RIBA KATIKA UISLAM
Kwa mujibu wa Qur’an tukufu, kuchukua
riba ni dhambi ambalo linasababisha adhabu kali kabisa kutoka kwa Allah
swt. Adhabu za kuchukua na kutoza riba ni kali kabisa kuliko madhambi
mengine. Kama ilivyoelezwa katika Surah Aali Imran, 3, : 130 - 131:
‘Enyi Mlioamini! Msile riba, mkizidisha mara dufu kwa mara dufu; na mcheni Allah ili muweze kuwa na ufanisi’
‘Na ogopeni moto wa Jahannam ambao umetayarishiwa makafiri.’
Inamaanisha kuwa ukali wa moto ambao
umetayarishwa kwa ajili ya wale ambao huchukua riba kama vile moto
utakavyokuwa mkali kwa ajili ya makafiri.
Allah swt anatuambia katika Surah al Baqarah, 2, Ayah ya 275 :
‘ Wale wanaokula riba, hawasimami ila
kama anavyosimama yule ambaye Shaitani kamzuga kwa kumsawaa; na haya ni
kwa sababu wamesema, ‘biashara ni kama riba’, Allah ameihalalisha
biashara na kaiharamisha riba. N a aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa
Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali)
aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba)
basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.’
Ayah hiyo inatuthibitishia kuwa wale
wanaochukua riba watabakia kwa milele katika Jahannam (Motoni) na kamwe
hakutakuwa na uwokovu kwa ajili yao. Allamah Muhammad Husain Tabatabai
(a.r.) katika Tafsiri ya Al-Mizan , anasema:
“Adhabu aliyoiweka Allah swt kwa ajili
ya mla riba ni kali kabisa kwani hakuna mahala pengine palipozungumzwa
kwa ajili ya wale wavunjao kutoka Furu-i-Diin. Kosa lingine ni lile la
kulea urafiki pamoja na maadui wa Islam. Athari za riba zipodhahiri na
bayana kwetu sote. Kukusanya na kuficha mali ndiko kunako ongezea
tofauti kati ya tabaka la masikini na tajiri. Umasikini ni ugonjwa ambao
unamdhalilisha na kumshusha hadhi mgonjwa wake, unateketeza uthamini
wake na kuharibu maadili yake. Na haya yanaelekeza katika mutenda maovu,
uizi, ubakaji na mauaji. Walanguzi ndio watu wanaowajibika kwa
kuteketea kwa usawa wa kijamii, ambao wamejilimbikizia mali kupita kiasi
kwamba haiwafikii wanao hitaji na wenye dharura. Kwa kuvunjika
kikamilifu kwa mshikamano wa kijamii unaweza kuzua na kukuza vita vya
wenyewe kwa wenyewe au vita vya ndani na kuendelea hadi kuzuka kwa vita
vya dunia ambavyo hatima yake itakuwa ni mauaji na maangamizo. Katika
ulimwengu wa sasa ikiwa na silaha za kisasa za teknolojia ya hali ya juu
na ya maafa makubwa katika nuklia na kemikali, vita vinapozuka si
kwamba vinaleta mauaji ya wanaadamu tu bali humgeuza yeye kuwa ni picha
tu, mgonjwa na asiye na uwezo wowote na ameharibika kimwili kwa vizazi
na vizazi vijavyo.
Athari mbaya kwa jamii ya Waislamu kwa kutokana na urafiki na uhusiano pamoja na maadui wa Islam, yapo dhahiri na bayana.
Wanahistoria wamerekodi kuwa urafiki
pamoja na maadui wa Islam unanunuliwa kwa malipo. Na malipo katika swala
hili ni kuafikiana. Maafikiano katika misingi hii yanaipeleka nchi
katika kupoteza utamaduni na Uislamu vyote kwa pamoja yaani unafika
wakati ambapo nchi hiyo haitwi tena nchi au jamii ya Kiislamu.”
Riba inapingana na akili na Shariah
Aya za Surah Al-Baqarah zilizoelezwa
hapo juu, zinasema kuwa wale watu ambao wanachukua riba (riba katika
mikopo) watahesabiwa miongoni mwa vichaa (ambao wameguswa na Shaitani).
Siku ya Qiyama, watu watawatambua hawa kuwa ndio waliokuwa wakila riba
humu duniani kwamba watakuwa ni vichaa. Utukufu wao utakuwa umeshakwisha
teketea, kwa sababu wao humu duniani wamekuwa wakienda kinyume na akili
na Shariah. Wao wameshakwisha kusahau tangia zamani matakwa na
mahitajio ya binadamu. Wao hawakuwa na uhusiano wa usawa pamoja na
wengine na vile vile walikiuka kanuni za ushirikiano. Kwa hakika watu
hawa wamekuwa ni wapumbavu humu duniani, kwa sababu wao wamefuata
maagizo ya Shaitani na ndivyo maana wamekuwa wakitenda matendo ya
kipumbavu.
Je Biashara na Riba ni kitu kimoja ?
Mabishano haya yote kwa pamoja ni
upumbavu. Hakuna ulinganisho wowote baina ya biashara na riba. Katika
biashara kuna usawa kwa sababu humo kunakuwapo maelewano baina ya
mnunuzi na mwenye mali na wote kwa pamoja ama huweza kupata faida au
hasara. Katika biashara, muuzaji anauza bidhaa kwa mnunuzi kwa bei
wanayoafikiana wote wawili, na swala hili huishia hapo. Lakini kuchukua
riba ni swala la mkato la uchafuzi na kuteketeza. Mtu ambaye anayo mali
au mapesa ya ziada, ambayo yeye hazihitaji, humwazima au kumkopesha mtu
ambaye anakuwa na shida kali. Mtu mwenye shida kali anakubali kulipa
riba ambayo kwa hakika hana uwezo nayo ; si kwamba yeye anaikubalia bali
anakuwa ameshurutishwa na shida iliyomkaba vibaya sana wakati huo.
Riba na Utofauti wa Tabaka katika Jamii
Haina shaka, kuwa riba ni ubaya ambao
hauna haki na inayokandamiza katika jamii. Riba inapingana na maumbile
ya kibinadamu na hadhi ya mwanadamu. Hivyo huwaongezea utajiri wa
matajiri na kuwaangamiza kabisa walio wanyonge na wale wenye hali ndogo
kuingia katika umasikini.
Hakuna shaka, masikini aliyekwisha
haribiwa anaanza kuonesha chuki zake dhidi ya matajiri. Kizimba hicho
cha uchukivu unajipatia mwanya wa kutokea katika sura ya vurugu,
uporaji, machafuko na mapinduzi ya umagikwaji wa damu.
Katika kitabu ‘Islam and World Peace’ imeandikwa:
“Islam inasema kuwa mapato ya mtu
yatokane na kiwango cha juhudi na kazi iliyofanyika.” Kwa sababu
uwekezaji wenyewe haufanyi kazi wala jitihada ya aina yoyote ile. Hivyo,
mali ya matajiri haitakiwi kamwe kuongezeka kwa kutokana na riba.”
Kuiongezea utajiri mali iliyopo kwa
kupitia riba ni njia iliyo saheli kabisa ya kujipatia utajiri, lakini
imeharamisha kabisa hivyo. Mali haiwezi kuongezwa kwa kumnyonga mnyonge
atumbukie katika umasikini zaidi ya hali mbaya aliyonayo; na hicho
ndicho kinachofanywa na mtoza riba, husababisha kutokuwa na usawa katika
uchumi na kukanyaga haki za binadamu, usawa na haki. Maulana Sayyid
Abul ‘Ala Maududi wa Pakistan ameandika kitabu kivutiacho chenye
kuieleza na kuipambanua riba na ambacho kinaelezea athari mbaya za riba
kwa kutoa hata takwimu mbalimbali.
Mtu mwenye shida si kwamba anarudisha
kile alichokuwa amekopa kwa riba bali hulazimika kurudisha zaidi na
zaidi ya kiwango alichokuwa amekopa. Ziada hiyo huwa hata inazidi mara
dufu na zaidi kuliko kile kiwango alichokuwa amekopa iwapo malipo
yatakapotokea kucheleweshwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake. Kwa
hakika riba humtumbukiza mtu katika matatizo zaidi ya kifedha juu ya mtu
ambaye yupo tayari ameshatumbukia katika shida na hivyo kwa kutambua
hayo, bado ikiwa analazimishwa kulipa kile kilicho nje ya uwezo wake ni
udhalimu mbaya sana. Kimaadili, mtu mwenye shida asaidiwe kwa kupewa
mikopo bila ya kumtoza riba. Na kwa hayo kunaongezea mapenzi ya urafiki,
udugu, uhusiano na ushirikiano na ndivyo ni mambo mema.
Riba kwa ajili ya mikopo
Kutoa mikopo kwa kutoza riba si kwamba
inateketeza uwiano wa kiuchumi katika jamii, bali inalipua hisia za
chuki, uadui na ubinafsi.
Anayejitumbukiza katika riba anajikosesha mema
Yapo maovu mengi katika kutoza riba.
Mapato yanayotokana na riba huwa yanakosa baraka za Allah swt. Wakati
mapato yanyotokana na kuvuja jasho huwa yana baraka kwa wingi.
Mtume Muhammad s.a.w.w. anasema katika Hadith moja, katika Wasa’il al-Shiah :
“Ibada inayo sehemu sabini. Na muhimu kabisa ni mtu kujipatia kipato chake kilicho halali.”
Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Muhajjatul Baidha:
“Mfanyabiashara mwaminifu atahesabiwa pamoja na Mitume a.s. Siku ya Qiyama. Uso wake utakuwa uking’ara kama mbalamwezi.”
Mtoza riba huwa hamwamini Allah swt
Hasara nyingineyo aipatayo mtoza riba ni
kule kukosa kumwamini Allah swt. Yeye kamwe huwa haombi kwa Allah swt
amwongezee baraka kwani matumaini yake yote kwa pamoja huwa yako katika
riba anayoikusanya kutoka wadaiwa wake na hii ndiyo shirk kama vile
inavyozungumziwa katika maudhui ya Shirk katika vitabu vya Fiq-hi.
Jambo lingine la kutiwa maanani ni kuwa,
katika biashara za kawaida, mfanyabiashara huweza ama kujipatia faida
au hasara. Kwa hivyo daima mfanya biashara huyo huwa anajitahidi sana
katika biashara yake na humwomba Allah swt ampatie baraka na ufanisi
katika biashara yake hiyo ili apate faida. Lakini mtoza riba hana
wasiwasi na hasara na hivyo anaona hakuna haja ya kumwomba Allah swt
amjaalie riziki. Na hivyo hupoteza fursa hiyo ya kumnyenyekea Allah swt.
Thawabu ya kutoa mkopo ni zaidi ya kutoa sadaqa.
Mtoza riba hujipotezea malipo mema
(thawabu) zinazopatikana kwa kutoa mikopo njema. Kama yapo mema kumi
katika kutoa sadaqa, basi kutoa mikopo bila riba inayo kumi na nane.
Hivyo mikopo bila riba inayo thawabu mara dufu ya kutoa sadaqa katika
njia ya Allah swt. Mtu ambaye anawahurumia wadaiwa wake na hawatozi riba
basi hupewa thawabu sawa na kiasi hicho kwa kila siku kwa muda
atakaouongeza katika kulipwa deni lake. Kwa hakika mtoza riba hastahiki
kwa malipo hayo, badala yake yeye anajichumia madhambi. Kwa hakika
analaaniwa kwa uchoyo na uroho, ambayo magonjwa hayo huongezeka kila
siku. Kwa hakika mwisho wa uchoyo na uroho ni Jahannam (Motoni).
Hatima ya mtoza riba
Kama tulivyokwisha kuona katika Ayah za
Qur’an, Ahadith za Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na Maimau a.s. kuwa
adhabu ya mtoza riba ni kali na mbaya kabisa hata kuliko madhambi
mengine na tumezungumzia sababu zake pia. Islam imeiweka riba kuwa ni
Adh-Dhunubul Kabirah (Madhambi Makuu) na adhabu yake ni kali kabisa
kuliko zote. Iwapo mtoza riba hatafanya Tawba kwa matendo yake, hivyo
hatima yeke itakuwa pamoja na makafiri ambao hawana mahala pengine
isipokuwa ni Jahannam kwa milele. Na mtoza riba kamwe hataachiliwa
kutoka humo.
Qur’an Tukufu inarejea kutuambia katika Surah al-Baqarah, 2 Ayah 275 :
‘‘N a aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa
Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali)
aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba)
basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.’
Hata hivyo kuna baadhi ya njia ambazo
mtoza riba anaweza kufidia madhambi yake na kuomba Tawba kwa Allah swt.
Yapo madhambi ambayo Allah swt huzisamehe kwa kuomba msamaha (Tawba)
iliyo sahihi na kweli. Iwapo kafiri akitubu madhambi yake na akawa
Mwislamu, basi dhambi kuu kama la shirk linasameheka. Yeye hahitaji
kufanya lolote zaidi ya hayo. Lakini zipo baadhi ya madhambi ambayo
yanahitaji kulipia fidia sambamba na kufanya Tawba i.e. kama mtu ambaye
anayo qadhaa sala na saumu. Yaani pamoja na kufanya Tawba inambidi alipe
sala na saumu zote alizoziacha. Vivyo hivyo katika swala la riba, mtoza
riba itabidi afanye tawba na wakati huo huo awarudishie mapesa wale
wote aliokuwa amewatoza kama riba.
Hakuna Baraka katika riba
Ayah ya hapo juu ya Qur’an inaendelea Surah al-Baqarah, 2 Ayah 276 :
‘ Allah huyafutia (baraka mali ya )
riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa . Na Allah hampendi
kila kafiri (na) afanyaye dhambi.’
Sadaqa inaeneza amani, inaongeza
ukarimu, uwema na mapenzi katika jamii, ambapo riba inaangamiza amani na
kuzifanya nyoyo za watu ziwe ngumu.
Wakati riba inapotanda mizizi yake
katika jamii, basi watu katika jamii hawatasita kudhulumiana haki zao
miongoni mwao. Wao watakuwa wameghalibiwa na hisia za chuki, uadui na
uchu wa kulipiza kisasi. Jamii ambayo imeondokewa na ushwari, upendo na
ushirikiano basi kamwe haiwezi kujipatia maendeleo, kwa hakika
inajiangamiza kwa maovu yake yenyewe. Misaada na sadaqa kwa upande
mwingine, huongeza hisia na moyo wa urafiki, mapenzi na udugu. Hali ya
amani na baraka hutanda kote ambavyo ni changamoto kwa watu kundeleza
matendo mema.
Vita dhidi ya Allah swt na Mtume Muhammad s.a.w.w.
Qur’an Takatifu inatuambia Surah al-Baqarah, 2, Ayah 278 :
‘ Enyi Mlioamini ! Mcheni Allah, na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini.’
Ushahidi wa imani ya mtu katika utiifu wa Hukumu za Allah swt, ayah hiyo hiyo inaendelea :Al-Baqarah, 2, Ayah 279
‘Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa na vita na Allah na Mtume Wake….’
‘Na mkiwa mmetubu, basi matapata rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiane.’
Yeyote yule asiyeitii amri hii basi ajitayarishe kwa vita dhidi ya Allah swt pamoja na Mtume Muhammad s.a.w.w. .
Twapatiwa ufafanuzi wa Ayah hii katika
Tafsir Minhajus-Sadiqiin . Inaweza kumaanisha kuwa dhambi la riba ni
mbaya na ovu kabisa hadi kwamba iwapo Mtume Muhammad s.a.w.w.
angelikutana na mtoza riba humu duniani basi Mtume Muhammad s.a.w.w.
asingalisita kuutoa upanga wake na kupigana vita na huyu mtu punde
wangalikuwa wameonana uso kwa uso. Na huko Aakhera, Moto mkali wa
Jahannam utamweka katika adhabu kali yenye mateso kwa amri ya Allah swt.
Mtoza riba lazima apigwe vita vikali hadi hapo aache kutoza na kupokea
riba. Riwaya zinatuelezea kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. baada ya
kuteremka kwa Ayah hiyo, alimjulisha Gavana wa Makkah kuwa iwapo kabila
la Bani Mughaira hawataacha kutoza na kupokea riba, basi lazima vita
vitakatifu vitangazwe dhidi yao.
Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amezungumzi katika hotuba yake huko Makkah :
“Muelewe kuwa riba iliyokuwa imekusanywa
katika zama za ujahiliyya sasa imesamehewa kabisa. Kwanza kabisa mimi
binafsi nina wasameheni ile riba ( iliyopo shingoni mwenu) ya
(mjombangu) '‘Abbas ibn Abdul Muttalib."
Ahadith zinazokana riba
Imeripotiwa kutoka Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. kuwa, katika Al-Kafi :
“Kuchukua Dirham (au pesa moja) kama
riba ni vibaya sana machoni mwa Allah swt kuliko kuingiliana na mwanamke
aliyeharamishwa kwako.”
Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Wasa’il al-Shiah :
“Mtume Muhammad s.a.w.w. amemlaani
vikali yule ambaye anayekubali riba, anayelipa riba, aneyeinunua riba,
anayeiuza riba, yule anayeandika mikataba ya riba na yule anayekuwa
shahidi wa mikataba hiyo.”
Ibn Baqir anaripoti kuwa Al-Imam Ja’afer
as-Sadiq a.s. alijulishwa kuhusu mtu mmoja aliyekuwa akitoza na kupokea
riba kama ndiyo halali kama vile ilivyo halali maziwa ya mama. Kwa
hayo, alisema Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. katika Al-Kafi :
“Iwapo Allah swt atanipa uwezo mimi juu ya mtu huyu, basi nitamkata kichwa.”
Hivyo imetuwia dhahiri kuwa riba ni
haraam kabisa na hii ndiyo imani ya Mwislamu kukiri na kuamini na
kuifuata kuwa riba ni haraam. Iwapo mtu yeyote ataipuuza hivyo na
akasema kuwa riba si haraam, basi huyo atakuwa ni kafiri papo hapo. Na
hivyo Imam a.s. anaweza kumwua.
Riba imekanwa katika Qur’an
Samaa anasema kuwa yeye alimwuliza
Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. je ni kwa nini Allah swt ametaja
kuharamishwa kwa riba mahala pengi katika Qur’an. Al-Imam Ja’afer
as-Sadiq a.s. alimjibu, katika Wasa’il al-Shiah :
‘Ili kwamba watu wasiache tendo la kutoa misaada (kama vile kutoa mikopo bila ya riba).”
Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Wasa’il al-Shiah :
“Shughuli mbaya kabisa ni ile ambayo inahusisha riba.”
Mhalifu anakosa Imani ya Dini
Zurarah anasema kuwa yeye alimwuliza
Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. kuhusu Ayah ya Qur’an isemayo katika
Surah Al-Baqarah,2, Ayah 276:
‘‘ Allah huyafutia (baraka mali ya ) riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa .’
Na akaongezea kusema :
“Lakini mimi ninaona kuwa mali na utajiri wa watoza riba inaendelea kuongezeka tu kila siku.”
Amesema Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa’il al-Shiah :
“Loh ! hasara inawezekana kuwa kubwa
sana ? Kwa merejeo ya Dirham moja yeye anaipoteza Dini yake. Na iwapo
yeye atafanya Tawba humu duniani basi kutafikia mwisho kwa mali
aliyoichuma humu duniani kwa njia iliyo haramu na hivyo kuwa fukara.”
Matumbo ya watoza riba zitajazwa kwa moto
Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il :
“Yule anayechukua riba basi Allah swt
atalijazatumbo tumbo lake kwa moto kiasi hicho hicho. Iwapo yeye
amechuma zaidi kwa kutokana na mapato ya riba, basi Allah swt
hatakubalia matendo yake mema. Hadi kwamba kiasi cha punje moja kama
kitabakia ambacho kimepatikana kwa njia ya riba. Allah swt pamoja na
Malaika Wake wataendelea kumlaani huyu mtu.”
Adhabu za mpokea riba katika ‘Barzakh’
Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema :
“Usiku wa Me’raj Mimi niliwaona baadhi
ya watu waliokuwa wakijaribu kusimama lakini hawakuweza kufanikiwa kwa
sababu ya matumbo yao makubwa, niliuliza, ‘Ewe Jibraili ! Je ni watu
gani hawa ?’
Jibraili alijibu : “Hawa ndio wale
waliokuwa wakichukua riba. Sasa wao wanaweza kusimama tu kama wale
waliokamatwa na Mashetani.”
Mtume Muhammad s.a.w.w. aliendelea,
“Na hapo nikawaona wao wakikusanywa
katika njia za wafuasi wa Firauni. Kwa kuona uchungu wa joto la Moto
mkali, wao walipiga kelele : ‘Ewe Allah swt ! Je Qiyama itakuwa lini ?’
(Hivyo imekuwa dhahiri kuwa Moto unaozungumziwa katika riwaya hii ni adhabu katika Barzakh ).
Watoza riba kukanyagwa na miguu ya Firauni
Katika riwaya nyingine imeelezwa kuwa
watu hawa walipowaona watu wa Firauni, basi walijaribu kuinuka na kutaka
kukimbia, lakini kwa kutokana na matumbo yao kuwa makubwa kupita kiasi,
hivyo hawakuweza kuinuka na hatimaye wafuasi wa Firauni walipita na
kuwakanyagakanyaga kwa miguu yao, na wakaendelea mbele na safari yao.
Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. akisema, katika Mustadrakul Wasa'il :
“Wakati zinaa na riba vitakapokuwa ni
vitu vya kawaida katika mji wowote basi Allah swt huwapa ruhusa Malaika
kuwaangamiza wakazi wake.”
Ipo riwaya nyingine isemayo kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il kuwa :
“Utakapofika wakati Ummah wangu utaanza
kutoza na kupokea riba, basi mitikisiko na mitetemeko ya ardhi yatakuwa
yakitokea mara kwa mara.”
Riba ni mbaya kabisa kuliko hata Zinaa
Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, Wasa’il al-Shiah :
“Iwapo mtu atazini pamoja na mama yake
katika Al-Ka’aba tukufu, basi dhambi hili litakuwa hafifu mara sabini
kuliko tendo la kutoza na kupokea riba.”
Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa’il al-Shiah :
“Katika macho ya Allah swt, kuchukua
Dirham moja ya riba ni mbaya kabisa hata kuliko matendo thelathini ya
kuzini pamoja na maharimu wake yaani baba kuzini pamoja na binti yake.”
Hadith iliyopita inaelezea dhambi hili
kuwa ni mara sabini ya kuzidi dhambi la zinaa. Ipo riwaya nyingine
inayosema kuwa kuchukua Dirham moja ni sawa na matendo sabini kama hayo.
(Wasa’il al-Shiah )
Hata katika dunia ya leo, mabaya ya riba
yametapakaa kwa kiasi cha kutisha cha kwamba uchumi upo unaangamia.
Baadhi ya wanauchumi wanasema kuwa riba ni muhimu kwa maendeleo. Kama
hivi ndivyo ingalikuwa kweli, basi Dini ya Islam kamwe isingalikuwa
imeharamisha. Kwa sasa hivi zipo fikra mbili za kiuchumi ambazo fikra
zao haziendeshwi na riba. Moja ni Ukomunisti na nyingine ni Islam.
Wakati ambapo misingi ya mabepari ni riba. Hata hivyo kuna tofauti kubwa
baina ya Wakomunisti na Uchumi wa Kiislam.
Uislamu kamwe haujaona dharura ya
kupokea riba kama ndio uhai wake katika uchumi, ambapo ukomunisti
unapokea riba. Na hivyo haijawahi kusikika kuwa uchumi wa Kiislam
umedhoofika kwa kutokushirikisha riba.
Hivyo, tutakubaliana kuwa hivyo ni
lazima kwa wachache fulani walio na uroho wa kulimbikiza mali zaidi ya
kile walichonacho kwa kuwanyonya na kuwakandamiza wanyonge na wenye
shida. Madhumuni yao ni kuwafanya watumwa wao. Na sisi sote tunajua
habari zao.
Mikopo yenye kutoza riba
Mikopo inayotoza riba ni ile ambayo mtu
anapopewa mkopo anapewa masharti ya kuirudisha kwa wakati maalumu ikiwa
pamoja na nyongeza ya mapesa, sharti la lazima. Mkopo uliotolewa unaweza
kuwa wa mapesa au vitu vinginevyo, mfano, mtu anaweza kukopa vibaba
vitano za mchele na kutegemea kurudishiwa vibaba sita. Nyongeza
iliyoshurutishwa inaweza kuwa katika sura ya fedha au kitu kingine,
utumishi au upendeleo.
Mfano, mtu anaweza kutoa mkopo kwa
masharti kuwa mtu aliyekopa atazirudisha fedha hizo na atamfanyia kazi
mbalimbali nyumbani mwa mkopeshaji. Au mkopeshaji anaweza kumkopa mtu
kiasi fulani cha fedha kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa masharti kuwa
ataishi katika nyumba ya mwenye kukopa kwa mwaka mzima bila ya kulipa
kodi ya nyumba hiyo. Au mtu anaweza kutoa dhahabu kama mkopo na akimtaka
mtu aliyekopa amtengenezee vito bila ya kumtoza gharama. Yaani chochote
kile kitakachotakiwa kwa kuzidi kiasi cha kile kilichotolewa, bila ya
kujali aina ya kitu, ni riba ambavyo ndivyo Haraam katika Dini ya Islam.
Haidhuru kama masharti kama hayo yalikuwa yamewekwa kuanzia mwanzoni au
baadaye. Katika sura zote ni Haraam.
Mambo muhimu ya kuzingatia
Mapatano ya aina yoyote yale
yanayohusisha riba ni haraam. Kutoza riba pia ni haraam na kulipa riba
pia ni haraam vile vile. Iwapo mtu atakopa na atachukua fedha kwa riba
na akazitumia na kupata faida, basi atambue kuwa mwenye faida si yeye
bali ni mwenye kumkopesha. Kwa mfano iwapo yeye atakopa ngano na
kuzipanda shambani, basi mazao yanayoota kutokana na hayo, kwa hakika ni
mali ya mkopeshaji. Hata hivyo, iwapo mkopeshaji atakuwa amekubali kuwa
mkopo wake utumike hivyo, basi faida itakayopatikana itakuwa ni mali ya
mtu aliyekopa.
Iwapo mtu atampa mfanyabiashara kiasi
fulani cha fedha kwa maelewano kuwa yeye atamrudishia kasoro ya kiasi
hicho, inakubalika. Kwa mfano, yeye atampatia mfanyabiashara wa Bukoba
Shillingi elfu moja na akakubaliana kurudishiwa shilingi mia tisa na
tisini tu katika mji wa Mwanza, hivyo anaruhusiwa kufanya hivyo. Aina
hii ya mapatano inajulikana kama sarf-i-baraat, kwani humu riba
haikuhusishwa.
Iwapo wakati wa kutoa mkopo
hakukuzungumzwa riba na mtu aliyekopa anataka kurudisha mkopo huo ikiwa
pamoja na nyongeza kidogo kwa furaha yake mwenyewe bila ya
kushurutishwa, basi inakubalika na si haraam. Kwa hakika hivyo ndivyo
Sunnah. Vile vile ni Sunnah kulipa mkopo kabla ya wakati wake au kabla
aliyekopa hajazidai. Vile vile ni Sunnah kwa mtu aliyekopa kuongezea
chochote kidogo kama kazawadi wakati anapomlipa yule aliyemkopa. Lakini
ni lazima kuwa nyongeza hiyo iwe imenuiwa kuwa ni zawadi na kamwe si
riba. Hata isidhaniwe kuwa ni riba. Vile vile ni Sunnah kwa wakopeshaji
kupokea chochote kile cha ziada wanachopewa kama zawadi, wala wasidhani
kuwa ni riba, na hivyo wakubali ni kama ishara ya ukarimu.
Mapatano yanayohusiana na riba
Iwapo kutakuwapo na masharti yoyote yale katika mapatano , basi hayo mapatano yenye riba yatakuwa haraam :
Chochote kile kilichochukuliwa na
kilichorudishwa ni vya aina moja lakini idadi, uzani au ujazo wake si
sawa au iwapo idadi au uzani wake ni sawa, kunatofauti katika ubora
wake, n.k.
Iwapo kutakuwa na aina moja ya uzani na
uzito, kiasi kilichochukuliwa na kurudishwa vitakuwa vya uzito na uzani
tofauti. Hata hivyo, iwapo wakati wa kukopesha uzani ulikuwa katika
kilogramu na wakati wa kurudisha uzani ukawa katika ratili au seer,
hivyo pia inaruhusiwa. Vivyo hivyo iwapo vitu vilichukuliwa katika
vipimo vya mita na wakati wa kurudishia vikawa katika futi au yadi,
vyote vinaruhusiwa.
Vile vile ni haraam kwa mtu kumkopa mtu
mmoja kibaba kimoja cha ngano kwa mwezi mmoja na baadaye yeye mwenyewe
akakopa kibaba kwa miezi miwili kutoka kwa mtu huyo huyo. Ingawaje kiasi
kwa kipimo ni kile kile, mapatano hayo ni haraam kwa sababu swala la
muda nalo ni nyeti humo.
Mambo matatu yakuzingatia
Katika swala la riba, ngano na shayiri
ni vitu mamoja. Iwapo mtu atatoa chungu kimoja cha ngano na kupokea
chungu kimoja na nusu cha shayiri, basi hiyo ni riba na hivyo ni haraam.
Vivyo hivyo, chochote kile kinachofanya
kitu chenyewe inajulikana kama ni sawa kwa sawa. Kwa mfano, maziwa na
maziwa mgando, vyote ni sawa, siki ya zabibu na zabibu viko sawa, sukari
na miwa ni sawa vile vile. Vyote hivi kama vitakopeshwa basi lazima
virudishwe kwa vipimo hivyo hivyo ama sivyo vitahesabika katika riba na
hivyo kuwa haraam.
Iwapo mtu atatoa mkopo wa kibaba kimoja
cha ngano na kitambaa cha leso na kuchukua kibaba kimoja na nusu cha
chungu cha ngano, basi hii haisemwi kuwa ni riba na hivyo haiwi haraam..
Katika mapatano haya, chungu kimoja kitakuwa ni badala ya chungu kimoja
cha ngano na nusu chungu itakuwa ni badala ya kitambaa cha leso. Vile
vile inawezekana kuwa mtu akatoa kibaba kimoja cha ngano pamoja na
kitambaa cha leso na badala yake akapokea kibaba kimoja cha ngano na
kitu kingine badala ya kitambaa cha leso, kama vile sabuni. Katika hali
hii riba haikuhusishwa.
Iwapo mtu mwanzoni atauza kibaba kimoja
cha ngano kwa Shilingi mbili na baadaye akanunua kibaba kimoja na nusu
kwa shilingi mbili, inaruhusiwa. Kwa kuwa mapatano yote hayo ni
mbalimbali na yanajitegemea. Hivyo havihusishi riba.
Inawzekana vile vile kuwa Zaid anamwuzia
Khalid kibaba kimoja cha ngano na Khalid anampa kibaba kimoja na nusu
cha ngano Zaid kama zawadi. Haya pia yanaruhusiwa.
Wakati ambapo kuchukua riba inaruhusiwa
Kuna aina tatu za watu ambapo kuchukua na kulipa riba inakubaliwa:
Baba na mtoto Baba na mtoto wanaweza
kuingia katika mapatano ya riba. Lakini mapatano baina ya mama na mtoto
yanayohusisha riba ni haraam.
Mume na mke : Mume na mke wanaweza
kutozana riba. Kwa mfano iwapo mmoja atatoa Shilingi mia moja na badala
yake akadai Shilingi mia moja na hamsini. Inaruhusiwa.
Kafiri ambaye haishi katika nchi ya
Kiislamu. Kwa Mwislamu anaweza kuchukua zaidi lakini ni haraam kwake
Mwislamu huyo kutoa zaidi. Hadi hapo Kafir Dhimmi (ambaye anaishi katika
nchi ya Kiislamu) anahusika, ni hraam kuingia naye katika mapatano
yoyote yanayohusisha riba. Kulipa na kuchukua iba, vyote ni haramu
katika sura hii.
Nyongeza ya madondoo kutoka hapa na pale
MADHAMBI NA ATHARI ZAKE
1. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar ,j.77,uk.79 na
Mustadrak Al-Wasail ,j.11, uk. 330 :
“Msitazame udogo wa dhambi, lakini muangalie muliyemuasi (Allah swt).”
2. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Bihar al- Anwar ,j. 70, uk.18
“Iwapo mtu anapenda kujiona vile alivyo
mbele ya Allah swt, basi ajitathmini kwa madhambi na maasi yake mbele ya
Allah swt; basi kwa kipimo hicho ndivyo alivyo huyo mtu mbele ya Allah
swt.”
3. Al-Imam as- Sadique a.s. aliwauliza
watu ni kwa nini wanamwudhi Mtume s.a.w.w. Basi mmoja wa watu alimwuliza
Imam a.s. vipi, naye Imam a.s. aliwaambia, Usul-i-Kafi , j.1, uk.219 :
“ Je hamujui kuwa matendo yenu
yapoyanajulishwa kwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. na pale aanapoona madhambi
dhidi ya Allah swt miongoni mwao, basi husikitishwa mno. Kwa hivyo
musimuudhi Mtume wa Allah swt na badala yake munatakiwa kumfurahisha
(kwa kutenda mema).”
4. Amesema Ali ibn Abi Talib a.s. , Ghurur al-Hikam, uk. 235
“Kukosa kusamehe ni kasoro moja kubwa kabisa na kuwa mwepesi katika kulipiza kisasi ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa.”
5. Kutokea Asbaghi bin Nabatah kutokea kwa Ali ibn Abi Talib a.s. amesema, Al-Khisal,cha as-Sadduq, j.2, uk. 360
“Amesema Mtume s.a.w.w. kuwa Allah swt
anapoikasirikia Ummah na kama hakuiadhibu basi bei za vitu vitapanda juu
sana yaani maisha yatakuwa ghali, maisha yao yatakuwa mafupi, biashara
zao hazitaingiza faida, mazao yao hayatukuwa mengi, mito yao haitakuwa
imejaa maji, watanyimwa mvua (itapungua), na watatawaliwa na waovu
miongoni mwao.”
(Yaani Hadith hiyo juu inatubainishia
kuwa iwapo kutakuwa na jumuiya ambayo imejitumbukiza katika madhambi
basi wanabashiriwa kupatwa na mambo saba hayo yaliyotajwa. )
6. Al-Imam al-Baqir a.s. amesema kuwa
amekuta katika kitabu cha Al-Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s.
akisema kuwa Mtume s.a.w.w. amesema: Safinat –ul-Bihar, j.2, uk.630
“Wakati zinaa itakapokithiri katika
jumuiya basi idadi za mauti za ghafla zitakithiri; na patakapokuwa na
uovu basi Allah swt atawatumbukiza katika maisha ya ghali na hasara.
Wakati watu watakapoacha kulipa zaka , basi ardhi itazinyakua baraka
zake kutokea mazao, matunda, madini na vitu vyote kama hivyo. Wakati
watakapotenda bila haki kwa mujibu wa Shariah, basi itakuwa sawa na
kumsaidia dhalimu na ugaidi. Na watakapozikiuka ahadi zao, basi Allah
swt Allah swt atawafanya maadui wao kuwasaliti na kuwakandamiza. Wakati
watakapoacha uhusiano pamoja na ndugu na jamaa zao, basi yote yale
wayamilikiayo yatakwenda mikononi mwa waovu. Na wakati watakapojiepusha
na kutoa nasiha ya mambo mema na kuyakataza maovu na kama hawatawafuata
waliochaguliwa Ahl-ul-Bayt a.s., basi Allah swt atawasalitisha kwa walio
wenye shari miongoni mwao na katika hali hii, wataomba duaa lakini
hazitakubalika.”
7. Amesema Al-Imam Ali ibn Abi Talib a.s. , Bihar al- Anwar , j.70,uk.55
“Machozi hayaishi illa kwa nyoyo kuwa ngumu, na nyoyo haziwi ngumu illa kukithiri kwa madhambi.”
8. Allah swt alimwambia Mtume Dawud a.s.: Ithna-Ashariyyah, uk.59
“Ewe Dawud ! Wabashirie habari njema
wale watendao madhambi kuhusu msamaha wangu, ambayo inajumuisha kila
kitu kilichopo humu duniani, ili wasikate tamaa ya msamaha wangu; na
waonye wale watendao mema kwa adhabu zangu ili wasije wakajifanyia
ufakhari kwa utii wao, kwani ufakhari ni dhambi mbaya kabisa.”
ALLAH ANAJUA ZAIDI