Kwa
hakika kila sifa njema ni Zake Allaah, tunamtukuza Yeye, na tunamtaka
msaada Yeye na tunamuomba msamaha Yeye. Tunajilinda kwa Allaah kutokana
na maovu ya nafsi zetu na udhaifu wa vitendo vyetu. Aliyeongozwa na
Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotezwa na Allaah hakuna wa
kumuongoza. Nashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah
na nashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلا تَمُوتُنَّ إِلا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ
“Enyi mlioamini mcheni Allaah (kwa kuyatekeleza yote Aliyowaamrisha na kujiepusha na yote Aliyowakataza) kama ipasavyo kumcha wala msife ila mumekwisha kuwa Waislamu kamili” (Qur-aan 3: 102)
يَا
أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ
وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالا كَثِيرًا
وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالأرْحَامَ ۚ
إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا
“Enyi
watu mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi (asili -
Adam) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume
wengi na wanawake kutokana na wawili hao. Na mcheni Allaah ambaye kwaye
mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika Allaah ni Mlinzi juu yenu
(Anayajua mnayoyafanya).” (Qur-aan 4: 1)
يَا
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا
﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
“Enyi
mlioamini mcheni/muogopeni Allaah na mseme maneno yaliyo ya haki
(maneno ya kweli). (Allaah) Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu, na
Atakusameheni madhambi yenu. Na mwenye kumtii Allaah na Mtume Wake bila
shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.” (Qur-aan 33: 70-71)
Kwa hakika maneno ya kweli kabisa ni yale ya Kitabu cha Allaah, na uongozi ulio bora zaidi ni uongozi wa Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake). Na maovu yaliyo mabaya zaidi ni mambo ya kuzua (yaliyo mageni katika mafundisho ya Uislamu), na kila lenye kuzushwa katika dini ni bidaa (uzushi), na kila bidaa ni upotofu na kila upotofu mwisho wake ni katika moto.
Ndugu msomaji, Allaah Mtukufu Anasema:
تَبَارَكَ
الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾
الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ
عَمَلا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾
“Ametakasika
(Ametukuka) Yule ambaye mikononi Mwake upo ufalme na Yeye ni Muweza juu
ya kila kitu. Yeye (Allaah) ndiye Aliyeumba umauti na uhai ili apate
kuwajaribu ni nani kati yenu mwenye vitendo vizuri. Na Yeye (Allaah) ni Mwenye nguvu na ni mwingi wa kusamehe.” (Qur-aan 67: 1-2)
Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake) amesema:
“Sikuwa
mimi katika hii dunia isipokuwa ni mfano wa msafiri jangwani
aliyepumzika katika kivuli cha mti, kisha akaondoka na kukiacha kivuli
kile”. (Hadiyth sahihi: Al-Albaaniy, namba, 438).
Ndugu msomaji, Wa blog fahamu kuwa kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislamu, maiti ana haki nne anazopaswa kutendewa, ambazo ni:
1. Kuoshwa,
2. Kuvishwa sanda,
3. Kuswaliwa, na
4. Kuzikwa.
Hii
ina maana kuwa Waislamu watawajibika kuyafanya haya kwa kila maiti
Muislamu na si vinginevyo. Na watakapoacha kumfanyia maiti mambo hayo
watapata dhambi Waislamu wote wa sehemu ile.
Ndugu
msomaji, tunafahamu kuwa una hamu kubwa ya kuyajua kiundani mambo manne
tuliyoyataja hapo juu. Shaka ondoa, makala hii iliyo mikononi mwako
itakuonesha hayo kadiri utakapozidi kufungua kurasa zake.
Awali ya yote tunapenda kukujulisha itikadi ya Uislamu kuhusu maisha na uhai huu wa dunia.
Ndugu
msomaji, Waislamu wanaitakidi kuwa, kila kilichopo katika dunia
kitaondoka (kitakufa). Na hii ni kutokana na kauli ya Allaah Aliposema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ
“Kila kilicho juu ya ardhi ni chenye kufa…” (Qur-aan 55: 26)
Kama
ilivyozoeleka kuwa hakuna mwanzo usiokuwa na mwisho, wala hakuna mchana
usiokuwa na usiku, kadhalika hakuna uhai usiokuwa na mauti. Allaah
Anasema:
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ
“Kila nafsi itaonja umauti (Itakufa)…” (Qur-aan 21: 35)
Na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ameweka wazi katika Hadiyth tuliyoitanguliza hapo nyuma.
Ndugu msomaji, waweza kujiuliza kuwa umauti ni nini?
Nasi kwa kulifahamu hilo tuna haki ya kukufafanulia kama ifuatavyo:
Umauti
ni mtengano au mfarakano kati ya mwili na roho ya kila kiumbe hai, kama
mwanadamu, wanyama, majini n.k. Hapo huwa ndio mwisho wa kazi ya kila
kiungo cha aliyekufa; macho, mdomo, sikio, mikono, mguu na mfano wake.
Si
kama wanavyodai baadhi ya wasiokuwa na ufahamu sahihi na wasio na akili
zenye kuwatosha kuwa eti kuna baadhi ya watu ambao huwa wanakufa baadhi
ya viungo na baadhi havifi. Huu ni uongo wa wazi kabisa na kila mtu
aliye na akili timamu atampa msemaji wa maneno haya moja kati ya sifa
tatu zifuatazo:
1. Mjinga,
2. Punguani, hajui alisemalo,
3. Ni mtu aliyeamua kuifanya nafsi yake kuwa pumbavu, mfano wake ni
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.
Haiingii
akilini kabisa kuwa mtu afe halafu mguu wake usife au mkono wake au
macho yake yasife au tupu yake isife. Hii haihitaji Aayah, Hadiyth, wala
elimu kubwa wala muujiza, kwani akili inamtosha mwenye nazo na
akazitumia. Ama yule asiyekuwa na akili basi Aayah, Hadiyth wala elimu
yoyote pia haitamfaa.
Ndugu
msomaji, katika hili tunaomba mchango wako wa kiakili na kujiuliza
kuwa, Je, inawezekana kweli mtu afe baadhi na baadhi abaki kuwa hai
halafu aitwe maiti? Jawabu liwe akilini mwako.
Mpendwa msomaji, baada ya kupata jawabu, sasa nikueleze yale mambo manne anayopaswa kufanyiwa maiti wa Kiislamu.
Jambo La Kwanza Ni Kuosha
Waislamu wanaosha maiti kwa sababu hayo ni mafundisho ya dini, na ni shari’ah.
Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
ametufundisha hayo katika Hadiyth ya Swahaba (mfuasi wa karibu) mtukufu
Ibnu ‘Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake) katika kitabu cha Imam
Al-Bukhaariy na Muslim kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika kitabu
chake Ahkaamul Janaaiz, na Abuu Nu’am katika al-Mustakhraj Hadiyth
namba, 139-140:
Maana ya Hadiyth:
“Siku
moja mtu mmoja alikuwa amesimama ‘Arafah, ghafla mtu huyo akaanguka
kutoka katika mnyama wake na yule mnyama akamkanyaga na kufa papo hapo.
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akasema: “Muosheni kwa maji na majani ya mkunazi na mumvishe sanda…”
Hivyo basi kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
Waislamu wanawajibika kuosha maiti yao pale linapowezekana, kwa sababu
hayo ndiyo mafundisho ya dini yao na si vinginevyo, wala si kama
wasemavyo wenye chuki dhidi ya Uislamu kuwa eti Waislamu wanaosha maiti
kwa sababu huenda ina janaba (yaani ilizini).
Swali
la kujiuliza, Je ni kitabu gani kinachozungumzia hayo? Jibu ni hakuna
ushahidi juu ya hayo katika kitabu chochote au mafunzo yoyote ya Uislamu
wala hakuna ushahidi wowote wa kimazingira. Unaweza kujiuliza, kwa nini
basi wanasema wasiyo na ushahidi nayo? Jibu linaloweza kupatikana ni
moja tu, nalo ni chuki dhidi ya Uislamu.
Ndugu
msomaji, ukweli ulio wazi ni kuwa chuki dhidi ya Uislamu imewapelekea
watu (maadui) kuuzungumzia Uislamu na kuuzushia mambo ambayo hayapo na
hayana ushahidi wowote. Muradi wao ni kuupiga vita Uislamu katika hali
yoyote ile iwayo, na hili Allaah Mtukufu Amelitanabahisha katika
Qur-aan, Aliposema:
ولا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ
“Hawataacha kukupigeni kwa chuki walizo nazo mpaka wakutoeni katika dini yenu watakapoweza kufanya hivyo” (Qur-aan 2:217)
Ndugu msomaji, suala la zinaa limekatazwa katika Qur-aan kuanzia katika hatua zake za mwanzo. Allaah Mtukufu Amesema:
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَا ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا
“Wala msikaribie zinaa kwani huo ni uchafu na ni njia iliyo mbaya kabisa” (Qur-aan 17:32)
Haifai
kumtazama mwanamke kwa matamanio, imekatazwa pia kupeana mikono na
mwanamke/mwanamume ambaye si ndugu yako wa karibu, si hilo tu, Uislamu
hauruhusu wanaume kuchanganyika na wanawake katika hali yoyote ile. Kama
hilo halitoshi, mwanamke katika Uislamu anatakiwa avae hijabu, vazi
lisilo bana mwili wala lisilovutia na linalofunika mwili mzima. Katika
hali hii na kwa mazingira haya, iweje Muislamu azini? Hapo ndipo
utagundua kuwa aliyesema haya ima alitoka usingizini au hatumii akili.
Ndugu
msomaji, fahamu kuwa hakuna mfumo au utaratibu wa maisha wenye
kumuhimiza na kumuhitaji mtu kuwa mbali na zinaa kama utaratibu wa
Kiislamu. Ndio maana Uislamu ukahimiza kuoa na ukakemea vikali uhuni na
ukapera (kuto oa). Tunakushauri ndugu msomaji, uusome Uislamu, na hii
ndio njia pekee ya kuujua ukweli, badala ya kusikiliza maneno ya watu
wenye chuki na uadui dhidi ya Uislamu, ambao wengine wanadai kuujua
Uislamu lakini kiukweli ni kuwa wanachotafuta ni kuwadanganya wasiokuwa
Waislamu ili kupata muradi wao wa siku.
Namna Ya Kuosha Maiti
Ni
nani mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti? Kwa mujibu wa mafundisho ya
Uislamu, mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti ni yule mwenye ufahamu
sahihi juu ya utaratibu wa kuosha maiti na Sunnah[1] zake, na hasa akiwa ni katika jamaa zake kama vile, mkewe/mumewe, mwanawe n.k.
Waoshaji
huwa ni wawili au watatu kulingana na hali halisi. Watu hawa hawana
majina maalum kishari’ah, kama wanavyodai baadhi ya watu kuwa eti kuna
kiguzo, kigingi, na mshika kata; huu ni uzushi. Vitabu vinaonesha kuwa,
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alioshwa na ‘Aliy akisaidiwa na Al-Fadhlu ibnu ‘Abbaas na Usaamah bin Zayd (Radhi ya Allaah iwe juu yao), wala hawakupewa majina maalumu. Haya yameelezwa na Abuu Daawuud kwa mapokezi sahihi juzuu ya pili (2) ukurasa wa 69.
Hatua Ya Kwanza:
Maiti
itavuliwa nguo kwa upole na kufunikwa shuka ndefu baada ya kumfumba
macho kama ilivyopokewa na Imaam Muslim, Ahmad na Al-Bayhaqiy kitabu cha
tatu (3) ukurasa wa 334 na kama alivyoeleza Shaykh al-Albaaniy katika
Ahkaamul Janaaiz ukurasa wa 12 katika Hadiyth ya Ummu-Salamah amesema:
“Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) kwa Abu-Salama akamkuta macho yake yapo wazi akamfumba, kisha akasema “ hakika roho inapotolewa macho huifuata iendapo…”
Huu ni uthibitisho wa mwongozo sahihi wa Uislamu katika kumuosha maiti, si kama wanavyodai maadui wa Uislamu.
Hatua Ya Pili:
Baada
ya kuvuliwa nguo, haraka iwezekananvyo, maiti itaoshwa. Yataandaliwa
maji ambayo yatakuwa yamechanganywa na majani ya mkunazi[2]
na kaafuur. Maji si lazima yawe ya moto, ila ikiwa kuna baridi kali
maji yawe ya uvuguvugu. Atakayesema kuwa maji lazima yawe ya moto, huyo
ni muongo kwani haya yameelezwa katika vitabu vya kishaafi’iy kama kitabu cha shekhe ‘Abdullaah bin Abdir-Rahmaan al-Hadharamiy (850-918) ukurasa wa 48 hadi 49, katika mlango wa Al-Janaaiz.
Maiti
ataoshwa majosho matatu au matano kulingana na hali halisi ya maiti
huyo. Hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah kuwa:
“Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
wakati tukiwa tunamuosha binti yake, Zaynab, akasema: Muosheni mara
tatu au mara tano au mara saba au zaidi ya hapo ikiwa mtaona haja ya
kufanya hivyo....”[3]
Ikiwa maiti ni wa kiume, nywele zake zitaachwa kama
zilivyo ila zitaoshwa vizuri na wala hakitakatwa chochote kwenye mwili
wake, si nywele wala kucha. Na ikiwa maiti ni wa kike, nywele zake
zitafumuliwa ikiwa zimesukwa, kisha zitaoshwa, halafu zitasukwa tena
njia tatu zikielekezwa kisogoni mwake. Na hii ni kutokana na Hadiyth
iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah.[4]
Hatua Ya Tatu:
Ndugu
msomaji, muoshaji atafunga kitambaa au atavaa kitu chochote mkononi
mfano wa glovu, kisha ataosha sehemu za siri za maiti, baada ya
kumpapasa tumboni kwa taratibu, ili kuondoa uchafu ulio karibu kutoka.
Muoshaji atayafanya hayo bila kuangalia uchi wa maiti. Ni uzushi na ni
uongo mkubwa kudai kuwa maiti wa Kiislamu hukamuliwa kwa Nguvu tumboni,
kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu.
Muoshaji
atatupa kitambaa cha kwanza, kisha atachukua kingine na kuanza
kusafisha meno ya maiti, baada ya kulowanisha kitambaa hicho kwa maji.
Baada ya hapo, muoshaji na msaidizi wake watamtawadhisha[5]
maiti, Wudhuu kamili. Watayafanya hayo yote kwa kuanzia kuliani kwa
maiti na kumalizia kushotoni kwa maiti. Kwa mfano, wataosha mkono wa
kulia halafu wa kushoto na mfano wa hayo.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa maiti haitaingizwa maji mdomoni au masikioni au popote pale kwani hakuna ushahidi wowote juu ya hilo katika mafundisho ya Uislamu. Yeyote atakayeleta madai ya namna hii una haki ya kumtaka atoe ushahidi juu ya hilo.
Baada ya kutawadhishwa, maiti ataoshwa mwili wote mara tatu, tano, saba au zaidi ya hapo, kama
tulivyoelezea hapo nyuma. Atamwagiwa maji upande wa kulia, kisha upande
wa kushoto na kuoshwa vizuri kabisa. Na iliyo bora ni kuchanganya maji
ya kuoshea kwa majani ya mkunazi kama
tulivyokwisha elezea hapo awali katika Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyah. Lililo
bora katika osho la mwisho ni kuchanganya maji na kaafuur. Hii ni aina
ya manukato yanayowekwa kwenye maji.
Kufikia hapa ndugu msomaji, tunataraji utakuwa umefahamu usahihi wa kuosha maiti, japo kwa ufupi.
Pamoja na hayo, ndugu msomaji, una haki ya kufahamu mambo yafuatayo:
Hataoshwa maiti aliyekufa shahidi[6], bali atazikwa na nguo zake hizohizo. Hii ni kutokana na dalili nyingi, miongoni mwazo ni ile Hadiyth ya Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake) pale Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliposema kuwaelekeza katika kuwazika Maswahaba[7] waliofariki katika vita ya Uhudi kuwa, “Wazikeni na damu zao…”[8]
Fahamu
pia kuwa, aliyekufa hali ya kuwa amehirimia (ameshakuwa tayari na
amekusudia) kufanya hija, mtu huyo naye hatapakwa manukato wala
hatafunikwa kichwa chake.
Ikiwa
maiti itaharabika kutokana na namna ya kifo chake, kama vile kutokana
na ajali ya gari, kuungua moto, kuangukiwa na nyumba, n.k, basi maiti
huyo atatayamamishwa (yaani badala ya kutumika maji utatumika udongo
ulio safi na twahara), na kama itashindikana basi, uwajibu (ulazima) wa
kufanya hivyo utaondoka. Allaah, Mtukufu, anasema katika Qur-aan 2:286:
لا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلا وُسْعَهَا
“Allaah Haikalifishi (hailazimishi) nafsi ila kwa yaliyo sawa na uwezo wake…”
Pia Wanachuoni wa kanuni za Fiqh (Usuul al-Fiqhi) wana msemo usemao:
“Hakuna uwajibu endapo hauwezekani (hautekelezeki)…” (La waajiba ma’al ‘ajzi). Na Allaah ni Mjuzi zaidi.
Hutokea baadhi ya nyakati kuwa, mathalani, mtu kafariki na baadhi ya viungo vyake, kama
mikono au mguu, vimekosekana. Na maiti huyu ameoshwa, kaswaliwa, na
hatimaye kuzikwa akiwa hana viungo vyote. Mara tu baada ya kuzikwa
kikaonekana kiungo au baadhi ya viungo vilivyokosekana, Je, kiungo au viungo hivyo vitaoshwa na kuswaliwa? Ndugu msomaji, suala hili aliwahi kuulizwa Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn[9] (Allaah Amrehemu), akajibu:
“Viungo vidogo vidogo kama mikono na miguu vitakapopatikana na maiti ameshaswaliwa, viungo hivi havitaoshwa wala kuswaliwa kwa kuwa ameshaswaliwa.”
Akaendelea kusema:
“Ama itakapokuwa maiti haikupatikana bali kimepatikana kiungo katika mwili wake kama vile kichwa au mguu au mkono, basi kitaswaliwa na kuzikwa kilichopatikana baada ya kuoshwa vizuri na kuvishwa sanda[10].
Mpaka
hapa tuna imani kuwa tumeondoa kiu yako juu ya moja kati ya mambo mane
anayopaswa kufanyiwa maiti. Hatua inayofuata baada ya hii ni kuvishwa
sanda.
Kuvishwa Sanda
Baada
ya maiti kuoshwa vizuri, hatua inayofuata ni kuvishwa sanda, nguo au
shuka ndefu yenye uwezo wa kufunika mwili wote wa maiti. Ni bora zaidi
na inapendeza shuka hiyo ikiwa nyeupe. Na hii ni kutokana na Hadiyth
sahihi ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliposema:
”Pendeleeni kuvaa mavazi meupe kwani hayo ni katika mavazi bora kwenu na mukafini (muwavishe) maiti wenu kwa hizo sanda.”[11]
Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhi ya Allaah iwe juu yake) aliyesema:
“Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alikafiniwa (alivishwa sanda) katika nguo tatu…”[12]
Ndugu
msomaji, hakuna tofauti kati ya sanda ya maiti mume na sanda ya maiti
mke, na hii ni kutokana na kukosekana ushahidi sahihi juu ya hilo, na kama
upo, basi ni Hadiyth ambazo hazikusihi upokezi (sanadi) wake. Mfano wa
Hadiyth dhaifu inayotumiwa na baadhi ya watu ni Hadiyth ya Layla bint
Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa
shuka mbili, kikoi, kanzu, na kilemba. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake
ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja,
anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo[13].
Uandaaji Wa Sanda
Shuka hizo kwa ajili ya sanda zitatandikwa sehemu safi. Kisha zitafukizwa udi na manukato mazuri mara tatu, kama alivyoelekeza Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake):
“Mtakapoweka manukato ya maiti basi wekeni mara tatu.”[14] Isipokuwa sanda ya aliyehirimia kufanya hija haitapakwa manukato wala haitafukizwa udi.”
Hii imeesimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake) kwamba Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) amesema:
“…Msimpake manukato wala msimfunike kichwa chake kwani huyo atafufuliwa siku ya kiama hali ya kuwa analeta talbiya”[15] (Al-Bukhaariy na Muslim).
Baada
ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake. Itachukuliwa ncha ya
upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto
itafanywa hivyo hivyo. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya
tatu. Kisha itachukuliwa kuanzia kichwani na itafungwa na miguuni pia
itafungwa. Pia itawekwa pamba iliyolowanishwa manukato mazuri na
itawekwa juu ya macho yake na mdomoni mwake kama alivyoelekeza Shaykh
Ibn ‘Uthaymiyn. Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya
kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa.
Kumswalia Maiti
Ndugu msomaji, ni wajibu kumswalia kila maiti wa Kiislamu isipokuwa hawa wafuatao:
1. Mtoto mdogo ambaye hajafikia kubalehe. Na hii tunaipata katika Hadiyth iliyosimuliwa na bi Aaisha (radhi ya Allaah iwe juu yake) kuwa:
“Alikufa Ibraahim mtoto wa Mtume wa Allaah na hali ya kuwa ana miezi minane na Mtume hakumswalia.”[16]
2. Mtu aliyekufa shahidi (aliyekufa vitani) kwani Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) hakuwaswalia waliokufa katika vita vya Uhud.
Ndugu
msomaji, fahamu kuwa tunaposema kuwa si wajibu kuwaswalia watu wa aina
hii hatuna maana kuwa ni haraam kuwaswalia, bali tunamaanisha kuwa
hakuna ulazima au uwajibu wa hilo. Lakini wakiswaliwa inafaa kwa kuwa kuna ushahidi juu ya hilo kama alivyosimulia ‘Aaishah, mama wa waumini, anayesimulia:
“Aliletwa mtoto kwa Mtume wa Allaah (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) miongoni mwa watoto wa answaar (watu wa Madiynah) na Mtume akamswalia”.[17]
Ndugu msomaji, ni matarajio yetu kuwa utangulizi huu utakuwa ni mwanzo wa kuifahamu vizuri Swalah ya Jeneza.
Namna Ya Kumswalia Maiti
Maiti huswaliwa kwa kufuata utaratibu huu:
Atasimama
Imaam (kiongozi wa Swalah) upande wa kichwa, kama maiti ni mwanaume, na
hii imethibiti katika Hadiyth ya Abu Ghaalibi al-Khayyaat, amesema:
“Nimemshuhudia Anas bin Maalik akiswalia maiti ya kiume akasimama usawa wa kichwa chake.”
Pia
Imaam atasimama usawa wa katikati wa ikiwa maiti ni mwanamke, kama
ilivyothibiti katika Hadiyth ya Samurah bin Jundub, anasema:
“Nimeswali nyuma ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) naye akimswalia mama wa Ka’ab….akasimama katikati yake.”
Kisha,
Imaam ataleta takbira kwa kusema, ‘Allaahu Akbar’, (Allaah ni mkubwa)
mara nne au tano au tisa, kwani aina zote hizi zimethibiti kutoka kwa
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake). Lakini mara nyingi Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alileta takbira nne (4).
Katika takbira ya kwanza, itasomwa suratul-Faatihah, baada ya kumlaani Shaytwaan, bila kudhihirisha sauti.
Katika takbira ya pili, itasomwa Swalah ya Mtume kwa ukamilifu wake.
اَللّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا صَلَّيْتَ
عَلَى اِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ اِبْرَاهِيمَ و بارك على محمدٍ وعلى آلِ
محمدٍ كما باركتَ على إِبراهيم وعلى آلِ إبراهيمَ إِنَّكَ حَميدٌ مَجيد
Katika takbira ya tatu itasomwa du’aa ya kumuombea maiti, nazo ni nyingi zilizothibiti kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake).
Katika
takbira ya nne, ambayo ni ya mwisho, itasomwa du’aa yoyote au
atanyamaza (anayeswali) na kisha atatoa salamu. Namna zote hizi mbili
zimethibiti.[18]
Ndugu
msomaji, ni muhimu ufahamu kuwa kuna nyakati tatu muhimu ambazo haifai
kuswali ndani yake ila kwa dharura. Nyakati hizo zimebainishwa katika
Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhi ya Allaah iwe juu yake) anayesimulia:
“Alikuwa Mtume (Rehma na amani za Allaah iwe juu yake) anatukataza kuswalia au kuzika maiti katika nyakati tatu:
Kwanza - wakati wa kuchomoza jua mpaka linyanyuke juu,
Pili
– wakati anaamka aliyelala qayluulah (yaani saa 6:00 mchana wakati jua
linapokuwa utosini au katikati mpaka lihame kuelekea upande wa
Magharibi).
Tatu – wakati jua linapokaribia kuzama mpaka lizame kabisa.”[19]
NB: Suala hili lina mitazamo tofauti miongoni mwa wanachuoni wa Ahlus Sunnah wal-Jama’ah[20]
juu ya kufaa kuswalia jeneza na kuzika katika nyakati hizi. Lakini
wengi kati yao wanaliona hilo halipendezi kishari’ah (makruhu) nao ni
kama vile ‘Atwaa, An-Nakha’iy, Al-Awza’iy, Ahmad, Is-haaq, na
Ath-Thawriy. Ash-Shaafi’iy yeye anaona kuswalia wakati wowote na kuzikwa
inafaa[21]. Kauli ya jamaa (ya kwanza) ni bora kwa kuwa imeafikiana na Hadiyth.
Kuzikwa
Jambo
la nne analopaswa kutekelezewa maiti ni kuzikwa. Kaburi ni lazima liwe
refu kwenda chini na liwe pana. Kina cha kaburi kiwe sawa na kimo cha
mtu mzima na kunyoosha mkono, na litachimbwa kiasi maiti akilazwa kwa
ubavu wa kulia atakuwa anaelekea Qiblah[22].
Kaburi
likiwa tayari, maiti atachukuliwa katika jeneza na kuwahishwa katika
kaburi. Wakati wa kusindikiza jeneza (kumpeleka maiti kaburini), mambo
yafuatayo yanapaswa kuchungwa:
Kwanza, lisifuatwe jeneza kwa sauti wala kwa moto. Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) amesema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah:
“Msifuate jeneza kwa sauti wala kwa moto.”[23]
Hapa inamaanisha sauti yoyote ya mwanadamu. Pia haifai kubeba chetezo cha ubani chenye moto wakati wa kusindikiza jeneza.
Pili, jeneza lisifunikwe na chochote. Kufunika jeneza au kaburi wakati wa kuzika ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na ushahidi[24].
Baada ya maiti kuwasilishwa kaburini, watatakiwa watu baadhi washuke
ndani ya kaburi, na iliyo bora zaidi ni kuwa watakaoingia ndani ya
kaburi wawe ndugu wa marehemu.
Allaah Mtukufu Anasema:
وَأُولُو الأرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
“Na
jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi (katika
kurithiana na mambo mengineyo) katika Kitabu cha Allaah. Hakika Allaah
ni Mwenye kujua kila kitu”[25]
Maiti atalazwa kama tulivyoelezea katika uandaaji wa kaburi, huku wakisema wanaomlaza maiti kwenye mwana-ndani:
“Kwa jina la Allaah na juu ya mila ya Mtume wa Allaah” au “Kwa jina la Allaah na juu ya Sunnah ya Mtume wa Allaah.” Haya yamethibiti kwa riwaya zote.
Wanaotakiwa
kuyasema maneno haya ni wale wanaomuweka maiti katika mwanandani
(sehemu ndogo inayochimbwa ndani ya kaburi kwa ajili ya kumlaza maiti
kwa ubavu wake wa kulia) na sio walio juu ya kaburi. Haya yameelekezwa
na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Bayadhi kuwa:
“Maiti
anapolazwa katika kaburi basi aseme yule anayemuweka katika kaburi
wakati wa kumuingiza katika mwanandani; Kwa jina la Allaah na kwa ajili
ya Allaah na juu/kwa kufuata mila ya Mtume wa Allaah.”[26]
Baada ya maiti kulazwa katika mwanandani, kaburi litafukiwa na mwisho litainuliwa kiasi cha shibri[27] moja tu. Na hili linathibitika kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhi ya Allaah iwe juu yake) amesema:
“Kwa hakika Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliwekwa katika lahdi (mwanandani) na yakawekwa nyuma yake matofali na likanyanyuliwa kaburi lake kiasi cha shibri moja.”[28]
Kujengea Kaburi
Kwa taratibu na mafunzo sahihi ya Kiislamu, kaburi halitajengewa. Haikupata kuonekana zama za Mtume (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake)
kaburi likajengewa na yeye akiwa hai, bali alionekana na kusikika kwa
kinywa chake akilikemea vikali suala hili. Dalili juu ya hili zipo
nyingi, mojawapo ni Hadiyth hii ambayo ameisimulia Abuu Ya’ala akisema,
“Amekataza Mtume wa Allaah kujengwa juu ya kaburi na kukaa au kukanyaga juu yake na kuswali kwa kuyaelekea makaburi.”[29]
Ndugu
msomaji, jua ya kwamba makaburi ya Baqiy (sehemu walikozikwa Waislamu
wa mwanzo, Maswahaba) mpaka sasa yapo na Waislamu wanaendelea kuzikwa
katika eneo hilo. Waliojaaliwa kwenda Hijja ni mashahidi kwani huwa
wengi wanayazuru makaburi haya na hayajajengewa. Suala la kujiuliza ni
Je, kama makaburi hayo yangekuwa yanajengwa ingewezekana leo kuwepo eneo
la kuzikia hadi sasa? Hasa ukizingatia kuwa kutoka Mtume (Juu yake rehma na amani ya Allaah) alipokufa mpaka sasa ni zaidi ya miaka 1400 imeshapita? Ni wazi kuwa kusingekuwa na nafasi tena ya kuzikia.
Kwa
msingi huu tunatumia fursa hii kumuusia kila asomaye Makala haya kuwa
maiti hanufaiki na na wala hana haja na vitu vya duniani, si vigae,
marumaru, wala jengo la aina yoyote katika kaburi, bali anachohitaji
zaidi maiti ni du’aa yako. Mkumbuke, kisha muombee msamaha kwa Allaah
Ampunguzie adhabu za kaburi bila kutumia utaratibu maalum, hapo utakuwa
umemfanyia jambo kubwa sana.
Kutokana na Hadiyth tuliyoinukuu punde tunajifunza mambo kadhaa ambayo huwa tunayafanya bila kujua ubaya wake. Mfano wa hayo ni kama
kukalia na/au kukanyaga makaburi. Haya tunayashuhudia wakati maiti
anapofikishwa katika eneo la makaburi, watu husimama juu ya makaburi na
wengine huyakalia. Hili ni suala la kuwa makini nalo na kujichunga
wakati tukiingia makaburini tusiyakanyage wala kuyakalia.
Kuzika Maiti Msikitini
Ndugu
msomaji, miongoni mwa makatazo ni kuzika maiti Misikitini. Imekuwa
kasumba ya baadhi ya watu kuacha wasia kuwa wakifa wazikwe Misikitini
kwa kuwa pengine wao ndiwo waliotoa maeneo yaliyojengwa Misikiti hiyo au
vinginevyo. Hii inawapelekea watu kuswali kwa kuyaelekea makaburi,
jambo ambalo limekatazwa na shari’ah ya Kiislamu. Jambo hili limekuwa ni
fitna kubwa miongoni mwa Waislamu kwani miongoni mwa madhara makubwa
yatokanayo na jambo hili ni kwa watu kuanza kuomba na kufanya tawassul
(kumuomba Mola kupitia makaburi hayo) na hatimaye kuabudiwa kabisa
makaburi hayo. Haya ni masikitiko makubwa.
Aliulizwa mmoja wa wanachuoni, Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn kuwa ni ipi hukumu ya Swalah kwenye Msikiti wenye kaburi?
Akajibu akasema,
“Ikiwa
kaburi limeutangulia Msikiti (yaani kaburi lilikuwepo kabla Msikiti
haujajengwa) basi ni wajibu kuuhama Msikiti huo na ubomolewe na liachwe
kaburi. Na kama Msikiti umelitangulia kaburi basi ni wajibu kufukuliwa
(kuhamishwa) kaburi hilo na maiti akazikwe makaburini.”
Pia Shaykhul Islaam amesema,
“Wala haitaswihi (haitafaa) Swalah kwenye makaburi au kwa kuyaelekea makaburi, na katazo hili ni kwa kuziba mianya ya shirki”[30]
Kuhusu Kaburi La Mtume (Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake)
Maswali huja kuwa mbona kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
liko ndani ya Msikiti na limejengewa? Katika kulifafanua hili
inahitajika kwa wewe msomaji kuzingatia kwa umakini, kwani jambo hili
linatatiza wengi katika watu.
Historia
inaonesha kuwa Msikiti wa Madiynah haukujengwa juu ya kaburi lolote
kwani Msikiti ulijengwa mwaka wa kwanza wa Hijrah (mwaka wa Kiislamu) na
wakati huo Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akiwa hai.
Pia haikushuhudiwa kuwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliwahi kumzika yeyote katika Maswahaba zake katika Msikiti.
Tatu, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
hakuzikwa ndani ya Msikiti, na yeye mwenyewe alikemea hilo la kuzika
watu Misikitini kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na ibn Mas’uud
(Allaah amuwie radhi) kuwa,
“Hakika
miongoni mwa viumbe waovu ni wale ambao kitafika Qiyamah hali ya kuwa
wapo hai na wale ambao wameyaweka makaburi Misikitini (wamezika watu
ndani ya Misikiti).”[31]
Maswahaba ni mfano bora wa kuigwa kwani wao waliyazingatia vilivyo na kuyafanyia kazi maneno na mafunzo ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake),
kiasi waliweza kufikia kutoa mali zao na nafsi zao kwa ajili yake.
Unaweza kujiuliza, inawezekana kweli watu hawa (Maswahaba) wakakiuka
maelekezo ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) na hatimaye wamzike Msikitini? Kama hawakumzika Msikitini, je ni nani aliyeliingiza kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) Msikitini, na wapi lilikuwa kabla?
Jawabu ni kuwa aliyeliingiza Msikitini kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ni ‘Umar bin Abdil-‘Aziyz kwa amri ya mtawala wa zama hizo aitwaye Al-Waliyd bin ‘Abdil-Malik katika mwaka wa 88 H.
Inafahamika kuwa nyumba ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
ilikuwa inapakana na Msikiti kwa kutengwa na ukuta mmoja upande wa
kushoto na hasa chumba cha Bibi ‘Aaishah (Allaah awe radhi naye) ambacho
ndiko alikozikwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake),
pamoja na Maswahaba zake wawili, Abu Bakr na ‘Umar (Allaah awawie radhi
wote wawili). Baada ya Msikiti kupanuliwa, makaburi hayo
yakaingia/yakaingizwa Msikitini, na hii ni kwa sababu Al-Waliyd bin
‘Abd-l-Malik alikuwa hana elimu juu ya hilo. Baadhi ya wafuasi wa
Maswahaba (Taabi’iyn) walipojaribu kulipinga hilo walionekana hawana
kauli. Miongoni mwao ni Sa’iyd bin al-Musayyib, yeye alijaribu kushauri
kuwa basi chumba cha Bibi ‘Aaishah (Allaah awe radhi naye) (mke wa
Mtume), ambako alizikwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
kisiingizwe ndani ya Msikiti, bila mafanikio. Kwa kuwa Al-Waliyd
alikuwa ndiye mwenye mamlaka, akamlazimisha ‘Umar bin ‘Abdil-Aziyz
kubomoa ukuta uliokuwa unatenganisha makaburi hayo na Msikiti na kwa
hiyo makaburi yakajumuishwa ndani ya Msikiti. Kwa ufafanuzi huu mfupi,
ni wazi kuwa hakuna hoja ya kudai kuwa inafaa kuzika au kujengea
makaburi.[32]
Kuwekea Alama Makaburi
Je,
ni namna gani unaweza kulitambua kaburi au kuliwekea alama kaburi? Hilo
linajibiwa katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu
Al-Muttwallib bin Abi Wadaa (Allaah amuwie radhi) kuwa, pindi alipokufa ‘Uthmaan bin Madh’uun, ndugu wa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) kwa kunyonya ziwa moja, baada ya kumaliza kufukia kaburi, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alibeba jiwe na akaliweka upande wa kichwani kisha akasema,
“Nimeliweka jiwe hili ili nipate kulijua kaburi la ndugu yangu na nizike pembeni yake atakayekufa katika jamaa zangu”[33]
Baada Ya Kuzika
Ndugu
msomaji, kinachofuatia baada ya kufunika kaburi ni kukaa kwa ajili ya
kuwakumbusha waliohudhuria mazikoni, kama alivyofanya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth ya Al-Baraa bin ‘Aazib iliyopokelewa na Jama’ah.[34]
Fahamu
kuwa hakuna kitu kinachoitwa talaqini baada ya maziko, kwani mapokezi
juu ya jambo hilo ni dhaifu na hayakusihi kabisa. Hadiyth inayozungumzia
talaqini ni dhaifu na haifai kuitumia katika hoja, na yeyote anayefanya
talaqini anahesabika kuwa ni mzushi[35].
Mtume (Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake) Alikuwa Akifanya Nini Alipomaliza Kuzika?
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akishamaliza kuzika (yaani baada ya kufukia kaburi) alikuwa akisimama na kisha husema maneno haya:
“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumuombee uthabiti, kwani hakika sasa hivi anaulizwa maswali”[36] kama ilivyokuja katika Hadiyth ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan.
Pia
ifahamike kuwa, haifai kwa Muislamu kuzikwa katika makaburi ya
wasiokuwa Waislamu, wala wasiokuwa Waislamu kuzikwa katika makaburi ya
Waislamu[37].
Kufikia
hapa mpendwa msomaji, tunataraji kuwa, kwa mapenzi ya Allaah, utakuwa
umefahamu, japo kwa ufupi, ukweli kuhusu mazishi sahihi ya Kiislamu.
Tunataraji
pia kuwa, utakuwa umebaini uzushi na uongo kuhusu mazishi ya Kiislamu.
Utaufahamu uongo huo pale utakapoona au kusikia watu wanasema au kufanya
kinyume na haya tuliyoeleza, halafu yakawa hayana ushahidi, au ushahidi
upo lakini ni dhaifu.
Tukupe
changamoto ndugu msomaji, pindi ikitokea unahudhuria muhadhara wake,
fanya kumuomba akupe ushahidi kutoka katika Qur-aan au katika Hadiyth za
Mtume, kama ambavyo tumekuwa
tukibainisha katika makala hii. Hapo ndipo utakapogundua hila yake yeye
pamoja na wengine wanoupaka matope Uislamu.
Fahamu pia kuwa, ibada yoyote utakayoona inafanywa na Muislamu lazima iwe na uthibitisho kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake), kinyume chake huo utakuwa ni uzushi katika dini.
Tunamuomba Allaah Ajaalie Makala hii iwe chachu ya Waislamu kuipenda dini yao na kujifunza na kuyatekeleza yaliyo sahihi katika dini.
Tunamuomba Allaah Atusamehe madhambi yetu na walio kufa kabla yetu katika Imani.