DALILI ZA KIAMA
MwenyeziMungu Subhanahau wa
Taala anasema:-
"Yeye ndiye Mjuzi wa siri wala hamdhihirishii yeyote siri
Yake isipokuwa aliyemridhia katika mitume Yake".
Al Jinn- 26-27
Kutujulisha Mtume(SAW) kwa
siri za Dalili za (kukaribia kwa) Siku ya Kiama, dalili ambazo hazikudhihirika
isipokuwa katika wakati wetu huu, ni ushahidi wa ukweli wa ujumbe wake na pia
kunathibitisha kwamba Kiama kipo kweli na kwamba kimekwisha karibia
MIONGONI MWA DALILI ZILIZOKWISHA ONEKANA NI HIZI ZIFUATAZO
1)Mambo Makuu Ambayo
Waliotutangulia Hawakuweza hata Kuyafikiria.
Maajabu hayo na mambo
makubwa mengi yaliyovumbuliwa pamoja na mambo ya kisiasa, nidhamu mbali mbali,
sayansi pamoja na mambo yanayotokea kila siku duniani, ni mambo ambayo
waliokuja kabla yetu wakiwa ni Waislamu au makafiri, hawakuweza kuyafikiria
kabisa.
Mtume (SAW) ametujulisha
juu ya mambo haya aliposema;
"Haitosimama saa
(kiama) mpaka mtakapoona mambo makubwa makubwa ambayo hamkuwa mkiyaona wala
hamkuweza kuyafikiria katika nafsi zenu".
2) Waendao Miguu Chini Wasiomiliki Nguo Wanaochunga mbuzi Wanaoshindana
Kujenga Majumba Marefu Marefu
Mtu asiyemiliki viatu,
anaetembea uchi, asiyemiliki nguo ya kuweza kumsitiri mwili wake wote, na
anategemea chakula chake kwa wengine, asiye na kazi isipokuwa kuchunga mbuzi.
Isingempitikia mtu yeyote
hapo zamani kwamba mwenye sifa kama hizo ataweza kujenga nyumba yoyote, sembuse
aweze kujenga nyumba refu, tena aweze kushindana na wenzake kwa kujenga majengo
marefu kisha kushindana huko kwa watu wa nama hii, kuwe ni jambo la kawaida tu
(mtindo) sio kwamba ni mtu mmoja tu atakayefanya hivyo, bali ni wengi sana
miongoni mwa wachunga kondoo wasio na viatu wasio na nguo, wasiojitegemea, ni
mambo ambayo mtu asigeweza kuyafikiria kwamba yatatokea.
Lakini haya yametokea baada
ya MwenyeziMungu kuwafungulia Waislamu na wengineo katika mali zilizomo ardhini
na hasa Petroli, tukawaona wachunga kondoo wasiovaa viatu, wala nguo (hata nguo
zao wanategemea kushonewa na mataifa mengine), wasiojitegemea, wankishindana
kujenga majumba marefu, kama alivyokwishatuelezea Mtume(SAW) na akatubainishia kwamba hizi ni miongoni mwa
Dalili za kukaribia kwa Kiama.
Akasema;
"Mtakapowaona wasiovaa
viatu, wasiovaa nguo, wasiojitegemea wenyewe, wachunga kondoo, wakishindana
kujenga majumba mrefu, basi muisubiri Saa (Kiama).
(Bukhari na Muslim)
3) Kuja Kwa Wanawake Waliovaa Huku Wakiwa Uchi, Wakiyumba Na Kuyumbisha Na Vichwa Vyao (viko) Kama Nundu
Ya Ngamia
Kulikuwa na tatizo katika
kuwafahamu wanawake aliowataja Mtume (SAW) watakaokuja mwisho wa Umma huu, na
kwamba watakuwa wanavaa nguo na wakati huo huo wako uchi.
Mtu anaweza kushangaa vipi
mtu anaweza akawa amevaa nguo na yupo uchi
wakati mmoja, mpaka tulipoyaona
wenyewe katika wakati wetu huu. Utaona mwanamke amevaa nguo lakini zinambana
ama ni nyepesi zikimkashifu sehemu zake za aibu na kuzidhihirisha, (au atakuwa
amevaa nguo nyingi lakini fupi) au atakuwa mwenye kuvaa nguo mahali mwengine na
mahali mwengine anazivua (Sehemu za mabwawa ya kuogelea au pwani).
Wanawake hao pia wanakuwa
wanayumba yumba na huku wakiyumbisha.
Kumekamilika kuyumba kwao
baada ya kuyumba mbali na njia iliyoonyooka, na kukapatikana kuyumba kwa miili
yao walipowatilia visigino virefu katika viatu vyao ili wakamilishe kwa
kuiyumbisha miili yao pia, na kwa njia hiyo wanayumbisha wengi miongoni mwa
vijana wa kiume wakibabaika na urembo wao wanaoutembeza.
Na maana ya 'Vichwa vyao
kama nundu ya ngamia inayoyumba';
Haya tunayashuhudia wakati
wetu huu (kwa wanaovaa mawigi na katika staili mbali mbali za usukaji), yote
haya yakisadikisha hadithi ya Mtume (SAW) aliyefunuliwa haya na Mola wake mia
elfu na mia nne iliyopita aliposema:
"Aina mbili katika
umati wangu ni katika watu wa Motoni, sikuwaona: Wanaume wenye viboko mikononi
mwao (urefu wake) kama mikia ya ngo'mbe, wanawapiga watu (kwa kuwadhulumu na
kuwaonea). Na wanawake waliovaa nguo (huku) wakiwa uchi walioyumba na
kuyumbisha, vichwa vyao (wanawake hao)
mfano wa nundu la ngamia linaloyumba. (Watu hawa) Hawataingia Peponi wala hawataipata (hawataionja) harufu yake".
(Ahmad na Muslim)
4) Kuzungumza Kwa Vitu
Mtume (SAW) amesema:-
"Moja katika dalili za
kukaribia kwa Kiama ni kuwa mtu aliyetoka nyumbani kwake, anaporudi anakuta
viatu na fimbo yake vikimuelezea yote yale waliyofanya watu wake baada ya
kutoka kwake".
(Imetolewa na Attirmidhy na
Al Hakim.)
Kiatu ni kitu kisichokuwa
na roho na fimbo ni kitu kisichokuwa na roho. Isingempitikia mtu wakati ule
kufikiria kwamba vitu kama hivyo vingeweza kusema, lakini katika zama zetu hizi
tunaviona vitu hivi vikisema.
Vipi kiatu na fimbo
vitamueleza mtu yale yaliyotokea nyumbani?
Hivi sasa vimekwishaundwa
vyombo ambavyo mwanaadmu anavibeba na vinamletea habari na sauti kutoka
nyumbani kwake au kutoka nyumba za wenzake. (Hakuna kilichobaki isipokuwa
kiundwe chombo (iundwe kamera) mfano wa fimbo ili ibebeke kwa urahisi au
kiwekwe chombo hicho mahali ndani ya kiatu ili kisionekane), au kiwezekane
kuwekwa katika sehemu ya fimbo au katika sehemu yoyote ya kiatu bila kuonekana.
Kuzuilika Kwa Elimu, Wingi Wa Mitetemeko Ya Ardhi Na Kukaribiana Kwa
Wakati, Kuenea Kwa Fitina Na Kwa Majengo Marefu.
Kuzuilika kwa Ilimu maana
yake ni Kufa kwa maulamaa na kutokupatikana kwa maulamaa wengine kuchukua
nafasi zao, na makusudio yake ni maulamaa wa Kiislamu kama ilivyotufahamisha
Hadithi.
Na Kukithiri kwa Mitetemeko
ya ardhi, maana yake ni hiyo mitetemeko inayoangamiza tunayoiona na kuisikia
kwa wingi siku hizi.
Na kukaribiana kwa wakati
*, maana yake ni kwenda haraka kwa siku bila kuzihisi utafikiri masaa machache
tu yamepita, na hii inatokana na mambo
mengi yanayotokea ulimwenguni na
kutufanya tusizihisi siku zinavyokwenda, na MwenyeziMungu ndie anayejua zaidi,
kwani unapokuwa umejishughulisha na kazi saa hupita bila kuhisi kama kwamba ni
dakika chache tu, lakini unapokuwa bila ya kazi wakati unauona mrefu, hauendi,
na wakati wetu huu umejaa mambo mengi yanayosababisha siku zipite haraka sana. [1]
Kuenea kwa Fitna, maana
yake ni wingi wa maasia yanayomtia mtu katika mitihani ya dini yake. Na maasia
hayo hufanyika wazi wazi bila ya kificho.
Ama urefu wa majumba, ni
juu yako msomaji kulinganisha majengo yaliyokuwa miaka hamsini iliyopita na ya
hivi sasa na uone vipi yalivyorefuka.
Yote hayo amekwishatueleza
Mtume wa Mwenyezi Mungu(SAW), aliposema:-
"Hakitosimama kiama
mpaka izuilike ilimu na ikithiri mitetemeko ya ardhi na wakati ukaribiane na
kuongezeka kwa mitihani na watu wawe wanashindana kwa kujenga majumba
marefu."
Bukhari na Muslim
Kuhusisha Salamu, Kuenea Kwa Biashara, K upigana
Pande Ndugu wa Nasaba, Kusoma Kwingi Na Ushahidi Wa Uwongo.
Kuhusisha salamu; ni kule
kuwatolea salamu watu makhsusi.
Kuenea kwa biashara; ni kule kuenea kwake.
Na Kuenea kwa kalamu; ni kuongezeka utumiaji wake nayo ni dalili ya
kusoma na kuandika kwa wingi.
Haya yote yameelezwa katika
hadithi ya Mtume (SAW) isemayo:
“Kwa hakika kinapokaribia
Kiama watu watawasalimia watu makhsusi, na biashara itaenea hata mke atakuwa
akimsaidia mumewe katika kazi za biashara, na kupigana pande ndugu wa nasaba,
na kuenea kwa kalamu na kuongezeka kwa ushahidi wa uongo na kuficha ushahidi wa
kweli.
(Imetolewa na Bukhari).
Kuongezeka Uzinzi Na Ulevi
Mtume (SAW) amesema:-
"Hakika katika dalili
za kukaribia kwa Kiama, ni kutoweka kwa Ilimu, kuongezeka ujinga, kuongezeka
uzinzi, na kuongezeka kwa unywaji wa pombe.
Bukhari na Muslim
(Kongezeka Ujinga Maana
Yake Ni Kuongezeka kwa ujinga wa Kutoijuwa Dini).
Kuenea Ulaji Wa Riba
Mtume (SAW) amesema:-
"Utawafikia watu
wakati, hapatakuwepo mmoja wao asiyekula riba, na yule asiyekula basi litamfikia
vumbi lake.
Abu- Daud na Ibnu Maajah
Wakati wetu huu sasa ulaji
wa riba umekwisha enea kwa njia za mabenki na njia nyengine juu ya kuenea kwa
benki za Kiislamu ambazo hazijishughulishi na ulaji wa riba, basi tunamwomba
MwenyeziMungu aziongeze benki za aina hii.
9) Kusalimiana Kwa Kulaaniana,
Na Wanaume Kujifananisha Na Wanawake Na
Wanawake Kujifananisha Na Wanaume
Uislamu unatuamrisha
tutoleane salamu njema na kuzijibu vyema. Hivi ndivyo walivyokuwa Waislamu hapo
zamani, mpaka ulipofika wakati wetu huu tukaona watu wanasalimiana kwa
kulaaniana.
Mtume(SAW) alisema:-
"Umma utakuwa bado
unafuata sheria njema iwapo hayajawatokelea mambo matatu;
Iwapo bado hawakuzuwiliwa
elimu, na hawakuongezeka miongoni mwao watoto wa haramu na kutokea miongoni mwao
Al Saqaarun.
Wakauliza : Ni nani hawa Al
Saqaarun?
Akasema : Vijana
watakaotokea katika zama za mwisho watakuwa pale wanapokutana wanasalimiana kwa
kulaaniana".
Ahmed na Al Hakim na Al
Tabarani
Hapakuwa na mtu aliyeweza
kufikiria kwamba iko siku mwanamme atajifananisha na mwanamke au kinyume cha
hivyo mpaka ukatufikia wakati ulipotujia msiba huu.
Lakini Mtume (SAW)
alikwisha kutupa habari hiyo.
MwenyeziMungu alimjulisha
juu ya yale yatakayotokea ndipo Mtume (SAW) aliposema:-
"Miongoni mwa alama za
kukaribia kwa Saa (Kiama) ni wanaume kujifananisha na wanawake na wanawake
kujifananisha na wanaume".
Imepokelewa na Abu Daud
10) Na Kundi Likidhiihirisha
Haki
Kama utakavyozidi ufisadi,
MwenyeziMungu kwa hikima yake ametaka libaki kundi la watu likiidhihirisha
haki. (Kundi hilo) Linawasimamishia watu hoja kwa dalili huku likiwalingania na
kuwaita katika njia ya MwenyeziMungu na katika kushikamana na kitabu chake na
Mafundisho ya Mtume wake (SAW).
Na haya ndio
tunayoyashuhudia sasa, kila mahali hawakosekani watu wanaoidhihirisha dini ya
MwenyeziMungu wakishikamana na kitabu cha MwenyeziMungu na Mafundisho ya Mtume
wake (SAW).
Kuhusu watu hawa Mtume
amesema:-
"Litaendelea kubaki
kundi miongoni mwa umma wangu
likiidhirisha haki (wala) hawadhuriki na wale wanaowaachia mkono mpaka
itakapotokea amri ya MwenyeziMungu".
(Attirmidhy Na Abu Daud).
Haya ni machache tu
miongoni mwa mengi aliyotujulisha Mtume(SAW) tokea miaka elfu na mia nne
iliyopita, yakiwa ni ushahidi juu ya ukweli wa bishara zake na yakithibitisha kwamba ameletwa kuwa mwonyaji
kwetu juu ya adhabu kali itakayowakuta (wanaomuasi MwenyeziMungu).
Basi kama tunavyoziona
dalili za kukaribia kwa Kiama hivi sasa, tutakuja kukiona Kiama chenyewe kesho,
kwa sababu aliyetujulisha juu ya yote hayo ni mmoja, naye ni msema kweli
anayesadikiwa, Muhammad bin Abdillah (SAW).
USHAHIDI KATIKA QURANI TUKUFUKU JUU YA KUBADILIKA KWA NIDHAMU ZA MAUMBILE
MwenyeziMungu ameumba
ulimwengu na anauendesha kwa nidhamu iliyo thabiti, lakini anapotaka,
hubadilisha nidhamu hizo ili kuupa nguvu ushahidi wa Mitume yake na ili
wasadikiwe.
Miongoni mwa mifano hiyo ni
yale yaliyotokea mikononi Mtume wetu (SAW), nayo ni mengi yakiwa ni ushahidi
uliowafanya watu wengi waukubali ukweli wa ujumbe wake na utume wake, yakiwemo
yafuatayo:-
1) KUPASUKA KWA MWEZI
Nidhamu iliyoumbiwa mwezi
ni kuwa Mwezi ni kitu kimoja, hapana
awezaye kuupasua sehemu mbili isipokuwa MwenyeziMungu, lakini makafiri
walipomkadhibisha Mtume (SAW) na kutaka dalili ili wamsadiki, MwenyeziMugnu
akaupasua mwezi pande mbili na Mtume (SAW) akawaambia makafiri;
"Shuhudieni"
Lakini makafiri walipoona
vile wakasema;
"Ameturoga
Muhammad".
Lakini hawakuikadhibisha
dalili hiyo walipoiona, ndipo MwenyeziMungu alipoteremsha kauli Yake isemayo:-
"Saa (kufika kiama) imekaribia;
na mwezi umepasuka. Na wakiona Muujiza hugeuka upande na kusema; "Uchawi
tu (huu wake) unazidi kundelea!".
(Al Qamar 1-2)
ISRAA NA MIRAJI
MwenyeziMungu alitaka kumpandisha Mtume
wake(SAW) na kumfikisha penye "Sidratul Muntaha (mkunazi wenye kumalizika
mambo yote) uliopo juu ya mbingu saba, na hakupandishwa kutokea Makka, bali
alimpeleka katika usiku mmoja kutoka Makka hadi Baitul Maqdis (Jerusalem), na
kutoka hapo ndipo alipopandishwa.
Kupelekwa kwake kutoka
Makka hadi Baitul Maqdis katika usiku mmoja kulikuwa ni dalili kwa makafiri
ikithibitisha ukweli wake, kwa sababu walimkadhibisha Mtume(SAW), kisha wakampa
mtihani ili wahakikishe ukweli wake.
Wakamtaka awaelezee wasfu
wa Baitul Maqdis, wakiwa wanaelewa kuwa yeye hajapata kuuona msikiti huo kabla
ya hapo. Mtume(SAW) akawaelezea jinsi ulivyo msikiti huo kwa kuzitaja pembe
zake zote. Kisha wakamuuliza juu ya msafara wa jamaa zao walokuwa wakiusubiri
(ukitokea huko Jerusalem), akawaeleza mahali msafara huo ulipo kwa wakati huo,
idadi ya watu waliokuwemo ndani yake msafara huo, kabila zao, aina ya ngamia
waliokuwa nao, na akawaelezea hata wasfu wa ngamia anayeutangulia msafara huo
na nini amebeba ngamia huyo, na akawaelezea hata wakati gani utawasili msafara
huo, na ukawasili wakati ule ule alowaambia kuwa utawasili.
Haya yote yakawa ni
ushahidi wa kupelekwa kwake Baytul Maqdis(Israa), na kwa hivyo unakuwa pia ni
ushahidi wa kupandishwa kwake mbinguni (Miraji).
Qurani imeelezea juu ya
Israa.
Mwenyezi Mungu anasema:-
"Utukufu ni wake Yeye
ambaye alimpeleka mja wake usiku mmoja tu kutoka msikiti mtukufu wa (Makka)
mpaka msikiti wa mbali wa (Baitul Maqdis-Palastina) ambao tumeubariki na
(tumevibariki) vilivyoko pembezoni mwake."
Suratul Israa (Bani Israil
) -1
Ama kuhusu Miraji
(kupandishwa mbinguni), MwenyeziMungu anasema:-
"Jee! Mnabishana naye
juu ya yale anayoyaona (daima)?
Na Mtume akamuona (Jibril)
mara nyengine (kwa sura ile ile ya Kimalaika katika usiku wa Miraji). Penye
mkunazi wa kumalizikia (mambo yote). Karibu yake kuna hiyo Bustani, (Pepo)
itakayokaliwa maisha (na hao watu wema). Kilipoufunika mkunazi huo
kilichoufunika (katika mambo ya kiajabu ya kimbinguni). Jicho halikuhangaika
wala halikuruka mpaka huo(uliowekwa). Kwa yakini aliona (Nabii Muhammad) Mambo makubwa kabisa katika alama, (Qudra) za
Mola wake".
(An Najm 12-18).
Pepo na Moto ni katika
miujiza ya MwenyeziMungu aliyoyaona Mtume(SAW).
Hakika Israa na Miraji ni
miongoni wa ubadilishaji wa nidhamu alizoziumba MwenyeziMungu na akazijaalia
kuwa ni ushahidi wa kuthibitisha ukweli wa Mtume wake(SAW).
UPEPO NA ASKARI WASO ONEKANA UNAPIGANA VITA KUMSAIDIA MTUME NA SAHABA ZAKE
Waislamu walikuwa upande
mmoja wa handaki kubwa walochimba ili kuwazuia washirikina wasiweze kuwafikia,
na makafiri walikuwa upande mwingine wa
handaki hilo.
Ghafla upepo mkali ukatokea
pamoja na askari waso onekana, na upepo huo ukazima moto wa makafiri na
kuwapeperushia mbali vitu vyao pamoja kubomoa majumba yao na kun'goa mahema yao
na kuwakimbiza farasi na ngamia wao.
Tahamaki washirikina waliokuja
kutoka sehemu za mbali na kuwazunguka Waislamu kwa siku nyingi, wakaona
wanafukuzwa wakitaka wasitake. Wakarudi huku wakiwa wamehizika. Waislamu pamoja
na Mtume(SAW) wakawa wanaisoma na kuikariri kauli ya Mtume(SAW):-
"Alhamdu lillahi
wah-dahu sadaqa waa-dahu wa nasara abidahu wa a-azza jundahu, wa hazama l Ah-
zaaba wahadahu."
"Shukurani zote anastahiki MwenyeziMungu
Peke Yake, amesadikisha ahadi Yake, amemnusuru Mtumwa Wake, kawatukuza askari
wake na akayashinda majeshi ya makafiri (Ahzabu) peke Yake".
Na kutokana na haya ndipo
MwenyeziMungu alipoteremsha kauli yake katika Suratul Ahzab aliposema:-
"Enyi mlioamini!
kumbukeni neema za MwenyeziMungu zilizo juu yenu; yalipokufukieni majeshi,
tukayapelekea upepo na majeshi msioyaona (ya Malaika), na MwenyeziMungu
anayaona (yote) mnayoyafanya".
(Ahzab 9)
4) USINGIZI MVUA NA MALAIKA WALITEREMKA KUWASAIDIA WAISLAMU
Waislamu walikuwa wakielekea "Badar"
kupambana na washirikina huku wakiwa na hofu kwa ajili ya uchache wao na
udhaifu wao. MwenyeziMungu akawateremshia usingizi ili iwe alama ya usalama juu
yao. Wengine wakaota, na shetani akaanza kuwatia wasiwasi na kuwafanya waogope
kufa wakiwa na janaba ili warudi nyuma wasipigane vita.
MwenyeziMungu akateremsha
mvua ili waweze kukoga (kujitahirisha na janaba) na ili mchanga ukazane chini
ya miguu yao (isizame ndani ya mchanga) wanapokwenda vitani. Kisha yalipokutana
majeshi mawili hayo, Malaika wakateremka, na makafiri wakashindwa vibaya sana
katika pambano la mwanzo baina ya makafiri na Waislamu. Ndipo ilipoteremka
kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-
"(Kumbukeni)
alipokuleteeni usingizi uliokuwa(alama ya) salama itokayo kwake, na
akakuteremshieni maji mawinguni ili kukutahirisheni kwayo na kukuondoleeni
uchafu wa shetani na kuzipa nguvu nyoyo zenu kuithubutisha miguu yenu chini
(isiwe inazama zama mchangani) (kumbukeni) Mola alivyowafunulia Malaika
akawambia (Malaika); Hakika mimi ni pamoja na nyinyi, basi watieni nguvu wale
walioamini nitatia uwoga katika nyoyo za makafiri. Basi wapigeni katika shingo (zao)
na wakateni katika kila ncha ya vidole vyao".
(Al Anfal 11-12)
5) MAASKARI WA MWENYEZIMUNGU WANAMSAIDIA MUHAMMAD(SAW) DHIDI YA MAKAFIRI KATIKA HIJRA
Makureish waliamua kumuua
Muhammad (SAW), na vijana wao wakaizunguka nyumba yake, lakini Mtume(SAW) alitoka
mbele yao huku MwenyeziMungu akiwa amewaziba macho, na akajificha katika pango
liitwalo (Ghaari Hiraa) yeye na sahibu yake Abu Bakar Al Siddique (RA)
aliyekuwa akihofia wale makafiri walokuwa wakiwatafuta wasije wakachungulia
ndani ya pango hilo na kuwaona, lakini askari wa Mwenyezi Mungu waliwafanya
wasichungulie ndani ya pango.
Mpanda farasi hodari Suraqa
bin Malik aliwafuata Mtume(SAW) na sahibu yake baada ya kutoka pangoni, lakini
alipowakaribia miguu ya farasi wake ilizama ndani ya mchanga mpaka tumbo la
farasi huyo likagusa mchanga na akaanguka kutoka juu ya farasi wake. Ndipo
Suraqa alipoomba amani kutoka kwa Mtume (SAW).
Na haya yanaelezwa katika
aya ya Qurani inayosema:
"Kama hamtamnusuru
(Mtume), basi MwenyeziMungu alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru; alipokuwa
(mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake, (peke yao) walipokuwa wote wawili katika
pango; (Mtume) alipomwambia sahibu yake, "Usihuzunike kwa yakini
MwenyeziMungu yuko pamoja na sisi" MwenyeziMungu akamteremshia utulivu
wake na akamnusuru kwa majeshi msiyoyaona, na akafanya neno la wale waliokufuru
kuwa chini; na neno la MwenyeziMungu ndio la juu. Na MwenyeziMungu ndie mwenye
Hikima".
(Attawba -40)
SUALI NA JAWABU
Mtu anaweza kuuliza:
"Inawezaje imani yangu
juu ya miujiza hii iliyotokea, ikawa sawa na imani ya wale walioshuhudi
yakitendeka?"
Jawabu;
"Kwa kuyazingatia, na
kwa kutumia akili utaifikia imani hiyo;
Kwa mfano Muujiza wa Upepo
na askari wasioonekana, na Muujiza wa Kugawika kwa mwezi, haya yametokea mbele
ya mamia na maelfu ya Waislamu pamoja na washirikina, Kisha (aya katika) Qurani
ikateremshwa na kuyaelezea matukio hayo. Waislamu wakasikia na makafiri
wakasikia jinsi Qurani ilivyoyaelezea matukio hayo. Waislamu wakasadiki
yaliyoelezwa na Qurani yale waliyoyaona kwa macho yao tena mbele yao yakitokea
na hii ikasababisha kuipa nguvu zaidi Imani zao pamoja na kuwafanya wawe
thabiti katika Jihadi na Ibada zao.
Makafiri pia wakasadiki
yaliyoelezwa na Qurani juu ya Miujiza iliyotokea mbele yao, na wala
hawakuyakanusha isipokuwa walifasiri kupasuka kwa mwezi na miujiza mingine kuwa
ni uchawi unaoendelea. Makafiri hao hao baadae wakaingia katika dini ya
Kiislamu, wakawa wao ndio walioiyanyua dini hii na kuineza Mashariki ya ardhi
na Magharibi yake.
MwenyeziMungu ameihifadhi
Qurani isiweze kubadilishwa kwa namna yoyote ile na kama unavyoona kuwa Msahafu
uliopo Marekani uliopo Uchina uliopo Bara Hindi uliopo Urusi uliopo Ulaya
uliopo Afrika, ni Msahafu ule ule uliosomwa na baba zetu na babu zetu katika
Mashariki ya ardhi na Magharibi yake na ndio huo huo aloteremshiwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu Muhammad (SAW).
Kutokana na haya tunaelewa
kwamba miujiza hiyo imeandikwa katika kitabu kitukufu kuliko vitabu vyote,
kitabu ambacho watu wote ulimwenguni wanakubaliana juu ya ukweli huu. (kwamba
yaliyomo ndani ya Qurani hivi sasa, ni yale yale yaliyokuwemo wakati ule Mtume
(SAW) alipokuwepo duniani, bila ya kupunguzwa wala kongezwa neno).
Ingelikuwa Qurani imetoa
habari juu ya jambo kwamba limetokea na kumbe halikutokea, mfano wa Kugawika
kwa mwezi au Kusalitishiwa upepo mkali washirikina katika vita vya Al -Ahzab,
basi wangeyakanusha hayo makafiri na Waislamu, na kwa hivyo asingebakia mtu
katika dini ya Kiislamu.
Lakini yaliyotokea ni
kinyume na hayo na huu ukawa ni ushahidi kwamba yote yaliyoelezwa katika Qurani
ni ukweli uliotokea na kushuhudiwa na Waislamu pamoja na makafiri.
Na MwenyeziMungu
ameyahifadhi yote hayo katika Qurani bila kuongezwa wala kubadilishwa.
USHAHIDI KATIKA KATIKA HADITHI ZA MTUME (SAW) JUU YA KUBADILIKA KWA NIDHAMU ZA MAUMBILE
Waislamu wameyahifadhi
maneno ya Mtume wao (SAW), vitendo vyake pamoja na yale aliyoyakubali, na
wakazihifadhi sifa za mwenendo wake na za umbile lake na kila kinachohusiana
naye, na wakaelezea juu ya miujiza ambayo MwenyeziMungu ameijaalia itendeke
mikononi mwake, miujiza iliyosababisha wengi wao Wasilimu na kuzinukuu habari
hizo vizazi baada ya vizazi.
Maulamaa wa hadithi za
Mtume(SAW) nao wakahangaika kuhakikisha ukweli wa hadithi hizo vizazi baada ya
vizazi wakiyaweka sawa maneno na wakihakikisha juu ya ukweli wa mlolongo wa
majina ya wapokezi wa hadithi hizo (narrators).
Miujiza mingi sana
ilitendeka mikononi mwa Mtume (SAW) na kutajwa katika vitabu vya hadithi zake
(mafundisho). Tutaelezea baadhi ya miujiza hiyo:
KUYAZIDISHA MAJI KIDOGO YAKAWA MENGI
Waislamu walikuwa na shida
ya maji ya kutawadhia hapo Madina.
Anas(RA) amesema;
"Mtume (SAW) alikuja
na chombo mahali paitwapo Zawraa akiwa pamoja na Sahaba wake. Akauweka mkono
wake ndani ya chombo hicho na maji yakaanza kutoka vidoleni pake, watu wote
wakatawadha."
Akasema Qatada;
"Nilimuuliza Anas:
Mlikuwa wangapi?
Akasema;
"Mia tatu".
Bukhari na Muslim
Na Imam Bukhari anasema:
"Yakatokea kama haya
wakati Mtume (SAW) alipokuwa safarini pamoja na Masahaba sabini."
"Yalitokea tena kama
hayo walipokuwa Hudaibiya na idadi ya Waislamu ilikuwa elfu na mia nne,
yalipoongezeka maji kisimani".
Bukhari
Yakatokea tena Mtume(SAW)
alipokuwa safarini pamoja na sahaba zake, alipogusa vyombo viwili vya maji vya
bibi mmoja vilivyokuwa havina hata tone ya maji ndani yake, vikajaa, wakanywa
Waislamu na idadi yao ilikuwa ni wanaume arobaini. Kisha kila mmoja akajaza
kiriba chake, hata yule bibi akasema;
"Nimeonana na mchawi
kupita wote ama yeye ni Mtume kama wasemavyo"
Watu wa kabila lake wote
wakasilimu.
Bukhari
2) CHAKULA KICHACHE KUONGEZEKA KIKAWA KINGI
Mtume (SAW) alikuwa na njaa
akamjia sahaba mmoja aitwaye Abu Talha
akiwa na mikate michache ya ngano, Mtume (SAW) akawaamrisha masahaba wake
waikate vipande vidogo vidogo, kisha akamwomba MwenyeziMungu Subhanahu wa Taala
na akawataka masahaba waile mikate hiyo watu kumi kumi mpaka wote wakashiba na
idadi yao ilikuwa ni watu sabini au themanini.
Njaa kali sana ilimshika
Mtume (SA) pamoja na sahaba zake walipokuwa wakichimba handaki (Siku ya vita
vya Khandaq). Jabir (RA) mmoja wa sahaba zake akachinja kondoo mdogo kwa ajili
ya Mtume (SAW) na baadhi ya sahaba zake, lakini Mtume(SAW) akawakaribisha kula
chakula hicho wote walokuwa wakichimba handaki hilo na idadi yao ilikuwa
elfu moja (RA), na MwenyeziMungu
akaibariki nyama na mikate ile, wakala wote mpaka wakashiba.
Bukhari
Katika vita vya Khandaq
(handaki) na katika vita vya Tabuk,
Waislamu walikuwa na shida kubwa ya chakula, wakamtaka ruhusa Mtume (SAW)
wachinje ngamia.
Omar(RA) akatoa rai kwamba
watu wote wakusanye vyakula vyao mahali pamoja kisha wamwombe Mtume(SAW) ili
amwombe MwenyeziMungu awabarikie chakula hicho, Mtume(SAW) akakubali na
Mwenyezi Mungu akawabarikia chakula hicho hata
watu wote kambini humo waliweza kujaza vyombo vyao chakula.
Kisha akasema:-
"Nashuhudia kwamba
hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa MwenyeziMungu (Allah) na kwamba mimi ni
Mtume wa MwenyeziMungu."
3) KUSIKITIKA KWA SHINA LA MTENDE NA CHAKULA KUMSABIHI MWENYEZI MUNGU
Mtume(SAW) alipoacha
kuliegemea shina la mtende anapowahutubia Waislamu Hutuba ya Ijumaa baada ya
kutengenezwa membari, shina hilo la mtende alokuwa akiliegemea miaka mingi
lililia kwa masikitiko na kutoa sauti mfano wa ngamia anavyolia, hata
likakaribia kupasuka, na Mtume (SAW) akalikumbatia shina hilo mpaka likatulia.
Bukhar, Attirmidhy na
Annasai.
Imeelezwa na Maimam Al
Bukhary na Attirmidhy kuwa masahaba walikuwa wakisikia chakula kikimsabihi
MwenyeziMungu huku kikiingia kinywani mwa Mtume (SAW).
4) KULINDWA KWA MTUME (SAW) KUTOKANA NA MAADUI ZAKE
Abu Jahal aliapa kwamba ataipindapinda shingo ya Mtume(SAW) kwa
miguu yake atakapomwona anasali. Na alipomuona akisali, alimwendea ili
aitimize ahadi yake hiyo, lakini mara
akaonekana akirudi kinyume nyume huku akijikinga kwa mikono yake.
Akaulizwa;
"Vipi, una nini"?
Akajibu;
"Baina yangu na yeye,
pana shimo kubwa la moto na mnyama mkubwa wa kutisha mwenye mabawa".
Bibi mmoja wa kiyahudi pia
alifanya njama ya kutaka kumwua Mtume(SAW), akatia sumu katika nyama ya mbuzi
aliyomkaribisha Mtume wa MwenyeziMungu(SAW), Mtume akajuwa kuwa ina sumu,
akaitema, lakini sumu ile iliwasibu baadhi ya masahaba (walokula nyama hiyo).
5) KUJULISHA MAMBO YA GHAIBU
Mtume(SAW) aliwajulisha
sahaba zake yale yatakayotokea akiwepo duniani na baada ya kufa kwake hadi siku
ya kiama.
Sababu ya kusilimu kwa watu
wa Yemen ni kuwa Mtume(SAW) aliwajulisha Wafursi na Wayemen kwamba mfalme wa Wafursi
keshauliwa, na kwamba Mwenyezi Mungu amefanya hivyo ili kulipa kisasi cha Mtume
wake(SAW), na Mtume(SAW) akawatajia mpaka usiku aliouliwa Kisraa mfalme wa
Wafursi.
Na hii ndiyo sababu
iliyowafanya watu wa Yemen pamoja na Wafursi walokuwa wakiishi huko kuingia
katika dini ya MwenyeziMungu makundi kwa makundi.
UTABIRI JUU YA KUJA KWAKE (SAW) ULIOMO KATIKA VITABU VILIVYOTANGULIA
Hapana awezaye kudai kwamba
Muhammad(SAW) ndiye aliyewaandikia Mayahudi,
Manasara, Majusi,(walokuwa wakiabudu moto), na Mahindu katika vitabu vyao wanavyovitukuza, juu ya
wasfu wake, jina lake, wakati gani atakuja pamoja na nchi yake, hayo
yakishuhudia kuwa yeye ni Mtume aliyeletwa na MwenyeziMungu, maana yote hayo
yameandikwa katika vitabu vyao karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwake (SAW).
MwenyeziMungu anasema:
"Na haya (yaliyomo
ndani ya Qur-ani) yamo katika vitabu vya kale".
Ashuraa - 196
Kutabiriwa huko
kulisababisha vizazi baada ya vizazi vya Manasara na Majusi na Wahindu kumkubali kwamba yeye ni Mtume wa
kweli wa Mwenyezi Mungu.
Isipokuwa wale waliopania
kumfanyia uadui Mtume(SAW) wakabadilisha na kuongeza katika bishara hizo. Juu
ya hayo, katika vitabu hivyo, bado zingalimo bishara zinazoshuhudia ukweli wa
Utume wake Mohammad (SAW).
ZIFUATAZO NI BAADHI YA BISHARA HIZO:-
KATIKA TAURATI (TORAH)
Katika Taurati imeelezwa
kwamba Nabii atatokea Makka (Nyumba alokuwa akiishi Qaydara), mmoja wa wana wa
Ismail (AS), na Qaydara huyu aliishi
Makka kama inavyoelezea Taurati.
Na kwamba jina lake
litanyanyuliwa hapo, na kwamba anapanda ngamia na anapigana kwa panga na kwamba atashinda yeye na watu wake, na kwamba atabarikiwa kila siku (na hivi
ndivyo wafanyavyo Waislamu wanapotoa shahada (katika Sala zao), na kwamba
wafalme wa Yemen watakuja kwake wakiwa na wanyama wa sadaka, na kwamba alama ya utukufu wake yenye ukubwa
wa yai la njiwa ipo juu ya bega lake, (alama hii ilikuwepo begani mwa Mtume
(SAW)) .
Maelezo haya hayalingani na
mwengine yeyote isipokuwa Muhammad (SAW).
Vile vile imeandikwa katika
Taurat kwamba MwenyeziMungu amejitukuza juu ya
watu mahali patatu:-
1) SINAI:
Alipoteremshiwa Nabii Musa(AS) Taurati
2) SAIYR:
(Jabali katika Palestina) Alipoteremshiwa Nabii Issa (AS) Injili.
3) MAKKA: (Parani)
alipoteremshiwa Mtume Muhammad(SAW)
Qurani.
Taurati iliyo mikononi mwa
Mayahudi hadi hivi sasa inasema;
"Bwana alitoka Sinai,
akawaondokea kutoka Saiyr, aliangaza katika kilima cha Parani".
Parani ni jina la zamani la
mji wa Makka kama ilivyoelezwa katika Taurati.
Kumbukumbu la Taurati
21:22.
Wanavyuoni walikwisha eleza
kwamba hata Qurani imezungumzia hayo katika kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-
"Naapa kwa Tini na
Zaituni (miti hii inaota Palastina).
Na kwa mlima Sinai
(alipopewa kitabu Nabii Musa).
Na kwa mji huu wenye amani
(Makka alipopewa utume Nabii Muhammad (SAW)."
(Suratul - Tiyn -1-2-3)
KATIKA INJILI
Katika injili ya Barnaba
mlango wa 220 imeeleza hivi:
"Issa (AS) Aliwaambia
wafuasi wake:
"Haya yatabaki mpaka
atakapokuja Muhammad Mtume wa MwenyeziMungu ambaye atakapokuja atazikashifu
hizi hadaa kwa wale wanaoamini sheria za MwenyeziMungu )".
Na katika Yohana:16/7-14 -
Injili inasema kwamba Issa (AS) aliwaeleza watu wake juu ya Nabii atakayekuja
baada yake, aliposema:
"Hata hivyo bado
ningali ninayo mengi ya kuwaambieni, lakini hamwezi kustahamili hivi sasa,
lakini atakapokuja huyo roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote, kwa
maana hatonena kwa shauri lake mwenyewe, bali kila atakalosikia atanena na
atakuelezeeni juu ya yatakayokuja yote".
MwenyeziMungu amesema:-
"Na (wakumbushe)
aliposema (Nabii)Issa bin Maryam (kuwaambia Mayahudi) "Enyi wana wa
Israil)! Mimi ni Mtume wa MwenyeziMungu kwenu nisadikishaye yaliyokuja kabla
yangu katika Taurat na kutoa habari njema ya Mtume atakaekuja nyuma yangu
ambaye jina lake litakuwa Ahmad "(Muhammad na maana ya majina mawili hayo
ni moja, na maana yake ni mwenye kuhimidiwa kwa maneno yake mazuri), lakini
alipowajia kwa hoja zilizo wazi walisema: "Huu ni udanganyifu ulio
dhahiri."
Suratus Saff - 6
KATIKA VITABU VYA WAHINDU
Katika kitabu kiitwacho
(Alsa Mafida), kitabu kitakatifu cha Mahindus (Mabaniani), huko Bara Hindi,
katika Ibara ya sita na ya nane katika sehemu ya pili imeandikwa ifufatavyo:-
"Ahmad anapokea sheria
kutoka kwa Mola wake nayo imejaa hekima".
Na katika kitabu kiitwacho
(ADRUW AFIDAM) kitabu kingine kitakatifu kwa Wahindu imeandikwa:-
"Wakati huo
utakapofika ataletwa mgeni aitwaye Mahaamid[2] atakayejulikana kuwa ni
Mwalimu wa ulimwengu[3] na Mfalme, akitahirisha
kwa Tano zilizo tahiri[4]
"Enyi watu sikieni
mfikiri, ataletwa Muhammad juu ya migongo ya watu na utukufu wake utashukuriwa mpaka Peponi
naye ni mwenye Kuhimidiwa."
Na katika kitabu kiitwacho
(PHUSH PRANIM) ambacho pia ni miongoni
mwa vitabu vitakatifu kwa Kihindu imeandikwa;
Hii ni katika juzuu ya
pili sehemu ya tatu ibara ya tatu na
kuendelea[5]
KATIKA VITABU VYA WAMAJUSI
Imeandikwa katika kitabu
kiitwacho ‘ZINDA AFASTA’ kwamba Mungu atamleta Mtume na wasfu wake ni huu:
Rehma kwa walimwengu
Atapambana na adui aitwaye
Abu Lahab na atawalingania watu wamwabudu Mungu Mmoja.
Haya yanasadikisha kauli ya
MwenyeziMungu isemayo:
"Wale tuliowapa kitabu
wanamjua kama wanavyowajua watoto wao".
(Al - Baqarah -146).
Mayahudi na manasara ndio
Ahlul Kitab (Watu walioteremshiwa vitabu), lakini Mtume (SAW) ametuamrisha
tuwape heshima ya Ahlu Kitab Wahindu na Wamajusi (Zorosti), isipokuwa tusile
nyama walochinja wala tusiowe wanawake wao, na Mwenyezi Mungu anajuwa zaidi,
lakini huenda sababu yake ikawa ni kule kupitiwa na miaka mingi kwa vitabu vyao
pamoja na mikono mingi iliyobadilisha na kugeuza yaliyomo.
Ubashiri huu ndio
ulosababisha kusilimu kwa wingi kwa Mayahudi wa zamani, Manasara, Majusi na
Wahindu.
TABIA NA MWENENDO WAKE UNAOSHUHUDIA UKWELI WA UTUME WAKE(SAW)
Yeyote atakayechukuwa
jukumu la kuongoza watu, lazima atachunguzwa na watu ili wazijuwe Tabia na
Mwenendo wake, na hautopita muda mrefu, watu watajuwa. Hasa mtu huyo
atakapoingia katika mapambano baina ya udhaifu na nguvu, hofu na amani, ufakiri
na utajiri, kuwa na wafuasi wachache dhidi ya wafuasi wengi, shida na utulivu
kama ilivyomtokelea katika maisha yake Mtume (SAW) .
Tukiizingatia hali aloishi
nayo, tutaiona kuwa ni hali asiyoweza kuwa nayo mwengine isipokuwa Nabii.
Miongoni mwa Hali hizo ni:-
1) UKWELI
Watu wake walikuwa
wakimjuwa kuwa ni Msema kweli, na hata kabla hajapewa Unabii alikuwa
akijulikana kwa jina la; 'MSEMA KWELI, MWAMINIFU'.
Abu Jahal aliwahi
kumwambia;
"Sisi hatukukadhibishi
wewe isipokuwa tunayakadhibisha hayo ulokuja nayo".
Ndipo MwenyeziMungu
alipoteremsha kauli yake:-
"Basi wao
hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu hao wanakanusha hoja za
MwenyeziMungu".
(Al An- Am -33).
Alijulikana kuwa ni Msema
kweli katika kila jambo lake, hata anapofanya mzaha (SAW). Na hii ni tabia
isiyopatikana isipokuwa kwa Nabii aliyeletwa na MwenyeziMungu.
2) KUTIMIZA KWA UKAMILIFU YOTE ANAYOWALINGANIA WATU
Nafsi ya Mwanaadamu kwa
kawaida huchukizwa kutenda jambo kwa kulazimishwa, hasa mtu huyo anapokuwa
keshajimakinisha baina ya watu.
Tukiichunguza hali alokuwa
nayo Mtume(SAW), tutaona kuwa alikuwa mchaMungu kupita wote na mkamilifu wa
tabia njema kupita wote, na alikuwa akifanya ibada nyingi kupita wote.
Alikuwa akifunga sana hata
watu wake walimdhani hali chakula, na alikuwa akisali usiku mpaka miguu yake
ikivimba.
Bibi Aisha (RA) aliwahi
kumuuliza;
"Kwa nini unafanya
yote hayo na MwenyeziMungu
keshakughufiria madhambi yako yalotangulia na yanayokuja?"
Mtume(SAW) Akajibu;
"Basi nisiwe mja
mwenye kushukuru?"
Bukhari na Muslim
Alikuwa akitumia mali yake
yote katika njia ya Mwenyezi Mungu, hakuwa akibakisha chochote nyumbani kwake,
na alipokufa, ngao yake ilikuwa imewekwa rehani kwa Myahudi.
Kutokana na Utajo wa Mwenyezi Mungu(Dhikri) pamoja na Dua
zilizohifadhiwa kutoka kwake kunashuhudia kuwa alikuwa anamdhukuru Mola wake
kila wakati usiku na mchana na katika kila jambo analotenda.
Alifanya yote haya akiwa ni
Mtume wa MwenyeziMungu, Mlinganiaji wa watu katika dini ya Mwenyezi Mungu, Mkuu
wa majeshi ya Waislamu. Na pale vita vikipamba moto, Waislamu walikuwa
wakijikinga kwa kujificha nyuma yake(SAW). Alikuwa akipigiwa mfano katika
ushujaa na ujasiri, na haya yalionekana katika vita vya Hunayni alipopigana na
kuthibiti Yeye na Masahaba wake mia moja tu, dhidi ya washirikina elfu, na
MwenyeziMungu akawapa ushindi juu ya maadui.
Washirikina wa Makka
walimtaka achague iwapo anataka apewe Mali kiasi atakacho pamoja na Heshima na
Ufalme ili aiache dini yake au achaguwe vita na kutiwa adabu iwapo atashikilia
kutaka kuitangaza dini yake.
Akachaguwa kuufikisha
ujumbe alopewa na Mola wake.
Na pale dunia nzima
ilipokuwa chini ya amri yake, iliteremka kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-
"Ewe Mtume waambie
wake zako ikiwa mnapenda maisha ya (hii) dunia na uzuri wake (mimi sinayo na
siwezi kukulazimisheni kukaa na mimi (katika hali ya ufakiri); basi (mkipenda
nikuacheni), njooni nitakupeni kitoanyumba na kukuacheni mwacho mzuri."
(Al Ahzab -28).
Lakini (wake zake) wote
wakachagua kuishi na Mtume wa Mwenyezi Mungu(SAW), wakawa wachaMungu na
kuyaacha matamanio na mapambo yote katika maisha yao ya hapa duniani.
Alikuwa mfano wa hali ya
juu katika kuhukumu baina ya watu kwa uadilifu, akasema;
"Lau angeiba Fatima
binti Muhammad, basi Muhammad angemkata mkono wake".
Alikuwa mfano wa hali ya
juu katika kila jambo, ndio maana kila mmoja katika umma wake anajaribu kuigiza
mwenendo wa Mtume wa MwenyeziMungu (SAW) katika kila nyanja za maisha yake na
wala hapana anayeweza kuifikia daraja yake.
Bila shaka mkusanyiko
uliokamilika wa mfano wa hali ya juu kama huu katika kila nyanja ya maisha,
haupatikani isipokuwa kwa Mtume aliyeletwa na MwenyeziMungu, aliyeshuhudia Mola
wake kwa kauli Yake isemayo;
"Hakika wewe ni mwenye
tabia tukufu."
(Al Qalam 21)..
Na MwenyeziMungu
aliyetukuka akataka awe mfano mwema baina ya watu, aliposema:-
"Bila ya shaka mnao mfano
mwema (ruwaza nzuri) kwa Mtume wa MwenyeziMungu
kwa mwenye kumuogopa MwenyeziMungu na siku ya mwisho na kumtaja
MwenyeziMungu sana".
(Al Ahzab -21)
ALIVYOUSIMAMIA UJUMBE NA KUUFIKISHA KWA WATU
Mtume (SAW) ameifanya kazi
yake kwa ukamilifu na ameufikisha ujumbe kwa watu kama alivyotakiwa.
Wakati mwingine alikuwa
akiwaendea watu maalum au huwaalika watu chakula, na mara nyengine hujitolea
kuyaendea makabila mbali mbali huku akiwa na subira juu ya yale yanayomkuta, na
kabila moja baada ya moja humkatalia. Wakati mwingine huwaita watu ili akutane
nao au huwaendea pale walipo, na mara nyingine huwatuma walinganiaji katika
Sahaba zake (RA), na mara nyingine
hutuma wajumbe kwa wafalme na ma gavana, mara nyingine hupigana Jihadi dhidi ya
wale wanaowazuia watu kuilingania njia ya MwenyeziMungu.
Makafiri walipambana na
uenezi huu pamoja na waenezaji kwa kila namna ya ukatili, nguvu na udhia.
Maqureish wakati mwingine
walikuwa wakiwafanyia mzaha Mtume (SAW) na Sahaba zake (RA), kisha ghafla
wanawavamia baadhi ya Waislamu na kuwaunguza kwa moto, kuwauwa au
kuwaadhibisha. Waliwapiga pande Waislamu na kuwazunguka wakiwemo katika nyumba
za Abu Talib kwa muda wa miaka mitatu, hata iliwabidi Waislamu wale ngozi na
miti. Udhia ukazidi na Masahaba wa Mtume(SAW) ikawabidi wahame na
kukimbilia Uhabeshi (Ethiopia) mara
mbili, kisha wakahamia Madina.
Maqureish wakafanya njama
ili wamuuwe Mtume wa MwenyeziMungu(SAW), lakini MwenyeziMugu akamwamrisha ahame
ili aokoke na hila zao.
Alikuwa akiwaelezea watu
yote aliyotakiwa na MwenyeziMungu ayaeleze. Alitujulisha hata yale yaliyo na
makatazo kwake yeye binafsi kutoka kwa MwenyeziMungu:
Mfano wa kauli ya
MwenyeziMungu:
"Alikunja (Mtume )
paji na akageuza uso.
Kwa sababu alimjia kipofu.
Na nini kilichokujulisha
(ya kuwa huyo Sahaba pofu hahitaji mawaidha mapya?) Labda yeye atatakasika (kwa kusikia mawaidha
mapya).
Au atakumbuka
(aliyoyasahau). Ukumbusho huo upate kumfaa.
Ama ajionaye hana haja (ya
dini).
Wewe ndie
unayemshughulikia?
Na si juu yako kama
hakutakasika.
lakini anayekukimbilia.
Naye anaogopa.
Wewe unampuuza (Usifanye
hivyo)".
(Abasa -1-10).
Aliambiwa haya kwa sababu
Mtume(SAW) alipokuwa akiwalingania baadhi ya viongozi wa makafiri alijiwa na
kipofu Mwislamu aitwae Ibn Ummi Maktoum akimuuliza masuali, na Mtume (SAW) alichukizwa
kwa kuulizwa masuali wakati alipokuwa akijaribu kuwasilimisha wakubwa wa
makabila ambao wangelisilimu wao pamoja na wafuasi wao ingepatikana kheri kwa
Waislamu.
Mtume (SAW) hakumfanyia
lolote la zaidi kipofu huyo isipokuwa alikunja uso wake tu. Na Ibn Ummi Maktoum
kwa vile ni kipofu, hawezi kuuona uso wa Mtume (SAW) ulokunjwa na kwa hivyo
hakuudhika.
Lakini MwenyeziMungu
akamteremshia Mtume(SAW) makatazo, na akayafikisha makatazo hayo kama
yalivyoteremshwa.
Lengo la Mtume (SAW) katika
maisha yake yote lilikuwa ni kuyafikisha yale aliyoamrishwa na Mola wake bila
ya kujali ukubwa wa taabu au vikwazo atakavyopambana navyo.
Katika Hijja yake ya mwisho
(Hijjatul Wadaa) aliwauliza Waislamu;
"Je!
nimefikisha?"
Wakashuhudia kuwa amewafikishia
kikamilifu dini ya MwenyeziMungu;
Kisha akasema:-
"MwenyeziMungu
shuhudia".
Hakika ya hali yake
ilivyokuwa katika kila nyanja ya maisha yake inashuhudia kuwa sifa kama hizi
hawezi kuwa za mtu wa aina nyingine isipokuwa ni sifa za Mtume wa MwenyeziMungu
(SAW) na mjumbe Wake.
HALI ZA WAFUASI WAKE NA MAADUI ZAKE ZINAZOTHIBITISHA
UKWELI WA UJUMBE WAKE
Uhodari wa mwalimu
unaonekana katika wanafunzi wake, na ustadi wa mkufunzi unaonekana kwa wale
anaowapa mafunzo, na ukweli wa Mtume unadhihirika katika wafuasi wake, kwa
sababu wao ndio waloishi naye, akawalea, akawatakasa na kuwafunza.
Atakayezingatia hali za
Masahaba (RA) atauona ukweli wa wasfu alowapa Mwenyezi Mungu aliposema:-
"Nyinyi ndio umma bora
kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu".
(Al -Imran -110)
Mataifa yote ya ulimwengu
wakati ule yalishuhudia kwamba Waislamu walikuwa ni Umma bora ulodhihirishiwa
watu.
Hii ni kwa sababu ya
kawaida ijulikanayo kwamba nchi yoyote au umma wowote ukifanya vita na kuiteka
nchi nyingine basi kuteka huko kunasababisha chuki na wivu baina ya mataifa
hayo, na haya yanaonekana mpaka hivi sasa baina ya wakoloni na wanaowatawala.
Lakini kawaida hii
ilitoweka kwa wafunguzi wa Kiislamu waliokuwa mabwana wa ulimwengu wakati wao.
Ushindi wa Waislamu baada
ya kuziteka nchi hizo ulisababisha mapenzi, nusura, utiifu na mchanganyiko
baina ya Waislamu na wengine hata mataifa hayo yaliyoshindwa na Waislamu
yalikuwa yakimshukuru MwenyeziMungu kwa kuletewa wafunguzi hawa wa Kiislamu.
Ukiitafuta sababu utaona
kwamba mapambano yaliyopo baina ya watu ni kugombania matamanio ya dunia,
lakini Waislamu walijitolea kukataa matamanio ya dunia kwa ajili ya
kuwafurahisha watu huko Peponi, na hii ni kwa sababu waliiamini Akhera kama
ilivyopaswa kuaminiwa na kwa sababu imani na mwenendo wao huo yalikuwa ni
matunda ya usadikisho kamili wa ushahidi alokuja nao Mtume wa MwenyeziMungu
(SAW) juu ya ukweli wa ujumbe wake na kwa matendo yake yaliyoeneza imani katika
maisha yake (SAW).
MAADUI ZAKE
Baada ya kumfanyia inda
muda mrefu sana, maadui zake wakageuka kuwa ni walinzi wake wakubwa kabisa na
wengi miongoni mwa Ahlul Kitab wa mwanzo nao pia wakasilimu.
Yalipatikana yote haya
baada ya kumsadiki Mtume wa MwenyeziMungu (SAW) na kumwamini.
KUFAA KWA SHERIA (ZA KIISALMU ) ZAMA ZOTE NA MAHALI POPOTE
Utungaji wa sheria na
nidhamu yoyote ile unategemea elimu kamili juu ya yule anayetungiwa sheria hiyo
na mazingara yanayoambatana naye.
Mwanadamu hauelewi uhakika
wa roho yake na yale atakayokumbana nayo siku za usoni, na hii ndiyo sababu ya
kushindwa kwake kutunga sheria na kanuni zilizo thabiti atakazoweza kuzitumia
wakati wowote na zama zozote.
Lakini muumbaji Subhanahu
wa Taala ndiye mwenye kujua uhakika wa kuumbwa kwa mwanadamu.
MwenyeziMungu amesema:-
"Oh! asijue aliyeumba!
naye ndiye avijuaye visivyojulikana na vinavyojulikana".
(Suratul -Mulk -14)
Na Yeye ndiye
aliyekizunguka kila kitu kwa kukijuwa, anayajuwa yaliyopita na yatakayokuja, na
hii ndiyo sababu mwanadamu hawezi kuja na sheria iliyo thabiti, lainifu na
inayoweza kunasibiana na kila zama na kila mahali, isipokuwa mtu huyo awe
amepewa sheria hiyo na Mola wake Subhanahu wa Taala.
Waislamu waliitawala
Mashariki ya ardhi na Magharibi yake kwa karne nyingi, na sheria ya Kiislamu
ilifaa kuhukumu karne zote hizo katika
mazingara na sehemu mbali mbali.
Sheria ya Kiislamu imeweza
kubaki hadi wakati wetu huu juu ya udhaifu wa Waislamu, na Umoja wa Mataifa
umekubali kuitumia sheria hii kuwa ni moja katika misingi ya kutunga sheria zao
ulimwenguni wakati kanuni za Kirusi na za Kimarekani hazitambuliwi kama ni
msingi wa kanuni za Ulimwengu.
Na wataalamu mbali mbali wa
kanuni ulimwenguni (wasiokuwa Waislamu) wamekubali kuwa sheria ya Kiislamu
inafaa kwa kila zama.
Dr Ezekio Ensaba Tohin -
Mmoja wa wataalamu wa kanuni ulimwenguni amesema;
"Dini ya kiislamu
inakubaliana na kila kinachowalazimikia watu, kwa hivyo inaweza kustawi na
kujiendeleza na kutumika bila ya kudhoofika kupitia karne na karne huku
ikijihifadhi kwa nguvu zake zote za maisha pamoja na ulaini wake. Dini hii
imeupa ulimwengu sheria iliyo thabiti kuliko zote. Sheria yake ni bora sana
kuliko sheria zinazotumika katika nchi za Ulaya."
Mkutano wa ulimwengu wa
sheria uliofanyika huko Lahai mwaka 1932, ndio ulioutaka Umoja wa Mataifa
uikubali sheria ya Kiislamu kutumika kama ni msingi katika misingi ya kutunga
kanuni za ulimwengu baada ya kukiri kwa wataalmu wa kanuni ulimwenguni juu ya utukufu wa sheria hiyo na
kwa ajili ya faida kwa watu katika wakati huu.
Ama mkutano wa kimataifa juu ya
ulinganishi wa kanuni uliofanyika huko Paris mwaka 1952, ulilitaka baraza la
ulimwengu la kutunga sheria uruhusu kufanyika mkutano wa kimataifa juu
"Fiq-hi ya Kiislamu" kila mwaka badala ya kila miaka kumi, na sababu
waliyotoa ni kuwa wanataka kujifunza zaidi na kupata faida nyingi kutokana na
kuidurusu sheria ya Kiislamu, na wakasema katika mkutano wao huo:
"Kutokana na
yaliyothibiti kwa walioshiriki katika mkutano juu ya faida iliyopatikana katika utafiti uliofanywa
katika "Wiki ya Fiq hi ya Kiislamu", na kutokana na yaliozungumzwa
katika utafiti huu pamoja majadiliano, imetuthibitikia kwamba Fiq hi ya
Kiislamu imesimama katika misingi ilio na kima kikubwa kabisa, na haya ni yenye
uhakika usio na shaka yoyote juu ya manufaa yake, na kwamba misingi ya hitilafu
iliyopo katika sheria hii kuu inatokana na utajiri (hazina) wa rai mbali mbali
za fani ya sheria (fiq-hi) ambayo huipa sheria hii uwezo wa kunasibiana na hali
zote za maisha ya kisasa kwa ulainifu wake mkubwa.
Kwa hivyo wajumbe wa
mkutano wanatoa mapendekezo yao kuwa; " Wiki ya Fiq-hi ya Kiislamu
iendeleze kazi yake kila mwaka."
Basi atawezaje mtu asiyejua
kusoma wala kuandika, aliyekuja miaka elfu moja mia nne iliyopita, aje na
sheria kama hii, iwapo mtu huyu si Mtume aliyeletwa na Mola wake?
Utashangazwa kuwaona
wajinga miongoni mwa Waislamu wanaotaka sheria hii ya MwenyeziMungu ifutwe na
kubadilishwa na sheria za wanadamu.
KUITAKASA IBADA
KWANZA: NINI IBADA ?
Ibada ni jina lililokusanya
kila anachokipenda MwenyeziMungu na kuridhika nacho na akakiamrisha.
Kwa hivyo kila
alichotuamrisha MwenyeziMungu kukitenda ni ibada, na kila alichotukataza
kujiepusha nacho ni ibada. Ama matendo ya kawaida yaliyoruhusiwa na sheria kama
vile kula, kunywa na kuvaa huwa ni ibada yakikusudiwa kufuata amri ya
MwenyeziMungu na kusaidia katika kumtii MwenyeziMungu.
Ibada haisihi isipokuwa iwe
halisi kwa ajili ya MwenyeziMungu, ikubaliane na sheria yake na ikusanye baina
ya utiifu mkubwa na unyenyekevu kwa MwenyeziMungu pamoja na ukamilifu wa
kumpenda.
MwenyeziMungu katika
kuwasifia walioamini, anasema:-
"Lakini walioamini
wanampenda MwenyeziMungu zaidi sana".
(Al - Baqaraha -165)
Kwa ajili ya Ibada ndiyo
Mwenyezi Mungu ameumba viumbe na kuwapelekea Mitume.
MwenyeziMungu
amemdhalilishia mwanadamu vyote vilivyo mbinguni na ardhini ili naye avitumilie
hivyo katika kumtii Yeye Subahanahu wa Taala.
MwenyeziMungu anasema:
"Jee! Hamuoni ya
kwamba MwenyeziMungu amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na
akakukamilishieni neema zake zilizo dhahiri na za siri".
(Luqman -20).
Na anasema:-
"Sikuwaumba majini na
watu ila wapate kuniabudu."
(Adh -Dhariat -56)
Na akasema:-
"Na bila ya shaka
tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba mwabuduni MwenyeziMungu na mwepukeni
mwovu (Iblisi au kila kinachoabudiwa kisichokuwa MwenyeziMungu). "Basi
wako miongoni mwao ambao MwenyeziMungu amewaongoa, na wako miongoni mwao ambao
upotofu umethubutu juu yao".
(An - Nahli -36)
Yafuatayo ni Masharti
Mawili Ya Msingi Na Haikubaliwi Ibada Yoyote Bila Ya Kuyatimiza Masharti Hayo:-
KUITAKASA KWA AJILI YA MWENYEZIMUNGU
Na
maana yake ni kuwa; Ibada yoyote isikusudiwe kwa ajili ya mwengine asiyekuwa
Allah, na kusudi lake liwe kwa ajili ya kutaka radhi za MwenyeziMungu Subhanahu
wa Taala.
MwenyeziMungu
anasema:-
"Wala hawakuamrishwa
ila kumuabudu MwenyeziMungu kwa kumtakasia dini, wawache dini za upotofu na
wasimamishe Sala na kutoa Zaka, hiyo ndiyo dini liliyo sawa."
(Al - Bayinah -5)
KUMFUATA MTUME (SAW)
Nako ni kutomuabudu
MwenyeziMungu isipokuwa kwa njia aliyotufundisha Mtume wake(SAW).
MwenyeziMungu anasema:-
"Sema", Ikiwa
nyinyi mnampenda MwenyeziMungu basi nifuateni (hapo) MwenyeziMungu atakupendeni
na atakughufirieni madhambi yenu."
(Aali - Imran -31)
Na anasema:-
"Oh! Wana washirika
(wa MwenyeziMungu) waliowawekea dini asiyoitolea MwenyeziMungu ruhusa
(yake)?"
(Ash - Shuraa -21)
Kwa hivyo anayesali
Magharibi raka nne kwa mfano, basi sala yake inabatilika na anayesali raka tatu
inakuwa sawa. Hii ni kwa sababu njia ya pili ndiyo aliyotufundisha Mtume(SAW),
ama ya kwanza ni kinyume na mafundisho
ya Mtume (SAW).
Na Mtume (SAW) amesema:-
"Atakayeongeza jipya
katika amri yetu hii jambo ambalo halimo, basi halitakubaliwa."
Bukhari na Muslim
PILI: AINA ZA IBADA
Ibada sahihi inapatikana
pale unapopatikana unyenyekevu kamili tena halisi ndani na nje yake mwanadamu,
itikadi iwe moyoni na kwa kutamka na kwa vitendo. Vyote hivyo vikiwa kwa ajili
ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.
IBADA ZIKO AINA NYINGI; MIONGONI MWAKE:
IBADA ZA ITIKADI
1)
Kuamini Kuwa Hapana Mola Anayepaswa Kuabudiwa
Isipokuwa Allah Na Kwamba Muhammad Ni Mtume Wa Allah:-
Haya
hupatikana kwa njia ya elimu sahihi
inayoondowa kila aina ya shaka.
MwenyeziMungu
anasema:-
"Juwa ya kwamba hakuna
aabudiwaye kwa haki ila MwenyeziMungu na
omba maghufira kwa dhambi zako."
(Muhammad - 19)
Na anasema:-
"Je! Anayejua kwamba
yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki (akayafuata basi) ni kama
kipofu? Wenye akili ndio wanaozingatia".
(Raad -19).
2)
Kumpenda MwenyeziMungu Aliyetukuka:
MwenyeziMungu
anasema:
"Lakini
walioamini wanampenda MwenyeziMungu zaidi sana”.
(Al
-Baqraha - 165)
Nayo ni mapenzi
yaliyofungamana na udhalilifu na unyenyekevu pamoja na kusalimu amri, mapenzi
ambayo hayapatikani isipokuwa kwa kufuata alokuja nayo Mtume (SAW).
MwenyeziMungu
anasema:-
"Sema; 'Ikiwa nyinyi
mnampenda MwenyeziMungu basi nifuateni, hapo MwenyeziMungu atakupendeni."
(Al - Imran 31)
Katika ukamilifu wa
kumpenda MwenyeziMungu ni kumpenda Mtume wake (SAW) na kuipenda dini ya
Kiislamu.
Ama kuwapenda watoto na
jamaa sio ibada kwao maana hulazimiki kuwa mnyenyekevu na kusalimu amri kwao.
Na juu ya hayo kwa Muislamu mapenzi hayo hayawi makubwa kuliko mapenzi yake juu
ya MwenyeziMungu na Mtume wake (SAW). Na iwapo mapenzi ya MwenyeziMungu na
Mtume wake yatapambana na mapenzi mengine basi pendo lisilokuwa la
MwenyeziMungu litatoweka katika moyo wa Muislamu.
MwenyeziMungu mtukufu
anasema;
"Sema kama baba zenu
na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na
biashara mnazoogopa kuharibikiwa na majumba mnayoyapenda (ikiwa vitu hivi) ni
vipenzi zaidi kwenu kuliko MwenyeziMungu na Mtume wake na kupigania dini yake,
basi ngojeni MwenyeziMungu alete amri yake na MwenyeziMungu hawaongozi watu
waasi(njia iliyonyoka)."
(At - Tawba - 24)
3)
Kumuogopa MwenyeziMungu Pamoja Na Kuwa Na Tamaa
Katika Rehma Yake:
MwenyeziMungu anasema:-
"Jee! afanyae ibada
nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa akhera na kutarajia rehema
ya Mola wake (ni sawa na asiyefanya hayo) sema; "Jee! wanaweza kuwa sawa
wale wanaojua na wale wasiojua?"
Az - Zumar -9
MwenyeziMungu akatoa wasfu
wa wasioamini aliposema:-
"Na ambao wanaiogopa
adhabu itokayo kwa Mola wao hakika adhabu ya Mola si ya kusalimika nayo mtu
(mbaya)."
Al - Maarij - 27-28
Huenda mtu akawa na hofu
juu ya baadhi ya mambo ya kidunia, lakini hofu hii sio ibada juu ya yale
anayoyaogopa, maana hofu hiyo ni ya kimaumbile ambayo mwenye kuamini anaamini
kuwa MwenyeziMungu ndiye aliyemkadiria, na hofu hiyo haifikii daraja ile ya
kumuogopa Mola wake, maana anaamini ya kuwa MwenyeziMungu anaweza kumuepusha na
kila ovu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kama MwenyeziMungu
akikugusisha madhara (taabu) basi hakuna yeyote awezaye kuyaondoa ila Yeye; na
kama akikugusisha kheri (hakuna awezaye kuiondoa ila Yeye tu peke Yake ) Yeye ndiye mwenye uwezo wa juu ya
kila kitu"
Al - Anam -17
4)
Kurejea Kwa MwenyeziMungu:
Nako ni kukimbilia kufanya
yanayomridhisha MwenyeziMungu na kurudi kwake na kuomba maghufira na kutubia.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na rejeeni kwa Mola
wenu na mnyenyekeeni kwake kabla ya kukujieni adhabu kisha hamtanusurika. Na
fuateni yaliyo bora katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu kabla ya kukujieni adhabu kwa
ghafla na hali hamtambui."
Az Zummar -54-55
Katika kuelezea wasfu wa
Waislamu, MwenyeziMungu pia anasema:-
"Na ambao wanapofanya
uchafu (kufanya dhambi kubwa) au kudhulumu nafsi zao (kwa kufanya dhambi ndogo)
hukumbuka MwenyeziMungu na kuomba msamaha kwa dhambi zao. Na nani anayeghufiria
dhambi isipokuwa MwenyeziMungu? Na hawaendelei na (maovu) waliyoyafanya hali
wanajua (kuwa hayo ni maovu)".
Aali - Imran –135
5)
Kumtegemea MwenyeziMungu Na Kumuomba Msaada:
Uhakika wa kutegemea: Ni
ukweli wa moyo unaomtegemea MwenyeziMungu katika kutafuta yenye manufaa na
kujiepusha na madhara katika mambo ya kidunia na ya akhera.
MwenyeziMungu amekadiria na
akauwekea ulimwengu nidhamu kwa kukadiria kila kitu, akauwekea mwenendo maalum
na akaziwekea sababu zake, ili tumuabudu
kwa kuzifuata hizo sababu.
Miongoni mwa sababu kubwa
kabisa ni kumtegemea MwenyeziMungu:
MwenyeziMungu anasema:
"Na anayemtegemea
MwenyeziMungu, yeye humtoshea. Kwa yakini MwenyeziMungu anatimiza kusudi lake
(lolote alitakalo; hakuna wa kumpinga). Hakika MwenyeziMungu amekwisha kiwekea
kila kitu kipimo chake ".
At Talaq -3
Na anasema:-
"Ikiwa nynyi
mumemuamini MwenyeziMungu, basi mtegemeeni yeye kama nyinyi ni Waislamu
kweli."
Yunus - 84
Na anasema:-
"Na Waislamu
wamtegemee MwenyeziMungu tu".
At Taghabun -13
MwenyeziMungu
akawafaradhishia waja wake katika kila Sala waseme:
"Wewe tu ndie tunayekuabudu na Wewe tu ndie tunayekuomba msaada".
"Wewe tu ndie tunayekuabudu na Wewe tu ndie tunayekuomba msaada".
Fatiha -5)
Na Mtume (SAW) akasema:
<< Ukitaka kuomba
msaada muombe MwenyeziMungu >>.
(Sehemu ya hadithi sahihi
iliyotolewa na Ahmad na Al Tirmidhy ilopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas)
IBADA ZA MATAMSHI
1) Kuzitamka Shahada Mbili
Hauwi
sahihi Uislamu wa mtu iwapo hajazitamka shahada
mbili, isipokuwa bubu ambaye vinatosheleza vitendo vyake vitakavyoonyesha
dalili ya imani yake.
Mtume (SAW)amesema:
<<Nimeamrishwa
nipigane vita mpaka watu washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa
isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa MwenyeziMungu na wasimamishe
Sala na Watoe Zaka. Watakapotimiza hayo watakuwa wamezuilika kwangu damu zao na
mali zao ila kwa haki ya Uislamu [6]na hesabu yao itakuwa kwa MwenyeziMungu>>.
(Bukhari na Muslim).
1) Kumdhukuru(kumtaja)
MwenyeziMungu, Kumsabihi(kumtukuza) na Kumwomba Maghufira
MwenyeziMungu anasema:
"Enyi mlioamini!
Mkumbukeni MwenyeziMungu kwa wingi na mtukuzeni asubuhi na jioni".
(Al - Ahzab -41 -42)
Na akasema:-
"Na ili muombe msamaha
kwa Mola wenu, kisha mtubie(mrejee) kwake.
Atakustarehesheni kwa starehe nzuri mpaka mda maalum (mtapoondoka
ulimwenguni). Na atampa (akhera) kila
mwenye fadhila, fadhila yake, na kama mtakengeuka basi nakukhofieni adhabu ya (hiyo) siku kubwa."
(Hud-3)
Na akasema:
"Basi (hapo) mtakase
Mola wako pamoja na kumsifu na umuombe maghfira (msamaha) ; hakika Yeye ndiye
Apokeaye toba ".
(Nasr -3)
3) Dua
Na Kuomba Msaada
Atakayeomba dua, au msaada,
hatokuwa mwenye akili (iwapo atamwomba asiyemsikia) isipokuwa huyo anayemuomba awe
ni mwenye kumsikia na kuwasikia wengine kila wakati, kila mahali na kwa kila
lugha.
Hatokuwa mwenye akili
isipokuwa awe na yakini kwamba yule anayemuomba anao uwezo kwa njia za ghaibu
wa kulijibu ombi lake na kumfariji dhiki zake, na awe na uwezo wa kimiujiza
unaoweza kufanya jambo lolote katika ulimwengu huu.
Mwenye uwezo huu
hawezi kuwa mwingine
isipokuwa MwenyeziMungu. Hawezi kuyafanya haya kiumbe chake chochote, aliye hai au
aliyekwisha kufa.
Mwenye kuamini kwamba
asiyekuwa MwenyeziMungu anao uwezo wa kufanya lolote katika hayo, kisha
akamulekezea dua yake, basi atakuwa amefanya
kiendo cha Shirki.
MwenyeziMungu anasema:-
"Huyo ndiye
MwenyeziMungu, Mola wenu, Mwenye ufalme, na wale mnaowaabudu kinyume chake, wao
hawamiliki hata utando (ngozi) wa kokwa ya tende, kama mkiwaomba hawatakujibuni
na siku ya kiyama watakataa ushirika wenu wala hatakuambia kama (akuambiavyo
MwenyeziMungu) Mjuzi wa kweli kweli".
(Fatir - 13 - 14)
Na anasema:-
"Na Mola wenu akasema
"Niombeni nitakujibuni”. Kwa hakika wale wajivunao kufanya ibada yangu
bila shaka wataingia Jahannam, wadhalilike".
(Al - Muumin - Ghafir- 60).
Na akasema:-
"Na waja wangu
watakapokuuliza hakika yangu Mimi niko karibu nao. Naitikia maombi ya muombaji
anaponiomba. Basi waniitikie na waniamini ili wapate kuongoka".
Al - Baqarah - 186
Iwapo mjinga yeyote
ataelekeza dua yake kwa mwengine asiyekuwa MwenyeziMungu, basi ni wajibu wa
anayeelewa kumbainishia, na anapaswa huyo asiyeelewa kufuata na kuiokoa nafsi
yake isiingie katika Shirki.
4) Kuapa Kwa Jina La
MwenyeziMungu
Mwislamu hali kiapo isipokuwa kwa jina la
MwenyeziMungu, kwa sababu ya kumtukuza na kumheshimu.
Mtume wa MwenyeziMungu
(SAW) amesema:
<<Atakae kula kiapo,
ale kiapo kwa jina la MwenyeziMungu au anyamaze.>>
Bukhari, Muslim, Ahmad na
Annasai
Atakaekula kiapo kwa
asiyekuwa MwenyeziMungu, akamtukuza kama anavyotukuzwa MwenyeziMungu na
akamwogopa kama anavyomuogopa MweyeziMungu basi atakuwa amefanya kitendo cha
Shirki.
Mtume (SAW) amesema:-
<<Atakaekula kiapo
kwa asiyekuwa MwenyeziMungu anakuwa keshafanya (kitendo cha) Shirk>>.
Attirmdhiy, Ibn Majah,
Ahmad, Annasai, na Addarimy
Pia haijuzu mtu kuapa kwa
'Amana'.
Mtume (SAW) amesema:
<<Atakayeapa kwa
Amana hayupo pamoja nasi>>.
Ahmad na Abu Daud.
5) Kulingania
Watu Katika Njia Ya MwenyeziMungu, Kuamrisha Mema Na Kukataza Mabaya
MwenyeziMungu anasema:-
"Ni
nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye viumbe (viumbe) kwa MwenyeziMungu
na (mwenyewe) akafanya vitendo vizuri na kusema: "Hakika mimi ni miongoni
mwa Waislamu".
Haa -
Miym - Sajdah (Fussilat -33 )
Na
anasema:-
"Sema":
Hii ndio njia yangu; ninaita (ninalingania) kwa MwenyeziMungu kwa ujuzi wa
kweli; mimi (nafanya hivi) na (kila) wanaonifuata. Na MwenyeziMungu ametakasika
na kila upungufu, wala mimi simo miongoni mwa wanaomshirikisha
(MwenyeziMungu)".
(Yusuf
- 108).
Na
anasema;
"Na
wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na
wakakataza maovu na hao ndio watakaotengenekewa".
(Aal -
Imran -104)
IBADA ZA VITENDO
1) Kusimamisha
Sala
MwenyeziMungu
anasema:
"Wala hawakuamrishwa ila kumwabudu
MwenyeziMungu kwa kumtakasia dini, wawache dini za upotofu (upotevu) na
wasimamishe Sala na kutoa Zaka, hiyo ndio dini iliyo sawa .
(Suratul - Bayyinah - 5)
Na anasema katika kuelezea
wasfu wa walioamini:
"Watu ambao biashara
wala kuuza hakuwashughulishi (hakuwasahaulishi) kumkumbuka MwenyeziMungu na
kusimamisha Sala na kutoa Zaka, wanaiogopa siku ambayo nyoyo zitadahadari na
macho pia",
(An - Nur -37).
Na anasema:
"Wale ambao tukiwamakinisha
(tukiwaweka uzuri) katika ardhi, husimamisha Sala na wakatoa Zaka na
Wakaamrisha yalio mema na Wakakataza yalio mabaya. Na marejeo ya mambo ni kwa
MwenyeziMungu".
(Al - Hajj - 41).
Na anasema:-
"Na waamrishe watu
wako kusali na uendelee mwenyewe kwa hayo. Hatukuombi riziki bali Sisi ndio
tunaokuruzuku na mwisho mwema utawathubutukia wamchao Mungu."
(Taha - 132)
2) Kutoa Zaka
MwenyeziMungu anasema:-
"Wala hawakuamrishwa
ila kumuabudu MwenyeziMungu kwa kumtakasia dini, wawache dini za upotofu(upotevu)
wasimamishe Sala na watoe Zaka hiyo ndiyo dini iliyo sawa .
(Suratul - Bayyinah -5).
Na anasema:-
"Na simamisha Sala na
toeni Zaka na kheri mtakazozitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtazikuta kwa
MwenyeziMungu ………"
(Al Baqarah - 110)
Na anasema:-
"Lakini wale waliozama
barabara katika elimu miongoni mwao (hawa waliopewa kitabu) na Waislamu (ambao
wote hao) wanaamini yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla yako, na
(wale) wanaodumisha Sala na kutoa Zaka na wanaomwamini MwenyeziMungu na (wanaamini) Siku ya mwisho. Hao tutawapa
malipo makubwa ".
(An - Nisaa -162)
2) Kufunga
mwezi wa Ramadhani
MwenyeziMungu anasema:-
"Enyi mlioamini
mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuja kabla yenu ili
mpate kumcha Mungu".
(Al - Baqarah -183).
Na anasema:-
"(Mwezi huu mlioambiwa
mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao
imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu na hoja
zilizo wazi wa uwongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batil) atakae kuwa katika
mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge."
(Al - Baqarah - 185)
Na Mtume (SAW) amesema:-
<<Atakae funga
Ramadhan kwa Imani na kwa (nia ya) kutaka Ridhaa za Mwenyezi Mungu, anasamehewa
madhambi yake yaliotangulia >>.
Bukhari, Muslim, Abu Daud,
Attirmdhyna, Ibni Majah,na Ahmad
4) Kuhiji Makka (Kaaba)
Kwa Mwenye Uwezo
MwenyeziMungu anasema:-
"Na MwenyeziMungu
amewawajibishia watu wafanye Hijja katika nyumba hiyo; yule awezaye kufunga
safari kwenda huko na atakae kanusha (asende na hali ya kuwa anaweza ) basi
MwenyeziMungu si mhitaji kuwahitajia walimwengu "
Aal - Imran -97).
Na anasema :-
"Na (tukamwambia)
"Utangaze kwa watu habari za Hijja watakujia (wengine) kwa miguu na
wengine juu ya kila mnyama aliyekonda (kwa machofu ya njiani) wakija kutoka njia
ya mbali".
(Al - Hajj - 27).
Na Mtume (SAW) akasema :-
<<Uislamu umejengeka
juu ya nguzo tano; kubaini kwa moyo na kutamka kwa ulimi kuwa hapana Mola
apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah, na Muhammad ni Mtume wa MwenyeziMungu,
Kusimamisha Sala. Kutoa Zaka, Kuhiji Makka na Kufunga mwezi wa
Ramadhani>>.
Bukhari na Muslim
2)
Kuhukumu Kwa Sheria Iliyoteremshwa na MwenyeziMungu
Hana haki mtu yeyote ya kuwawekea wanadamu
sheria, isipokuwa yule Aliyewaumba - Subhanahu wa Taala.
MwenyeziMungu anasema:-
"Fahamuni kuumba (ni
kwake tu MwenyeziMungu) na amri zote ni zake (MwenyeziMungu) ametukuka kabisa
MwenyeziMungu Mola wa walimwengu wote".
(Al -Aaraf 54).
Kwa hivyo mwenye kujipa
yeye mwenyewe, au kumpa mtu mwengine haki ya kuwatungia wanadamu sheria na
nidhamu ambazo MwenyeziMungu hajazitolea amri yake, atakuwa ametenda kitendo
cha shirki na atakuwa amewalingania watu wamwabudu asiyekuwa MwenyeziMungu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Oh! Wana washirika wa
(MwenyeziMungu) waliowawekea dini asiyoitolea MwenyeziMungu ruhusa (yake)?"
(Ashuraa - 21)
Na anasema:-
"Haikuwa hukumu ila
hii ya MwenyeziMungu tu; ameamrisha msimuabudu yeyote yule isipokuwa Yeye
tu".
Yussuf -40
Kwa hivyo Mwislamu anatakiwa asalimu amri
mbele ya sheria ya MwenyeziMungu na aitii sheria hiyo kwa nafsi
iliyoridhika.
MwenyeziMungu anasema:-
"Naapa kwa haki ya
Mola wako, wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye (wewe ndie)
hakimu (mwamuzi) katika yale wanayokhitilafiania kisha wasione uzito nyoyoni
mwa juu ya hukumu uliyoitoa, na wanyenyekee kabisa."
(AN - Nisaa -65)
3)
Kuipigania Dini Ya MwenyeziMungu
"Enyi mlioamini! Jee!
nikujulisheni juu ya biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?
(Basi biashara yenyewe ni
hii): Muamini MwenyeziMungu na Mtume wake piganieni dini ya MwenyeziMungu kwa
hali zenu na nafsi zenu, haya ni bora kwenu ikiwa mnajua (kuwa ni bora basi
fanyeni)".
(As - Saff -10 11)
Na anasema:
"Jee! Mnadhani mtaingia Peponi hali
MwenyeziMungu hajapambanua wale waliopigania dini ya MwenyeziMungu miongoni
mwenu, na kuwapambanua wale walofanya subira?”
(Aal - Imran - 142)
4)
Kuweka Nadhiri Kwa Ajili Ya MwenyeziMungu.
MwenyeziMungu anasema:
"Wanaotimiza wajibu
(wao) (Nadhiri walizoziweka) na wanaoigopa siku ambayo shari yake itaenea
(sana)".
(Ad - Dahr -7)
Na Mtume (SAW) amesema:-
<<Aliyeweka nadhiri
ya kumtii MwenyeziMungu, basi amtii, ama
aliyeweka nadhiri ya kumuasi MwenyeziMungu) basi asimuasi>>.
(Bukhari, Ahmad, Attirmdhy
na wengine na imepokewa kutoka kwa Bibi Aisha (RA).
5)
Kutufu Nyumba Tukufu Ya MwenyeziMungu:
MwenyeziMungu anasema:-
"Na tulimuusia Ibrahim
na Ismail (tukawaambia): "Itakaseni (isafisheni) nyumba yangu kwa ajili ya
wale wanaozunguka kwa ajili ya kutufu na
wanaokaa hapo na (kwa ajili ya) wanaorukuu na kusujudu hapo pia".
(Al - Baqarah - 125)
Na anasema:-
"Na waizunguke nyumba
ya kale (Nyumba kongwe Al-Kaaba)”.
(Al - Hajj -29)
6)
Kuchinja Kwa Ajili Ya MwenyeziMungu
MwenyeziMungu anasema:-
"Sema hakika Sala
zangu na Ibada zangu (zote nyengine) na uzima wangu na kufa kwangu (zote) ni
kwa MwenyeziMungu. Mwumba wa walimwengu wote. (Likinisibu jambo limenisibu kwa
kutaka MwenyeziMungu. Si kwa kutaka viumbe vyake, na yote ninayofanya nafanya
kwa ajili yake) Hana mshirika wake, na haya ndiyo niliyoamrishwa na mimi ni wa
kwanza wa waliojisalimisha (kwa MwenyeziMungu)”.
(Al - Anam -162-163)
Na kuchinja ni miongoni mwa
ibada maana MwenyeziMungu anasema:-
"Basi Sali kwa ajili
ya Mola wako na Uchinje (kwa ajili ya Mola wako).
(Na kila utakalolifanya
lifanye kwa ajili ya Mola wako siyo mizimu wala mapango wala makaburi )."
(Suratul - Kawthar - 2)
Ameeleza Imam Ali ibn Abi
Talib(RA), kwamba Mtume (SAW) amesema:-
<<MwenyeziMungu
amemlani (kila) anayechinja kwa (ajili ya mwengine) asiyekuwa
MwenyeziMungu)>>.
(Muslim, Ahmad, Annasai)
KWANZA - UKWELI WA AZMA YA KUTAKA KUFANYA IBADA
Mwenye kutaka kumuabudu
Mola wake anahitaji azma ya kweli, yenye kuweza kuushinda uvivu na kuishinda
tabia ya kupuuza, ili azma hiyo imwezeshe kufanya juhudi katika kumtii
MwenyeziMungu na ili kauli yake isadikishe vitendo vyake (afanye vitendo na sio
kusema tu).
MwenyeziMungu anasema:-
"Enyi mlioamini! Mbona
(kwa nini) mnasema msiyoyatenda?"
(As - Saff-2)
Kwa anayetaka msaada kwa
ajili ya kuiongeza nguvu azma yake basi inampasa kufuatana na watu wanaopenda
kukaa katika vikao vya kheri.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na siku hiyo dhalimu
atajiuma mikono yake (vidole) na huku akisema: "Laiti ningelishika njia
(ya haki) pamoja na Mtume! " "Eee ole wangu , (adhabu yangu) Laiti
nisingelimfanya fulani kuwa rafiki. Amenipoteza nikaacha mawaidha baada ya
kunijia. Na kweli shetani anamtupa mwanaadamu".
Surat Al Furqan - 27-29
PILI - KUAMINI KUWEPO KWA MALAIKA
Kuamini kuwepo kwa Malaika ni nguzo katika nguzo
za Imani, na hii inatokana na kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-
"Mtume ameamini
yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na Waislamu, (pia wameamini hayo):
Wote wamemuamini MwenyeziMungu na Malaika wake".
(Al - Baqarah - 285)
Na anasema:-
"Na Malaika
wanamtukuza Mola wao na kumshukuru na kuwaombea msamaha walio katika
ardhi".
(Ash -Shuraa -5)
Na anasema:-
"Wale walioko kwa Mola
wako (nao ni Malaika) hawajivuni (wakaacha) kumuabudu (Mola wao kwa kuwa ni
wakubwa la; bali) na wanamtukuza na kumsujudia".
(Al - Aaraf - 206)
Na anasema:-
"Anayemfanyia ushinde
MwenyeziMungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibrili na Mikail (anatafuta
kuangamia) kwani MwenyeziMungu atakuwa mshinde wa makafiri hao".
(Al -Baqarah - 98)
Ushahidi upo mwingi katika
Qurani na katika Mafundisho ya Mtume(SAW) juu ya kuwajibika kuwaamini
(Malaika), na kwamba MwenyeziMungu amewaumba kwa Nuru.
Na Imani juu ya kuwepo Malaika: Ni kukiri na
kutokuwa na shaka yoyote juu ya kuwepo kwao, na kwamba wao ni viumbe na watumwa
wa MwenyeziMungu, wanaamrishwa na wamekirimiwa.
MwenyeziMungu anasema:-
"Hawamtangulii kwa
neno (Lake analosema) Nao wanafanya kwa amri Zake (zote)".
(Al - Tahriym - 6)
Na anasema :-
"Na walioko kwake (Malaika)
hawatakabari na kumuabudu wala hawachoki (hawapumziki) Wanamtukuza usiku na
mchana hawanyong'onyei (hawafanyi
uvivu)."
(Al - Anbiyaa - 19- 20)
MwenyeziMungu amewagawa
Malaika makundi mbali mbali:
Miongoni mwao wamo wenye
kazi ya kuwapelekea Wahyi Mitume naye ni
Mhuyisha sheria Mwaminifu Jibrili (AS), yupo mwenye kutoa roho, naye ni (Malak
al Maut) Malaika wa kifo na wasaidizi wake, yupo aliyepewa kazi ya kupiga
baragumu (Siku ya Kiama), naye ni Israfiyl na aliyepewa kazi ya kuleta mvua
Mikail, na wapo Malaika wanaosimamia amali za viumbe nao ni Malaika wanaoandika
mema na maovu tutendayo, na wamo waliopewa kazi ya kumlinda kiumbe mbele na
nyuma yake, nao ni Walinzi.
MwenyeziMungu anasema:-
"Ana (kila mtu) kundi (la Malaika) mbele yake
na nyuma yake; wanamlinda kwa amri ya MwenyeziMungu".
(Ar - Raad -11)
Wamo pia walinzi wa Pepo na
neema zake, nao ni Radhwan na wenzake, na wamo waliopewa kazi ya motoni
(Jahannam) na adhabu zake, nao ni Malik
na wenzake, na miongoni mwa Malaika wa motoni wapo pamoja na viongozi wao kumi
na tisa.
Wamo pia wenye kazi ya
adhabu za kaburini nao ni Munkar na Nakir na wamo wabebaji Arshi, na wamo wenye
kazi ya kushughulikia manii katika matumbo ya uzazi, kuanzia kuingia kwake (Manii hiyo) hadi
kufikia wakati wa kuandikiwa kheri na shari ya kizazi kipya.
Katika hao wamo wanaoingia
katika Nyumba inayozuriwa daima, (Baitul Maamur), wanaingia humo kila siku
Malaika elfu sabiini kisha hawarudi tena mahali hapo, na wamo Malaika
wanaotembea na kufuatilia vikao vya wenye kumtaja (Kumdhukuru) Mola wao, na
wamo waliopangwa wakiwa wamesimama wala hawainami na wengine wanaorukuu na
kusujudu na wala hawainuki na wamo wanaofaya mengi yasiyotajwa humu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Wala hapana yoyote
ajuaye majeshi ya Mola wake ila Yeye tu; na wala haikuwa ila ukumbusho wa
viumbe."
( Al -Mudathir - 31)
Ushahidi juu ya ugawaji huu
(wa kazi za Malaika) ni mwingi, na umeelezewa katika Qurani na Sunnah, na ni
maarufu miongoni mwa Maulamaa.
TATU – KUVIAMINI VITABU VILIVYOTANGULIA
Imani juu ya vitabu maana
yake ni kuamini bila ya kuwa na shaka yoyote kwamba vitabu vyote (Taurat,
Injili, Zaburi na Qurani) vimeteremshwa kutoka kwa MwenyeziMungu na kwamba
MwenyeziMungu amevitaja kwa uhakika.
Mwenyezi Mungu anasema:-
"Enyi mliamini
muaminini MwenyeziMungu na Mtume wake na kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume
wake na vitabu alivoteremsha zamani. Na mwenye kumkanusha MwenyeziMungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake
na Siku ya mwisho basi bila ya shaka amepotea (upotevu) ulio mbali(na haki)".
(AN - Nisaa -136)
Miongoni mwa vitabu hivyo (asili yake)
vilitokana na maneno ya MwenyeziMungu
kwa Mitume yake moja kwa moja bila kupitia kwa mwakilishi (Jibril AS),
na mengine ni kupitia kwa Malaika (Jibrili AS) na yapo aliyoyaandika
MwenyeziMungu mwenyewe "Subhanahu wa taala."
MwenyeziMu;ngu anasema:-
"Na haikuwa kwa mtu
kwamba MwenyeziMungu anasema naye ila kwa ilhamu (anayotiwa moyoni mwake) au
kwa nyuma ya pazia la (kumsikilizisha sauti inayotokana na MwenyeziMungu pasi
na kumwona) au humtuma mjumbe (Jibril) naye hufunulia (humletea wahyi ) kiasi
anachotaka kwa idhini yake.”
(Ashu - araa -51).
Na akamwambia Musa(AS)
“Akasema(MwenyeziMungu)
"Ewe Musa! mimi nimekuchagua juu ya watu wote kwa ujumbe wangu na kwa
kusema nawe kwangu. Basi pokea haya niliyokupa na uwe miongoni mwa
wanaoshukuru."
(Al -Aarar-144)
Na anasema pia:-
"Na MwenyeziMungu
akamsemeza Musa.”
(An - Nisaa -164)
Ama kuhusu Taurat
MwenyeziMungu anasema:-
"Na tukamuandikia
katika mbao kila kitu mauidha (ya kila namna) na maelezo ya kila jambo".
(Al - Aaraf -145)
Na akasema juu ya Issa (AS)
"Na tukampa
Injili".
(Al - Hadiyd - 27)
Na akasema:-
"Na Daud tukampa
Zaburi".
(An - Nisaa -163)
Na juu ya Qurani akasema;
"Lakini MwenyeziMungu
anayashuhudia aliyokuteremshia (kuwa ni haki) ameyateremsha kwa ilimu yake na
Malaika pia wanashuhudia. Na MwenyeziMungu anatosha kuwa shahidi".
(An - Nisaa -166)
Na pia akasema:
"Na Qurani imegawanywa
sehemu mbali mbali (kwa kuiteremsha kidogo kidogo) ili uwasomee watu kwa kituo;
na tumeiteremsha kidogo kidogo (ili iwe nyepesi kuhifadhika)".
BANI ISRAIL (Israa -106)
Na akasema:
"Na bila ya shaka hii
Qurani ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameteremsha haya Mhuyisha
sheria mwaminifu (Jibrli(AS)) juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji
kwa lugha ya kiarabu wazi wazi (fasihi)."
(Ash - Shuraa - 192 -195)
Na MwenyeziMungu pia
akasema:-
"Haitaifikia batili
mbele yake wala nyuma yake; kimeteremshwa na mwenye hekima ahimidiwaye".
HAA MYM SAJDAH (Fusilat -
42).
Vitabu alivyovitaja
MwenyeziMungu katika Qurani ni:
Qurani, Taurat, Injili,
Zaburi na vitabu (sahifa) za Nabii Ibrahim na Musa (AS).
MwenyeziMungu anasema:-
"MwenyeziMungu hakuna
aabudiwaye kwa haki isipokuwa Yeye - Mwenye uhai wa milele na Mwendeshaji wa
mambo yote Amekuteremshia kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla
yake na aliteremsha Taurat na Injili".
(Aal - Imrani -2 - 3)
Na akasema:
"Na Daud tukampa
Zaburi ".
(An - Nisaa -36- 37)
Na pia akasema:-
"Au hakuambiwa
yaliyomo katika vitabu vya Musa? Na vya Ibrahim aliyetimiza ahadi (ya
MwenyeziMungu )".
(An - Najim -36 - 37)
Akavitaja vyengine kwa
pamoja akasema:-
"Kwa hakika
tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili wazi wazi na tukaviteremsha vitabu na uadilifu
pamoja nao ili watu wasimamishe uadilifu".
(Al - Hadiyd -25)
QURANI TUKUFU
DARAJA YAKE KATIKA VITABU VILIVYOTANGULIA
MwenyeziMungu anasema:-
"Na tumekuteremshia
kitabu kwa ajili ya kubainisha haki kinachosadikisha vitabu vilivyokuwa kabla
yake na kuvihukumia(Wa Muhayminan) kama haya ndiyo yaliyoharibiwa au ndiyo
yaliyosalimika".
(Al - Maidah -48).
Na akasema:-
"Na haiwezekani kuwa
hii Qurani imetungwa haitoki kwa MwenyeziMungu (kama mnavyodai). Bali imetokana
na MwenyeziMungu inayasadikisha yaliyo mbele yake na ni maelezo ya vitabu
(vilivyopita) Haina shaka kuwa imetokana kwa Mola wa walimwengu (wote)".
Yunus - 37)
Neno "Wa
muhaiyminan" na maana yake ni "Kuvihukumia", na maana yake ni
kuwa Qurani imepewa jukumu la kutoa hukmu juu ya vitabu vilivyokuja kabla yake.
Na neno “Kuvisadikisha”, maana yake ni kusadikisha yaliyomo, yale ya kweli na
kukanusha yaliyoongezwa, yaliyobadilishwa au kugeuzwa pamoja na kuyaamulia
kufutwa na pia kuyathibitisha yaliyo
sahihi.
Haya ndiyo anayotakiwa
kufuata kila anayeshikamana na vitabu vilivyotangulia, yule ambaye hataki
kurudi nyuma akawa kafiri.
Kama alivyosema
MwenyeziMungu:-
"Wale tuliowapa kitabu
kabla ya hii (Qurani) baadhi yao wanaiamini hii (Qurani) na wanaposomewa
husema; ‘tunaiamini bila ya shaka hii ni haki itokayo kwa Mola wetu; kwa yakini
kabla ya haya tulikuwa wenye kujisalimisha (kwa MwenyeziMungu).”
(Al - Qasas -52)
UMMA WOTE UNAWAJIBIKA KUKIFUATA
Watu wote wanawajibika
kukifuata kitabu hiki kwa dhahiri na kwa siri na kushikamana nacho na
kukisimamia kama ipasavyo.
MwenyeziMungu anasema:-
“Na hii (Qurani) ni kitabu
tulichokiteremsha (kwenu) kilicho na baraka nyingi basi kifuateni na muwe wacha
Mungu ili Mrehemiwe".
(Al - An - Am - 155)
Na akasema:-
"Fuateni mliyoteremshiwa
kutoka kwa Mola wenu wala msifuate (hao mnaowaitakidi) kuwa walinzi badala
yake".
(Al - Aaraf -3)
Na pia akasema:-
"Na wale wanaokishika
kitabu (cha MwenyeziMungu kweli kweli) na wakasimamisha Sala (tutawalipa mema)
Hakika sisi hatupotezi malipo ya wafanyao mema.”
(Al - Aaraf -170)
Aya zinazoelezea haya ni
nyingi, na Mtume (SAW) ameusia juu ya kushikamana na kitabu cha MwenyeziMungu
akasema:-
<<Kikamateni kitabu
cha MwenyeziMungu na mshikamane nacho>>.
Na katika hadithi
iliyoelezwa na Sayiduna Ali(RA) aliyoinyanyua kwa Mtume(SAW), alisema kuwa
Mtume (SAW) alisema:-
“Zitakuwa fitina nyingi”.
Nikasema:
“Tufanye nini ili tuepukane
nazo ewe Mtume wa MwenyeziMungu?”
Akasema:
“Kitabu cha MwenyeziMungu”.
(Imetolewa na Attirmidhy).
KUSHIKAMANA NACHO NA KUKISIMAMIA KAMA KINAVYOSTAHIKI
Uislamu umeshurutisha
wafuasi wake kukihifadhi, kukisoma na kukisimamia vilivyo kitabu hiki (Qurani
tukufu) usiku na mchana. Kuzizingatia aya zake, kuhalalisha yale
yaliyohalalisha kitabu hiki, kuharamisha yaliyoharamisha pamoja na kuzifuata amri zake, kujiepusha na
makatazo yake, kujifunza kutokana na mifano yake, kuwaidhika na visa vyake,
kuzifuata vilivyo aya zake zile zilizo wazi maana yake na kusalimu amri juu ya
zile zinazotatanisha maana yake (kwa kujiepusha na kuzifasiri kwa matamanio
yetu), kutoivuka mipaka yake, kukilinda kutokana na wabadilishaji na waongezaji
(wazidishaji mambo yasiyokuwemo ndani yake) walaghai waongo, na kunasihi
kutokana nacho kama ipasavyo na kuilingania kwa ujuzi wa kweli.
WAADI WA MWENYEZIMUNGU WA KUIHIFADHI(Qurani).
MwenyeziMungu
amekwishadhamini kuihifadhi Qurani isifikiwe na mikono ya uongezaji na
upunguzaji na ubadilishaji.
MwenyeziMungu anasema:-
"Hakika sisi ndio
tulioteremsha mauidha haya (Qurani); na hakika sisi ndio tutakayoyalinda".
(Hijr- 9)
MwenyeziMungu ametaka iwe
hivyo ili kuidumisha hoja yake kwa watu na kuifanikisha mpaka hapo
atakapoirithi ardhi pamoja vilivyo juu yake (siku ya Kama).
Na hoja hiyo haitoweza kudumu isipokuwa kwa
kuendelea kuwepo kwa Qurani hii baina ya watu, huku ikiwa imehifadhika mpaka
siku ya Kiama na ili iwe marejeo yao katika mambo ya Itikadi zao za Dini,
Misingi yake, Chimbuko lake, Lengo lake na ili tuweze kuzijuwa Sheria za
MwenyeziMungu na kubainika kwa wajibu wa yale yanayobainisha(Qurani) na
maharamisho yanayokataza na ili kuzijuwa fadhila za kibinadamu pamoja na
ukamilifu wa tabia inayofundisha kitabu hiki na kuyaamrisha katika hayo pamoja
na kufaidika kutokana na yaliyomo ndani yake katika mongozo ya sheria na kwa
kila lililo muhimu katika maisha ya wanadamu.
Tunatakiwa pia kuyasoma mawaidha yake (Qurani),
nasaha zake, mifano yake, na mafudisho yake pamoja na yote yaliyomo yenye
bishara njema, maonyo, makemeo na njia zote za mafunzo ya malezi ya kila namna
inayotuongoza kuelekea njia iliyonyooka.
USHAHIDI WA KUHIFADHIKA KWAKE.
Inampasa kila mwenye akili
timamu aamini na awe na uhakika kuwa Qurani anayoisoma leo, ndiyo ile ile
aliyoteremshiwa Muhammad(SAW), na iwapo mtu atachukua aya yoyote ile katika aya
za Qurani akaenda nayo London, Paris, Moscow, Washington, Peking au Tel aviv na
akatembea nayo katika miji ya Afrika, Australia kisha akenda Makka au Madina au
akachukua msahafu kutoka kila mji miongoni mwa miji hiyo na akafungua sura
ambazo aya hizo zimetolewa, atagundua kwamba Qurani zote ni moja, na kwamba aya
alizozitoa ndani yake ni moja, bali atagundua kwamba kila kilicho ndani ya
msahafu wowote ule ni maneno yale yale, hayakugeuzwa wala kubadilika.
MwenyeziMungu amesadikisha
aliposema:-
"Hakika sisi ndio
tulioteremsha mawaidha haya (hii Qurani) na hakika sisi ndio
tutakayoyalinda".
(Al - Hijri 9)
SUNNAH, INAYOIBAINISHA QURANI NA KUIHIFADHI
MwenyeziMungu anasema:-
"Na tumekuteremshieni
mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na ili wapate
kufikiri."
(An - Nahl-44)
Mtume(SAW) amekibainisha
kitabu cha Mola wake kwa watu kwa kauli zake, matendo yake na kukubali kwake.
MwenyeziMungu ameuhifadhi
ubainisho huu wa kinabii katika yale yalioandikwa na watu ndani ya vitabu vya
Sunnah za Mtume (SAW), na MwenyeziMungu amezihifadhi Sunnah hizo kwa kuwajaalia
wengi wa viumbe vyake kuzihifadhi hadithi za Mtume(SAW) kwa moyo wakiziwekea
vikao vya elimu ili kumuelimisha kila asiyezijua, hata wakapatikana miongoni
mwa umma wa Muhammad(SAW) wanaohifadhi kwa moyo maelfu ya hadithi pamoja na
milolongo ya majina ya wapokezi wa hadithi hizo pamoja na daraja zake, mfano wa Al Bukhari, Muslim na wale Maimamu
sita, ambao kila mmoja wao ameandika kitabu cha hadithi za Mtume (SAW) na
wengineo.
Hii ni kwa sababu hadithi
za Mtume (SAW) zinabainisha mafundisho yaliyomo katika Qurani, na ni sehemu ya
dini inayomfundisha Muislamu kwa ukamilifu mwenendo wake wa kila siku katika
Sala zake, Funga zake, Hija yake, kuuza na kununua kwake, kuoa na kuacha kwake,
pamoja na uhusiano wake na ukoo wake na jirani zake n.k. Na pia Sunnah ya
Mtume(SAW) inamfundisha Mwislamu yale yanayompasa mbele ya Mola wake na mbele
ya Umma wake na yote hayo yameandikwa na kudhibitiwa na kuhifadhiwa.
MWENYEZIMUNGU AMEUCHAGUA UMMA ULIO BORA KUKIHIFADHI KITABU CHAKE NA SUNNA ZA MTUME WAKE (SAW).
Kwa vile Mtume wa Mwenyezi
Mungu(SAW) ni Mtume wa mwisho, kwa hivyo MwenyeziMungu amechukuwa dhamana ya
kuihifadhi dini aliyokuja nayo kutokana na kubadilishwa, kuongezwa au
kupunguzwa mpaka siku ya Kiama.
MwenyeziMungu akawaandaa
kwa kazi hiyo Masahaba wa Mtume(SAW) na akasema juu yao:
"Nyinyi ndio Umma bora
kuliko Umma zote zilizodhihirishiwa watu".
Aal - Imran -110).
Na akasema juu yao:-
"Na vivyo hivyo
tumekufanyeni Umati bora, ili muwe mashahidi juu ya watu na Mtume awe shahidi
juu yenu".
(Al - Baqarah -143).
Na Mtume (SAW) amewaelezea Masahaba wake (kwa
kuwapa sifa ya) kuwa ni:
‘Karne iliyo bora kupita zote’.
Kwa vile sababu kubwa ya kuongeza, kupunguza au
kubadilisha ni kufuata matamanio ya nafsi, MwenyeziMungu aliwaandaa masahaba wa
Mtume (SAW) mwandao mahsusi ili waisimamie dini na kuihifadhi kwa ajili ya
walimwengu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na jueni ya kwamba Mtume wa MwenyeziMungu
yuko pamoja na nyinyi (basi msikilizeni anavyokwambieni) Lau yeye angekutiini
katika mambo mengi (mnayoyasema) bila shaka mngetaabika lakini MwenyeziMungu
ameupendezesha kwenu Uislamu na ameupamba nyoyoni mwenu na amekufanyieni
muuchukie ukafiri na ufasiki na uasi".
(Al - Hujurat -7)
Kwa uandalizi huu
walistahiki kusifiwa na MwenyeziMungu kwa sifa zifuatazo;
MwenyeziMungu anasema:-
"(Basi) wapewe (mali
hayo ) mafakiri wakimuhajiri ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao
(wakahiari kuacha hayo) kwa ajili ya (kutafuta) fadhila za MwenyeziMungu na
radhi (yake) na kuinusuru (dini ya) MwenyeziMungu na Mtume wake. Basi hao ndio
Waislamu wa kweli. Na (pia wapewe) wale waliofanya maskani yao hapa (Madina )
na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya (kuja) hao (Muhajiri huko
Madina) na wakawapenda hao waliohamia kwao wala hawapati (hawaoni) dhiki
nyoyoni mwao (Muhajiri) na wanawapendelea kuliko nafsi zao, hao ndio wenye
kufaulu kweli kweli.
(Al - Hashr -8 - 9)
MwenyeziMungu anasema:-
"Na walioamini
wakahama (kuja Madina na wakaipigania dini ya MwenyeziMungu (nao ni Muhajiri).
Na wale waliowapa Muhajiri mahali pa kukaa na wakainusuru (dini ya
MwenyeziMungu na Mtume wake) (Nao ni Ansari) Hao ndio Waislamu wa kweli.
Watapata msamaha (wa MwenyeziMungu) na kuruzukiwa kuzuri (kabisa huko
akhera)".
(Al - Anfal -74).
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kama wakitaka
kukuhadaa basi MweyeziMungu atakutosheleza, Yeye ndiye aliyekusaidia kwa nusura
yake na kwa waliokuamini".
(Al - Anfal -62).
MwenyeziMungu anasema:-
Muhammad ni Mtume wa
MwenyeziMungu, na walio pamoja nae ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na
wenye kuhurumiana wao kwa wao, utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu
(pamoja) wakitafuta fadhila za MwenyeziMungu na radhi (yake). Alama zao zi
katika nyuso zao kwa taathira (athari) ya kusujudu".
(Al - Fath -79)
"Kwa hakika
MwenyeziMungu amewapa radhi Waislamu walipofungamana nawe chini ya mti; na
Alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao na akawapa
kushinda kwa zama za karibu".
(Al - Fath -18).
SIFA ZA MASAHABA ZILIZOWAFANYA WATEULIWE KUWA NI MAIMAMU (VIONGOZI) WA DINI NA DUNIA.
Aya zilizotajwa kabla
zimeelezea kwamba Masahaba (RA) wanasifika na sifa zifuatazo:
Umma ulio bora kuliko umma
zote zilizodhihirishiwa watu.
Umati bora uliochaguliwa kuwa mashahidi juu ya watu.
MwenyeziMungu
aliupendezesha kwao Uislamu, akaupamba nyoyoni mwao na akawafanya wauchukie
ukafiri na ufasiki na uasi.
Wao ni wasema kweli
waliofaulu na walioamini kikweli.
Wenye nyoyo thabiti kwa makafiri, wenye kuhurumiana
wao kwa wao.
Wanaorukuu na kusujudu
ambao MwenyeziMungu alitizama yaliyo ndani ya nyoyo zao na akawa radhi nao.
Kwa ajili ya yote hayo,
wakastahiki kufanywa na MwenyeziMungu kuwa Makhalifa katika ardhi na
kuwatimizia yale aliyowaahidi na hayo yalipatikana wakati wa utawala wa
Makhalifa walioongoka – Al Khulafaa Al Rashidiyn(RA)[7].
MwenyeziMungu anasema:-
"MwenyeziMungu
amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, kuwa
atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwako
kabla yao. Na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea na atawabadilishia
amani baada ya hofu yao, wawe wananiabudu, hawanishirikishi na chochote. Na
watakaokufuru baada ya hayo basi hao ndio wavunjao amri zetu".
(Annur -55)
Kama walivyostahiki kuwa
Maimamu – Viongozi - katika mambo ya kidunia na kwa kupitia mikononi mwao kuweza
kuisimamisha dini aliyoridhika nayo MwenyeziMungu, basi walistahiki pia kuwa
Maimamu wa dini, ili MwenyeziMungu awe radhi nao pamoja na watakaowafuata kwa
wema.
MwenyeziMungu anasema:
"Na wale waliotangulia
wakawa wa kwanza katika (Waislamu), Muhajiri na Ansari na wale waliofuata kwa
mwenendo mzuri “MwenyeziMungu atawapa radhi nao wamridhie MwenyeziMungu kwa
hayo atakayowapa”, na amewaandalia mabustani yapitayo mito mbele yake wakae
humo milele, huku ndiko kufuzu kukubwa."
(At-Tawba -100)
Huu ndio Umma ambao kwao MwenyeziMungu
ameihifadhi dini, akaridhika nao na Umma zote na mataifa mbali mbali pia
yakaridhika nao, wakawafuata na kuwapenda juu yahitilafu ya utaifa, rangi na
lugha zao.
Nne - KUIAMINI MITUME (Alayhimu Salaam)
Kuamini Mitume ni nguzo katika
nguzo za Akida (Itikadi ya dini) kwa ajili hiyo inamwajibikia kila mtu kuiamini
Mitume ya MwenyeziMungu yote bila ya kutofautisha baina yao.
MwenyeziMungu anasema:-
"Semeni nyinyi
(Waislamu): "Tumemwamini MwenyeziMungu na yale tuliyoteremshiwa na yale
yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is haqa na Yakubu na kizazi (chake
Yakubu) na waliyopewa Musa na Issa na pia yale waliyopewa Manabii
(wengine)kutoka kwa Mola wao; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao (wote
tunawaamini) Na sisi tumenyenyekea kwake."
(Al - Baqarah - 136).
MwenyeziMungu akabainisha
pia kuwa hii ndiyo imani ya Waislamu, akasema:-
"Mtume ameamini
yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na pia Waislamu (pia wameamini hao)
Wote wamemwamini MwenyeziMungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume yake
(Na husema Waislamu na Mtume wao husema); Hatutofautishi baina ya yeyote katika
Mitume yake (wote tunawaamini)." Na husema "Tumesikia na tumetii
(tunakuomba) msamaha Mola wetu! Na marejeo ni kwako."
(Al - Baqarah - 285)
MwenyeziMungu akatujulisha pia kuwa wema umo
katika imani hii, akasema:-
"Sio wema (tu huo peke
yake) kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi (katika
kusali. Yako na mema mengine.) Bali wema (hasa) ni (wa wale) wanaomwamini
MwenyeziMungu na siku ya mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii …."
(Al - Baqarah -177)
Kwa hivyo mtu anapoamini
baadhi ya Mitume na asiwaamini wengine na akawabagua katika kuwaamini basi
anakuwa kafiri.
MwenyeziMungu amesema:-
"Hakika wale
wanaomkanusha MwenyeziMungu na mitume yake na wanataka kutenga baina ya
MwenyeziMungu na Mitume yake kwa kusema; "Wengine tunawaamini na wengine
tunawakataa" na wanataka kushika njia iliyo kati kati ya haya (si ya
kiislamu khasa wala ya kikafiri) Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia
adhabu idhalilishayo. Na waliomwamini MwenyeziMungu na Mitume yake wala
wasimfarikishe yeyote katika wao, hao atawapa ujira wao na MwenyeziMungu ni
mwingi wa kurehemu."
(An - Nisaa -150- 152)
HEKIMA YA KULETWA MITUME.
1) MWENYEZIMUNGU AMELETA
MITUME ILI WAWAJULISHE WATU JUU YA MOLA WAO NA MUUMMBA WAO, NA PIA ILI
KUWALINGANIA WATU WAMWABUDU MWENYEZIMUNGU MMOJA TU, NA KUIKANUSHA MIUNGU YA
UWONGO
MwenyeziMungu anasema:-
"Bila shaka
tumempeleka Mtume katika kila umma (awaambie) ya kwamba "Mwabuduni
MwenyeziMungu na muepukeni (Iblis) muovu".
(An - Nahl -36)
Na akasema:-
"Na kawaulize Mitume
wetu tuliowaleta kabla yako; “Jee! Tulifanya miungu mengine iabudiwe badala ya
Mwingi wa rehema?"
(Az - Zukhruf 45)
Na akasema:-
"Na hatukumtuma kabla
yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna aabudiwae ila mimi basi
niabuduni".
(Al - Anbiyaa -25)
2) MWENYEZI MUNGU AMEWALETA
MITUME ILI KUISIMAMISHA DINI, KUIHIFADHI, KUKATAZA MFARAKANO, NA ILI IHUKUMIWE
KWA HUKMU ALIYOITEREMSHA MWENYEZI MUNGU;
MwenyeziMungu anasema:-
"Amekupeni Sharia ya
dini ile ile aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe na tuliowausia Ibrahim na
Musa na Isa, kwamba simamisha dini wala msifarikiane kwayo”.
(Ash - Shuraa -14).
Na akasema:-
"Hakika tumekuteremshia kitabu(hiki) hali ya kuwa kimeshikamana na haki ili upate kuhukumu
baina ya watu kama alivyokufahamisha MwenyeziMungu wala usiwe mwenye kuwatetea
wafanyao hiyana."
(An - Nisaa -105).
3) AMEWATUMA KWA AJILI YA
KUWAPA HABARI NJEMA WAISLAMU JUU YA YALE ALIYOWAANDALIA KATIKA NEEMA ZA MILELE,
JAZAA YA UTIIFU WAO, NA ILI KUWAONYA MAKAFIRI JUU YA ADHABU WATAKAYOPATA ILI
IWE JAZAA YA KUKANUSHA KWAO, NA ILI KUONDOA UDHURU KWA WATU NA KUWASIMAMISHIA HOJA KUTOKA KWA MOLA
WAO
MwenyeziMungu anasema:-
"(Hao ni) Mitume
waliotoa habari nzuri kwa (watu wema), wakawaonya (wabaya) ili watu wasiwe na
hoja juu ya MwenyeziMungu baada ya (kuletwa hawa) Mitume. Na MwenyeziMungu ni
Mwenye nguvu na Mwenye hikma."
(An - Nisaa -165)
4) AMEWATUMA ILI WAWAFUNDISHE
WATU NA KUWA MFANO MWEMA KATIKA MWENENDO WAO, IKHLAQI NJEMA, KUWAFUNDISHA
KUMWABUDU MOLA WAO KWA NJIA ZILIZO SAHIHI NA ILI KUWAONGOZA KATIKA NJIA YA
MWEYEZIMUNGU ILIYONYOKA.
MwenyeziMungu anasema juu
ya Mtume wetu(SAW):-
"Bila ya shaka mnao
mfano mwema(Ruwaza nzuri) kwa Mtume wa MwenyeziMungu kwa mwenye kumuogopa
MwenyeziMungu na Siku ya mwisho, na kumtaja MwenyeziMungu sana".
(Al - Ahzab -21).
5) MWENYEZIMUNGU AMEWALETA ILI
KUWAOKOA WATU WASIKHITILAFIANE KATIKA MAMBO MUHIMU YA MAISHA YAO NA KUWAONGOZA
KATIKA HAKI AITAKAYO MUUMBA WAO.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na hatukukuteremshia
kitabu (hiki) ispokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana, na pia (kiwe)
uongozi wa rehma kwa watu wanaoamini."
(An - Naha 64)
6) AMEWALETA ILI WABAINISHE
AMALI NJEMA ZINAZOITAKASA NAFSI YA BINAADAMU NA KUITAHIRISHA NA KUPANDA NDANI
YAKE MBEGU ZA KHERI.
MwenyeziMungu anasema:-
"Yeye ndie aliyeleta
Mtume katika watu wasiojua kusoma, anayetokana na wao awasomee Aya zake na kuwatakasa na kuwafunza Kitabu (Qurani) na
Hikima (ilimu nyenginezo). Na kabla ya haya walikuwa katika upotofu (upotevu)
ulio dhahiri".
(Al - Jumua -2)
SIFA ZA MITUME (AS)
Kila Mtume Lazima awe mkamilifu wa sifa za
kimaumbile, awe na tabia njema za hali ya juu kabisa, awe na akili timamu na awe
msema kweli, awe mwaminifu katika kuyafikisha aliyokalifishwa kuyafikisha,
aepukane na kila sifa mbaya, awe na ukamilifu wa kiwiliwili (asiwe na kilema),
na awe na nguvu ya kiroho ili isiwezakane kwa nafsi ya mwanadamu au jinni
kuitawala mtawalo wa kiroho, na hii ni kwa sababu MwenyeziMungu anamnyoshea
msaada kutoka kwake.
Lazima kila Mtume awe na
sifa hizi kwa sababu sifa zao zikiwa duni kuliko za wengine walioishi wakati
wao, au akili zao zikiwa na udhaifu fulani au kuwa na udhaifu wa kiroho hata
waweze kutawaliwa na nguvu za kiroho za watu wengine, au udhaifu wa nafsi,
udhaifu wa azma hata washindwe kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu, makatazo
Yake, pamoja na kushindwa kutii kikamilifu au kushindwa kuyafikisha kikamilifu
yale waliyokalifishwa kuyafikisha kwa sababu ya hofu, tamaa, kusahau au kwa
sababu nyengine zozote zisizokuwa hizo.
Wangelikuwa na upungufu wa
lolote miongoni mwa hayo, wasingefaa kwa kazi ya MwenyeziMungu makhsusi kama
hii ya kuchaguliwa kuwa Watume na kupokea Wahyi pamoja na kuonyeshwa siri za
elimu ya MwenyeziMungu walizofunuliwa.
Wasingefaa kuchaguliwa na
Mwenyezi Mungu kwa kazi hii pia ingelikuwa miili yao ina vilema vinavyoweza
kuwafanya watu wajiepushe nao, na kwa njia hiyo makafiri wangepata hoja za
kuwatia ila katika ulinganio wao.
Ama kinyume na hayo Mitume ni wanadamu kama
wanadamu wengine, huwasibu yote yanayowasibu wanadamu wenzao na hufanya kama
wanavyofanya, wanakula na kunywa, wanalala, wanaowa, wanaumwa na huenda
wakasahau baadhi ya mambo yale yasiyohusiana na ujumbe waloamrishwa na
MwenyeziMungu kuufikisha na huenda wakakosea katika baadhi ya mambo ya
kibinadamu waliyoruhusiwa kufanya kwa jitihada zao katika kuyaamua.
Lakini wao hukumbushwa na
kujulishwa makosa yao kwa njia ya Wahyi ili makosa hayo yasije kuonekana kuwa
ndiyo sahihi inayotakiwa.
Na huenda mikono ya
madhalimu ikawafikia na wakakumbana na mateso na adhabu na huenda hata
wakauwawa, hasa kwa wale Mitume wasioamrishwa kupigana jihadi.
MITUME ILIYOTANGULIA
Wamo miongoni mwao wale
alotuhadithia MwenyeziMungu juu yao na kuyataja majina yao na wengine
hukutuhadithia habari zao.
MweyeziMungu anasema:-
"Na (tuliwapa wahyi)
Mitume tuliokuhadithia (habari zao) zamani na Mitume ambao hatukukuhadithia
(habari zao) na MwenyeziMungu akamsemeza Musa".
(An - Nisaa -164)
Kwa hivyo sisi tunawaamini
Mitume wote, mmoja mmoja, pale alipowataja MwenyeziMungu kwa kuwachambua au kwa
ujumla pale alipowajumuisha.
Ama wale alotuhadithia
habari zao ni wale waliotajwa katika kauli ya MwenyeziMungu:-
"Na hizi ndizo (baadhi
ya) hoja zetu tulizompa Ibrahim juu ya watu wake.Tunamyanyua katika vyeo yule
tumtakaye (kwa kuwa anakwenda mwendo tunaoutaka). Hakika Mola wako ndiye Mwenye
hekima na ndiye Ajuaye.
Na tukampa (Ibrahim mtoto
anayeitwa Is-haqa na (mjukuu anayeitwa) Yakubu wote tukawaongoa. Na Nuhu
tulimwongoa zamani na katika kizazi chake (Nuhu tulimwongoa) Daudi na Suleiman
na Ayub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tulipavyo wafanyao wema Na
(tukamwongoa) Ismail na Al Yasaa (Ilisha) na Yunus na Luti Na wote
tukawafadhilisha juu ya walimwengu (wote katika zama zao)".
(Al - An - Am -83- 86).
Na akasema:-
“Hakika Mwenyezi Mungu
alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha
Ibrahimu na kizazi cha Imrani (Babake Musa na Imrani mwengine aliye babake
Maryamu) juu ya walimwengu wote (wa zama zao)”.
Aali Imran - 33
Na akasema:-
"Na kwa Adi
tuliwapelekea ndugu yao Hud".
(Huud -50)
Na akasema:-
"Na (mtaje) Ismail na
Idris na Dhul Kifli wote walikuwa miongoni mwa wanaosubiri".
(Al - Anbiyaa -85)
"Na kwa Thamud
tukampeleka ndugu yao Saleh".
(Huud -61)
Na akasema:-
"Muhammad si baba wa
yeyote katika wanaume wenu bali yeye ni Mtume wa Mungu na mwisho wa
Mitume".
(Al - Ahzab -40)
Mitume hii imeletwa na
MwenyeziMungu katika zama zote zilizopita, na hakukuwa na Umma uliokosa Mtume
aliyekuwa akiwalingania katika njia ya MwenyeziMungu na kuwaongoza katika njia
iliyo sawa.
MwenyeziMungu anasema:-
"Wallahi sisi tulituma
(Mitume) kwa Umma zilizokuwa kabla yako".
(Al - Nahl -63).
Na akasema:-
"Na hakuna taifa
lolote ila alipita humo muonyaji (Mtume kuwaonya)".
(Fatir -24)
Na kasema:-
"Na kila kaumu ina
muongozaji."
(Ar - Raad -7)
MUHAMMAD (SAW)
Hapo mwanzo, Mitume ilikuwa
ikitumwa kwa ajili ya kaumu zao tu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kila kaumu ina
muongozaji."
(Ar - Raad -7)
Lakini Muhammad (SAW) ametumwa
kwa ajili ya watu wote .
MwenyeziMungu anasema:-
"Nasi hatukukutuma
(hatukukuleta) ila uwe rehema kwa
walimwengu wote".
(An - Biyaa - 107)
Na akasema:-
"Ni mwenye kuleta
baraka (kweli kweli) yule aliyeteremsha Qurani kwa mja wake ili awe muonyaji
kwa walimwengu (wote)".
(Furqan -1)
Miujiza ya Mitume
iliyotangulia ilikuwa ikitendeka na kuonekana mbele ya macho ya watu waliokuwa
wakiiona, ama wengine waliobaki walikuwa wakihadithiwa tu na wenzao wengi
waliyoiona miujiza hiyo ikitendeka. Lakini MwenyeziMungu amejaalia Dalili na
Muujiza wa Muhammad (SAW), yenye kuusadikisha ujumbe wake kuwa ni thabiti na
isiyokonga mpaka Siku ya kiama ili iwe hoja juu ya watu wote.
Muhammad (SAW) ni Nabii na
Mtume wa mwisho; hapana mtume baada yake. Ndiyo maana MwenyeziMungu akaihifadhi
dini aliyokuja nayo na akaihifadhi Miujiza yake inayosadikisha Utume wake
(SAW).
TANO – IMANI JUU YA SIKU YA KIAMA.
Imani juu ya Siku ya mwisho
ni nguzo mojawapo katika nguzo za imani,
ni wajibu kuiamini, pamoja na kuziamini alama za kukaribia kwa Siku ya kiama
pamoja na ishara zake zitakazo onekana kabla ya kufika siku hiyo, na pia imani
juu ya kufa na yale yanayofuatia baada yake katika misukosuko ya kaburini na
adhabu zake pamoja na neema zake, na juu
ya kupulizwa kwa baragumu na watu kutoka makaburini, na juu ya vitisho vya Siku
ya Kiama na kukusanywa kwa watu na kugawiwa kwa madaftari (yaliyoandikwa ndani
yake mema na maovu) na kuwekwa kwa mizani na Sirati (njia) na Hodhi na Shafaa
kwa wale watakaoruhusiwa na MwenyeziMungu, na juu ya Pepo na neema zake, na
Moto na adhabu zake, na mengi mengineyo yaliyotajwa katika Qurani na katika
hadithi za Mtume (SAW) zilizo sahihi.
DALILI ZA IMANI JUU YA SIKU YA MWISHO (KIAMA)
1) USHAHIDI WA KUNUKUU:-
MwenyeziMungu ametujulisha
juu ya Siku ya Kiama katika kauli Yake:
“Alif Lam Mim.
Hiki ni Kitabu kisichokuwa
na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu.
Ambao huyaamini ya ghaibu
na hushika Sala, na hutoa katika tuliyowapa.
Na ambao wanayaamini yaliyo
teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo”.
(Al - Baqarah -1 - 4)
Na katika kauli Yake:-
"Na mwenye kumkanusha
MwenyeziMungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume yake na Siku ya mwisho basi bila ya shaka
amepotea upotofu (upotevu) ulio mbali(na haki)".
(An - Nisaa -136)
Na katika Kauli yake:-
"Hakika wale
wasiotaraji kukutana nasi na wakawa radhi na maisha ya dunia na wakapoa moyo
kwa hayo, na wale wanaoghafilika na Aya zetu. Wote hao makazi yao ni Motoni kwa
sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma".
(Yunus - 7 - 8)
Na akasema:-
"Bila shaka
mnayoahidiwa ni ya kweli na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea".
(Ad - Dhariyat -5-6)
Na akasema:-
"Na kwamba Kiama
kitakuja, hapana shaka ndani yake na kwa hakika MwenyeziMungu atawafufua walio
makaburini."
(Al - Hajj -7)
Na akasema:-
"Waliokufuru wanadai
kuwa hawatofufuliwa. Sema; "Kwa nini? Kwa haki ya Mola wangu nyinyi lazima
mtafufuliwa; kisha lazima mtajulishwa mliyoyatenda na (mlipwe kwayo). Na hayo
ni sahali (mepesi) kwa MwenyeziMungu".
(Attaghabun -7)
Na katika kauli Yake:
"Jee! wao hawafikiri
ya kwamba watafufuliwa katika siku hiyo iliyo kuu siku watakaposimama watu wote
mbele ya Mola wa walimwengu wote".
(Al -Mutafifin -5)
Na katika kauli yake:
"Naapa kwa Siku ya
Kiama. Tena naapa kwa nafsi inayojilaumu; (kuwa mtafufuliwa na mtalipwa)
anadhani mtu kuwa sisi hatutaikusanya mifupa yake? Kwanini! Sisi tunaweza
(hata)kuzisawazisha ncha za vidole vyake".
(Al - Kiyama - 1-4)
MwenyeziMungu akasema pia:-
"Nao (wakaapa) kwa
jina la MwenyeziMungu kwa kiapo chao cha nguvu (kwamba)
MwenyeziMungu hatawafufua wafao. (kwa nini
asiwafufue?) Ni ahadi iliyolazimika kwake (kuwafufua na kuwalipa), lakini watu
wengi hawajui.
Atawafufua ili
kuwabainishia yale waliokhitilafiana, na ili wajue waliokufuru kwamba wao
walikuwa waongo.
Kauli yetu kwa kitu
tunachokitaka (kiwe) ni kukiambia "Kuwa ". Basi kinakuwa tu".
(An - Nahl 38- 40)
Na Aya kama hizo zipo
nyingi sana.
2) Kujulishwa na Mtume
(SAW) kama pale alipoulizwa na Jibrli (AS)
"Nijulishe juu ya Imani”
Mtume(SAW) akajibu;
"Kumwamini MwenyeziMungu na Malaika wake na
vitabu vyake na Mitume wake, na Siku ya Kiama na kwa Qadari, kheri yake na
shari yake".
(Bukhari na Muslim)
Hadithi za mfano huo zipo nyingi sana.
1. Kukubaliana kwa dini zote
zenye asili ya kushushiwa Wahyi, pamoja na imani ya mamilioni ya viumbe
wakiwemo Mitume, Manabii, watu wenye Hekima, Maulamaa na Wacha Mungu, wote
wakiamini kuwepo kwa Siku ya Kiama pamoja na yote yaliyoelezewa kuwa yatatokea
siku hiyo na kuwa na imani isiyokuwa na shaka juu ya hayo.
2. Uwezo wa MwenyeziMungu
aliyeumba wa kuwarejesha tena viumbe vyake baada ya kuwafanya watoweke, kwa
sababu kuwarudisha tena, si kazi ngumu kuliko kuumba mara ya mwanzo, pale
alipoweza kuumba pasipo na mfano wake.
3. Tunapata uhakika juu ya
haya pia, kutokana na ukweli wa Mtume (SAW), "Msema kweli" mwenye
miujiza na dalili zinazoilazimisha akili kuukubali ukweli wa ujumbe wake.
Tumejulishwa pia kuwa MwenyeziMungu alimpandisha Mtume wake mbinguni na akaiona
Pepo na Moto, na akatuletea maneno ya MwenyeziMungu aliyeumba uhai wa dunia na
uhai mwingine na akatujulisha pia juu ya uhai unaotusubiri baada ya kufa kwetu.
4. Kwa hivyo elimu yetu juu ya
makazi ya akhera imetujia kutokana na asili zenye kuaminika kabisa. Kutoka kwa
Yule aliyeumba dunia na akhera, na kutoka kwa Mtume wake aliyeziona Pepo na
Moto.
5. Hiyo ni ahadi ya
mwenyeziMungu na MwenyeziMungu havunji miadi yake
6. Mtume (SAW) ametuelezea pia
juu ya ishara zitakazoonekana duniani, zikiwa ni alama za kukaribia kwa saa, na
tukazishuhudia nyingi katika alama hizo, jambo linalotuhakikishia ukweli wa
yale aliyotueleza Mtume(SAW) juu ya Siku ya Kiama.
7. Kwa hivyo kama tulivyoziona
alama hizo hapa duniani kweli kweli baada ya kupita miaka elfu moja na mia nne
(tokea alipokuja Mtume(SAW)), basi
tutaziona pia Pepo na Moto kweli kweli.
8. MwenyeziMungu anasema:-
9. "Na watu wa Peponi
watawaita watu wa motoni (waseme) "Sisi tumekuta aliyotuahidi Mola wetu
kuwa ni kweli. Jee na nyinyi (Pia) mmekuta aliyokuahidini Mola wenu kuwa ni
kweli?”
10. Wakasema (watu wa motoni)
"Ndiyo" Basi mtangazaji atatangaza baina yao (aseme); "Laana ya
MwenyeziMungu iko juu ya Madhalimu (waliodhulumu nafsi zao)".
11. (Al - Aaraf -44).
1) Aliyemuumba mwanadamu bila
shaka atakuwa mkamilifu kuliko mwanadamu, na mwanadamu kwa kawaida hupenda uadilifu. Bila shaka MwenyeziMungu ndie
aliyeumba mapenzi hayo ya uadilifu ndani ya nafsi za binadamu waliotangulia na
watakaokuja. Na uadilifu wa binaadmu wote pamoja, ni sawa na cheche ndogo tu
ukilinganisha na uadilifu wa MwenyeziMungu. Kwani MwenyeziMungu ndiye Muadilifu
Mwenye Hikima.
Na katika
uadilifu ni kulipwa mema kila atendae mema na kutiwa adabu mwenye kufanya
maovu, lakini hapa duniani hapawezi kupatikana uadilifu huo kwa ukamilifu. Kwa
vile tumekwishauelewa uadilifu wa MwenyeziMungu, kwa hivyo akili inahakikisha
kwamba Mwenyezi Mungu lazima ataisimamisha mizani za uadilifu katika uhai ujao.
MwenyeziMungu anasema:-
"Jee!Tuwafanye wanaotii sawa na waasi?
Mmekuwaje! Mnahukumu namna gani?".
(Al -Qalam -35 - 36)
Na akasema:-
"Nasi tutaweka mizani za udadilifu Siku ya
Kiama, na nafsi yoyote haitadhulumiwa hata kidogo".
(Al - Anbiyaa - 47)
2) Tukizingatia jinsi mbingu
na ardhi zilivyoumbwa tunaona kuwa kila kitu kimewekwa mahali panaponasibiana
napo sawa sawa. Mbingu na vilivyomo ndani yake kama vile nyota na sayari, usiku
na mchana. Ardhi na vilivyomo ndani yake pia kama vile mimea na wanyama na
wanaadamu na vitu visivyo na uhai, kila kitu kipo mahali panapostahiki kuwepo
sawa sawa.
Moyo upo mahali pake na jicho lipo mahali pake na
jani lipo mahali pake juu ya mti, na ua lipo mahali pake na hivi ndivyo ilivyo,
hapana kitu chochote kilichohalifu amri
na kisiwe mahali pake kama kinavyotakiwa isipokuwa katika hali za
wanadamu.
Tunamuona dhalimu yupo mahali asipostahili kuwepo,
na utamuona Nabii aliyetumwa akifukuzwa na kuudhiwa na masafihi.
Kwa nini
basi hatuioni haki ikisimama katika maisha ya wanaadamu kama ilivyosimama
katika kila kilichokuwemo ardhini na mbinguni?
Akili inatujulisha kuwa Aliyeumba mbingu na ardhi
kwa haki, lazima siku moja ataisimamisha haki kwa ajili ya watu pia. Na iwapo
haya hayawezi kutimia hapa duniani kwa vile hapa ni mahali pa majaribio na
mitihani, basi hapana budi haki itasimama Siku ya Kiama.
"Jee! Wanafikiri wale waliofanya maovu kuwa
tutawafanya kama wale walioamini na kutenda mema kwamba maisha yao yawe sawa
sawa? Ni hukumu mbaya wanayoihukumu (ya kuwa wote watakuwa sawa) Na
MwenyeziMungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki na ili kila nafsi ilipwe yale
iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa”.
(Al - Jathiya - 21 22)
Mwanadamu akitafakari namna gani MwenyeziMungu alivyomhifadhi na
asimpoteze tokea pale alipokuwa tone la maji yaliyo dhalili (Manii) au pale
alipokuwa kidonge cha damu, na pia namna gani MwenyeziMungu alivyochukuwa
jukumu la kumhifadhi katika maisha yake yote.
Atakayetafakari juu ya yote haya, atakuwa na uhakika
kwamba MwenyeziMungu hatompoteza mwanadamu kwa njia ya kifo na kumfanya apotee
bure. Kwa sababu Mwenye Hikima anayezihifadhi sehemu ndogo ndogo za mwili,
hatokipoteza kile alichokiumba kwa ukamilifu (ambaye ni mwanadamu aliye
kamili).
MwenyeziMungu amesema:-
"Jee! anafikiri binaadamu kuwa ataachwa bure?
Jee hakuwa tone la manii lililotonwa kisha akawa kidonge cha damu kisha akaumba
na akamsawazisha (mwanadamu kamili)? Kisha akamfanya namna mbili, mwanaume na
mwanamke. Jee! Hakuwa huyo ni muweza wa kuhuisha waliokufa ?
(Al - Qiyama -36 - 40).
MAISHA YA BARZAKH (BAADA YA KUFA)
Mwislamu anaamini kwamba Neema za kaburini na Adhabu
zake pamoja na masuala atakayoulizwa na Malaika wawili kaburini mwake, ni haki
na kweli kutokana na ushahidi ufuatao:-
MwenyeziMungu anasema:
"Hapana! Hakika hili ni neno tu analolisema
yeye (aliye mwovu anapofikiwa na mauti) na mbele yao kuna maisha ya baada ya
kufa (ya taabu kwa wabaya na ya raha kwa wazuri) mpaka siku
watakapofufuliwa!".
(Al - Muminun - 100)
Na akasema:
"Na adhabu mbaya ikawazunguka hao watu wa
Firauni pamoja naye. Adhabu ya Motoni wanadhihirishiwa (makaburini mwao)
asubuhi na jioni na siku ile kitakapotokea Kiama (kutasemwa); "Waingizeni
watu wa Firauni katika adhabu kali zaidi".
(Al - Muminun - 45 - 46)
Na pia akasema:-
"MwenyeziMungu huwathubutisha wale walioamini
kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika akhera."
(Ibrahim - 27)
Na Mtume (SAW) amesema:
<<Hakika mja baada ya kuwekwa kaburini mwake,
pale watu wake wanapoondoka huwa anasikia vishindo vya viatu vyao. Basi hujiwa
na Malaika wawili wakakaa naye na kumuuliza: "Ulikuwa ukisema nini juu ya
mtu huyu (aitwae) Muhammad (SAW)?"
Muislamu hujibu:
"Ninashuhudia kwamba yeye ni mjumbe wa
MwenyeziMungu na Mtume wake."
Ndipo atakapoambiwa;
"Yaangalie (yaliyokuwa) makazi yako ya Motoni,
MwenyeziMungu amekupa badala yake makazi ya Peponi".
Kisha atayaona makazi yote mawili, na kaburi
litapanuliwa ili pawe na nafasi kubwa.
Ama mnafiki au kafiri anapoulizwa;
"Ulikuwa ukisema nini juu ya mtu huyu?”
Yeye hujibu;
"Sijui! Nilikuwa nikisema kama wasemavyo
watu."
Basi huambiwa;
"Hukujua wala hukusoma"
Kisha anapigwa kwa nyundo ya chuma pigo moja, na
hupiga ukelele unaosikika na viumbe vyote waliokuwa naye isipokuwa wanadamu na
majini>>.
Na Mtume (SAW) pia akasema:
<<Mmoja wenu anapokufa huonyeshwa makazi yake
mchana na usiku. Akiwa katika watu wa
Peponi basi (huonyeshwa) ya Peponi na akiwa katika watu wa Motoni basi (huonyeshwa) ya Motoni, kisha huambiwa;
"Haya ndiyo makazi yako atakapokufufua
MwenyeziMungu Siku ya Kiama>>.
Siku moja Mtume(SAW) alipokuwa akipita baina ya
makaburi mawili alisema:
(1)<<Hawa wanaadhibiwa, na wala hawaadhibiwi
kwa makubwa, (bali hivyo) bali mmoja wao alikuwa akifanya Namima (na maana yake
ni ‘kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule) ama mwengine alikuwa hajikingi
na mkojo wake>>[8].
Na katika dua zake, Mtume (SAW) alikuwa akisema:
<<MwenyeziMungu najikinga kwako kutokana na
Adhabu ya Kaburini na Adhabu ya Motoni na kutokana na mitihani ya maisha na ya
kifo>>.
Zipo hadithi nyingi kama hizo za kuaminika kabisa
zilizofikia daraja la ‘Tawatur’.
USHAHIDI WA KIAKILI.
1)
Imani juu ya MwenyeziMungu na Malaika wake na Vitabu
vyake na Mitume yake na juu ya Siku ya Kiama, inamlazimisha mtu kuamini pia juu
ya adhabu za kaburini na neema zake na kila kinachotendeka humo, na hii ni kwa
sababu vyote hivyo ni katika Elimu ya Ghaibu.
Kwa hivyo anayeamini baadhi ya hayo, akitumia akili
yake ataona kwamba hana budi kuyaamini yote yaliyobaki.
2)
Adhabu na neema za kaburini pamoja na masuali
yanayoulizwa na Malaika wawili si katika mambo ambayo akili haiwezi kuyakubali
na wala si jambo lisilowezekana kuwa, bali kinyume cha hivyo, akili inayakubali
na kuyashuhudia hayo.
Mtu anapolala (kwa mfano), huota na kuyaona mambo
anayoyapenda na akayaonea raha, yakamfurahisha nafsini mwake, jambo ambalo
humfanya ahuzunike pale anapoamka na kukatika utamu wa ndoto yake.
Wakati huo huo mtu anaweza kuota ndoto asiyoipenda,
ikamhuzunisha na kumfanya amshukuru yule aliyekuja kumwamsha.
Hizi ni Neema au Adhabu za usingizini tu, huingia
katika roho kwa uhakika, na roho huathirika nazo; na haya ni matukio ambayo
hatuyahisi wala kuyashuhudia kwa uhakika, lakini hakuna anayeyakanusha.
Vipi basi mtu anakanusha adhabu za kaburini na neema
zake?
VITISHO VYA SIKU YA KIAMA
Tunavishuhudia vitisho vya Siku ya Kiama katika aya
mbali mbali za Qurani.
Miongoni mwa aya hizo ni kauli yake MwenyeziMungu
isemayo:
"Jua litakapokunjwakunjwa.
Na nyota zitakapopukutika.
Na milima itakapoendeshwa (angani kama vumbi).
Na ngamia wenye mimba pevu watakapokusanywa.
Na bahari zitakapowashwa moto.
Na roho zitakapounganishwa (na viwiliwili vyake).
Na mtoto mwanamke aliyezikwa hali ya kuwa yu hai
atakapoulizwa kwa makosa gani aliuawa?
Na madaftari ya amali yatakapoenezwa (kila mtu apewe
lake).
Na utando wa mbingu utakapotanduliwa.
Na Jehannam itakapochochewa.
Na Pepo itakaposogezwa".
(At - Takwiyr -1 - 13).
Na katika kauli Yake:-
"(Wakumbusheni) Litakapotokea tokeo (hilo la
Kiama).
Ambalo kutokea kwake si uwongo.
Lifedheheshalo (wabaya). Litukuzalo (wazuri).
Ardhi itakapotetemeshwa mtetemeko mkubwa.
Na milima itakaposagwa sagwa.
Iwe mavumbi yanayopeperushwa".
(Al - Waqiah - 1 - 6)
Na katika kauli Yake:-
"Enyi watu! Mcheni Mola wenu, hakika utetemeko
wa Kiama ni jambo kubwa (kabisa).
Siku mtakapokiona (hicho Kiama) kila mwanamke
anyonyeshaye atamsahau amnyonyeshaye na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake
(kabla ya wakati kufika).
Na utawaona watu wamelewa kumbe hawakulewa.
Lakini ni adhabu tu ya MwenyeziMungu (hiyo) iliyo
kali."
(Al - Hajj - 1 - 2)
Na katika kauli Yake:
"Basi itakapokuja sauti kali iumizayo
masikio(sauti ya baragumu la Kiama).
Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye na mamaye na
babaye.
Na mkewe na wanawe.
Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na hali
itakayomtosha mwenyewe (hana haja ya wenziwe)".
ABASA - 33 -
37
PEPO NA MOTO
PEPO
Ni makazi
ya wanaomuabudu Mungu mmoja tu, na makazi ya walioamini na kutenda mema, na ya
waliomcha Mungu wao, na ya waja wa Mungu waliosafishwa, na ni makazi ya wale
wanaomuogopa Mungu wao na ya wanaotimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu wanapoahidi,
na ya wapiganao Jihadi katika njia ya MwenyeziMugnu kwa nafsi zao na mali
zao, na wanaotubu, wanaomuabudu
MwenyeziMungu na kumshukuru, wanaomsujudia na ya wenye kuamrisha mema na
kukataza maovu.
Na Mwenyezi
Mungu Subhanahau wa Taala amekwisha bainisha wazi katika kitabu chake kitukufu
juu ya Pepo na neema zake na Mito yake na Miti yake na Matunda yake na Vyakula
na Vinywaji vyake, na juu ya Nguo na Mavazi na Mapambo yake, na juu ya Nyumba
zake na Vyumba vyake, Wanawake wake walio wazuri. Akaeleza kwamba neema zake
hazifanani hata kidogo na neema za hapa duniani.
MwenyeziMungu anasema:-
"Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo
yanayofurahisha macho (huko Peponi); ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
(As - Sajdah - 17)
Na Mtume (SAW) katika hadith ya Al Qudusiy akasema:-
MwenyeziMungu anasema;
<<Nimewatayarishia waja wangu walio wema yale
ambayo hapana jicho lililowahi kuyaona wala sikio kuyasikia, na wala hayakupata
kumpitikia mtu yeyote (akilini mwake)>>.
MOTO.
1 ya makafiri na wanaotakabari katika kumtii
MwenyeziMungu na katika kumuabudu.
MwenyeziMungu ametujulisha juu ya wasfu wa kuni zake na moto wake
unaowaka vikali kabisa, na akaelezea juu ya vyakula na vinywaji vya watu wa
Motoni, na akaelezea pia adhabu zake kwa ajili ya kuingiza hofu katika nyoyo za
wahalifu, na ili kumtisha kila mwenye kutakabari na kujifanya kuwa ni jabari
muovu, ili ayaache maovu anayoyafanya.
Mwenye kupata adhabu hafifu kabisa katika watu wa
motoni ni yule atakayekewa viatu viwili au nyuzi za viatu za moto chini yake
vinamuunguza mpaka ubongoni mwake kama inavyoungua sufuria ya kuchemshia maji,
na hujiona kama kwamba yeye ndiye anayeadhibiwa kupita wote Siku ya Kiama.
Kwa atakae maelezo zaidi juu ya wasfu wa Pepo na
Moto basi asome Qurani na hadithi za Mtume (SAW) na atapata mengi yakutosheleza
humo.
FAIDA YA KUAMINI SIKU YA KIAMA.
Kuwa na Imani juu ya Siku ya Kiama kunayafanya maisha yetu yawe na
maana na yawe na lengo lililo bora, lengo ambalo linamfanya mtu apende kufanya
yaliyo mema na kuacha maovu, kujipamba kwa fadhila na kujiepusha na maovu
yanayodhuru miili na kuidhuru dini na heshima na yanayodhuru akili na mali.
VIPI TUTAFUFULIWA
ASILI TATU ALIZOUMBIWA MWANADAMU
Mwanadamu ameumbwa kutokana na Asili Tatu:-
1) Asili ambayo ameirithi
kutoka kwa Adam (AS) ambayo imekuja pamoja na tone la manii (mbegu).
2) Udongo, ulioingia mwilini
kwa njia ya chakula, mwili ukakuwa na kujengeka pamoja na asili ya mwanzo
aliyoirithi kutoka kwa Adam (ambayo ni mbegu).
3) Roho, iliyopulizwa katika
mwili wa kiumbe akiwa bado yumo tumboni mwa mamake.
WAKATI WA MTIHANI NA MWISHO WAKE
Kutokana na mchanganyiko wa vitu hivyo vitatu (asili
hizo tatu) na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, anapatikana mwanadamu aliye hai
mwenye kupitisha wakati wake wa mtihani hapa duniani.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni
(kukufanyieni mtihani) ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri
zaidi".
Al Mulk - 2
Muda wa mtihani utakapomalizika, na wakati wa kutoka
na kwenda kwenye makazi ya malipo utapofika, ndipo mauti yanapokuja.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Utakapowafikia muda wao hawatakawia (hata) saa
moja wala hawatatangulia (kabla haujafika)".
Al Aaraf -34
Na anasema:
"Lakini Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yo
yote inapokuja ajali yake"
Al Munafiqun - 11
MTU ANAPOKUFA, ZILE ASILI TATU KILA MOJA INARUDI MAHALA PAKE PA ASILI
Kwa kifo, udongo ambao kwao ndio mwili ulijengeka,
unarudi mahala pake pa asili napo ni ardhini.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Kwa hakika tunajua kiasi cha kila
kinachopunguzwa na ardhi katika miili yao (wakati wanapooza huko makaburini) Na
kwetu kiko kitabu kinachohifadhi (kila kitu)".
Qaf -4
Kinachobaki katika mwili wa mwanadamu ni kitu kidogo
kinachoitwa "Ajabu dhanab" (kilichoingia pamoja na mbegu). Hii ni
sehemu ambayo ndani yake mtu aliumbiwa, na kitu hiki asili yake kilikuwa katika
uti wa mgongo wa Baba yetu Adamu(AS), kwa vile kitu hiki ni kidogo sana
(Hakiwezi kuonekana ila kwa kutumia microscope zenye nguvu sana), ndiyo maana
uti wa mgongo wa Baba yetu Adamu(AS) uliweza kuzibeba asili hizi zote za
wanawe.
Na sehemu hii iitwayo "Ajabu dhanab"
haiozi wala haivurugiki.
Mtume(SAW) amesema:-
<<Mwili wote wa mwanaadamu unaoza isipokuwa
"Ajabu dhanab", kutokana nayo ameumbwa na kutokana nayo atakusanywa
tena >>.
Bukhari – Muslim – An Nasai, Malik katika Muwata a
na Abu Daud.
Ama Roho itarudi mahali anapopataka MwenyeziMungu
(katika Barzakh) mpaka Siku ya Kiama.
SIKU YA KUFUFULIWA ZILE SEHEMU TATU ZINAKUSANYIKA TENA
Unapofika wakati wa kufufuliwa, MwenyeziMungu
atateremsha mvua na kuifanya ile mbegu isiyooza "Ajabu dhanab”, imee tena.
Mtume (SAW) amesema:-
<<Kisha inateremshwa mvua na watamea kama
imeavyo mboga, na hapana katika mwili wa mwanadamu kisicholiwa na ardhi
isipokuwa fupa moja nalo ni "Ajabu dhanab" ndani yake humo watakusanywa
viumbe Siku ya Kiama>>.
(Bukhari, Muslim, Imam Malik, Abu Daud na AnNasaiy)
Yaliyofanana na haya yanatokea duniani kila siku.
Panapotokea ukame, tunaona miti ikianguka na kufa (na kutoweka). Hauonekani mti
wowote wala mmea. Lakini Mwenyezi Mungu amejaalia ndani ya ardhi au ndani ya
mawe kuwemo mbegu, na mbegu hizo hazionekani kwa macho, isipokuwa mvua
inaponyesha ndipo hupasuka na kuchipua miti na mimea mbali mbali.
MwenyeziMungu anasema:-
"Hukitoa kilicho hai katika kilichokufa na
hukitoa kilicho kufa katika kilicho hai na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake
na hivyo ndivyo mtakavyofufuliwa".
(Al - Rum - 19).
Mtu mmoja alimuuliza Mtume (SAW):-
"Ewe Mtume wa MwenyeziMungu, namna gani
MwenyeziMungu atawarudisha tena viumbe, na nini dalili yake?”
Mtume (SAW)
akamjibu;
"Uliwahi kupita bondeni kijijini kwenu wakati
wa ukame (miti yote ikiwa imekufa), kisha ukapita tena wakati miti (imeota tena
na) imejaa na ardhi ikageuka (na kuwa) rangi ya kijani?
Akasema:- "Naam".
Mtume(SAW) akamjibu:
"Basi hiyo ndiyo dalili ya MwenyeziMungu katika
kuumba kwake na hivyo ndivyo atakavyowafufuwa wafu".
(Imam Ahmad )
(Siku ya Kiama), Pale Ajab dhanab itakapochipua na
kutoka ndani ya ardhi na mwili ukarudi tena, ndipo zitakapokuja roho na kuingia
kila moja katika mwili wake.
Ndio sababu MwenyeziMungu akasema:
"Na nafsi zitakapounganishwa (na viwiliwili
vyake)."
(At - Takwiyr - 7)
Na hivi ndivyo watakavyorudi viumbe mara ya pili
kama walivyoanzishwa hapo mwanzo.
MwenyeziMungu anasema:-
"Kama tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha
tena, ni ahadi ilio juu yetu, bila shaka sisi ni wenye kufanya (tusemavyo).”
(Al - Anbiyaa -104).
JIBU KWA WANAOIKADHIBISHA SIKU YA KIAMA.
Inatosha kuwajibu wanayoikanusha Siku ya Kiama kama
walivyojibiwa na MwenyeziMungu, katika kauli yake:-
"Enyi watu! Kama mumo katika shaka juu ya
ufufuo; (mnaona haimkiniki kufufuliwa) basi (tazameni namna tulivyokuumbeni)
Kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo (Mzee wenu Nabii Adam), kisha (tukawa
tunakuumbeni nyinyi) kwa manii (mbegu ya uhai) kisha (yanageuka) kuwa kipande
cha damu, kisha huwa kipande cha nyama kinachoumbika (kinachofanyika sura) na
kisichoumbika ili tukubainishieni (Kudra yetu). Nasi tunakikalisha matumboni
tunachokitaka mpaka muda uliowekwa, kisha tunakutoweni kwa hali ya utoto, kisha
(tunakuleeni) ili mfike baleghe yenu. Na kuna wanaokufa (kabla ya kufikia hali
hii). Na katika nyinyi wako wanorudishwa katika umri dhalili; asijue chochote
baada ya kule kujua kwake; na unaiona ardhi imetulia kimya lakini
tunapoyateremsha maji juu yake, inataharaki na kukua na kuotesha kila namna ya
mimea mizuri.
Hayo ni kwa sababu MwenyeziMungu yuko, na kwamba
Yeye huwahuisha wafu, na kwamba Yeye ndiye Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Na kwamba kiyama kitakuja, hapana shaka ndani yake;
na kwa hakika MwenyeziMungu atawafufua walio makaburini".
(Al - Hajj - 5 - 7)
Na katika kauli Yake:-
"Jee! Mwanaadamu hatambui ya kwamba tumeemuumba
kwa tone la manii. Amekuwa hasimu yetu aliye dhahiri (sasa)?
Na akatupigia mfano na akasahau kuumbwa kwake(kwa
manii) akasema: "Nani atakaeihuisha mifupa na hali imesagika?"
Sema: “Ataihuisha yule aliyeumba mara ya kwanza naye
ni Mjuzi wa kila (namna ya) kuumba”. Ambaye amekufanyieni moto katika mti
mbichi, (nanyi) mkawa kwa (mti) huo mnauwasha.
Jee yule aliyeziumba mbingu na ardhi (mnaona) hana
uwezo wa kuumba (mara ya pili) mfano wao (wanadamu)? Kwa nini? Naye ni muumbaji
mkuu, Mjuzi wa kila jambo.
Hakika amri yake anapotaka chochote (kile kitokee)
ni kukiambia "Kuwa," basi mara huwa. Ametukuka yule ambaye mkononi
mwake umo ufalme wa kila kitu; na kwake mtarejezwa nyote."
(Yaasin -77 -84)
Na kauli Yake MwenyeziMungu;
"Qaf. Naapa kwa hii Qurani tukufu (kuwa
mtafufuliwa).
Bali wanastaajabu ya kwamba amewajia muonyaji kutoka
miongoni mwao (Wanataka awe Malaika). Na wakasema makafiri "Hili jambo la
ajabu!"
Kuwa tutakapokufa na tukawa udongo (kuwa
tutafufuliwa)?
Marejeo hayo ni ya mbali kabisa (hayawezi kuwa).
Kwa hakika tunajua kiasi cha kila kinachopunguzwa na
ardhi katika miili yao (wakati wanapooza makaburini). Na kwetu kiko kitabu
kinachohifadhi (kila kitu).
Lakini waliikadhibisha haki ilipowajia na wamo
katika jambo la mkorogeko.
Jee! hawazioni mbingu zilizo juu yao! tumezijengaje
na tumezipambaje wala hazina nyufa".
(Qaf - 1- 6)
SITA: IMANI JUU YA QADAR "KUDRA" (Majaliwa- YALIYOKWISHA ANDIKWA)
MAANA YA KUDRA
MwenyeziMungu alitaka kuumba viumbe(akaumba), kisha
akavipangia ajali zake na kuvipa viumbe hivyo vipimo maalum.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo
(chake)".
(Furqan - 7)
Kwa vile Yeye ni Mwenye kujua kila
kitakachowatokezea viumbe vyake, akaiamrisha kalamu iandike katika ubao
uliohifadhiwa (Lauhi l Mahfudh) yote yatakayo tokea hadi Siku ya Kiama.
MwenyeziMungu anasema:-
"Jee! Hujui ya kwamba MwenyeziMungu anajua
yaliyoko mbinguni na ardhini? Bila ya shaka (yote) hayo yamo Kitabuni (mwake);
Hakika (kudhibutu) hayo kwa MwenyeziMungu ni sahali".
(Al - Hajj - 70)
Na kila
kilichokuwepo ulimwenguni katika vinavyotaharaki na vilivyotulia, vyote hivyo huwa kama apendavyo MwenyeziMungu na
kwa uwezo wake Subhanahu Wa taala.
MwenyezMungu anasema:-
"Anaumba apendavyo; Naye ni Mjuzi Mwenye
uweza."
(Ar - Rum - 54)
Wala hakitendeki chochote ila kwa uwezo wa
MwenyeziMungu na kama apendavyo.
MwenyeziMungu anasema:-
MwenyeziMungu anasema:-
"Wala usiseme kamwe kwa lolote lile kuwa
"Nitalifanya kesho" Isipokuwa uongeze "Inshaallah"
(MwenyeziMungu akipenda)."
(Al - Kahf - 23 - 24)
Kwa hivyo atakacho MwenyeziMungu kinakuwa, na
asichotaka hakiwi.
IMANI JUU YA QADAR “KUDRA’.
Imani juu ya Kudra (Majaliwa) ni nguzo mojawapo
katika nguzo za Imani kama alivyotubainishia Mtume (SAW) katika hadithi ya
Jibril(AS), aliposema:-
Na uamini juu ya Kudra, kheri yake na shari yake.
Mwanadamu yeyote hawezi kuzizunguka kwa kuzijua siri
za MwenyeziMungu isipokuwa labda elimu yake iwe sawa na ilimu ya MwenyeziMungu
- na hili ni jambo lisilowezekana.
Huoni basi mfano wa kazi wanazofanya madaktari na
wenye ujuzi na wahandisi katika kazi ambazo wengine wasiokuwa wao hawazijui
sawa sawa, isipokuwa yule ambaye elimu yake imefikia daraja ya elimu zao?
Kwa mfano mtu mjinga, asiyeijua kazi ya madaktari
anapomwona daktari anapasua tumbo la mgonjwa na kuanza kukata matumbo yake,
hatokubali, na huenda akafanya zogo,
lakini mara atakapoelewa kwamba daktari ni mtu mwenye hekima na kwamba anaijua
kazi yake vizuri, mtu huyo ataacha ubishi wake huku akikiri juu ya ujinga wake
na kusalimu amri mbele ya elimu ya Daktari.
Mwislamu anauelewa vizuri ukamilifu mkubwa kabisa wa
Mola wake, ndio maana anaamini kwamba lolote linalotokea, basi haliwi isipokuwa
lina hekima ya MwenyeziMungu ndani yake.
Na iwapo hajaielewa hekima ya MwenyeziMungu katika
jambo lolote lile, huutambua ujinga wake mbele ya elimu ya MwenyeziMungu, na
kwa ajili hiyo huacha kubisha kwake na kujisalimisha mbele ya Mwenye Hekima,
Mwenye Ujuzi, Mwenye Ilimu anayesema:-
"Haulizwi (MwenyeziMungu) anayoyafanya (Kwani
yote ni ya haki) lakini wao viumbe wataulizwa".
(Al Anbiyaa - 23)
KATIKA MATUNDA YA KUAMINI KUDRA (KUDRA)
Mwenye kuamini kwamba MwenyeziMungu ameumba kila
kitu kwa kukikadiria, utamwona anajitahidi sana katika kutafuta mambo
yaliyokadiriwa ya kheri ili apate kuyasukumizia mbali yale ya shari.
Anaondoa Kudra(majaaliwa) ya njaa kwa kutumilia
kudra(majaaliwa) ya chakula, na kudra ya ugonjwa kwa kutumia kudra ya dawa na
kudra ya ufakiri anaiondoa kwa kutumia kudra ya kutafuta riziki.
Kwa yule mwenye Imani kamili juu ya kudra, utamwona
hahuzuniki kwa jambo lolote lile alolikosa au kumpotea, na wala havunjiki moyo
anapopatwa na masaibu, wala hajifakharishi au kutakabari anapofanikiwa au
kubahatika na jambo lolote lile, siku
zote anaiamini kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-
"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi
zenu ila umekwisha andikwa katika kitabu (cha MwenyeziMungu) kabla hatujauumba.
Kwa yakini hilo ni sahali kwa MwenyeziMungu. Ili msihuzunike sana juu ya kitu
kilichokupoteeni wala msifurahi sana kwa alichokupeni na MwenyeziMungu hampendi
kila ajivunae na ajifakharishae."
(Al - Hadid -22-23).
Mwenye kuamini Kudra ya MwenyeziMungu na uwezo Wake
na matakwa Yake kisha akaujua udhaifu wake(mwanadamu huyo) na jinsi
anavyomuhitajia Muumba wake, utamwona siku zote ni mkweli katika kumtegemea
Mola wake.
Anakubali kwamba kila kinachomfikia au kumsibu kuna
sababu ambayo MwenyeziMungu keshazikadiria, na humuomba Mola wake msaada kwa
yale asiyomuwezeshea.
Kila wakati huikariri kwa yakini kauli ya
MwenyeziMungu isemayo:-
"Sema 'Halitatusibu ila alilotuandikia
MwenyeziMungu, Yeye ni Mola wetu', basi Waislamu wamtegemee MwenyeziMungu
tu".
(At - Tawba -21)
MAMBO MAWILI YANAYOBABAISHA WATU
La kwanza:
Baadhi wa wajinga wanadai kwamba MwenyeziMungu ndiye
aliyewafanya wao wapotee na kuwafanya wasisali wala kufunga wala kutii amri
nyengine zozote za dini, na akawaongoza wengine. Kisingizio chao kikiwa ni katika
kauli ya MwenyeziMungu alipomwambia Mtume wake (SAW):-
"Kwa hakika wewe huwezi kumuongoza umpendae,
lakini MwenyeziMungu humuongoza amtakaye, naye anawajua waongokao (kwa hivyo
anawaongoa, na anawajua wasiotaka kuongoka kwa hivyo anawachilia mbali)".
(Al - Qasas -56).
Wale
wanaopenda kuzungumza juu ya mambo haya yanayobabaisha, hawaelewi kwamba
hidaya imegawika sehemu mbili;
1) Hidaya ya Kuongoza.
2) Hidaya ya Msaada.
Hidaya ya Kuongoza, ni mfano wa mtu anayekuonyesha
njia ya kukufikisha nyumba uitakayo kisha akakuacha baada ya kukuongoza na
kukufikisha penye njia itakayokupeleka huko.
Mitume ya MwenyeziMungu(AS), kazi yao ndio hii ya
kuongoza wanaadamu na kuwaonyesha njia itakayowafikisha Peponi.
MwenyeziMungu akimwambia Mtume wake(SAW) anasema:-
"Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia
iliyonyooka".
(A- Shuraa -52)
Ama hidaya ya Msaada, mfano wake ni mfano wa mtu
aliye karimu, mwenye huruma, mpole, unapomuuliza njia ya kukufikisha nyumba
uitakayo, akakuonyesha njia hiyo, kisha ukamuomba akusaidie zaidi, akakuchukua
katika gari lake na akakushika mkono mpaka akakufikisha pale unapotaka kwenda.
Hii ndiyo hidaya ya Msaada, na hidaya hii haipati
isipokuwa yule aliyeikubali kwanza hidaya ya kuongozwa, kisha akaomba msaada wa
kufikishwa.
Kwa vile Mitume ya Mwenyezi Mungu(AS), kazi yao ni
kuwapa watu hidaya ya Kuongoza, wao hawana uwezo wa kuwapa watu hidaya ya
Mafanikio au ya Msaada, kwa sababu mwenye kutoa hidaya hii ni Mwenyezi Mungu aliyetukuka, na hampi
isipokuwa yule tu anayemjua kuwa anastahiki kupewa.
MwenyeziMungu akimuambia Mtume wake(SAW) anasema:-
"Kwa hakika wewe huwezi kumuongoza umpendaye,
lakini MwenyeziMungu humuongoza amtakaye, naye anawajua waongokao (kwa hivyo
anawaongoa na anawajua wasiotaka, kwa hivyo anawachilia mbali)".
(Al - Qasas -56)
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu ambaye ni Muadilifu,
anawaahidi wale waliyoikubali hidaya ya Kuongozwa na kuwapa hidaya ya Mafanikio
na Msaada.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na wale wanaokubali kuongoka anawazidishia
uongofu na anawapa (jaza) ya ucha Mungu wao".
(Muhammad - 17)
Kwa hivyo MwenyeziMungu hamuachi kupotea isipokuwa
yule tu anayestahiki kuachwa kwa kuikataa hidaya ya Kuongozwa na kuendelea
kwenda mbali na njia ya haki.
MwenyeziMungu anasema:-
"Basi walivyoendelea na uovu wao, MwenyeziMungu
aliziachilia nyoyo zao zipotoke (kama walivyotaka wenyewe) na MwenyeziMungu
hawaongoi watu waovu (wenye kutoka katika utiifu wake".
(As - Saaf
-5)
La Pili:
Baadhi ya wajinga wanasema;
"Kwa vile MwenyeziMungu keshaandika kila kitu
juu ya ubao (Lauhu l mahfudh) ndio maana ikawafanya wasiosali wasisali na wanaosali wawe wanasali".
Haya ni mawazo ya kipuuzi kwani anayesali huwa
anasali kwa hiari yake mwenyewe bila ya kulazimishwa, na asiyesali huacha
kusali kwa hiari yake mwenyewe pia bila ya kulazimishwa wala kuambiwa.
Kila mtu anayaelewa haya vizuri kabisa, kwa sababu
MwenyeziMungu ametaka aumbe mwanaadamu (na akamuumba) akiwa amempa uhuru na
hiari ya kujichagulia alipendalo.
Mtu huenda akauliza:-
"Kwanini basi isiwe yale yaliyokwisha andikwa
katika ubao ndiyo yanayomlazimisha mtu afanye hayo, kwa sababu yameandikwa
tokea dunia ilipoumbwa".
Tunasema hivi;
Jibu lake ni rahisi, na tutalifafanua kwa mfano huu:
Huoni kwamba mwalimu aliye hodari anayewajua vizuri
wanafunzi wake, anapotoa masuali ya mtihani, iwapo ataandika katika karatasi
majina ya wanafunzi ambao ana hakika kuwa watafeli katika mtihani huo, na
akaandika majina ya wale ambao ana hakika kwamba watapasi, kisha mtihani
ukafanywa na matokeo yakajulikana, kisha wakaja wale waliofeli wakamlaumu
mwalimu wakisema:
"Kwa vile mwalimu keshaandika majina yetu
kwenye karatasi yake kwamba tutafeli basi yeye ndiye sababu ya kufeli
kwetu".
Jee! udhuru wao utakubalika? Ama wataambiwa kwamba:
"Alivyoandika mwalimu katika karatasi
kunaambatana na kukujueni vizuri nyinyi wanafunzi wake, na kufeli kwenu
kunatokana na uzembe wenu, kwa hivyo msiutafutie uzembe wenu kisingizio na
kumlaumu mwalimu wenu kwa sababu ya kukujueni vizuri (yupi katika yenu
anayejitahidi na yupi mchezaji)".
MwenyeziMungu ndie mwenye sifa Tukufu zaidi, kwani
Yeye Aliyetukuka Muumba wa viumbe ndie anayewajua vizuri viumbe wake.
MwenyeziMungu anasema:-
"Oh! Asijue aliyeumba! Naye ndie avijuaye
visivyojulikana na vinavyojulikana".
(Al - Mulk 14)
MwenyeziMungu Mtukufu ametuumba ili tupitishe wakati
wa kufanyiwa mtihani hapa duniani akiwa Yeye Mwenye Shani ya juu kabisa anajua
matokeo ya mtihani huo, akawaandikia
(kuwa watatenda) maovu wale waovu na akaandika yaliyo mema kwa walio wema,
kutokana na elimu Yake iliyokizunguka
kila kitu. Kwani Yeye ndiye anayejua yaliyokuwa na yatakayokuwa.
Huenda Mwalimu akakosea katika kukadiria matokeo ya
mtihani wa mwanafunzi wake, lakini MwenyeziMungu hawezi kukosea katika
kukadiria amali za viumbe vyake, na maandishi yaliyo katika ubao (Lauhul Mahfudh)
yanaambatana na elimu ya MwenyeziMungu iliyokitangulia kila kitu.
Kwa hivyo kutokusali, ni jambo lililoambatana na
uasi na uzembe wa yule aliyeacha kusali.
Wajinga wanataka kuutafutia udhuru upotevu wao huo
na maasi yao hayo, kwa kuisingizia ilimu ya MwenyeziMungu na Ukamilifu wake.
Elimu ya MwenyeziMungu imetangulia kuvijua vitendo,
lakini haimlazimishi mtu kutenda (kila mtu ana hiari ya kutii au kuasi), na
MwenyeziMungu amekwishamjulisha Mtume wake (SAW) yale yatakayotokea hadi Siku
ya Kiama na tumeona hapo mwanzoni katika Dalili za Kiama kwamba mengi ya yale
aliyoyataja Mtume(SAW) kuwa yatatokea yale ambayo Waislamu waliyaandika katika
vitabu vya hadithi za Mtume(SAW), tunayaona yakitokea hivi sasa.
Jee anaweza mtu kudai kwamba kwa vile Waislamu waliyaandika
katika vitabu vyao, ndio sababu yakatokea?
Sivyo. Bali elimu ya MwenyeziMungu juu ya matokeo
hayo imetangulia kwa kujua ni nani atakayeyaleta hayo matokeo, lakini
hayakumlazimisha mtu kuyatenda.
MATENDO YANAYOIJENGA YA IMANI
1- KUYAKUBALI NA KUYASADIKI YOTE YALIYOKUJA KUTOKA KWA MWENYEZIMUNGU
Mwislamu anatakiwa ayakubali yote aliyotujulisha
MwenyeziMungu katika kitabu chake, pamoja na yote aliyotamka Mtume wake
mkarimu(SAW). Ayakubali na kuyasadiki
usadikisho wa kweli usio na shaka yoyote ndani yake.
Mwislamu anatakiwa pia aamini kwamba lolote lile
lililopingana au linalopingana na yale aliyotujulisha MwenyeziMungu ni batil na
halifai hata wakilipambaje wenye hilo jambo au kuligeuza geuza.
Hii ni kwa sababu itikadi yake ni kuwa Dini inatoka
kwake Mwenye Kujua, Mwenye Hikima, Aliyekizunguka kila kitu kwa ilimu yake.
MwenyeziMungu anasema:-
"Basi ni lipi likupalo kukadhibisha Malipo
baada (ya kuona hayo)?
Jee! MwenyeziMungu si Hakimu Muadilifu kuliko
mahakimu wote?(basi si lazima atawalipa kwa mema yao na mabaya kwa mabaya
yao?)”
At Tiyn- 7-8
2- KUMTII MWENYEZIMUNGU NA KUMTII MTUME WAKE(SAW)
Hii ni kwa sababu anayemwamini MwenyeziMungu na
akamwamini Mtume wake, kisha akawa na yakini kwamba waadi wa MwenyeziMungu ni
wa kweli na kwamba MwenyeziMungu keshatayarisha malipo na thawabu kwa yule
atakaemtii Yeye na akamtii Mtume wake(SAW) kisha akafuata amri Zake na amri za
Mtume wake(SAW).
Kwa Imani yake hiyo, atalazimika ajisalimishe kwa
kuzifuata amri za MwenyeziMungu na za Mtume wake(SAW), na hii ni kwa sababu
Mwislamu anatakiwa awe anachunga kila alitendalo likubaliane na mafundisho ya
kitabu cha MwenyeziMungu pamoja na Sunnah (mafundisho) ya Mtume wake (SAW).
MwenyeziMungu anasema:-
"Na wenye kumtii MwenyeziMungu na Mtume, basi
hao watakuwa pamoja na wale aliowaneemesha MwenyeziMungu; Manabii na Masidiki
na Mashahidi na Masalih (watu wema). Na uzuri ulioje (kwa mtu) watu hao kuwa
rafiki (zake).”
(An - Nisaa -69)
Na akasema:-
"Mwenye kumtii Mtume (basi) amemtii MwenyeziMungu
(kwani anayoamrisha Mtume yanatoka kwa MwenyeziMungu) Na anayekengeuka
(anajidhuru mwenyewe). Hatukukupeleka wewe kuwa mlinzi juu yao (wakipotea
ulaumiwe wewe, la hatukufanya hivyo)".
(An - Nisaa - 80)
Na Mtume (SAW) amesema:-
<<Umma wangu wote utaingia Peponi isipokuwa
waliokataa>>.
Akaulizwa "Ni nani hao waliokataa?"
Akasema;
<<Atakayenitii ataingia Peponi na atakayeniasi
basi amekataa>>>
Bukhari katika sahihi yake na imepokelewa kutoka kwa
Abu Hurairah
3- KUTEKELEZA FARADHI
Imani inapoingia na kujaa moyoni, itavifanya viungo
vya mwili vifanye amali njema inayolingana na Imani hiyo na kumfanya mwenye Imani hiyo kujitahidi
kuyatekeleza yale aliyofaradhishiwa.
Ama yule asiyetekeleza faradhi zake huku akijidai
kuwa yeye ni Mwislamu, bila shaka ni mwongo aliyedanganywa na shetani
akampambia amali zake mbovu hizo azione nzuri.
Lau kama moyo wake ungetengenea kwa Imani kikweli,
basi kiwiliwili chake chote kingetengenea na kutekeleza faradhi zake.
Mtume (SAW)
amesema:-
<<Hakika katika mwili kuna kipande cha nyama,
kikitengenea hutengenea mwili wote na kinapoharibika huharibika mwili wote, kwa
hakika (eleweni kuwa) kipande chenyewe ni Moyo>>.
(Bukhari na Muslim)
4)- KUTIMIZA YALIYOWAJIBISHWA NA KUYAACHA YALIYO HARAMISHWA.
Imani ya mtu haiwi kamilifu bila kutimiza yale
aliyowajibishiwa na MwenyeziMungu na kuyaacha yale aliyoharamishiwa, kama
alivyotufundisha Mtume wa MwenyeziMungu (SAW).
Mwenyezi Mungu anasema;
“Na anachokupeni
Mtume basi pokeeni na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na muogopeni
MwenyeziMungu. Kwa yakini MwenyeziMungu ni mkali wa kuadhibu”.
(Al - Hashr - 7)
5- TOBA NA KUOMBA MAGHUFIRA:
Mwislamu anapotelezeshwa na shetani akatenda katika
yale yaliyoyaharamisha na MwenyeziMungu, hufanya haraka sana kutubu na kujuta
juu ya yale aliyoyapunguza katika haki ya MwenyeziMungu, na wala haendelei
kumuasi Mola wake, bali huomba maghufira kutoka Kwake.
MwenyeziMungu anasema akitoa wasfu wa waja wake
walioamini:-
“Na ambao wanapofanya uchafu (kufanya dhambi kubwa)
au kudhulumu nafsi zao (kwa dhambi ndogo ndogo) humkumbuka MwenyeziMungu na
kuomba msamaha kwa dhambi zao. Na ni nani anyeghufuria dhambi isipokuwa
MwenyeziMungu? Na hawaendelei na (maovu) waliyoyafanya hali wanajua (kuwa hayo
ni maovu).”
(Aal - Imran - 53)
Na akasema:-
"Sema "Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi
zenu! Msikate tamaa na rehema za MwenyeziMungu; bila shaka MwenyeziMungu
husamehe dhambi zote; hakika Yeye ni Mwingi wa kurehemu".
(Az - Zummar - 53)
KUAMRISHA MEMA NA KUKATAZA MABAYA.
Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni katika dalili
za ukamilifu wa Imani na ni moja katika sifa za Mwislamu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na wanaoamini wanaume na wanaoamini wanawake,
ni marafiki wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na kuyakataza yaliyo mabaya”.
(At - Tawba - 71).
Uhusiano uliopo baina ya nguvu ya Imani katika moyo
wa Mwislamu na katika kuifanya kazi ya kukataza mabaya na kuamrisha mema, ni
uhusiano ulio thabiti (Madhubuti)
Mtume SAW) amesema:-
<<Atakayeona miongoni mwenu jambo baya basi alizuie
kwa mkono wake, asipoweza basi kwa ulimi wake, asipoweza basi kwa moyo wake na
huo ni udhaifu wa imani >>.
Na katika hadithi nyengine:
<<Hapana katika kufanya hivyo (katika kuzuwia
mabaya kwa moyo) Imani hata iliyo na ukubwa wa chembe ya hardali >>.
(Imetolewa na Muslim , Abu Daud, Al Tirmidhy na Ibn
Majah Na imepokewa kutoka kwa Abu Saeed Al Khudry).
Mwislamu asiiache kazi hii ya kuamrisha mema na
kukataza mabaya, kwa sababu anapoiacha,
matokeo yake ni kula hasara na
kwenda mbali na njia ya Waislamu wa
kweli.
MwenyeziMungu anasema:-
"Naapa kwa zama (zako ewe nabii Muhammad ).
Kuwa binaadamu yuko katika hasara.
Isipokuwa wale walioamini na wakafanya
mema.Wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira
(kustahamiliana)".
(Asri - 1-3)
KULINGANIA WATU KATIKA DINI YA MWENYEZMUNGU NA KUWAPIGA VITA WANAOZUIA WATU KATIKA NJIA YA MWENYEZIMUNGU
Mja akeshaonja utamu wa Imani, na mapenzi ya
Mwenyezi Mungu yakaingia moyoni mwake, hufanya jitihada kubwa ili ajiepushe
yeye, jamii yake, pamoja na watu wote kutokana na kiza cha kufru, kutoamini
Mungu na kughafilika, na atafanya jitihada apate kuwaingiza watu katika Nuru ya
Imani na Qurani na uongofu.
Huwalingania watu katika dini ya MwenyeziMungu huku
akistahamili udhia wao, akitegemea ujira na thawabu kutoka kwa MwenyeziMungu
aliyetukuka.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na ni nani asemaye kauli zaidi kuliko aitaye (viumbe)
kwa MwenyeziMungu na (mwenyewe) akafanya vitendo vizuri na kusema "Hakika
mimi ni miongoni mwa Waislamu".
Haam - mym Sajdah (fusilat - 33)
Na akasema:-
"Sema hii ndio njia yangu; ninaita
(ninalingania) kwa Mwenyezi Mungu kwa ujuzi wa kweli; mimi (nafanya hivi) na
(kila) wanaonifuata. Na Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu; wala mimi
simo miongoni mwa wanaomshirikisha (Mwenyezi Mungu)".
Yusuf _108
Na Mtume (SAW) amesema:
<<Atakayewalingania watu katika uongofu, atapata ujira wake sawa
na watakaomfuata bila ya kupunguziwa kitu katika ujira wao>>.
Imetolewa na Muslim na wengineo na Imepokelewa
kutoka kwa Abu Hurairah (RA)
Ama kwa wale wanaozuwia watu katika njia ya Mwenyezi
Mungu na wakasimama imara kuwazuwia wasiingie katika dini ya Mwenyezi Mungu,
basi Waislamu wamefaridhishiwa kupigana nao Jihadi mpaka dini ya Mwenyezi Mungu
iweze kuwafikia watu wote ili aamini
atakayeamini baada ya kubainishiwa na aangamie atakayeangamia baada ya
kubainishiwa.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Enyi mlioamini Je! Nikujulisheni biashara
itakayokuokoeni na adhabu iumizayo? (Basi biashara hiyo ni hii) Muaminini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganieni dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu
na nafsi zenu, haya ni bora kwenu; ikiwa mnajua (kuwa ni bora basi fanyeni).
(Mkifanya haya):- Atakusameheni dhambi
zenu na atakuingizeni katika Mabustani yapitayo mito mbele yake na (atakupeni)
maskani mazuri mazuri katika Bustani za milele; huku ndiko kufuzu kukubwa. Na
(atakupeni) kingine mnachokipenda; nayo ni Nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu na
ushindi ulio karibu. Na wapashe habari njema Waislamu".
Al Anfal - 39
8- KUWAPENDA (KUWANUSURU) WAISLAMU NA KUJITENGA NA MAKAFIRI
Kunusuru
(wilaa) ni kupenda, kusahibiana na kusaidiana baina ya Waislamu. Na katika
masharti ya Imani ni kwa Mwislamu kuwanusuru Waislamu wenzake.
Mwislamu hatakiwi kukipa utiifu wake kwa kukinusuru kisichokuwa na
msingi wa Imani ya Kiislamu.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Rafiki yenu khasa (wa kumsafishia nia) ni Mwenyezi Mungu na Mtume
wake na walioamini ambao husimamisha Sala na hutoa Zaka, na hali ya kuwa
wananyenyekea. Na atakayefanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na
walioamini (atafuzu) kwani (watu wa) kundi la Mwenyezi Mungu ndio
watakaoshinda".
Al Maidah - 55-56
Na akasema:
"Na wanaoamini wanaume na
wanoamini wanawake, ni marafiki wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na
kuyakataza yaliyo mabaya, na husimamisha Sala na hutoa Zaka na humtii Mwenyezi
Mungu na Mtume. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye Nguvu na Mwenye Hikima".
At Tawba - 71
Mwenyezi amewapa Waislamu mfano bora katika
kujitenga na makafiri.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Hakika nyinyi mnao mfano mzuri kwa (Nabii)
Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye, walipowaambia jamaa zao (makafiri);
"Kwa yakini sisi tu mbali nanyi, na mbali na hayo mnayoyaabudu kinyume cha
Mwenyezi Mungu, tunakukataeni umekwisha dhihiri uadui na bughudha ya daima
baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomwamini Mwenyezi Mungu peke yake".
Mumtahinah – 4
MATENDO YANAYOIHARIBU IMANI - KWANZA - KUFRU NA AINA ZAKE
a- KUFRU YA KUKADHIBISHA
Nako ni kukadhibisha chochote katika aliyokuja nayo
Mtume (SAW).
Mwenyezi Mungu anasema:
"Na kama wanakukadhibisha, basi walikwisha
kadhibisha wale wa kabla yao. Mitume wao waliwajia kwa dalili wazi wazi na kwa
madaftari na kwa vitabu vyenye nuru (wakakadhibisha). Kisha niliwakamata
(niliwatia mkononi) wale waliokufuru; basi adhabu ilikuwa (kali) namna
gani".
Fatir - 25-26
b- KUFURU YA KUTOTII NA KUTAKABARI
Mfano wake ni mfano wa kufru ya Ibilisi, maana yeye
hajaikanusha amri ya Mwenyezi Mungu pale alipotakiwa asujudu wala hakuikataa,
(alikuwa akijua kuwa aliyetoa amri hiyo ni Mwenyezi Mungu), lakini aliikabili
amri hiyo kwa kutokutii na kwa kutakabari. Yeye ni mfano wa yule ajuwae kwamba
dini ya Kiislamu ni dini ya haki itakayomfaa hapa duniani na akhera, lakini
akaiacha na kufuata dini au madhehebu yaliotungwa na mwanadamu.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Na (wakumbushe watu habari hii) Tulipowaambia
Malaika: "Msujudieni Adam", wakamsujudia wote isipokuwa Iblisi
akakataa na akajivuna; na (tokea hapo) alikuwa katika makafiri".
Al Baqarah - 35
c- KUFRU YA KUKATAA KUFUATA
Nako ni kukataa kuyafuata yale aliyokuja nayo Mtume
(SAW), hata kama hakuyakubali wala hakuyakanusha, isipokuwa awe amekataa tu
kuyafuata.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule
anayekumbushwa aya za Mola wake akazikataa? Hakika sisi ni wenye kuchukua
kisasi kwa wale wabaya".
Sajda _22
d- KUFRU YA KUTIA SHAKA
Nako ni kutia shaka katika yale alokuja nayo Mtume
wa Mwenyezi Mungu (SAW) hata bila kutoa uamuzi wa kusadikisha wala
kukadhibisha.
Mwenyezi Mungu anasema;
"Na wakasema 'Hakika sisi tunakataa mliyotumwa
nayo na hakika sisi tunayo shaka ituhangaishayo kwa hayo mnayotuita' (Ya
kumwabudu Mungu mmoja)".
Ibrahim _9
e- KUFRU YA KUKANUSHA
Yote sawa ikiwa kukanusha mengi katika aliyoteremsha
Mwenyezi Mungu au kukanusha jambo moja tu katika yale yajulikanayo kuwa ni ya
lazima kuyaamini katika Uislamu.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Na wakazikanusha, na hali ya kuwa nafsi zao
zina yakini nazo; kwa dhuluma na kujivuna. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa
wafanyao ufisadi".
An Naml -14
Na akasema:
"Tunajuwa ya kwamba yanakuhuzunisha yale
wanayoyasema (katika kukutukana na kukukadhibisha). Basi wao hawakukadhibishi
wewe lakini madhalimu hao wanakanusha hoja za Mwenyezi Mungu (Mungu
atawalipa)".
Al An Aam -
33
PILI - SHIRKI NA AINA ZAKE
Mwenyezi Mungu anasema:
“Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa wale
waliokuwa kabla yako (maneno haya); ‘Kama ukimshirikisha (Mwenyezi Mungu) bila
shaka amali zako zitaruka patupu, (hutazipatia thawabu japo ni amali njema); na
lazima utakuwa miongoni mwa wenye hasara”.
Azumar – 65
Na akasema;
"Hakika Yeye hasamehe kushirikishwa; na
husamehe yasiyokuwa haya kwa amtakaye na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu bila
shaka amebuni dhambi kubwa".
An Nisaa - 48
Shirki haikubaliani na Imani, nayo ipo aina nyingi:
a- SHIRKI YA ANAYEMWAMINI MWENYEZI MUNGU LAKINI ANAMSHIRIKISHA NA MWENGINE KATIKA UFALME, KATIKA UWEZO WA KUFANYA ALITAKALO JUU YA VIUMBE, KATIKA KUUMBA, KUTOA MAISHA, RIZIKI, MAUTI, MADHARA NA MANUFAA
Shirki hii ni sawa na ile ya Manasara (Wakristo)
na Wamajusi, maana Manasara wanaamini
kwamba Mwenyezi Mungu amegawika sehemu tatu- Mwenyezi Mungu ametakasika na
kuepukana na hayo wayasemayo uepukano mkubwa kabisa - na Wamajusi wanaamini
kwamba Yeye ni wawili - Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wayasemayo.
Mwenyezi Mungu aliyetakasika anasema:
"(Mwenyezi Mungu) ambaye ni wake (peke yake)
ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuzaa mtoto wala hana mshirika katika ufalme
(Wake) na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo (chake)".
Al Furqan- 2
b- SHIRKI YA MTU KUJISIFIA MWENYEWE AU KUMSIFIA MTU MWENGINE KWA SIFA ZA UKAMILIFU
Hizi ni sifa ambazo hana mwengine isipokuwa Mwenyezi
Mungu peke Yake. Mfano wake ni mfano wa kauli ya Firauni aliposema:
"Mimi ndie Mola wenu mkuu (huyo Mola wa Nabii
Musa ni mdogo)".
An Naziat -24
Au kwa yule anayekanusha moja wapo ya sifa za
ukamilifu wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, mfano wa kauli ya Firauni:
"Na nani huyo Mola wa ulimwengu".
Ash Shuaraa -23
Au kauli ya
makafiri wa Kiquraishi kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
"Na wanapoambiwa 'Msujudieni Rahmani’; husema:
‘Ni nani Rahmani? Je! Tumsujudie unayetuamrisha wewe tu? 'Na maneno namna hii
yanawazidisha chuki".
Al Furqan - 60
Na akasema:
"Na wao wanamkufuru (Mwenyezi Mungu) Rahmani.Sema:
'Yeye ndiye Mola wangu, hakuna aabudiwaye (kwa haki) ila Yeye; nimemtegemea
Yeye na marejeo yangu ni kwake”.
Ar Raad - 31
c- SHIRKI YA KUMUABUDU ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU KWA NAMNA YO YOTE YA IBADA
Mwenyezi Mungu anasema:
"Mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe
na cho chote".
An Nisaa - 36
Na akasema:
"Sema: 'Je! Mnaniamrisha niabudu asiyekuwa
Mwenyezi Mungu enyi wajinga!".
Az Zumar - 64
Na akasema:
"Kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa wale
waliokuwa kabla yako (maneno haya): 'Kama ukimshirikisha (Mwenyezi Mungu) bila
shaka amali zako zitaruka patupu (hutazipatia thawabu japo ni amali njema) Na
lazima utakuwa miongoni mwa wenye hasara. Bali mwabudu Mwenyezi Mungu tu na uwe
miongoni mwa wenye kushukuru".
Az Zumar - 65-66
TATU - KUTOKA KATIKA DINI -"KUR-TADI"
MwenyeziMungu anasema:-
"Wala hawataacha kupigana nanyi, mpaka
wakutoeni katika dini yenu, kama wakiweza. Na watakaotoka dini yao katika
nyinyi, kisha wakafa hali ya kuwa makafiri, basi hao ndio ambao amali zao zimeharibika
katika dunia na akhera. Nao ndio watu wa Motoni. Humo watakaa milele."
(Al - Baqarah
-217).
Na "Murtadi" ni yule aliyeiacha dini ya
Kiislamu akiwa na akili timamu, amejiamulia mwenyewe bila kulazimishwa na mtu
kuingia katika dini nyingine kama vile Ukristo
au dini ya Kiyahudi au kutokuwa na dini kama vile Ukoministi au hata
akakanusha jambo lolote lile lijulikanalo kama ni la lazima katika dini kama
vile kuwajibika Kusali, Kutoa zaka au akafanya jambo dhidi ya Uislamu au dhidi
ya sheria zake zilizo dhahiri au akatamka kauli ambayo haina tafsiri nyengine
isipokuwa kukufuru.
NAMNA GANI HUPATIKANA KUR-TADDI (KUTOKA KATIKA DINI)
A - KUR-TADDI KWA ITIKADI NAYO NI KAMA IFUATAVYO:-
1- Maulamaa
wote wa Kiislamu wamekubaliana kwamba yeyote anayemshirikisha MwenyeziMungu au
kumpinga au akakanusha moja wapo ya sifa zilizothibitika katika sifa Zake
ikijulikana wazi kuwa mtu huyo lazima anazielewa vizuri sifa hizo, au
amsingizie Mwenyezi Mungu jambo ambalo Yeye mwenyewe amelikanusha, mfano; kuwa
na mtoto, au kukanusha kuwepo kwa Malaika au vitabu au Mitume au kuikanusha
Siku ya Kiama au Qadari kheri yake na shari yake au akatae jambo lolote
lijulikanalo kwamba ni la lazima katika dini,
basi mtu huyu huwa ni Murtadi, kafiri (ametoka katika dini).
2- Inajulikana
kwamba anahesabika kuwa Murtadi, Muislamu yeyote anayeipinga au kuikanusha
Qurani yote, au sehemu yoyote ya Qurani au hata aya moja katika aya za Qurani.
Huhesabiwa kuwa amertadi pia, yule mwenye itikadi kwamba Qurani inakhitalifiana
yenyewe kwa yenyewe au ina khitilafu ndani yake au kuwa na shaka katika miujiza
yake au kujigamba kuwa ana uwezo wa kuleta mfano wake, na pia mwenye kuivunjia
heshima yake(Qurani), au kuongeza au kupunguza ndani yake.
3-
Anahesabiwa kuwa kafiri Aliyertadi, mwenye kuitakidi kwamba Mtume (SAW)
amesema uwongo katika baadhi ya aliyokuja nayo, na pia yule anayeitakidi kuwa
ni halali jambo lolote liloharamishwa kama vile kuzini kunywa pombe n.k.
B- KURTADI KWA MATAMSHI, KAMA IFUATAVYO:
1- Anayeapa
kwa mila nyengine isiyokuwa ya Kiislam.
Ameelezea
Thabit bin Dha-Haak kwamba Mtume (SAW) amesema:-
"Atakaekula kiapo kwa mila isiyokuwa ya
Kiislamu (kwa mfano akadai kwamba yeye ni mkristo ilihali uwongo) basi anakuwa
kama alivyosema".
(Mfano wake ni baadhi ya watu wanaopenda kuwaiga
wazungu katika kula kiapo kwa kusema; ‘Yesu kristo’ au kwa lugha yoyote ile,
viapo vya aina hiyo).
(Imetolewa na wote isipokuwa Abu Daud).
Na kutoka kwa Buraida(RA), ameeleza kuwa Mtume (SAW)
amesema:-
"Atakayesema; ‘Mimi si Muislam’, ikiwa anasema uwongo basi kama
alivyosema na ikiwa anasema kweli basi hatorudi katika Uislamu akiwa
amesalimika".
(Abu Daud , Annasai na Ibn Majah ).
2- Atakae
mtukana Mwenyezi Mungu au akaitukana Qurani au akamtukana Mtume (SAW) au moja
wapo wa Mitume ya Mwenyezi Mungu, basi anakuwa amekufuru japo kuwa amesema kwa
mzaha au kweli au kwa istihizai.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kama ukiwauliza (kwa nini wanaifanyia mzaha
dini)? Wanasema; "Sisi tulikuwa tukizungumza zungumza na kucheza
tu." Sema; "Mlikuwa mkimfanyia
mzaha MwenyeziMungu na Aya zake na Mtume wake?
"Msitoe udhuru (wa uwongo) umekwisha kudhihiri
ukafiri wenu (mlokuwa mkiuficha) baada ya kule kuamini kwenu (kwa
uwongo)."
(At - Tawba - 65 - 66)
3- Maulamaa
wote wamekubaliana kuwa kila atakaemsingizia uwongo bibi Aisha (RA) katika kile
kisa cha uwongo alichozuliwa (hadithi ya "Al-Ifki") wakati
MwenyeziMungu kishamtakasa basi anakuwa si Muislamu tena.
MwenyeziMungu anasema:-
"Hakika wale walioleta uwongo huo (wa
kumsingizia bibi Aisha(RA) mkewe Mtume(SAW) kuwa amezini)) Ni kundi miongoni
mwenu (ni jamaa zenu) msifikiri ni shari kwenu bali hiyo ni kheri kwenu. Kila
mtu katika wao atapata aloyachuma katika madhambi yao na yule aliyejitwika
sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa (zaidi).
Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na
wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa
hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na
rehema yake katika dunia na
Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa
kwa sababu ya yale mliyo jiingiza.
Mlipoupokea (uwongo huo mkawa mnautangaza) kwa ndimi
zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe
mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa.
Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii
kuzungumza haya. Subhaanaka (Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?
Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirudi kabisa (msirejee
tena) kufanya kama haya, ikiwa nyinyi ni Waumini! (Waislamu) kweli.”
An Nur– 11-17
Kwa hivyo atakaerudia kueneza uwongo huo hatakuwa
Muislamu tena.
4- KUITUKANA DINI
Yeyote atakayeituhumu, kuishambulia au kuitukana
dini ya MwenyeziMungu au kuwataka watu wafuatae siasa ya kutoamini Mungu au
kuwataka wakufuru basi anakuwa Murtadi.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi
kwao na wakatukana dini yenu, basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri. Hakika
viapo vyao havina maana wauweni (piganeni nao) ili wapate kujizuia (na kufanya
ubaya wao).”
(At - Tawba -12)
"KUR-TADI" KWA VITENDO, NAYO NI KAMA IFUATAVYO:
1- Maulamaa
wa Kiislamu wote wamekubaliana kuwa amefanya kitendo cha kurtaddi Muislamu
yeyote atakayeutupa msahafu mahala panapotupwa taka, au kuuchafua (kwa
kukusudia) kwa kuumwagia taka, na pia kuvifanyia hivyo hivyo vitabu vya hadithi
za Al Qudusiy au vya hadithi za Mtume (SAW) na pia atakayeufanyia dharau
msahafu.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na kama ukiwauliza (kwa nini?) Wanasema;
"Sisi tulikuwa tukizungumza zungumza na kucheza tu, Sema; "Mlikuwa
mkimfanyia mzaha MwenyeziMungu na aya zake na Mtume wake?".
(At - Tawba -65)
2- Wamekubaliana Maulamaa
kwamba Mwislamu yeyote akilisujudia sanamu, juwa au mwezi au akasema neno au
kufanya kitendo kinachoonesha wazi kuwa kaifanyia istihizai dini, basi anakuwa
ametoka katika dini ‘Amertadi’.
3- Mwislamu
yeyote atakayekimbilia nchi ya makafiri wanaowapiga vita Waislamu na akaungana
nao katika kupigana vita hivyo dhidi ya Waislamu, basi kesha kuwa kafiri, na
hii ni kutokana na kauli ya MwenyeziMungu isemayo:
"Na miongoni mwenu atakayefanya urafiki huo
nao, basi huyo atakuwa pamoja nao.
Hakika MwenyeziMungu hawaongozi (njia ya kheri
watu madhalimu)."
(Al - Maidah -51).
Mtume(SAW) pia amekataza kufanya hivyo na akajiweka
mbali na aina hiyo ya watu.
4- Mwislam
yeyote atakayeipiga vita sheria ya Kiislamu na akaibadilisha kwa kanuni za
wanadamu kwa nia ya kuizuia sheria ya Kiislamu isitumike, basi amekuwa kafiri.
MwenyeziMungu anasema:-
"Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha
MwenyeziMungu basi hao ndio
makafiri".
(Al - Maidah - 44)
NNE- UNAFIKI
Unafiki
ni mtu kujidhihirisha mbele ya Waislamu kuwa na Imani kama yao, na kujifanya
kama mwenzao, wakati moyoni mwake ni kafiri anayeukadhibisha Uislam.
Katika
itikadi ya Kiisilamu, Unafiki ni kufru, isipokuwa mnafiki hatendewi kama
anavyotendewa kafiri kwa sababu ya kutoudhihirisha ukafiri wake.
MwenyeziMungu
anasema:
“Wanapokujia
wanafiki, husema; "Tumeshuhudia kwa yakini wewe ni Mtume wa
MwenyeziMungu". Na MwenyeziMungu anajua kuwa wewe ni Mtume wake na
MwenyeziMungu anashuhudia ya kuwa hakika wanafiki ni waongo. (wanasema
wasiyoyasadiki)."
Al -
Munafiqoun - 1
Na
anasema:
“Na
hayo ni kwa kuwa waliamini kisha wakakufuru; kwa hivyo muhuri umepigwa juu ya
nyoyo zao; kwa hivyo hawafahamu lolote".
Al -
Munafiqoun - 3
Na upo Unafiki wa Vitendo ulio
tofauti na ule wa Unafiki wa Imani, kwa mfano;
Kufanya
khiyana katika amana, kusema uongo au kutotekeleza ahadi (kuvunja ahadi).
Huyu
mnafiki wa vitendo hahisabiwi kuwa ni kafiri, lakini huhisabiwa kuwa ni
"fasiki” mtenda maasi na anayo
sehemu ya unafiki moyoni mwake.
SIFA ZA WANAFIKI
Miongoni
mwa sifa maarufu za wanafiki ni hizi zifuatazo:
A- KUFANYA UFISADI ULIMWENGUNI KWA KUIPIGA VITA SHERIA YA MWENYEZIMUNGU NA KUWATUHUMU WAISLAMU KUWA NI WAPUMBAVU
MwenyeziMungu akiuelezea wasfu wa wanafiki wa aina
hii anasema:
“Na
wanapoambiwa "Msifanye uharibifu ulimwenguni”, Husema; "Sisi ni
watengenezaji”. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui, na
wanapoambiwa; "Aminini kama
walivyoamini watu", Husema; "Oh! tuamini kama walivyoamini
wapumbavu?" Hakika wao ndio wapumbavu lakini hawajui."
Al
Baqarah 11-13
B- KUWAFANYIA HADAA WAISLAMU KWA KUJIONESHA MBELE YAO KUWA WAO NI WAISLAMU KISHA KUUDHHIRISHA UKAFIRI WAO MBELE YA MABWANA ZAO
MwenyeziMungu
anasema:
“Na
wanapokutana na walioamini husema; "Tumeamini", na wanapokuwa peke
yao kwa mashetani wao husema; "Hakika tu pamoja nanyi, tunawacheza shere
tu".
Al -
Baqarah – 14
KUPINGA KUHUKUMU KWA SHERIA YA MWENYEZIMUNGU NA KUWAZUIA WATU WASIZITUMIE SHERIA ALOZITEREMSHA MWENYEZI MUNGU
MwenyeziMungu
anasema:
“Huwaoni
wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa kabla
yako? Nao wanataka wakahukumiwe kwa njia isiyowafiki sheria; na hali
wameamrishwa kukataa njia hiyo. Na
shetani anataka kuwapoteza upotofu (upotevu) ulio mbali (na haki). Na wanapoambiwa; "Njooni katika yale
aliyoyateremsha MwenyeziMungu na (njooni) kwa Mtume", utawaona wanafiki
wanajiweka mbali nawe kabisa".
An -
Nisaa -60 - 61
D- KUAMRISHA MAOVU NA KUKATAZA MEMA
MwenyeziMungu
anasema:
“Wanaume
wanafiki na wanawake wanafiki wote ni hali moja, huamrisha yaliyo mabaya na
kukataza yaliyo mazuri na kuizuilia
mikono yao (hawasaidii mambo ya kheri). Wamemsahau MwenyeziMungu (wamepuuza
amri zake) na Yeye pia amewasahau (amewapuuza). Hakika wanafiki ndio wavunjao
amri".
At -
Tawba -67
E- KUWAFANYA MAKAFIRI KUWA MARAFIKI BADALA YA WAISLAMU
MwenyeziMungu
anasema :
“Waambie
wanafiki kwamba watapata adhabu inayo umiza, (wanafiki) ambao huwafanya
makafiri kuwa marafiki badala ya Waislamu,.. Jee! wanataka wapate utukufu kwao?
Basi utukufu wote ni wa MweyeziMungu.(hauko katika mkono wa mtu)."
An -
Nisaa -138 - 139
F- KUWAFANYIA UADUI WAISLAMU KWA AJILI YA IMANI YAO NA KUFANYA URAFIKI NA MAKAFIRI KWA UKAFIRI WAO
Anayefanya
urafiki na makafiri akawapenda na kuzitetea itikadi zao za kikafiri, huyo
atakuwa amekwishaiharibu imani yake:
MwenyeziMungu
anasema:
“Huwapati
(huwaoni) watu wanaoamini MwenyeziMungu na Siku ya mwisho, kuwa wanawapenda
wale wanaompinga MwenyeziMungu na Mtume
wake; hata wakawa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao."
Al -
Mujadilah - 22
Anayewafanyia
uadui Waislamu kwa kuwapiga vita, kuwachukia na akawanusuru maadui wao dhidi
yao kwa ajili ya imani yao, basi amekwishavunja imani yake.
MwenyeziMungu
anasema:
“Nao
hawajaona baya lolote kwa (Waislamu) ila kumuamini MwenyeziMungu Mwenye
kushinda (na) Mwenye kusifiwa.
Ambaye
ni Mwenye Ufalme wa mbingu na ardhi, na MwenyeziMungu ni Mwenye kuona kila kitu.
Hakika
wale waliowaadhibu Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, kisha wasitubie basi
watapata adhabu ya Jahannam na watapata adhabu ya kuungua (barabara)".
Al -
Buruj - 8 – 10
Wanafiki
hawa Siku ya kiama watakuja kujuta kwa sababu ya dharau yao na stihizai zao juu
ya Waislamu.
MwenyeziMungu
anasema:
“Bila
shaka kulikuwa na kundi katika waja wangu likisema; "Mola wetu! Tumeamini,
basi tusamehe na turehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanaorehemu.”
Lakini
nyinyi mliwafanyia stihizai hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa
mkiwacheka.
Hakika
leo ninawalipa (Pepo) kwa sababu ya kusubiri kwao bila shaka hao ndio wenye
kufuzu.”
Al -
Muuminun - 110 – 112
UJINGA WENYE HATARI
WAISLAMU LAKINI WAJINGA
Ujinga
wa kutoijua dini ya MwenyeziMungu umeenea
sana katika nchi za Kiislamu, hata anapatikana
Mwislamu mwenye Kuishahidia shahada ya; Laa Ilaha illa Llah, Muhammad Rasulu
Llah’, akasimamisha Sala na kutoa Zaka na kufunga mwezi wa Ramadhani, aka Hiji
Maka na akaamini yote yaliyomo ndani ya Qurani na akampenda Mtume (SAW) na
kumsadiki na Kuionea uchungu dini ya Kiislam, lakini juu ya yote hayo, utamuona
anafanya vitendo na kusema maneno na kuwa na itikadi zinazomfanya awe katika
Kufru au Shirki au Unafiki bila ya kuuelewa uhakika wake. Bali huenda akawa
anadhani kuwa hali hiyo aliyokuwa nayo ya shirki au kufru au unafiki kuwa ni
sawa na yenye kumridhisha Mwenyezi Mungu.
Yeye
ni Mwislamu mwenye kuionea uchungu dini yake,
lakini ameingia katika Kufru au Shirki kwa sababu ya ujinga wake ambao huenda
ukamtia katika adhabu ya Moto.
MJINGA ANASAMEHEKA, LAKINI NI WAJIBU WAKE KUJIFUNZA NA KUIFUATA HAKI PALE ITAKAPOMBAINIKIA
Mtu akishaingia katika Uislamu na
kumthibitikia Uislam, basi huendelea kuwa hivyo na hakimtowi katika Uislamu
kitendo chochote isipokuwa akitenda moja wapo ya yale mambo yenye kuiondoa sifa
ya Imani (yaliyokwishatajwa hapo mwanzo) tena atende jambo hilo kwa kusudi
akiwa na nia ya Kurtadi. Kwa sababu Nia ni sharti muhimu ili kitendo chochote
kikubaliwe na kuhesabiwa.
Kwa
hivyo mtu anapotenda kitendo chochote cha shirki au cha kufru kinachomuodolea
sifa za mwenye Imani, akiwa hakusudii kuibatilisha imani hiyo, basi mtu huyo
anasameheka, lakini inamwajibikia kujifunza yaliyo sahihi na kutubia sana.
Wanafunzi
wa Nabii Issa (AS) kutokana na ujinga wao walimuuliza Mtume wao huyo kama
ilivyonukuliwa katika Qurani. Mwenyezi Mungu anasema:
"(Kumbuka)
wanafunzi (wako) waliposema: "Ewe Issa mwana wa Maryam! Jee Mola wako
anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?" (Nabii Issa) Akasema;
"Mcheni MwenyeziMungu kama nyinyi ni wenye kuamini kweli."
(Al -
Maidah - 112)
Kwa
suala lao hilo, walionesha ujinga wao wa kutokujua kwamba MwenyeziMungu ni
Muweza wa kila jambo, na Mwenye kukanusha uwezo wa MwenyeziMungu anakuwa
kafiri, lakini kwa sababu ya ujinga wao huo, kumekuwa ni udhuru kwao mbele ya
MwenyeziMungu na Mtume wake (AS).
Na
Mtume (SAW) alipotoka pamoja na Sahaba zake(RA) kuelekea Khaybar, walipita
mahali penye mti uliokuwa umetundikwa vitu vilivyo kama hirizi juu yake, mahala
ambapo makafiri (Washirikina) walikuwa wakitundika panga zao wakati wa vita
wakiwa wanaamini kwamba hirizi hizo zanawasaidia katika ushindi vitani. Baadhi
ya Waislamu wakamuambia Mtume (SAW): "Tufanyie na sisi mti ulio na hirizi
kama waliokuwa nao makafiri."
Mtume
(SAW) akawambia:
<<Subhana
Llah! Maneno haya ni kama yale waliyosema watu wa Nabii Musa:
"Tufanyie
Mungu na sisi (yaani masanamu) kama wao walivyo na miungu>>.
(Al -
Aaraf - 138)
Mtume
(SAW) akaendelea kusema:
<<Naapa
kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, mtakuja fuata mwenendo wa
waliokuja kabla yenu.(Manasara na Mayahudi).>>
Imam
Ahmed na Attirmidhy
Waliouliza
masuala haya mawili kwa Musa na Muhammad (AS) kwa ujinga wao walifanya makosa
yanayoingiza katika shiriki, lakini jawabu ya Mtume (SAW) lilikuwa;
"Mtakuja
fuata mwenendo wa waliokuja kabla yenu"
Na
jawabu ya Musa (AS) lilikuwa:-
"Hakika
nyinyi ni watu mfanyao ujinga."
(Al -
Aaraf - 138)
Hakusema
yeyote kati ya Isa au Musa au Muhammad (Alayhimu Ssalaatu Wassalaam) kuwaambia
watu wao hao waliokufuru kwa ujinga wao
pamoja na kumshirikisha kwao MwenyeziMungu (bila kukusudia), kuwa wao ni
Makafiri au Washirikina.
MwenyeziMungu
anasema:
"Wala
si lawama juu yenu mkikosa, lakini (kuna lawama) katika yale ziliyoyafanya
nyoyo zenu kwa kusudi, na MwenyeziMungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa
Kurehemu ."
Al -
Ahzab – 5
HAPANA UDHURU KWA YEYOTE YULE BAADA YA KUELIMIKA
Ikiwa
mambo yamekuwa ni ya hatari kiasi hiki, basi inawapasa Maulamaa kuwabainishia
watu dini ya MwenyeziMungu na inampasa kila aliyefanya makosa katika Kukufuru
au kufanya kitendo cha Ushirikina bila ya kujua, afanye juhudi ya kutubia.
MwenyeziMungu
akitujulisha juu ya Maulamaa wanaoficha (mafundisho ya) dini ya MwenyeziMungu
anasema:-
"Hakika
wale wanaoficha tuliyoyateremsha - nazo ni hoja zetu zillizo wazi na uwongozi,
baada ya sisi kuzibainisha kwa watu kitabuni - hao anawalani MwenyeziMungu, na
anawalani (kila) mwenye kulani.
Ila
wale waliotubu na kutengeneza na kubainisha (yale waliokuwa wakiyaficha), basi
hao nitawapokea, na mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye rehema".
(Al -
Baqarah - 159)
Kisha
Mwenyezi Mungu akasema juu ya wale wanaoshikilia kwenda kinyume na dini ya
Mwenyezi Mungu pamoja na kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wake(SAW),
wakishikilia kufuata njia isiyokuwa ya Kiislamu hata baada ya kuwafikia
uongofu:
"Na
atakayemuasi Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu na akafuata njia isiyokuwa ya
Waislamu, tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na tutamuingiza katika Jahannam; napo
ni pahali pabaya kabisa kwa mtu kurudia".
An
Nisaa - 115
AINA MBALI MBALI ZA SHIRKI
KUMSHIRIKISHA MWENYEZI MUNGU KATIKA KUZIENDESHA HALI ZA VIUMBE
Kila
anayeamini kwamba yupo mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wa
kubadilisha hali yoyote ile katika dunia hii na kwamba ana uwezo wa kudhuru au
kunufaisha kwa njia za ghaibu na sio kwa njia za kikawaida alizowakadiria
Mwenyezi Mungu viumbe vyake. Kwa mfano akaamini kwamba mtu katika walio hai au
waliokufa anao uwezo wa kumjaalia akapata watoto au anaweza kujibu dua ya
mwenye dhiki au kuleta mvua au kuzilinda nyumba au wanyama au watoto au Bwana
na Bibi arusi kwa nguvu zilizojificha zenye uwezo wa kudhuru, basi anakuwa
amekwisha fanya kitendo cha Shirki.
Mwenyezi
Mungu amesema akijielezea Mwenyewe:
"Ufalme
wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu, Anaumba Apendavyo, Anampa Amtakaye
watoto wa kike na Anampa Amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya (watoto) wa
kiume na wa kike (kwa mtu mmoja), na Humfanya tasa Amtakaye; hakika Yeye ni
Mjuzi, Muweza".
Ash -
Shura -49-50
Na
anasema:
"Au
Yule anayemjibu anayedhikika amwombapo na kuondoa dhiki (yake) na kukufanyeni
wenye kuendesha dunia (siye bora?) Je, yuko Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni
kuchache kuwaidhika kwenu".
An
Naml - 17
Na
anasema:
"Na
kama Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara (taabu) basi hakuna ye yote awezaye
kuyaondoa ila Yeye; na kama akikugusisha kheri (hakuna wa kuweza kuiondoa ila
Yeye tu peke yake).Yeye ndiye Mwenye Uweza juu ya kila kitu".
Al An
Am - 17
Na pia
Mwenyezi Mungu anasema:
"Sema
'Mwaonaje, kama maji yenu yakiwa yamezama, (yamedidimia chini) basi nani
atakuleteeni maji (safi) yatiririkayo? (Ni Yeye tu Mwenyezi Mungu; basi
muabuduni Yeye tu)".
Al
Mulk - 30
Na pia
anasema:
"Anauwingiza
usiku katika mchana na kuuingiza mchana katika usiku, na amevitiisha jua na
mwezi vyote (vinakwenda mchana na usiku) mpaka muda maalum ufike.Huyo ndiye
Mwenyezi Mungu, Mola wenu, Mwenye Ufalme; na wale mnaowaabudu kinyume chake,
wao hawamiliki hata utando (ngozi) wa kokwa ya
tende".
Fatir
– 13
AINA MBALI MBALI ZA SHIRKI KATIKA IBADA
1- KUTOA SEHEMU YA RIZIKI KWA AJILI YA MWENGINE ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU
Yule
anayetoa samli au asali au chembe chembe za nafaka kwa ajili ya baadhi ya miti
au mawe au makaburi, na ye yote anayetoa nyama au maziwa kwa ajili ya majini,
au ye yote ambaye huchinja mwana wa mwanzo wa ng'ombe wake au mbuzi, kama ni
nadhiri kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Na Yule ambaye huvunja
yai au kuchinja mnyama mbele ya bwana na bibi harusi kwa ajili ya kuwaridhisha
majini, au kuchinja kondoo kila mwaka au hata mara moja ili kuilinda nyumba
yake au kisima chake; ye yote afanyaye hayo anakuwa amefanya kitendo cha
shirki, kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Na
neema yo yote mliyonayo basi imetoka kwa Mwenyezi Mungu. (Na nyinyi
hamumshukuru). Kisha inapokuguseni dhara mara Yeye mnamlilia (mnamlalamikia).
Kisha
anapokuondoleeni hiyo dhara, mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha
(tena) Mola wao.
Wanazikataa
zile neema tulizowapa. Basi stareheni kidogo. Karibuni hivi mtajua (ubaya
wenu).
Na
sehemu ya vile tulivyowaruzuku, wanawawekea (waungu wao) wasiofahamu
(wanayofanyiwa). Wallahi! Bila shaka nyinyi mtaulizwa juu ya yale mliyokuwa
mkiyazua".
An
Nahl - 53-56
Na
anasema:
"Na
wamemfanyia Mwenyezi Mungu sehemu katika mimea aliyoiumba (mwenyewe) na katika
wanyama aliowaumba (Mwenyewe) husema 'Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu' Kwa
madai yao (tu) 'Na hii ni ya (wale) tunaowashirikisha na Mungu', basi vile
walivyowakusudia waungu wao havifiki kwa Mwenyezi Mungu na vilivyokuwa vya
Mwenyezi Mungu hivyo hufika kwa waungu wao. Ni mabaya kabisa
wanayoyahukumu".
Al An
am - 136
Wanaingia
katika kundi hili pia wale ambao yanapon’goka meno yao hulitaka jua au
(kunguru) lichukuwe jino bovu na kumpa jino zuri badala yake.
KUCHINJA KWA AJILI YA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU
Atakayechinja
katika sehemu maalum kama vile chini ya mti, sokoni, kaburini n.k. (kwa nia ya
kutaka kujikurubisha na miti, masoko au maiti ‘Mawalii’) ni sawa na
uchinjaji wa wakati wa Jahilia (kabla ya
kuja kwa Mtume (SAW)) maana Mushrikina walikuwa wakichinja kwa ajili ya kafara
walizokuwa wakiwatolea masanamu yao.
Na
atakaejikurubisha kwa kuchinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu
basi amekwisha fanya kitendo cha shirki, kwa sababu kuchinja ni ibada.
Mwenyezi
Mungu anasema:
"Hakika
tumekupa kheri nyingi. Basi Sali kwa ajili ya Mola wako na uchinje (kwa ajili
ya Mola wako)”.
AL
Kauthar - 1-2
Na
akasema:
"Sema
'Hakika Sala yangu na ibada zangu (zote nyengine) na uzima wangu na kufa kwangu
(zote) ni kwa Mwenyezi Mungu. Muumba wa walimwengu. Hana mshirika wake. Na haya
ndio niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha kwa (Mwenyezi
Mungu)".
Al An
Am - 162-163
Imelezwa
na Imam Ali ibn Abi Talib(RA), kutoka kwa Mtume (SAW) kwamba:
<<Mwenyezi
Mungu amemlaani kila anayechinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Mwenyezi
Mungu>>.
Katika
baadhi ya nchi, watu wanaostahiki kupewa sadaka hukusanyika mwahali maalum
ambapo watu huamini kuwa ni patakatifu kwa ajili ya mzimu au Walii aliyezikwa
hapo n.k. Basi inapombidi mtu kuchinja na kugawa nyama katika sehemu za
mikusanyiko ya watu wa aina hiyo, (badala ya kwenda penye mizimu hiyo au
makaburi hayo na kuchinja katika sehemu hizo) ni bora ampeleke mnyama huyo
akiwa mzima na kuwapa wale wanaostahiki ili wachinje wenyewe, na kwa njia hii
huwa kuchinja huko si kwa ajili ya ye
yote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na kwa vyo vyote vile haijuzu kukusanyika watu
katika mikusanyiko kama hiyo.
3- KUOMBA DUA KWA MWENGINE ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU
Mwenyezi
Mungu Mtukufu amebainisha kwamba dua ni ibada, katika kauli yake:
"Na
Mola wenu anasema 'Niombeni nitakujibuni. Kwa hakika wale wajivunao kufanya
ibada Yangu bila shaka wataingia Jahannam wadhalilike".
Ghaafir
- (Al Muumin - 60)
Na
Mtume (SAW) pia alibainisha haya pale aliposema:
"Dua
ndio ibada".
Imepokelewa
na Ahmed na Attirmidhiy
Kwa
hivyo ye yote yule atakayemuomba mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu awe ni Malaika
aliyetukuzwa au Mtume aliyetumwa au Walii katika wacha Mungu au Jini katika
mashetani au mtu ye yote aliye hai au aliyekufa, anakuwa ametenda kitendo cha
shirki.
Mwenyezi
Mungu anasema:
"Na
(nikaambiwa): 'Wala usiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wale ambao hawakufai
(unapowaabudu) wala hawakudhuru (unapowacha kuwaabudu) basi ukifanya utakuwa
miongoni mwa madhalimu wa (nafsi zao).
Na
kama Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara basi hakuna ye yote awezaye kuiondoa
isipokuwa Yeye (Mwenyewe). Na kama akikutakia fadhila zake (Mwenyezi Mungu)
huzifikisha (fadhila hizo) kwa amtakaye katika waja wake. Naye ni Mwingi wa
kusamehe (na Mwingi wa Kurehemu)".
Yunus
- 106-107
Na
akasema:
"Hakika
wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja (watumwa) kama nyinyi. Hebu
waiteni, nao wakuitikieni ikiwa mnasema kweli".
Al
Aaraf - 194
Na pia
anasema:
"Sema
'Waiteni wale mnaodai (kuwa ni waungu) mkamwacha Yeye (ili akuondosheeni baa
zinazokufikieni) hawataweza kukuondosheeni shari wala kubadilisha (kuwa kheri).
Hao
wanaowaomba (wenyewe) wanatafuta ukaribiano na Mola wao; (hata) walio karibu
sana miongoni mwao (kama Malaika) wanatumai rehema Zake na wanaogopa adhabu.
Hakika adhabu ya Mola wako ni ya kuogopwa".
Israa
(Bani Israil) -56-57
4- KUHUKUMU KWA SHERIA NYENGINE BADALA YA SHERIA YA MWENYEZI MUNGU
Atakayeiacha
sheria ya Mwenyezi Mungu na kuikataa kwa ajili ya kufuata sheria iliyotungwa na
binadamu au iliyopangwa na kukubaliwa na watu na ikapingana na sheria ya
Mwenyezi Mungu basi anakuwa amemwabudu mwengine badala ya Mwenyezi Mungu kwa
sababu kuhukumu ni ibada.
Mwenyezi
Mungu anasema:
"Haikuwa
hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu, ameamrisha msimwabudu ye yote isipokuwa Yeye,
hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui".
Yusuf
- 40
Na
kuhukumu huko (kinyume na sheria ya Mwenyezi Mungu), hugeuka kuwa ni kuhukumu
kwa sheria ya shetani.
MwenyeziMungu
anasema:-
"Huwaoni
wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yaliyoteremshwa
kabla yako? Nao wanataka wakahukumiwe kwa njia isiyowafiki sheria; Na hali
wameamrishwa kukataa njia hiyo. Na shetani anataka kuwapoteza upotofu (upotevu
) ulio mbali (na haki)".
(An -
Nisaa - 60)
Na
akasema Subhanahu Wataala :
"MweyeziMungu
ni mlinzi wa wale walioamini. Huwatoa katika giza na kuwatia katika mwangaza.
Lakini waliokufuru, walinzi wao ni mashetani. Huwatoa katika mwangaza na
kuwaingiza katika giza. Hao ndio watu wa motoni humo watakaa milele".
(Al -
Baqarah - 257)
5- KUHALALISHA MAOVU NA KURIDHIKA KWA KUENEA KWAKE
Wale
wanaoridhika waziwazi na (pia) wanaoridhika kwa kificho nyoyoni mwao juu ya
kuenea kwa uovu, wakiuhalalisha uovu huo wanakuwa ni makafiri waliozipoteza
imani zao, hata wakijigamba kuwa eti wao ni Waislamu.
Itakuwaje
mtu ayakubali maovu (na maasi) na kuyapenda pamoja na kuyahalalisha kisha ajinasibishe na Uislamu huku akiwa anaona ni
halali akapenda pamoja na kuridhika kwa wanawake kutembea uchi (majiani),
masokoni, na katika mikusanyiko mbali mbali ya pamoja.
Kisha
aridhike kuwepo kwa mchanganyiko wa wanaume na wanawake katika sura hii huku
akijistarehesha nafsi yake kwa (kutizama) yaliyo ya haramu.
Au
mfano wa yule anaezitukana jamii za Kiislamu zinazojihifadhi kwa kufuata
maamrisho ya Kiislamu, akawakejeli na kuwatuhumu kuwa ni watu wasiostaarabika
na wasioendelea, na kuwapa kila sifa za upungufu, kisha akawa anaogopa kila
wanapoelezwa watu juu ya wajibu wa kuhukumu kwa kitabu cha MwenyeziMungu
Aliyetukuka, na hofu yake kubwa ni kuogopa yasije yakatoweka matamanio yake
haya yaliyoharamishwa, au kupigwa vita pombe.
Kwa
watu wa aina hii inasadikisha kauli ya Mtume wa MwenyeziMungu(SAW) aliposema:
<<Kila
Mtume aliyeletwa na MwenyeziMungu katika umma kabla yangu, alikuwa nao (katika
umma wake) Wanafunzi na Masahaba wanaoigiza mwenendo wake na kufuata amri zake.
Kisha huzaa baada yao vizazi wanaosema wasiyotenda na wanatenda wasiyoamrishwa.
Basi atakaepambana nao kwa mikono yake anakuwa ni mwenye Imani(Muislam wa
kweli) na atakaye pambana nao kwa ulimi wake anakuwa ni Mwenye imani, na atakae
pambana nao kwa moyo wake anakuwa ni Mwenye imani, na hakuna imani tena baada
ya hayo hata yenye uzito wa punje ya Hardali>>.
Muslim
na Ahmad na imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas
6- KUJIGAMBA KUJUA ELIMU YA GHAIBU
Yeyote
atayejigamba kuwa yeye au mwengine yeyote anajua elimu ya Ghaibu, basi atakuwa
amefanya kitendo cha Shirki na cha Kufru.
MwenyeziMungu
anasema:-
"Yeye
ndie Mjuzi wa siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake isipokuwa Mtume wake
aliyemridhia."
(Al -
Jinn - 26 - 27)
Na
akasema pia:
"Na
ziko kwake (MwenyeziMungu tu) funguo za siri; hakuna azijuae ila Yeye”.
(Al -
An - Am - 59)
MwenyeziMungu
pia akasema kwa kumfundisha Mtume wake (SAW) aseme:
"Sema;
"Sina mamlaka ya kujipa nafuu wala ya kujiondolea madhara ila apendavyo
MwenyeziMungu; na lau kama ningelijua Ghaibu ningejizidishia mema mengi; Wala
isingalinigusa dhara; mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoaji wa habari
njema kwa watu wanaoamini".
(Al -
Aaraf - 188)
Huu ni
mtihani mdogo MwenyeziMungu anawafedhehesha nao wale wanaojigamba kuwa wanajua
Ghaibu, nao ni kuwataka waijue biashara yenye faida na waifanye biashara hiyo,
ndipo watakapotajirika, au waelewe yale masaibu watakayopambana nayo ili
wajiepushe nayo.
Wanaingia
katika kundi hili wachawi na wapiga ramli kutokana na yale wanayoyafanya.
Mtume
(SAW) amesema:
<<Atakayemuendea mchawi na kumsadiki
ayasemayo, basi kesha yakufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad>>.
Imetolewa
na Ahmad na Al Tirmidhiy na Abu Daud na Al Nasai na Ibn Majah
Na
katika baadhi chache ya habari za kweli wanazotamka wapigaji ramli na wachawi
na mambo yenyewe ni nadra kutokea, huyapata kutoka kwa majini ambao huchanganya
ukweli mmoja pamoja na uongo tisini na tisa.
Na
wale wenye uwezo wa kuwasiliana na majini (na mashetani) ni watu wabaya kabisa.
MwenyeziMungu
anasema:-
"Jee!
Nikwambieni ambao mashetani wanawateremkia? Wanateremka juu ya kila mzushi
mkubwa mwenye madhambi (shetani hawateremkii watu wazuri) wanawapelekea (hao
wanaowafuga) yale wanayoyasikia (na wakaongeza yao ya uongo mtupu) na wengi
katika hao ni waongo".
As -
Shuaraa - 221 - 223
UCHAWI NA HADAA
Atakayefanya uchawi na kuomba kwa majina ya
mashetani, akapiga mafundo na kuvaa au kutundika hirizi ambazo huandikwa majina
ya majinni na akafanya uchawi ili mtu na mkewe wapendane au wachukiane basi
anakuwa keshafanya kitendo cha kufru.
MwenyeziMungu
anasema:
"Wakafuata
yale waliyoyafuata mashetani (wakadai kuwa yalikuwa) katika ufalme wa (Nabii)
Sulaiman; na Sulaiman hakukufuru bali mashetani ndio waliokufuru,
wakiwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakijua wenyewe tangu zamani) na (uchawi)
ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruta na Maruta, katika (mji wa) Babil. Wala
(Malaika hao) Hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie hakika sisi ni mtihani (wa
kutazamwa kutii kwenu); basi usikufuru. "Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo
hayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe (na mengineyo), wala hawakuwa wenye
kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya MwenyeziMungu. Na wanajifunza ambayo
yatawadhuru wala hayatawafaa na kwa yakini wanajua kwamba aliyekhiari haya
hatakuwa na sehemu yoyote katika akhera.
Na
bila ya shaka ni kibaya kabisa walichuouzia (starehe za) nafsi zao (za akhera);
laiti wangelijua (hakika wasingefanya hivi). Na lau wangeamini na kuogopa, bila
ya shaka malipo yatokayo kwa MwenyeziMungu yangekuwa bora kwao. Laiti
wangelijua”.
Al -
Baqarah - 102- 103
Miongoni
mwa mambo ya kichawi ni yale wafanyayo wenye kupandwa na jazba, wanaojipiga
vichwani na kujichoma miili yao kwa mapanga na majambia, na yale wanayofanya
wachawi wakaonekana kama kwamba wanatoa mawe matumboni mwa watu.
Mtume
(SAW) amesema:-
<<Hayuko
pamoja na sisi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa au (mwenye) kufanya
uchawi au kufanyiwa au mwenye kufanya (1)Tatayyur au mwenye kufanyiwa>>.
(Imetolewa
na Al - Bazaar)
(1)(Tatayyur
ni kuamini kwamba baadhi ya ndege wakiruka au sauti zao zina leta madhara au
nukhsi n.k.)
8- MAKAURE, HIRIZI, KULA MICHANGA YA MAKABURINi AU KUJIPANGUSIA NAO MWILINI
Miongoni
mwa ujinga, ni itikadi ya baadhi ya watu kuwa makaure yana uwezo wa kufukuza
majini, wakawavisha wanyama wao au watoto wao kaure hizo. Wengine hutundika
kamba na uzi au hutundika hirizi zenye majina ya majini na michoro
isiyotambulika au kula michanga ya makaburi au kujipangusia miili yao michanga
hiyo.
Yote
hayo ni katika upotofu na ujinga ambao kila Muislamu lazima aepukane nao, maana
hapana mwenye uwezo wa kudhuru au kufaa isipokuwa MwenyeziMungu tu, Subhanahu
Wataala.
MwenyeziMungu
amekwisha tukadiria yale yanayotudhuru tukayajua kwa akili zetu, kwa hivyo ni
wajibu wetu kuziondoa kwa qudra zenye manufaa. Kwa hivyo tunaiondoa qadar ya
njaa kwa qadar ya chakula na qadar ya maradhi kwa qadar ya dawa, tukishindwa
basi tunamuomba Mwenye funguo za kila kitu (Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala).
MAENDELEO TULIYOYATUPA NYUMA
Mwenye
kuzingatia hali za Waislamu atawaona kuwa wamekuwa ni wenye kutegemea mataifa
mengine katika kuyaendesha mambo yao ya kidunia kama vile viwanda, ukulima,
biashara na ujuzi wa kifundi.
Nini basi
sababu za kuwa nyuma katika mambo haya ya Kidunia, bali hata katika mambo ya
Kidini?
Baada
ya kudhoofika kwa Imani ndani ya nafsi zetu, na kudhoofika uhusiano wetu na
Mwenyezi Mungu, na kudhoofika tabia na mwenendo, ndipo ufisadi ukaanza kuenea
kidogo kidogo hata vikapatikana vizazi vilivyoipoteza Sala na kufuata
matamanio, Dhulma ikaenea baina ya watu na dhambi kuongezeka, ukaanza mvutano
baina ya Waislamu, ujinga katika mambo ya kidini na kidunia ukaenea, uzushi
katika mambo ya dini ukaongezeka pamoja na Ushirikina.
Waislamu
wakaupoteza umoja wao na undugu wao, na kwa ajili hiyo nguvu zao zikatoweka,
wakaanza kuanguka na kubadilika hali zao kutoka katika hali mbaya kuelekea
katika hali mbaya zaidi.
UKOLONI UMEZAMISHA MIZIZI YA OPOTOFU (UPOTEVU) NA SISI TUKAKUBALI
Ikiwa
Mwenyezi Mungu anasema:-
"Na
Mwenyezi Mungu hatawajaalia makafiri njia ya kuwashinda Waislamu".
(An -
Nisaa -141)
Kwa
hivyo Waislamu baada ya kuipoteza imani iliyo sahihi na kuchukua nafasi yake
ushirikina na Bid- aa, (uzushi wa mambo yasiyo na asili katika dini) isipokuwa
kwa wale wachache aliowarehemu Mola wao,
Waislamu wakawa katika hali ya kuanza kuikubali sheria ya makafiri
waliofanya juhudi kubwa ya kupiga vita kila kinachowaamsha Waislamu katika
mambo yanayohusiana na Dini yao na ya kidunia.
Na
kutokana na udhaifu wa imani, wakapatikana miongoni mwetu waliozikubali mbinu
za makafiri, bali na kuwasaidia katika kufanikiwa kwa mbinu hizo dhidi ya
Waislamu.
SABABU ZA MAENDELEO YA KIDINI NA YA KIDUNIA
Sababu
zitakazo waendeleza mbele Waislamu katika dini yao ni kuizamisha imani katika
nafsi zao, kuzidisha nguvu mawasiliano yao na Mola wao, kuzitakasa ibada zao
ili ziwe halisi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kufuata sheria zake, kufuata
mwenendo wa Kiislamu pamoja na kuwalea watoto katika njia hizo zote.
Iwapo
watatekeleza hayo, basi neno lao litakuwa moja, nguvu zao kuongezeka na
Mwenyezi Mungu atawanusuru na adui zao.
Na
sababu zitakazosababisha kunyanyuka hali zao katika mambo ya kidunia ni
kuutumia uchumi na kheri aliyowapa Mwenyezi Mungu katika ardhi zao, kwa njia
zilizo bora.
Ili
Waislamu wafanikiwe katika mambo haya, zipo njia nyingi zinazohitajika
kufuatwa, miongoni mwa njia hizo ni;
1- Kupatikana kwa wataalamu wenye ujuzi na
wafanyakazi waliopata mafunzo sawa sawa.
2- Kupatikana kwa mali pamoja na mali asili.
3-
Kueneza viwanda pamoja na kutafuta masoko ya kununua bidhaa zitakazopatikana
katika viwanda hivyo.
4- Kuwepo kwa nidhamu yenye uadilifu itakayowapa
moyo wafanyakazi ili waongeze juhudi, pamoja na kuwepo kwa nidhamu yenye uwezo
wa kuzuwia dhulma na uvukaji mipaka (katika maonevu).
Bila
shaka sababu hizi ni katika mema ambayo dini yetu inayatilia mkazo yafuatwe na
kushirikiana kwa ajili ya kuyafikilia, maana haya ni katika mambo muhimu
tunayoyahitajia sana. Ama sivyo siku zote Waislam watakuwa wakitegemea misaada
kutoka katika nchi zisizokuwa za Kiislam,
na siku zote watadhalilika mbele yao.
Mwenyezi
Mungu anasema:-
"Wala
hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini."
(A l -
Hajj - 78)
Mwenyezi
Mungu ametuamrisha kushirikiana katika mema yaliyo kama haya na mengineyo na
ametukataza kushirikiana katika dhambi na uadui wa kila aina.
Mwenyezi
Mungu anasema:-
"Na
saidianeni katika wema na ucha Mungu na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.
Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu."
(Al -
Maidah - 2)
Ikiwa
kila mtu atatoa mchango wa Shilingi mia kila mwezi, basi tunaweza kujenga
kitivo cha Sheria au cha Uhandisi au cha Madawa (Pharmacology) au cha Sayansi
au cha Ukulima au cha Tiba.
Na
kutokana na vitivo hivi tutaweza kuutambua uwezo wetu na kufaidika nao na
wakati huo huo tutaweza kupata waalimu wa kuwafundisha wenzao.
Ikiwa
kila mtu ataweza kulipa shilingi mia tu, basi tutaweza kusimamisha mashirika au
viwanda vitakavyofaa katika maendeleo yetu, itakuwaje basi ikiwa kila mwenye
uwezo zaidi, atatoa kiasi cha uwezo wake?
Na kwa
njia hii tutaifupisha njia ya kupata maendeleo ya kidunia na kupata mafanikio
katika miaka michache tu.
Mwenyezi Mungu
amezijaalia nchi za Kiislamu kuwa na utajiri mkubwa, lakini kwa udhaifu
wetu tumeshindwa kunufaika na kheri hizi sisi wenyewe isipokuwa tuwe chini ya
watu wengine wasiokuwa Waislamu.
WAKOLONI WAMEZIPIGA VITA NJIA ZOTE AMBAZO ZINGEWAFANYA WAISLAMU WAPATE MAENDELEO
Nchi
nyingi za Kiislamu na kwa miaka mingi zilikuwa chini ya utawala wa makafiri
walioitumia kila fursa wanayoipata katika kuipiga vita dini ya Kiislamu.
Wakaipiga
vita dini hii katika sehemu mbali mbali, kama vile:-
1- Kuifuta sheria ya Kiislamu isitumike katika
nchi za Kiislamu.
2- Kupiga vita masomo ya dini katika skuli na
vyuo vikuu.
3- Kuwapiga vita Maulamaa wa Kiislamu
wanaoifanyia kazi dini yao.
4-
Kuanzisha vyama vya siasa visivyoamini Mungu na vinavyopiga vita dini.
5-
Kutilia mkazo mambo ya Uzushi katika dini (Bida a) pamoja na Imani za kijinga
na za ushirikina na kuifanyia biashara dini.
6-
Kuwafisidi wanawake pamoja na kuufisidi ukoo na kuwaacha wanawake watembee uchi
pamoja na kuufisidi mwenendo wa Waislam.
7- Kutafuta kila njia ili kuleta kutokuelewana
na kufarikiana pamoja na uadui baina ya Waislamu.
Mwenyezi
Mungu amekwisha tutahadharisha juu ya kuwatii Ahli - lkitab (Wakristo na
Mayahudi) aliposema:
"Enyi
mlioamini! Mkiwatii baadhi ya wale waliopewa kitabu, watakurudisheni kuwa
makafiri baada ya Uislamu wenu."
(Al -
Imran - 100)
Ama
kuhusu makafiri kuipiga vita nguvu ya Waislamu, yafuatayo ni katika mambo
muhimu walioyafanya:
1- Kuweka mipaka ya kuwatenganisha Waislamu.
2- Kuutawala uchumi wa Waislamu.
3-
Kufanikiwa kupata vizazi miongoni mwa Waislamu, wale waliolelewa na kufunzwa
katika mikono ya makafiri na wale wataalamu wa mambo ya Bara la Asia
(Orientalist) na kuweza kuwadanganya kwamba Waislam hawatoweza kuendelea ila
baada ya kuipiga vita dini yao na kumfisidi mwanamke kwa kutumia mwito wa “Haki
za kinamama”, ili aufisidi mwenendo wake pamoja na fadhila zake na heshima yake
na pia kwa njia ya kuruhusu ulevi, uzinzi na kuipiga vita sheria ya Mweneyzi
Mungu na kuibadilisha kwa kanuni za wanaadamu.
Wakoloni
hawa badala ya kufanya kazi ya kueneza viwanda, mashirika, vyuo na vyuo
vikuu na maabara, wakafanya kazi ya kuwapiga vita Waislam
katika Itikadi zao, heshima zao, sheria ya dini yao pamoja na mwenendo wao, hata
ukafika wakati mtu anayesali anaonekana mbele yao kama mtu asiye endelea, yuko
nyuma, na kuacha Sala ndio maendeleo.
Na
mwanamke anayejihifadhi, huwa hakuendelea, yuko nyuma, na yula alie fasiqi
muhuni ndiye aliyeendelea.
Yule
anayeilinda akili yake na mwili wake kutokana na ulevi nae pia hakuendelea,
yuko nyuma, lakini mlevi ndiye aliyeendelea na yuko huru.
Viko
wapi viwanda? Yako wapi mashirika? Yako wapi maabara?
Wakoloni
na wanafunzi wao wametupotosha mbali na njia iliyo sawa ya kutaka kuendelea
vilivyo sahihi.
MAADUI WA WAISLAMU WAMEWAFANYA WAISLAMU DAIMA WAWE WANAWATEGEMEA WAO NA KUVITEGEMEA VIWANDA VYAO NA MAZAO YAO
Na ni
juu yetu pia kufahamu kwamba maendeleo yaliyopatikana katika nchi za kikafiri
hayakupatikana kwa sababu ya kukufuru kwao, kwani kufru imeanza zamani sana
hata kabla ya kudhihiri Uislamu, na kufru yao hiyo haikuwapatia hapo zamani
ndege wala roketi wala umeme wala cho chote kile. Lakini kuendelea kwao kidunia
kumepatikana kwa sababu wamefuata njia (na sababu) zilizowafikisha katika neema
ambazo Mwenyezi Mungu amewatandazia viumbe vyake.
Mwenyezi Mungu anasema:-
"Wote
hawa (wema na wabaya) tunawapa hawa na hawa - katika atiya (zawadi) za Mola
wako; na atiya za Mola wako hazizuiliki
(kumfikia kiumbe chake)".
(Bani
Israil – (Israa) - 20)
Kwa
hivyo wakapata atiya ya Mwenyezi Mungu na sisi tukakosa kwa sababu tulikuwa
wavivu.
NJIA YA KUFUZU
Siku Waislamu watakaposhikamana na Dini yao kama
inavyotakikana, hapo ndipo utukufu wao utakaporudi na ndipo Mwenyezi Mungu
atakapowanusuru kutokana na adui zao, na hapo itakuwa wepesi kwao kupata
mafanikio katika Dini na dunia yao.
<<Mola
wetu! usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuziongoza na utupe rehma itokayo kwako;
hakika Wewe ndiwe Mpaji mkuu>>.
Wasalamun
Alal Mursalina Walhamdu lillahi Rabbi L
–aalamin.
KIMEANDIKWA NA SHEIKH ABDUL
MAJEED AL ZINDANI
KIMEFASIRIWA NA MUHAMMAD
FARAJ SALEM AL SAIY
Huenda pia kukaribiana kwa
wakati ikawa ule urahisi wa kazi. Kwa mfano kazi iliyokuwa ikifanywa siku
nzima hapo zamani hivi sasa inafanyika katika dakika chache tu, au kazi
iliyokuwa ikichukua miaka hapo zamani, hivi sasa baada ya kuletwa makopyuta
na vyombo vingine vya kisasa huchukua masaa machache tu pamoja na safari
zilizokuwa zikichukua miezi mingi hapo zamani hivi sasa zinachukua masaa
machache tu.
|
[5]Yamenukuliwa kutoka kwenye kitabu kiitwacho "Mawimbi yaliyofichika
katika dini za kale za Wahindi”, kilichoandikwa na T. Muhammad
[6] "ILA KWA HAKI YA UISLAMU" = Zile hukumu za kisheria za Kiislamu
zilizowajibika kusimamishiwa Muislamu yeyote anapouwa, anapozini, anapoiba au
hukumu nyenginezo.
Makhalifa hao pia wameoleana na Mtume (SAW) -
Aisha (Umu I Muuminina)(RA) Mke wa Mtume(SAW), ni binti wa Abu Bakar Al Siddique(RA).
Hafsa(RA) - Mke wa Mtume (SAW), ni binti wa
Omar (RA)
Ruqayyah(RA) - Binti wa Mtume(SAW),
alimwozesha Othman(RA) na alipokufa bibi Ruqayyah(RA) Mtume (SAW) akamwozesha
Othman(RA) binti yake wa pili - Ummu Kulthum(RA), na ndio maana Othman(RA)
alikuwa akijulikana kwa sifa ya "Dhu Nnurayn" – Mwenye Nuru mbili -,
na hii ni kwa sababu ya kuoa mabinti wawili wa Mtume(SAW).
Mtume (SAW) akamwozesha Aliy bin Abi Talib
(RA) binti yake Fatma(RA) "Bibi wa kina mama Peponi".
Aliy bin Abu Talib(RA) pia alimwozesha Omar
bin Al Khatab(RA) binti yake Ummu Kulthum(RA) mwana wa Fatma(RA).
Makhalifa Al Rashidyni hawa walikuwa mawaziri
wa Mtume (SAW) na alikuwa akishauriana nao sana katika mambo yaliyo muhimu nao
pia walikuwa miongoni mwa Waislamu wa mwanzo wa Makka.
Na mwanzo wao kusilimu ni
Aliy bin Abi Talib baadaye Abu Bakar, akafuatilia Othman kisha Omar(R Anahum
Jamiy-an).
Zipo hadithi nyingi za
Mtume (SAW) zinazoelezea ubora wao kupita Masahaba wengine wote walio wema.
‘Wala hawaadhibiwi
kwa makubwa’ alikusudia kuwa watu hao walikuwa wakidhani kuwa madhambi yale si
makubwa.
Kisha
akasema; ‘Bali hivyo’, kwa lugha ya kiarabu alitamka; ’Balaa’ na hii maana yake
ni kukanusha kuwa; si kama walivyokuwa wakifiria wao, bali madhambi hayo
yalikuwa makubwa.
<<Mwenyezi
Mungu anamlani kila anayechinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu,
na Mwenyezi Mungu anamlani kila anayewalani wazazi wake, na Mwenyezi Mungu
anamlani kila anayemnusuru mwenye kuleta uzushi (katika dini), na Mwenyezi
Mungu anamlani kila anayesogeza mipaka (kwa ajili ya kuiba ardhi ya
mwenzake>>.
(Imetolewa
na Muslim katika "Sahih" yake, Ahmad katika "Musnad" yake
na An Nasai katika "Sunan" yake.)