zakatul-fitri, nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamume, mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).

*Watoto wadogo, Watumwa na pia Wanawake waliochini ya usimamizi wa Wanaume itawalazimikia zakah hio wasimamizi wao, ama Wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.

*Na inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya Swalah ya iddi.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنه ) amesema: Amefaradhisha Mtume (صلى الله عليه وسلم ) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana), mume na mke, mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha (hiyo zakah ya fitri) itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi). (Al Bukhariy na Muslim).

*Na wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji uliopo (ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg) takribani kwa nafaka kama mchele na mfano wake) (au thamani yake kwa baadhi ya wanachuoni).

2- Takbir, inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa Swalah ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, masokoni na hata majumbani.

3- Swalah ya iddi, kwa wanaume na wanawake.

*Na inasuniwa ifanyike katika viwanja, na hata akina mama walio katika siku zao (hedhi) inasuniwa na wao wahudhurie ingawa wao hawatoshiriki katika kuswali.

4- Na inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili ya Swalah ya iddi al-fitri.

5- Pia inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye Swalah ya iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه ) amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (صلى الله عليه وسلم ) inapokuwa siku ya iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).

6- Kuvaa mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.       
   
*Na inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).

7- Na pia inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani kufunga siku sita katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali). Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ):
{Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).(Muslim).

8- Na tukumbuke ya kwamba siku hii ya iddi inakatazwa (ni haramu) kufunga ndani yake.           Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy (رضي الله عنه ) :( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (صلى الله عليه وسلم ) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh`ha)). (Al Bukhariy na Muslim).
MWISHO.
 Namalizia makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (سبحانه وتعالى ) alie niwezesha kufanikisha lengo langu hili.

Na kisha natoa shukurani zangu za dhati kwa wale wote waliochangia kwa njia moja au nyengine kukamilika kwa makala hii.
Na ninamuomba Mwenyezi Mungu (سبحانه وتعالى ) atupe kila la kheri hapa duniani na kesho akhera.              Amiin.
وصلى الله على نبينا محمد وعلى آ له وصحبه وسلم .


*KILA MTU ANAYO HAKI NA ANASHAJIISHWA KUSAMBAZA MAKALA HII KWA NJIA YEYOTE ITAKAYO KUWA RAHISI KWAKE KWA SHARTI LA KUTO KUIFANYIA MAREKEBISHO YEYOTE KABLA YA KUWASILIANA NA MTAYARISHAJI WA MAKALA HII.
*UKIWA NA MASWALI MAPENDEKEZO MAREKEBISHO AU AINA YEYOTE YA USHAURI, WASILIANA NAMI KWA ANUANI IFUATAYO:
IBRAHIM   A.   H.   GHULAAM
P.O BOX  10957  DAR ES SALAAM TANZANIA.
SIMU NAMBARI: +255 777 306 307 / 0658 88 22 12
BARUA PEPE: ibralhamd2000@yahoo.com
Next
This is the most recent post.
Older Post