KUHUSU MAMBO YA MAITI
Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu,
sura ya 'TABARAKA' Aya ya kwanza na ya pili, Amesema hivi "Ametukuka
yule Ambaye Mkononi mwake umo ufalme wote; naye ni Mwenye uwezo juu ya
kila kitu. Ambaye Aliumba kifo na uzima ili kukujaribuni (kukufanyieni
mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni
Mwenye nguvu na Mwenye Msamaha. (67:1 na 2).
Kwa kuwa mauti ni haki na lazima, na
aendapo huko binadamu atayakuta aliyoyachuma mazuri au mabaya, na kila
nafsi ni rehani kwa aliyoyachuma, basi ayatende yale ya kumridhisha Mola
kwa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu, Mtukufu Mtume [s] nauwongozi
wa Ahlul Bait [a] watakatifu. Tusiwe miongoni mwa wale ambao Mwenyezi
Mungu Ameeleza katika Qur'ani habari zao. "Ni kipi kilichowapelekeni
Motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali, wala
hatukukuwa tukilisha Maskini na tulikuwa tukipiga porojo na kuzama
katika maasi pamoja na waliokuwa wakizama, na tulikuwa tukikadhibisha
Siku ya hukumu (Siku ya Qiyama) Mpaka mauti yakatufika". (74:42 hadi 47)
Mwenyezi Mungu Atubarikie "Husnul Khatimah" (Amin).
Kwa vile mauti ni lazima kwa kila kiumbe
kilicho hai, kwahiyo imekuwa ni lazima kwa kila kiumbe kufariki na
kuacha dunia. Basi ni lazima kwa kila Mwislamu anapoona alama za mauti
ausie (afanye wasia) kuhusu mali kama anayo, kuhusu madeni, amana za
watu, saumu, Hija (kama hakuhiji na hali ilikuwa fardhi kwake kuhiji) na
Sala kama ameacha hakuweza kukidhi. Ni Sunna mtu kuandika wasia wake na
akaweka chini ya mito yake.
HUKUMU KATIKA HALl YA "IHTIDHAAR" (KUKATA ROHO)
Mambo
anayofanyiwa mtu anapokata roho na baadaye: Mwislamu anapofika katika
hali ya Ihtidhari (wakati wa ukata roho), mwanamume au mwanamke, mkubwa
au mdogo; ni wajibu (ni fardhi) kwake kama anajiweza na anayo fahamu na
kama si hivyo basi kwa wale watu waliohudhuria hapo wamlaze huyo mgonjwa
chali, miguu na nyayo zake zielekee Qibla, na ikiwa haimkiniki kufanya
hivyo kwa ukamilifu basi kadri itakavyomkinika waanye, na ikiwa
haimkiniki kabisa basi wamkalishe kuelekea Qibla. Na kama hiyyo pia
haimkiniki basi wamlaze mkono wa kulia au wa kushoto kuelekea Qibla.
Ni Sunna:
Wakati ule waliohudhuria wamfahamishe na kumtamkia 'Shaadatain' na
majina matakatifu ya Maimamu kumi na wawili [a] na itikadi zote za haki,
akumbushwe (kwa utaratibu na upole si kwa haraka na ukali aweze
kufahamu kwa kukaririwa kaririwa).... Na pia asomeshwe dua maarufu
iitwayo, "KALIMAA-TUL FARAJ nayo ni hii:
LAA-ILAA-HA,
IL-LAL-LAA-HUL HALIMUL KARIM, LAA-ILAA-HA IL-LAL-LAA-HUL ALIYYUL ADHIM,
SUB-HAA-NAL-LAA-HI RAB-BIS-SAMAA WAA-TIS-SAB-I, WA RAB-BIL
ARA-DHIY-NAS-SABI-WAMAA FIY-HIN-NA, WAMAA BAY-NAHUN-NA, WAMAA
TAH-TA-HUN-NA WARAB-BIL AR-SHIL ADHIYM WAL-HAMDU LIL-LAA-HI, RAB-BIL AA
LAMIN, WAS SALA'A-TU ALAA MUHAMMADIN WA AALIHIT-TAYYIBEEN.
Ni Sunna:
Wakati ule asomewe sura ya YAASIN, WAS-SAAFATI, AHZABI, AYATUL KURSI",
na aya tatu za mwisho za sura ya BAQARAH, na pia kama iki Mkinika
asomewe sura zaidi. Kwa kufanya haya yule mgonjwa atakata roho kwa raha
bila ya taabu.
Mwenye
Janaba na mwanamke mwenye hedhi (ujusi) wakati wa kukata roho wasije na
wasimsogelee, kwani (Malaika hawatahudhuria ikiwa watu hao wapo hapo).
HUKUMU BAADA YA KUFA
Baada ya kufa ni sunna, (1) Kufumbwa
macho yakiwa wazi (2) Kuzibwa kinywa kwa utepe utakaopitishwa chini ya
taya na kufungwa tanzi juu ya kichwa, (3) Kunyooshwa mikono, miguu na
mapaja yake, (4) Kufunikwa shuka na kama amekufa usiku, mahala hapo
pawashwe taa wasimwache maiti kizani, (5) wapashwe wenye imani
(Waislamu) majira za mazishi ili waweze kuhudhuria mazishi yake, na
wafanye haraka upesi kuzikwa. Lakini kama hawana yakini kwa kufa kwake,
basi wasubiri hata wayakinishe, na kama maiti mwenye mimba, na mtoto yu
hai basi asizikwe mpaka apasuliwe upande wa kushoto na kutolewa mtoto na
baadaye ashonwe.
Mtu akishakufa na kupoa mwili wake mtu
yoyote atakayemgusa yule maiti kabla hajawoshwa ghusli tatu kwa viungo
au mwili wake,, kwa sehemu yoyote ya mwili wake itamlazimu aoge GHUSLU
MASSI Al- MAYYIT, yule mwenye kumgusa.
HUKUMU ZA KUMWOSHA MAITI
Ni
fardhi juu ya kila Mwislamu kumwosha maiti huyo, na kutengeneza mazishi
yake yote, lakini wakishajitokeza watu kumshughulikia huyo maiti basi
kwa wengine fardhi hiyo huondoka.
- Ni haramu mwanamke kuoshwa na mwanamume, au mwanamume kuoshwa na mwanamke, lakini mke ana weza kumwosha mume hata kama wapo wanaume, na mume anaweza kumwosha mke hata ikiwa wapo wanawake wa kumwosha.
- Mwanamume anaweza kumwosha mtoto wa kike asiyezidi miaka mitatu, na pia mwanamke anaruhusiwa kumwosha mtoto wa kiume asiyezidi miaka mitatu.
- Ikiwa hakuna mwanamume wa kumwosha mwanamume, wanawake walio karibu naye kwa ujamaa na damu wanaweza kumwosha, kama mama, dada, shangazi, mama mdogo (dada wa mama yake). Vivyo hivyo ikiwa maiti mwanamke na hakuna mwanamke wa kumwosha huyo maiti, basi majamaa waliokaribu naye kwa ujamaa na damu wanaweza kumwosha kama baba, ndugu, na mtoto wake na wale ambawo ni haramu kumuoa, kwa kisheria wanaitwa "MAH-RAM".
- Mtoto aliyezaliwa kwa kuharibika mimba, ikiwa mimba iko chini ya miezi minne (bado hakukamilishwa umbo lake) huyu hana haja ya kuogeshwa (kumuosha GHUSLI), ni lazima aviringishwe katika kitambaa na akazikwe. Lakini mimba ya miezi minne au zaidi (aliyekamilika umbo lake), lazima aogeshwe na kuvikwa sanda kama desturi.
- Mwenye kumwosha maiti lazima awe mwislamu, tena Shia, na awe amebalehe, mwenye akili, na ajue namna ya kumwosha maiti.
- Ni fardhi kumwosha Mwislamu hata akiwa wa madhehebu nyingine, lakini utamwosha kwa mujibu ya Madhehebu ya Shia lthnaasharia tu.
- Mwosha maiti anapomwosha maiti anuwie kama ninafanya kazi hii Qurbatan llal-Laahi Taala, na vitu vyote avitumiavyo kwa kumwosha maiti viwe vya halali, si vya kunyang'anya au kuiba hata maji na mahala atumiapo wakati wa kumwosha maiti pawe pa halali.
SUNNA ZA KUMWOSHA MAITI
- Awekwe mahala palipo juu, kama kitanda, au baraza n.k. na mahala pa kuwekea kichwa chake painuke zaidi kuliko miguu.
- Alazwe chali, miguu na nyayo zielekee Qibla (kama tulivyotaja katika mambo ya hali ya 'IHTIDHARI'.
- Maiti avuliwe nguo zote kwa upande wa chini (miguuni) hata ikibidi itatuliwe (ichanwe) lakini kwa idhini ya warithi wa maiti.
- Aoshwe chini ya sakafu, au banda au hema asioshwe chini ya mbingu.
- Uchimbwe "UFUO" wa kuingia maji ya kuoshea.
- Mwili wake wote uwe wazi isipokuwa utupu wake.
- Ufunikwe utupu wake hata ikiwa mkoshaji au watu wanaomuosha ni miongoni mwa wale wanaoruhusiwa kumwangalia.
- Mkoshaji apitishe mkono wake juu ya tumbo la maiti kwa taratibu lakini ikiwa maiti mwenye mimba ambaye mtoto pia amekufa tumboni hairuhusiwi kufanya hivyo.
- Mkoshaji asimame upande wa kulia wa maiti.
- Aanze kuosha upande wa kulia wa kichwa cha maiti.
- Mkoshaji aoshe mikono yake mara tatu hadi begani kwa kila 'GHUSLI' tatu.
- Mwoshaji anapokuwa anaosha kiwiliwili cha maiti anatakiwa aseme hivi: "Ewe Mola! Hiki ni kiwiliwili cha mja wako mwenye imani (Mumin) na umetoa roho yake kutoka kiwiliwili chake, na umetenga kati yao, basi msamehe kwako." Hasa wakati anapomgeuza.
- Asitangaze mwoshaji aibu yoyote aliyoiona mwini mwa maiti.
UTARATIBU WA KUMWOSHA MAlTI
(a)
Baada ya kusafishwa mwili wake wote kwa sabuni (au kitu kingine) na
kuondoshwa uchafu wa aina yo yote kama (madawa, marhamu au mafuta) ndipo
huyo mwoshaji Mwislamu atamwosha ghusli tatu (mara tatu kuoshwa). Ni
sunna kabla ya kuanza kumwogesha maiti ghusli tatu, atamwosha mikono
yake mara tatu, kwa kila ghusli.
(b)
Kwa mara ya kwanza, atachanganya katika maji ya kumwoshea maiti kidogo
SIDRI (majani ya mkunazi) kwa kutia katika pipa la maji anachochotea
maji ya kumwoshea huyo maiti (atayafikicha yale majani yapate kutoa
harufu), wala asitie majani mengi hata maji yawe mudhafu. Baada ya
kumaliza ghusli ya kwanza atakisuza kile chombo (pipa) kuondoa harufu ya
Sidri.
(c)
Na kwa mara ya pili atamwosha kwa maji yaliyochanganishwa na 'Kaafuri'
(Karafu maiti) kidogo tu, wala asitie nyingi hata maji yakawa mudhafu.
Tena atasuza pipa baada ya kumaliza ghusli ya pili ili kuondoa harufu ya
Kaafuri.
(d)
Na kwa mara ya tatu atamwosha (ghusli) kwa maji haya ya kawaida yaliyo
safi bila ya kuchanganywa na cho chote, na hii ndio mara ya mwisho. Ni
sunna mwoshaji katika muda anapomwosha maiti awe anasoma, "AFWAN AFWAN".
HADHARI:
Taratibu zote za kuosha ni lazima zifuatwe na kama si hivyo GHUSLI ya
maiti hubatilika na ni lazima uanze upya kwa utaratibu ule ule
tuliyoueleza.
Kwa
hivyo huyo maiti wa Ki-Islamu baada ya kuoshwa ghusli tatu hizo kama
tulivyoeleza, sasa atakuwa ametaharika, Mwislamu yo yote akimgusa wakati
huu, hakuna haja ya kuoga kwa yule mwenye kumgusa, lakini ikiwa baada
ya kutoka roho na kupoa mwili, na kabla hajapewa (maiti) hizo ghusli
tatu, akimgusa tu kwa mwili (si juu ya nguo) basi kwa kila mwenye
kumgusa ni fardhi juu yake aoge "ghusli massul Mayyit", (ghusli ya
kumgusa maiti). Na ghusli (kuoga) hiyo ni faradhi kwa mujibu wa
Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) tu.
NAMNA YA KUMWOSHA MAITI
Baada ya kusafishwa mwili wote wa yule
maiti hapo (yule mwoshaji) atanuia kuwa, namwosha (huyu maiti) ghusli ya
kwanza kwa maji yaliyochanganyishwa na majani ya mkunazi kama
tulivyoeleza huko nyuma.
(a) Kwanza ataanzia kwa kummwagia maji
kichwani (maji yafike hadi utosini kwenye ngozi) masikio, pua, mdomo,
macho na shingo pia aoshe. Ahakikishe kilmara anapomwosha, maji yafike
sehemu zote za mwili wake.
(b) Tena upande wa mbele wa kulia kutoka
begani chini ya shingo na pote kulia hadi kwenye nyayo tena baadaye
amlaze ubavu amwoshe sehemu ya nyuma kama alivyomwosha sehemu ya mbele
ya kulia.
(c) Baadaye atamwosha upande wa mbele wa kushoto na baadaye upande wa nyuma kama alivyomwosha upande wa kulia.
(d) Utupu wa maiti lazima uoshwe
anapokoshwa kila upande (maana yake kwa kila mwosho (ghusli) ataosha
utupu mara mbili). Ni haramu kuangalia utupu wa maiti na mwoshaji
akiangalia ametenda dhambi, lakini ile ghusli haibatiliki.
(e) Mwoshaji wakati anapoosha utupu wa
maiti Iazima aviringe kitambaa au avae mfuko wa kitambaa mkononi, ni
haramu kupeleka mkono upekee.
Hii ndio namna ya kumwosha maiti ambayo
utaratib huo kwa kisheria unaitwa "ALGHUSL AT-TAR-TIBI" na inambidi kwa
kila mwenye Janaba pia akitaka kuondo (kuoga) Janaba au mwanamke mwenye
hedhi au nifasi au kuoga ghusli za sunna lazima waoge vivyo hivyo kama
tulivyoeleza katika kitabu chetu cha Sala (mlango wa ukurasa wa 33).
Kwa kuoshwa ghusli tatu hizo, tena haina
haja kumwogesha, ghusli ya janaba au hedhi au nifas ikiwa maiti alikuwa
katika hali ile.
Ikiwa SIDRI (majani ya mkunazi) au
KAA-FUR (Kafuri maiti) zote mbili au mojawapo haipatikani, basi maiti
ataoshwa kwa maji haya ya kawaida kwa nia ya badala ya Sidri au Kafuri
mradi lazima maiti aoshwe Ghusli tatu tu (mara tatu).
(a) Ikiwa maji hayapatikani au maiti
ameungua au alikuwa na maradhi fulani na akitiwa maji nyama au ngozi
itatoka, basi badala ya maji atafanyiwa Tayamamu mara tatu kwa Ghusli
tatu.
(b) Tayamamu ni lazima ifanywe na yule
hai, na kumpaka maiti, na kama inamkinika kutayamamu kwa mikono ya maiti
pia ifanywe - (Namna ya Tayamamu angalia kitabu chetu cha 'Sala'
ukurasa wa 44 Mlango wa 8).
MAMBO YA FARADHI BAADA YA KUOGESHWA MAITI HADI KUZIKWA KWAKE
Haifai wakati anapooshwa maiti kuweko moto au kiteso cha kufukiza wala wakati wa mazishi hadi mwisho.
AL-HUNUUT:
Kupakwa maiti kafuri mahali maalum ni faradhi kwa Waislamu baada ya
kumwosha na kupanguswa (afutwe vizuri kwa nguo kavu) maiti kabla ya
kusaliwa na kuzikwa apakwe 'Kafuri' laini sehemu saba (viongo vya
kusujudia) navyo ni kipaji, viganja viwili, magoti mawili, ncha za
vidole gumba viwili. Na sunna kupakwa kwenye pua, vile vile sunna
kuwekwa pamba kwenye utupu wa maiti na kila penye tundu. Wakati wa
kupaka HUNUUT ni baada ya kuogeshwa na kupanguswa na kabla ya kuvikwa
sanda au wakati wa kuvikwa sanda.
Ikiwa
Kafuuri haikupatikana hatakumwoshea maiti, basi hapo faradhi ya HUNUUT
inaondoka, na kama amekogeshwa na Kafuuri lakini haikuzidi kwa ajili ya
HUNUUT basi si kitu.
AL-HUNUUT:
Kupakwa maiti Kafuri ni faradhi kwa kila maiti mdogo, mkubwa mwanamke,
mwanamume, huru au mtumwa isipokuwa maiti yule aliyekufa hali yuko
katika Ihramu ni haramu kumpaka Kafuri. Kafuri lazima iwe mpya si kukuu yenye kupotea harufu yake, na pia lazima iwe laini iliosagwa.
SANDA YA MAITI ILIYO WAJIBU
Ni faradhi kuvishwa maiti mwanamume au mwanamke mkubwa au mdogo vipande vitabu vya nguo:
(1) Kanzu (2) Shuka (3) Shuka
(1) Kanzu: Bila kuishona, itobolewe sehemu ya shingo tu halafu kitumbukizwe kichwa. Kuanzia begani hadi nusu ya miguu kupita goti.
(2) Shuka: Kama anavyovaa mwanamume kutoka kitovuni
hadi magotini, na ni bora si wajibu kuanzia kifuani hadi chini ya magoti.
(3) Shuka: Kitambaa
kikubwa cha kumfunika mwiIi wake wote mzima mbele na nyuma kwa urefu
hata uweze kufunga pande zote mbili (upande wa kichwa na upande wa
miguu) na kwa upana, ncha moja iweze kuja juu ya ncha va pili
SUNNA: Si wajibu bali ni sunna (a)
Kuvishwa mwanamume kiIemba, mwanamke sidiria na ushungi (b) Nguo nyeupe
isiyokuwa na rangi yoyote (c) Nguo iwe ya pamba (d) Ni bora kama aliwahi
kuhiji basi 'IHRAMU' itumiwe au nguo za kusalia ambazo akisali nazo.
SANDA: Kwa kiasi kilichofaradhi lazima
gharama yake na gharama ya vitu vya kumwoshea maiti, maji, Sidri,
Kafuri, ardhi pa kuzikiwa na gharama zake zote haya hutoka katika asili
ya mali ya maiti kabIa ya kulipwa deni au kufuatwa wasia wake. Na yako
mambo ya sunna katika sanda ikiwa ameusia sanda itolewe katika theluthi
(1/3) ya mali yake, au ameusia theluthi ya mali atumiliwe yeye basi
sanda itatolewa humo, na kama hakuusia theluthi (1/3) basi kiasi
kilichowajibu kitatolewa katika asili mali.
Sanda ya mke juu ya mumewe hata ikiwa
mke anayo mali ya kutosha, na vivyo hivyo yule mke aliyeachwa kwa mara
ya kwanza au ya pili na bado yupo katika eda, mume lazima atoe sanda.
Ikiwa mtu mwingine yoyote ametoa sanda ya yule maiti (mwanamke) basi
faradhi humuondokea mume.
Ni sunna kwa kila mwislamu kutayarisha
SANDA yake na kuiweka nyumbani, pia ni sunna kuiangalia hiyo sanda kila
mara. Mtukufu ,Mtume (s.a.w.) amesema, "Mwenye kutayarisha sanda yake,
huwa kila siku zipitazo kila huandikwa thawabu kila apoiangalia, na kwa
kufanya hivyo hatahesabiwa miongoni mwa waliomsahau Mwenyezi Mungu.
NAMNA YA KUMKAFINI (KUMVISHA SANDA MAITI)
Baada
ya kukatwa mapande hayo, kwanza utatandika ile shuka kubwa ya Namba 3:
Na ndio ya kwanza, baadaye utatandika Kanzu Kanzu kwa kuikunjua upande
mmoja, (na hii ni ya pili), baadaye utaliweka shuka kwa upana kwa
kukunjua. Ukisha tandika yote hayo vipande vitatu vya vitambaa vilivyo
wajibu, basi sasa atalazwa maiti juu ya mapande yote ya sanda.
- Kwanza utamfunga shuka na kuondoa kile kitambaa ulichotumia wakati wa kumwoshea kuficha utupu wake.
- Utaurejesha ule upande wa kanzu ulioukunjua kwa kupitisha kichwa cha maiti kwenye shingo.
- Ikiwa umeshafanya mambo ya 'AL-HUNUUT' basi utaikunja hiyo shuka kubwa kwa kuiweka ncha moja juu ya pili, na kama bado hujampaka AL-HUNUUT na mambo yake basi fanya, ndipo umalize kumfunika.
KUMSALIA MAITI
Sala Ya Mait: Lazima iwe baada ya
kuvishwa sanda na kutia HUNUUT (KUPAKA KAFURI kwenye VIUNGO VYA
KUSUJUDIA). Kuanzia maiti mwenye umri wa miaka sita (6) huwa faradhi
kusaliwa sala ya maiti.
Sala ya maiti haina Adhana wala Kukimu
na pia hakuna rukuu wala sijda, lakini inakusimama tu, na ina Takbira
tano tu (badala ya sala tano za faradhi za kila siku). Hakuna shuruti ya
kuwa na wudhuu lakini ni sunna kuwa nao. Ni sunna pia wakati wakutoa
kila Takbira, anyanyuwe mikono hadi masikioni mwake yule mwenye kuswali.
Namna Ya Kumsalia Maiti:
Mwenye kumsalia lazima asimame nyuma ya
jeneza (jeneza liwe mbele yake) asiwe mbali nae, aelekee Qibla, kichwa
cha maiti kiwe upande wa kulia wa mwenye kumsalia, na miguu upande wa
kushotona awe amesimama. Akiwa maiti mwanamume basi ni sunna kusimama
kati-kati na akiwa maiti mwanamke, asimame sawa na kifua cha maiti.
Huwezi kumsalia maiti asiyekuwa mbele yako ijapokuwa akiwa mjini humo.
Namna ya Kumsalia Maiti kwa Njia ndefu.
(1) Baada ya kupata
ruhusa kwa wafiwa ndipo kwanza atatia nia ya kumsalia huyo maiti aliyoko
mbele yake. Nia ni moyoni tu, kutamka si lazima katika ibada zote za
faradhi (isipokuwa katika mambo ya Hijani sunna kutamka).
(2) Baada ya Takbira ya kwanza atasema hivi:
ASH-HADU AN LAA ILAA-HA IL-LAL LAA-HU
WAH-DAHU LAA SHA-RIY-KA LAH, WA ASH-HADU AN-NA MUHAM-MADAN
AB-DUHU-WARA-SUU-LUH, AR-SALA-HU BIL-HAK-KI BASHIY-RAN WANA-ZIY-RAN
BAY-NA YADA-YIS-SAA-AH.
(3) Baada ya Takbira pili atasema:
AL-LAA-HUMMA SAL-LI ALAA MUHAM-MADIN WA
AALI MUHAM-MAD, WAR-HAM MUHAM-MADAN WA AALA MUHAM-MAD, KA-AFDHALI MAA
SAL-LAY-TA, WABAA-RAK-TA, WATA-RAH-HAMTA, ALAA IB-RAA-HIMA, WA AALI
IB-RAA-HIM- IN-NAKA-HAMIY DUN MAJIYD, WA SAL-LI ALAA JAMIY-IL AN-BIYAA-I
WAL MUR-SALIYN".
(4) Baada ya Takbira ya tatu atasema:
"AL-LAA-HUM-MAGH-FIR LIL MU'U-MINIY-NA
WAL MU'U-MINAAT WAL MUS-LIMINA WAL MUS-LIMAAT, AL-AHYAA-I, MIN-HUM
WAL-AMWAATI, TAA- BIU,BAY-NANAA- WA BAY -NAHUM BIL-KHAY-RAATI, IN-NAKA
MUJIY-BUD DA'AWAAT IN-NAKA ALAA KUL-LI SHAY-IN-QA-DEER".
(5) Baada ya Takbira ya nne atasema hivi:
AL-LAA-HUM-MA IN-NA HAA-DHAA, AB-DUKA
WAB-NU AB-DIKA,WAB-NU AMA-TIKA, NAZALA BIKA WA-ANTA, KHAY -RU
MAN-ZUU-LIN BIH, AL-LAA-HUM-MA, IN-NAA, LAA, NA'ALAMU MIN-HU, IL-LAA
KHAY-RAA, WA AN-TA, A'ALAMU, BI-HI MIN-NAA, ALLAA-HUM-MA IN- KAA-NA,
MUH-SINAN, FAZID FlY IH-SAA-NIH, WA-IN -KAA-NA, MUSIY-AN, FATA-JAA-WAZ
AN-HU-WAGH-FlR LAH, AL-LAA-HUM-MA, AJ-ALHU IN-DAKA FIY, A' ALAA IL-YEEN,
WAKH-LUF ALAA AH-LIHI, FIL GHAA-BIRIYN, WARHAM-HU, BIRAH-MATIKA YAA
AR-HAMAR-RAA-HIMIYN.
Akiwa Maiti ni Mwanamke baada ya Takbira ya nne atasema hivi :
AL-LAA-HUM-MA IN-NA HAA-DHIHI, AMATUKA
WAB-NATU AB-DIKA,WAB-NATU AMA-TIKA, NAZALAT BIKA WA-ANTA, KHAY -RU
MAN-ZUU-LIN BIH, AL-LAA-HUM-MA, IN-NAA, LAA, NA'ALAMU MIN-HA, IL-LAA
KHAY-RAA, WA AN-TA, A'ALAMU, BI-HA MIN-NAA, ALLAA-HUM-MA IN- KAA-NAT,
MUH-SINATA, FAZID FlY IH-SAA-NIHA, WA-IN -KAA-NAT, MUSIY-ATAN,
FATA-JAA-WAZ AN-HA WAGH-FlR LAHA, AL-LAA-HUM-MA, AJ-ALHA IN-DAKA FIY, A'
ALAA IL-YEEN, WAKH-LUF ALAA AH-LIHA, FIL GHAA-BIRIYN, WARHAM-HA,
BIRAH-MATIKA YAA AR-HAMAR-RAA-HIMIYN.
(6) Utatoa Takbira ya tano ni kama salamu ya hiyo Sala.
Pia kuna njia fupi ya kumsalia Maiti huyo, nayo ni na ifuatayo:
(1) Baada ya Takbira ya kwanza atasema "ASH-HADU LAA-ILAA-HA IL-LAL-LAAH WA ASH-HADU ANA-MUHAM-MADAR RASUU-LUL-LAAH."
(2) Baada ya Takbira ya pili atasema: AL-LAA-HUMA SAL-LI ALAA-MUHAMMADIN WA AA-LI MUHAMMAD.
(3) Baada ya Takbira ya tatu:
AL-LAA-HUM-MAGH- FIR LIL MU'U-MINIY-NA WAL MU' MINAA-TI.
(4) Baada ya Takbira ya nne atasema hivi:
AL-LAA-HUM-MAGH-FIR LI-HAA-DHAL, MAY-YIT
(5) Akiwa maiti ni mwanamke baada Takbira ya nne sema hivi:
AL-LAA-HUM-MAGH-FIR LI HAA DHIHIL, MAY-YIT.
(6) Utatoa Takbira ya
tano ni kama salamu ya hiyo na, hakuna faradhi ya kusoma kitu baada ya
hiyo Takbira tano, ni sunna kusema, "RAB-BANAA AATINAA, FIDUN-YAA,
HASA-NA- TAN, WAFIL AA-KHIRATI; HASANATAN, WA QINAA ADHAA-BAN NAAR."
Ukisali namna hiyo pia yatosha.
Ikiwa baada ya kusaliwa maiti,
ikajulikana kwamba maiti alipinduka kifudifudi, basi lazima awekwe chali
na asaliwe tena. Na kama kwa kusahaulika maiti hakusaliwa hadi akazikwa
ni wajibu asaliwe juu ya kaburi, na vivyo hivyo ikiwa baada ya kuzikwa
ikajulikana kuwa sala aliyosaliwa si sahihi.
ADABU NA SUNNA ZA KWENDA NA JENEZA:
Thawabu
ya kufuata Jeneza: Imepokewa hadithi kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.) kwamba
amesema: "Habari njema na (bishara) nzuri ya kwanza atakayopewa yule
maiti 'MUMIN' ataambiwa, 'Karibu' kwa hakika Mwenyezi Mungu Amemghufuria
kila mwenye kufuata Jeneza lako, na Dua zote za wale waliokuombea
ughufuriwe Ameyakubali. Imam JAFFER AS- SADIQ (A.S.) Amesema, "Kila
mwenye kufuatana na Jeneza la mumin (mwenye imani) kwa kila hatua moja
aaendayo mpaka arudipo mazishini ataandikwa thawabu elfu mia, na kufutwa
madhambi elfu mia na kuongezwa daraja peponi elfu mia kwa kila hatua.
Mtukufu Mtume (s.a.w.) Amesema:
Ni sunna kila mwenye kuona jeneza alikabili na kulipokea na kusema maneno haya:
Basi mwenye kusoma hayo, Malaika wote wa mbinguni watalia kwa kumhurumia msoma dua hiyo.
Wanatakiwa
watu waende na maiti kwa heshima na adabu wasiongee na kuzungumza hasa
mambo ya kidunia au habari ya yule maiti, bali waende na huku wanasoma
dhikri kama "BIS-MIL-LAA-HI WA BIL-LAA-HI WASAL-AL-LAAHU ALAA
MUHAM-MADIN WA AA-LI MUHAM-MAD AL-LAA-HUM-MAGH-FIR LIL MU'U-MINIY-NA
WAL-MU'U-MINA-AT." Au dhikri yoyote ya Mwenyezi Mungu. Haifai kucheka
wala kuamkiana (kutoa salamu) na kwenda mbele ya jeneza, wala kuendesha
jeneza mbio mbio, isipokuwa kama inaogopewa maiti hiyo kuharibika au
inanuka. lnafaa kuwa nyuma ya jeneza au pande mbili ya jeneza.
Ni sunna kubeba jeneza kwa mpango ufuatao:
- Kwanza beba upande wa kulia wa mbele wa maiti kwa bega lako la kulia (kushoto ya jeneza).
- Njoo kwenye mguu wa kulia wa maiti kwa bega lako Ia kulia (kushoto ya jeneza).
- Njoo kwenye mguu kushoto wa maiti kwa bega lako la kushoto (kulia ya jeneza).
- Nenda kwenye mkono wa kushoto wa maiti kwa bega lako la kushoto. Baadaye utarejea kama awali (Ia kulia mara moja tu ukishafuata sunna hiyo) unaweza kukamata mahali popote pa jeneza au fuata mpango ule ule wa awali.
NAMNA YA KUZIKA
(1)
Ni faradhi kaburi lichimbwe kiasi cha kumfunika huyo maiti asiweze
kufukuliwa na wanyama na isiweze kusikilizana harufu yake
atakapoharibika.
(2) Ni sunna kuchimba kiasi cha urefu wa binaadamu au uchimbe hadi shingoni.
(3) Alazwe katika ubavu wa kulia iwe sehemu yake yote yote ya uso, kifua, tumbo na miguu (mwili wake mzima umeelekea Qibla).
Na ya Sunna ni haya:
(a)
Ardhi ikiwa ngumu inayoweza kujishika, ni lazima ukeketwe ukuta wa
Qiblani kiasi cha urefu wake na kwa upana kiasi cha kuweza kukaa huyo
maiti, ni lazima aIazwe kwa ubavu wa kulia, hapo kwenye mkeketo huo,
unaitwa mwanandani. Na ubao au kitu kingine uwe mgongoni mwake.
(b)
Ama ikiwa ardhi laini kama hivi hapa kwetu pwani, na mahala pengine,
mwanandani hachimbwi kwenye ukuta; unachimbwa chini upande wa Qibla,
achimbwe kiasi cha kuweza kukaa mtu na ubao unamfunika juu: hau mfuniki
mgongoni.
(c)
Awekewe mawe nyuma ili asipate kupinduka na kulala chali. Ikiwa mtu
ametumbukia kisimani na akafa na haikumkinika kumtoa humo, yule maiti
basi kizibwe hicho kisima na litakuwa ndilo kaburi lake.
(d) Ni bora wateremke watu wasio jamaa lakini akiwa maiti mwanamke si halali kushuka humo asiyekuwa Mahram (jamaa wa karibu).
(e) Jeneza liwekwe upande utakaokuwa miguu ya maiti anapolazwa kaburini kwani hapo ni mlango wa kaburi.
(f) Jeneza liwekwe kidogo mbali na kaburi kiasi cha mikono miwili au mitatu (3), baadaye iondolewe na ku wekwa mara tatu mpaka kufika kwenye kaburi.
(g) Ni sunna wenye kushuka katika kaburi wawe na (Tahaara) wudhuu, kichwa wazi, miguu wazi na waka wa kutoka watoke upande wa mguu wa maiti.
(h) Atolewe maiti jenezani kwa kichwani, na kuteremshwa kaburini kwa upole bila haraka.
(i) Ikiwa maiti ni mwanamke, jeneza liwekwe upande wa Qibla na maiti atolewe kwa upana, na tangu wakati wa kutolewa maiti (mwanamke) mpaka kwisha funika mwana ndani, kaburi liwe limefunikwa nguo.
(j)
Kuna dua wakati wa kuteremsha maiti na kama hawajui basi wataje dhikri
yoyote ya Mwenyezi Mungu. Wakati wa kumtoa maiti humo jenezani na
kumlaza kaburini ni sunna kusoma hao wanaomtoana kumlaza dua ifuatayo:
BISMILLAHI
WA BIL-LAAHI WA 'ALA MILLATI RASULILLAH. ALLAHUMMA ILAA RAHMATIKA LAA
ILA 'ADHABIKA. ALLAHUMMA IFTAH LAHU FI QABRIHI WA LAQINHU HUJJATAHU WA
THABIT-HU AL-QAWL ATH-THAABIT WA QINA WA IYYAHU 'ADHABAL QABR.
Na wanapoliona kaburi waseme:
ALLAHUMAJ-ALHU RAWDATAN MIN RIYADIL JANNAH WA LA TAJ-ALHU HUFRATAN MIN HUFURIN-NAAR
(k)
Afunguliwe vile vitanzi, halafu iregezwe regezwe ile sanda, na kusogeza
sanda kwenye shavu la kulia mpaka lilalie mchanga, itakuwa vizuri kama
akitengenezewa mto wa mchanga kwenye kichwa chake.
JARIY-DATAIN
Ni sunna iliohimizwa sana kwa SHIA WA
AHLUL-BAIT (A. S.) kuwekewa maiti vijiti viwili vibichi vya mti wa
mtende, kiasi cha urefu wa kila kijiti kiwe mkono mmoja, ambao huitwa
"JARIY-DATAIN". Huandikwa juu ya maiti hayo jina lake na Ia baba yake
maiti na Shahadatain, na majina ya Maimamu kumi na wawili (a.s.). Maiti
huwa haadhibiwi vijiti vinapokuwa vibichi mpaka kukauka.
Sunna hii ya kuwekewa vijiti viwili vya
mtende imeanzia zama za Mtume ADAM (A.S.) alipofanya wasia na ikaendelea
zama za Mitume wote na ikawachwa zama za JAHILIA na Mtume wetu (s.a.w.)
akaanzisha upya, na inafaida sana kwa maiti. Siku moja Mtukufu Mtume
(s.a.w.) alipita kwenye kaburi la maiti ambaye alikuwa ana aadhibiwa
akaamrisha yaletwe vijiti vya mtende na papo hapo akakata vipande
viwili, kimoja akakifukia kwenye kichwa na cha pili kwenye miguu, na
akasema, "Sasa atapunguziwa adhabu".
Moja katika vijiti hivyo kiwekwe mkononi
ya kulia karibu na shingo la maiti kwa kugusanana maiti na cha pili
upande wa kushoto juu ya kanzu chini ya shuka. Vijiti hivi viwe vya
mtende au mkomamanga hata ya mnazi yanafaa, na ikiwa yote hayo
hayapatikani basi, vijiti vya aina yoyote vinafaa na bora vile
vinavyochelewa kukauka.


allah anajua zaidi shukra