MCHANGO WA UISLAMU
KATIKA
MAENDELEO YA MWANADAMU
Katika
maelezo mafupi namna hii haiwezekani kuwepo kwa suala la kutaka
kuorodhesha namna ambavyo utamaduni wa Kiislam ulivyochangia katika
maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu.
Hatuna
njia ila kutaja japo kwa uchache tu wa ugunduzi muhimu uliotokana na
vipaji vya watafiti wa Kiislam na pia kutaja wachache kati ya wasomi,
wanafalsafa na waandishi wa kiislam walioongeza hamasa katika elimu ya
sayansi na fasihi, na kuzivuta fikra za watu wa Magharibi (wazungu).
Unajimu (Astronomy): Elimu ya Anga na Sayari
Elimu
na sayansi za kwanza kuvuta shauku ya wasomi wa Kiislam zilikuwa ni
unajimu na Hisabati. Fikra zao zote bila ya shaka na mweleko wao
uliwafanya Waarabu kuiendea sayansi ya uhakika.
Unajimu hasa sio tu uliwavutia wanasayansi, bali pia Makhalifa wa Mashariki na wa Magharibi kutoka Hispania na wa Kirusi na Makhan
wa Kihindi pia walivutiwa na taaluma hii. Vituo vyya uchunguzi wa anga
vilianza kujengwa katika kila mji maarufu katika Himaya ya Kiislam. Vile
vya jiji la Baghdad, Cairo, Cordova, Toledo na Samarkand vilijipatia
umaarufu sana duniani.
Chuo cha Unajimu cha Baghdad kilijulikana tangu enzi za utawala wa AL-Mansur, Khalifa wa pili wa ukoo wa Abbassid aliyetawala miaka ya 754 na 775, na ambaye pia alikuwa mnajimu. Hata wakati wa tawala za warithi wake, Harun al-Rashid na AL- Mamun,
Chuo hiki kiliendelea kutoa kazi nzuri. Nadharia za zamani zilidurusiwa
na makosa kusahihishwa na pia Majedwali ya Kigiriki yalisahihishwa.
Chuo cha Baghdad kinastahili sifa kwa ugunduzi wa mizunguko ya sayari na
jua, tathmini ya upotofu uliokuwepo juu ya umbile lake na utaratibu wa
upunguaji wa mmuliko (ukali wa mwanga) wake, na pia ugunduzi wa kipimo
halisi cha hesabu ya mwaka.
Chuo
cha Baghdad kiligundua kuwa maeneo ya juu ya mwezi hayafuati kanuni
maalum. Pia walitabiri kuwepo kwa vituo vya jua, kupatwa kwa mwezi na
jua na kuwepo kwa vimondo na madude mengine angani. Walitafiti na
kubaini kuwepo kwa mzunguko wa dunia kwa jua. Pia walikuwa watafiti wa
kwanza kugundua Copernicus na Kepler.
Matokeo ya tafiti mbalimbali za vituo vilivyoasisiwa na Chuo cha Baghdad yaliwekwa kumbukumbu katika Jedwali la Unajimu lililothibitishwa, na Yahya bin Abu Mansur anaaminika kuwa muasisi na mtayarishaji wa jedwali hili.
Baadhi ya wasomi waliotokana na Chuo hicho ni pamoja na AL-Baitani,
ambaye Lalande amemworodhesha kuwa ni miongoni mwa wanajimu ishirini
(20) bingwa na maarufu waliowahi kutokea duniani. Mwingine ni Abu Wefa,
ambaye matokeo ya utafiti wake yalikuwa na ubora wa zaidi ya karne kumi
mbele ya ule ulio tolewa na Msomi wa Denmark aliyeitwa Tycho-Bracho,
ambaye alihusishwa na ugunduzi wa Abu Wefa kuhusu tofauti ya vipindi vya
mwandamo wa mwezi.
Ali Ibn Younis, mgunduzi wa (pendulum) timazi
au mizani ya saa na vipimo vya jua, ambaye Khalif AL-Haken aliyetawala
mnamo miaka ya 990 – 1021, alimwekea kumbukumbu kwa kujengewa kituo cha
utafiti wa anga katika Mlima Mucaddam, anaaminika kuwa mmojawapo wa
waanzilishi wa Chuo cha Cairo. Alilipitia jedwali la Hakim na kulihakiki
na kuliwekea usahihi ambao haukuwahi kufikiwa na mtu yeyote hapo nyuma.
Wakati huo huo, Hassan Ibn AL-Haitan, mnajimu mwingine na
mwanahisabati wa chuo cha Cairo, alitayarisha tasnifu (treatise) au
makala yake maarufu juu ya elimu ya Nuru (optics) au uoni, iliyosaidia
kuweka msingi wa kazi iliyofanywa baadae na Roger Bacon na Kepler.
Haishangazi kusikia kuwa Ibn Haitan alikuwa mtaalam wa kwanza
kupendekeza lijengwe Bwawa maarufu la Aswan nchini Misri ili kuinua
kiwango cha maji ya mto Nile.
Utafiti wa Anga ulitiliwa mkazo pia na utawala wa kiislam nchini Hispania. Amir wa Cordova, Abd aL-Rahman
wa pili, alionyesha shauku na nia ya kuendeleza elimu ya sayansi hii.
Kwa bahati mbaya ni tafiti ndogo tulizoweza kuzipata kutoka Hispania
ilipokuwa chini ya utawala wa kiislam. Karibu kazi zao zote ziliharibiwa
kutokana na vita vya kidini, ingawa tunaelewa kuwa kwa wakati huo,
vituo vya utafiti wa anga katika miji ya Toledo na Cordova vilikuwa
maarufu. Historia imeweza kutuhifadhia majina ya baadhi ya wasomi wa
Andalusia kama Maslamah AL-Mahrebi, Omar Ibn Khaldun, Ibn Rushd (Averroes)
na wengine wachache. Mtu anaweza kuhisi ubora wa kazi za Waislam hao
zilizoharibiwa kutokana na kazi zilzotolewa baadaye na wasomi wa
Kikristo waliosoma kwao na wengine waliosoma baadhi ya kazi za Waislam.
Hivyo, inaonyesha kuwa Majedwali ya kinajimu ya Mfalme Alfonso (X) wa Kumi, yalitokana na kwa kiasi kikubwa na kazi za wasomi wa Kiislam.
Vita
na migogoro ya ndani ambayo tangu karne ya kumi na moja vilivyozikumba
nchi za Asia, viliathiri sana maisha ya kisomi yaliyokuwa yamekwisha
jengeka katka jamii ya Kiislam. Bila shaka, vita hii ilizorotesha
maendeleo ya ustaarabu wa dunia, ingawa havikuyasimamisha kabisa. Chuo
cha Baghdad kwa mfano, kilinusurika na maanguko ya kisiasa ya Makhalifa
wa Nchi za Mashariki, yaliyoisambaratisha dola ya Kiislam. Ubunifu wa
Chuo hicho haukukoma ila uliendelea hadi katikati ya karne ya (15) kumi
na tano. Wakati huohuo, mvuto wake ulienea hadi kuzifikia nchi za Asia
ya Kati, India na hata Uchina. Mmojawapo wa wasomi wa Kiislam Abd aL-Rahman Mohammed bin Ahmad AL-Birun
aliyejenga mahusiano kati ya elimu ya Wasomi wa Shule ya Baghdad na ile
ya wasomi wa Kihindi, hakukosekana hata mara moja katika Ikulu ya Mahmud hapo Ghazna, aliyeishi mnamo miaka ya 997 – 1030. Mojawapo ya kazi zake nyingi ni uchapisho wa vipimo vya kijiografia vya Longitudo na Latitudo za miji mikubwa duniani.
Sultani wa Seljuk Malik Shah
aliyeishi mnamo (1072 – 1092), alikuwa msomi na mtawala aliyevutiwa na
taaluma ya unajimu. Uchunguzi alioukazania ulisababisha kufanyika kwa
marekebisho yaliyosahihisha na kuiboresha kalenda, karne kumi mbele ya
marekebisho yaliyofanywa kwenye kalenda ya Kigrigori (Gregorian calender). Heshima na sifa za marekebisho hayo yanamwendea hasa Abdur Rahman Hassan na Omar Khayyam, ambao kazi yao imewafanya kuwa watu mashuhuri wasioweza kusahaulika duniani.
Watawala wa Kimongoli nao waliikazania elimu ya sayansi. Hulagu,
mtawala aliyekuwa mkatili na ambaye ndiye aliyeuharibu mji wa Baghdad,
naye alijenga kituo cha utafiti wa anga hapo Meragah, na alimteua Nasr ed – Din Tusi
kuwa Mkurugenzi wake. Huyu alihusika na ukamilishaji wa vifaa
mbalimbali vilivyokuwa vikitumika kuchunguzia anga. Kutoka katika kituo
hicho kipya, matokeo ya kazi za Chuo cha Baghdad na Cairo yalifikishwa
hata Uchina ilipokuwa chini ya utawala wa Kubilai Khan.
Lakini ilikuwa ni wakati wa utawala wa Ulug Beg, mjukuu wa Tamburlaine, ambapo unajimu wa Waislam ulipopata mafanikio makubwa kabisa. Ulug Beg ambaye jina lake kama la baba yake Shah Ruh, linahusishwa kwa karibu sana na kazi nzuri za usanii na harakati za ufasaha (taaluma ya fasihi) zilizoendeshwa na Timuridh;
alikuwa mpenzi wa taaluma ya unajimu. Inaaminika kuwa alikuwa mmojawapo
wa wasomi wa mwisho mwisho waliotokana na Shule ya Baghdad. Kazi yake,
ambayo ilichapishwa mwaka 1437, ilitoa picha halisi juu ya maarifa ya
unajimu kwa siku hizo na mwelekeo wa taaluma hiyo kwa siku zijazo.
Somo la Hisabati (Mathematics)
Pamoja
na unajimu, Hisabati ni sayansi iliyopendwa sana na Waarabu. Kanuni
nyingi za hesabu, jiometri na aljebra ziligunduliwa na wasomi wa
Kiislam.
Katika
hesabu, mpaka leo bado tunatumia tarakimu na njia za kufanyia hesabu
zilizogunduliwa na Waarabu. Uvumbuzi wa aljebra unahusishwa moja kwa
moja na Waarabu. Wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Maarifa, Khalif AL- Mamun alimteua Mohammad Bin Mussa Bin Khwarizimi kuwa Mkuu wa Kituo hicho. Tasnifu yake katika aljebra inaitwa: "AL–Gebr WaL-Muqabala (yaani Hesabu kwa njia ya Alama)". Ni kutokana na sehemu ya kwanza ya kazi yake hii tulipopata jina la hesabu za "algebra" na kutokana na jina lake pia tumepata "algorithm". Kazi hii, kama ilivyotafsiriwa na Mzungu aitwaye Gerad mwenyeji wa Cremona, alisema: "baada
ya kuwa msingi wa jumba la hesabu lililojengwa na Waarabu waliomfuatia
baadaye, alikuwa na wazo la kuanza kuwafundisha watu wa Magharibi juu ya
ubora wa kutumia aljebra katika kufanya hesabu za ukokotozi (algebraic calculus) pamoja na decimali."
"Mojawapo
ya mawazo bora ya kisayansi toka kwa wasomi wa Kiislam, AL- Khwarismi
bila shaka ni mtu aliyetoa mchango bora katika maendeleo ya somo la
Hisabati wakati wa zama za karne za Kati na hata sasa", kama anavyodhani Philip Hitti.
Kazi yake iliendelezwa na Thabit bin Gharrah, aliyefasiri Almagest, kazi ya Ptolemy, aliyegundua matumizi ya algebra katika hesabu za changanuzi (jiometri au geometry).
Trigonometria
(elimu ya hesabu za pembe tatu) ni mojawapo ya elimu ya hesabu ambayo
Waarabu waliiendeleza kwa bidii kutokana na matumizi yake katika
uchunguzi wa anga.
Hatua
za awali katika elimu hii zinaanzia kwa AL-Baitani, aliyekuwa na kipaji
cha kugundua hesabu za vipande vya mduara (arc), ambazo Wagiriki
walizitumia katika kufanyia mahesabu yao. "AL- Baitani alikuwa wa
mwanzo kutumia katika kazi zake za mahesabu, maneno ya ‘sine’ na
‘cosine’. Pia alikuwa mwanzilishi wa hesabu za ‘tangent’ wakati huo
ikiitwa: kivuli endelevu (au extended shadow)."
Uanzishaji wa matumizi ya "tangent"
(au msitari unaogusa duara bila ya kuukatiza) umeonyesha kuwa na
manufaa makubwa. Wanahisabati wa zama zilizofuata hawakufurahishwa na
uvumbuzi huo hadi baada ya kupita miaka mia tano ambapo pia ulihusishwa
na Regimontanbus, lakini hata karne moja baadaye, Corpenius hakuwa na
taarifa nao.
Uvumbuzi wa namba "ZERO" wa Muhammad bin Ahmad
mwaka 976 ulileta mageuzi makubwa katika taaluma ya hisabati, ingawa
haikutumiwa katika nchi za Magharibi hadi mwanzoni mwa karne ya kumi na
tatu (13).
Mwisho
tunaweza kusema kuwa Nasr Ed-Din Tusi alikuwa mtu wa kwanza kutilia
mashaka kutoshambulika kwa jiometria ya Euclide. Anapaswa kuchukuliwa
kama mtu aliyekuwa amewatangulia tena kwa mbali kitaaluma akina
Lobatchevsky na Rieman katika jiometri isiyokuwa ya Ki- Euclide.
Somo la Fizikia (Physics)
"Ni Waarabu ambao wanapaswa kuchukuliwa waasisi wa elimu ya Fizikia", kama asemavyo A.Humboldt.
Ni bahati mbaya kwamba makala maalum kuhusu fizikia, nyingi
zilipotezwa. Nyingi zinajulikana tu kwa majina, ila chache tu ya kazi
zao zimeweza kupatikana na hili limethibitisha maoni ya Humboldt.
Tasnifu juu ya taaluma ya uoni (optics) au nuru ya Ali Haitan (Alhasen) aliyeishi mnamo 965 – 1039, lilikuwa ni jambo muhimu katika sayansi. M. Charles anasema kuwa: "lilikuwa ndilo chimbuko la sayansi ya leo kuhusu taaluma ya (uoni) nuru."
Kazi
hii inaeleza namna ya ujengekaji wa taswira katika kioo, maji na hata
viwango vya ukubwa wa taswira hizo, pamoja na matumizi ya vyumba vya
giza (dark rooms) katika taaluma ya utengenezaji wa picha. Utafiti wa
Hassan Ali Haitani kuhusu Lenzi za miwani na za kukuzia maumbo
(microscope), ulihamasisha kufanyika kwa majaribio mengi juu ya sayansi
ya uoni yaliyofanywa na Roger Bacon, Kepler na wengine wa nchi za
Ulaya. Akikosoa nadharia ya Euclid na Ptolemy, Alhasen alikuwa wa
kwanza kutoa maelezo sahihi juu ya sura halisi ya umbile la jicho, uono
wa Lenzi na darubini.
Elimu
ya Waislam juu ya Umekanika ilikuwa imeendelea hasa kwa wakati huo.
Tunaweza kupata dokezo kutokana na vifaa au zana walizokuwa
wamezitengeneza na kuzitumia katika tafiti zao mbalimbali na ambazo pia
zimetumiwa na watafiti wa nchi za Magharibi. E. Bernard kutoka
Oxford ameeleza maoni yake kwamba ni Waarabu waliogundua matumizi ya
(pendulum) timazi au mizania katika kutengeneza saa ya kuhesabia majira.
Kwa vyovyote vile, hakuna shaka walikuwa na chombo cha saa chenye
kutumia mizania tofauti na (clepsydra). Benjamin aliyekuwa mwenyeji wa
Tudela ambaye katika karne ya 12 alitembelea jamii za Kiyahudi hapo
Levant alielezea saa maarufu iliyokuwa ndani ya Msikiti Mkuu mjini
Damascus.
Hakuna
ubishi pia kuwa kompasi ilivumbuliwa na Wachina. Lakini ilirekebishwa
na kusahihishwa na wasomi wa Kiislam kwa kuiwekea mshale ulioendeshwa
kwa kutumia nguvu ya sumaku na kuiwezesha kutumika katika safari ndefu
hasa za baharini na jangwani.
Somo la Kemia (Chemistry)
Halitakuwa
jambo la ajabu mtu kusikia kwamba Kemia (elimu ya uchangayaji wa
kemikali) ni sayansi ambayo haikujulikana kabla ya matokeo ya utafiti wa
Waarabu. Bila shaka, Wagiriki walifahamu mambo kiasi katika elimu ya
madawa, bali hawakujua kuwapo kwa kitu chochote kiitwacho pombe, au
asidi ya salfuriki, naitriki n.k. Ni Waarabu waliogundua yote haya
yakiwemo matayarisho ya zebaki, silva natreti, potasium na sal
ammoniaki. Kama tukiongeza pia kwamba mojawapo ya taratibu (processes)
za kemia, kama utoneshaji (distillation), ni ugunduzi wa Waarabu, na
kwamba walikuwa watu wa mwanzo kutumia kanuni za usafishaji
(sublimation), ugandishaji (crystallization), uunganishaji (coagulation)
na chujaji (cupellation) wa kemikali mbalimbali. Hivyo, msomaji
analazimika kuamini kwamba mchango wa Waarabu ulikuwa ni wa msaada sana
katika maendeleo ya elimu ya sayansi.
Orodha
kubwa ya msamiati utumikao katika somo la kemia kama alcohol, alembic,
alkali, elixir, n.k, asili yake ni katika lugha ya Kiarabu.
Bila ya shaka yoyote, Mkemia maarufu sana wa Kiarabu alikuwa ni Abu Mussa Djafar AL- Kuhi (Djeber)
aliyeishi katika sehemu ya pili ya karne ya Nane (8). Kazi zake
zimefanywa kuwa ni sehemu ya ensaikolopidia ya Kisayansi na zimetoa
muhtasari na mwelekeo wa somo la Kemia kwa zama hizi. Nyingi katika kazi
zake kuhusu somo la Kemia zimefasiriwa katika Lugha ya Kilatin. Maarufu
kati ya hizo ni kitabu chake chenye maana ya "Jumuisho la Usahihi," kilichofasiriwa katika Lugha ya Kifaransa mnamo mwaka 1672.
Abu Bakr Zakaria AL- Razi (Razes), katika kitabu chake kiitwacho AL- Hawi,
anaonyesha kuwa mtaalamu wa kwanza kuelezea namna ya utengenezaji wa
salfuriki asidi na pombe kali (alcohol) kutokana na taratibu ya
utoneshaji wa nafaka zenye wanga au sukari, baada ya kuchachishwa kwa
kuvundikwa.
Katika sayansi hii, Waarabu waligundua kanuni nyingi kutokana na kuhusisha Nadharia katika ufanyaji wa Majaribio.
Majaribio
ya kemia katika taaluma ya madawa (pharmacy) ni mojawapo ya mchango
mkubwa na wenye manufaa kwa binadamu uliotolewa na wasomi wa Kiislam.
Idadi kubwa ya bidhaa zenye matumizi ya kila siku kama kafuri (camphor),
maji halisi yaliyotoneshwa (distilled water) kama yatumikayo kwenye
betri. Bidhaa zingine ni pamoja na plasta, shira (syrup) na dawa nyingi
za kujipaka (ointments) ni matokeo ya uvumbuzi wa Waarabu. Maendeleo yao
katika kugundua kemikali zenye matumizi ya viwandani yanaonyeshwa na
ufundi wao mkubwa katika kutia rangi nguo, utengenezaji na usindikaji wa
ngozi na uchovyaji wa vyuma.
Katika
uvumbuzi uliokuwa na maana sana kwa maendeleo ya viwanda, ni pamoja na
utengenezaji wa baruti, karatasi kutokana na pamba na marapurapu ya
nguo. Ugunduzi wa baruti kwa bahati mbaya ulikuwa umehusishwa na akina
Roger Bacon, Alberus Magnus na Berthold Shwarz. Na wakati mwingine
ulihusihwa na Wachina. Huu sio ukweli kwani utafiti uliofanywa na Reinud na Fave umeonyesha dhahiri kwamba "kutokana
na ugunduzi wa shura (saltpetre) wa Wachina, na matumizi yake katika
milipuko, ni Waarabu pekee waliovumbua baruti kama kitu chenye
kusababisha mlipuko. Na hii inaonyesha kuwa ndio waliokuwa wa kwanza
kutengeneza silaha za moto, walizozitumia mnamo mwaka 1342 kuihami
Algeziras iliposhambuliwa na Mfalme Alfonso wa XI."
Haitakuwa
vibaya kukazia tena ugunduzi wa karatasi, ugunduzi ambao ulifunua
ukurasa mpya katika ustaarabu wa mwanadamu. Kuenea kwa vitabu na zoezi
la kuanza kujifunza kusoma na kuandika, yote yamewezekana baada ya
Waarabu kuanza kutumia karatasi kama tuzijuavyo leo hii, badala ya
matumizi ya kizamani ya vipande vya ngozi na vipande vya nguo hasa za
hariri kama walivyokuwa wakivitumia Wachina.
Sayansi ya Maumbile (Natural Science)
Katika
sayansi asilia, baada ya kuelewa maoni ya waandishi wa Kigiriki,
Waarabu nao walianza kuitafakari na kuichunguza (nature) asili ya
maumbile na kutoa mahitimisho (observations) yao wenyewe. Kutokana na
juhudi zao waliweza kutaja nyongeza ya mimea 2000 katika idadi ya mimea
iliyokuwa inajulikana. Taaluma ya Waarabu ya Madawa ilihusisha matumizi
ya mimea na michanganyiko ya vitu ambavyo havikujulikana kwa Wagiriki.
Matumizi ya sukari badala ya asali yalisababisha kuwepo kwa madawa
mbalimbali yenye harufu na ladha ya kuvutia kwa wanywao katika uponyaji.
Kwa kutumia sukari, Waarabu waliweza kutengeneza madawa mbalimbali
pamoja na uwezo wa kuhifadhi mboga na matunda.
Waarabu
ndio waliowaonyesha Wazungu aina mbalimbali za manukato na viungo
vilivyotokana na mimea, maua, na mbegu mbalimbali. Kahawa, bidhaa muhimu
sasa hivi duniani asili yake ni katika nchi ya Yemen. Miongoni mwa
wanyama wa kufugwa, farasi bora anapatikana Uarabuni, na mbuzi bora pia
anapatikana Asia ndogo wakati kondoo wazuri wanapatikana nchini Morocco.
Waarabu ndio walioiendeleza elimu ya kilimo bora na pia
walijishughulisha na taaluma ya miamba (geology)
Elimu ya Madawa (Medicine)
Baada
ya hisabati na kemia, elimu ya utengenezaji wa madawa ilikuwa miongoni
mwa sayansi iliyowavutia sana Waislam. Wakati wa karne za mwanzo za
Hijra, taaluma hii ilifanywa kuwa mojawapo ya sehemu muhimu katika mfumo
wa elimu kwa jumla. Ndio maana walitokea madaktari wazuri na maarufu
pamoja na tasnifu (makala) zao mbalimbali juu ya taaluma hii.
Madaktari wa Kiislam walileta changamoto muhimu katika sayansi ya madawa kwa nchi za Magharibi. Kwa karne nyingi vitabu vya AL-Razi (Razes), Ibn Sina (Avicenna), Abul Cassis na Ibn Zohar
vimekuwa ni msingi wa elimu ya tiba katika Vyuo Vikuu vyote vya Ulaya.
Chuo cha Tiba hapo Salerno na hasa Montpellier kilisifika sana duniani.
Machapisho ya kazi za tiba ya AL-Razi yaliyojulikana kama Havi (au Maisha Bora), pamoja na kitabu chake kiitwacho Mansuri, viliendelea tena kwa karne nyingi kuwa vitabu vya kiada (miongozo) kwa taaluma ya tiba.
Havi,
ni mojawapo ya juzuu tisa (9) zilizokuwa katika Maktaba ya Kitivo Cha
Tiba cha mjini Paris, Ufaransa katika mwaka 1395. Humo kunapatikana
maelezo ya dalili za homa za magonjwa mbalimbali kama ya ndui na surua.
AL-Razi alianzisha matumizi ya dawa baridi za kumharisha mgonjwa katika
kulainisha tumbo lake. Pia alitoa dalili za ugonjwa wa kiharusi na
matumizi ya maji baridi (sponging) katika kupunguza homa kali. Anahusika
pia na ugunduzi wa seton, kwani alikuwa akiitumia mara
kwa mara. Vitabu vya AL-Razi vilitafsiriwa katika lugha ya Ki-Latin na
kuchapishwa nakala mara nyingi na hasa katika miaka ya 1505 hapo Venice,
mwaka 1428 na 1578 hapo jijini Paris, Ufaransa. Makala yake juu ya
ugonjwa wa ndui ilichapishwa tena mwaka 1745.
Abu Ali Al-Hussein Ibn Abdallah, aliyejulikana kote Ulaya kama Ibn Sina na kwingineko Ulimwenguni kama Avicenna, bila shaka alikuwa daktari maarufu. Kitabu chake cha Kanuni za Tiba (Canun Fi’l Tib) kilichapishwa
kwanza katika lugha ya Kiarabu hapo mjini Roma mwaka 1593. Kilitolewa
katika juzuu tano katika fani za fiziolojia (elimu ya viungo), kanuni za
Afya, patholojia (elimu ya magonjwa), elimu ya Tiba (therapeutics) na taaluma ya famasia (yaani ya utengenezaji wa madawa (pharmacy).
Kwa
takriban miaka mia sita hivi kuanzia karne ya 12 hadi ya 17, vitabu
hivi vilisaidia kuwa msingi wa Taaluma ya Tiba katika Vyuo Vikuu nchini
Italia na Ufaransa. Katika karne ya 15 vilihaririwa mara 15 katika lugha
ya Ki-Latin na mara moja katika Kiebrania (Kiyahudi).
Vilichapishwa
tena na tena hadi kufikia karne ya 18 na hata mwanzoni mwa karne ya 19
ambapo mihadhara kutokana na mafunzo yake, iliendeshwa katika Kitivo cha
Tiba cha Chuo Kikuu cha hapo Montpellier. Licha ya hayo, naye Ibn Sina
aliandika kitabu chake juu ya Tiba ya ugonjwa wa Moyo na hata mashairi
kuhusu elimu ya madawa. Kamusi yake yenye orodha ya madawa na tiba zake
iliainisha madawa yapatayo 760.
Mojawapo ya hatua muhimu iliyofikiwa na madaktari wa Kiislam ni katika nyanja ya upasuaji (surgery).
Hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 11 walishaelewa jinsi ya kutibu
magonjwa ya macho (hasa mtoto wa jicho), kutokwa na damu puani, na
matumizi ya tiba za dawa joto (caustics). Pia wasomi wa Kiislam walishajua matumizi ya ganzi (anaesthetics), ingawa
yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni uvumbuzi wa siku hizi. Wao, kabla ya
kumfanyia mgonjwa operesheni (upasuaji), walimnywesha kwanza dawa ya
kumtia usingizi mzito, iliyotokana na mmea ulioitwa ‘danel’, hadi hapo
alipoonekana kuzimia.
Daktari wa Kiislam maarufu katika upasuaji aliitwa Abul-Qasim Khalaf bin Abbas (Abulcassis), aliyeishi mjini Cordova na kufariki mwaka 1107. Mwanafisiolojia maarufu Haller anadai kwamba "kazi za Abulcassis ndizo zilizokuwa chanzo ya changamoto kwenye taaluma ya upasuaji hadi kufikia kwenye karne ya 15." Elimu ya upasuaji ya Abulcassis ilichapishwa kama kitabu katika lugha ya Ki-Latin mwaka 1497.
Chini ya tawala za Kiislam, Hispania nayo iliweza kutoa madaktari bingwa na miongoni mwao ni Ibn Zohar na Averroes (Ibn Rushd).
Ibn Zohar, alianzisha katika fani ya tiba, kanuni ya uchunguzi kwanza.
Jambo muhimu katika matibabu yake ni kuanzia kwenye mwili wenyewe kwamba
una uwezo asilia (immunity) wa kujikinga na baadhi ya magonjwa.
Alikuwa mtu wa kwanza kuunganisha somo la tiba, upasuaji na madawa na
kuliweka kama somo moja. Maandishi yake juu ya taaluma ya upasuaji ndiyo
ya mwanzo kuelezea sura halisi ya koromeo (bronchotomy), na maelezo ya
kina juu ya magonjwa ya mifupa, viungo na taratibu za tiba zake.
Averroes
(Abul Walid Mohammed Ibn Rushd) kama mtu aliyeendeleza kazi za
Aristotle, hatimaye alikuja kuwa daktari bingwa, na pia alitoa Tahariri (commentary)
juu ya kitabu cha Ibn Sina (Avicenna) kiitwacho "Canun" na pia kile cha
Galen. Kwake tumfaidika kutokana na makala yake kubwa kuhusu "theriac"
na pia kitabu chake juu ya homa na sumu mbalimbali pamoja na tiba zake.
Kazi yake kubwa ni pale alipotoa kitabu cha Tiba kiitwacho Kulliyet, kilichochapishwa
kwa mara ya kwanza mwaka 1490 hapo mjini Venice na baadae kiliendelea
kuchapishwa katika nchi mbalimbali duniani.
Tiba ya macho inayoendelezwa hivi sasa duniani asili yake ni katika elimu ya sayansi ya Waarabu. Kitabu cha "kumbukumbu ya Kanuni za Tiba ya Macho", alichotunga Ali Ibn Isaa
kiliendelea kutumika kama kitabu cha kiada (reference) hadi majuzi
kwenye karne ya 19. Operesheni ya kwanza ya kuondoa mtoto wa jicho
ilifanywa kwa mafanikio makubwa na Al Muhsin mwaka 1256, na ndiye aliyegundua sindano (hollow needle) yenye uwezo wa kuingiza dawa katika mwili wa mwanadamu.
Ibn AL-Nafis,
Msyria aliyefariki mwaka 1289 hapo Damascus, alikuwa ameshaelezea, tena
kwa usahihi kabisa mzunguko wa damu mwilini, miaka ipatayo 300 kabla ya
maelezo yaliyotolewa na Mreno aliyeitwa Serget, ambaye dunia imekuwa
ikimdhania kuwa mtaaalam wa mwanzo kuelezea jambo hili.
Maelezo juu ya sura ya Mapafu na mzunguko wa hewa ndani yake yalitolewa na msomi kutoka Misri aliyeitwa Muhy Al-Dine Tatarui, katika Tasnifu (thesis) yake aliyoitayarisha kabla ya kuhitimu kwake katika Chuo Kikuu cha Freiburg mwaka 1924.
Maelezo
mafupi juu ya somo la afya yanaweza kufanyika kama ifuatavyo. Sote
tunaelewa kwamba Dini ya Uislam imejaa kanuni bora kabisa juu ya
utaratibu unaomwezesha mtu kuishi kiafya, kama kuoga na kunawa mara kwa
mara, makatazo juu ya ulaji wa nyama ya nguruwe na unywaji wa pombe.
Zaidi ya hayo, Madaktari wa Kiislam walisisitiza zifuatwe taratibu za
kiafya wakati wa kutibu magonjwa. "Hospitali za Waarabu", anaeleza Gustave Le Bo, "zilijengwa
katika misingi bora ya afya kuliko hospitali nyingi za siku hizi.
Yalikuwa ni majumba makubwa makubwa yaliyoruhusu mzunguko huru wa hewa
na zilikuwa na maji ya kutosha kabisa,"
Somo la Falsafa (Philosophy)
Kuna
mambo mengi ambayo yametokana na mchango wa Uislam katika fani ya
Falsafa, kama mtu akifuatilia historia hatua kwa hatua. Hapa tutaeleza
mawazo ya jumla jumla tu ya Kiislam yaliyochangia kuleta maendeleo ya
somo la Falsafa hasa yaliyochukuliwa na wasomi wa nchi za Magharibi.
Katika
Ulimwengu wa Kiislam, mawazo ya Falsafa yalianza kuibuka mapema sana.
Kuna wakati baadhi ya waandishi walikataa kabisa falsafa ya Kiislam.
Walidai kwamba dhana yoyoye nje ya maelezo ya Qur’an au mawazo juu ya
kuwepo kwa dini nyingine hayakuwa na nafasi katika Uislam. Hivyo kikawa
ni kigezo cha baadhi ya wasomi hasa wa Magharibi kukataa utambuzi wa
mchango wa Uislam katika maendeleo ya somo la Falsafa.
Hivyo,
haikuchukuwa muda mrefu tangu vitabu vya Historia vilipoanza kufundisha
kwamba Waarabu walipovamia Misri, Khalifa Omar Ibn Khattab aliamrisha
ichomwe Maktaba maarufu ya mjini Alexandria, akidai kwamba "kama
vitabu vyake vinaendana na falsafa ya kiislam, basi havina maana yoyote,
na kwamba kama haviendani nayo basi ni vya hatari."
Hakuna
mtu leo mwenye kujua vizuri somo la Historia ya Uislam, anayeweza
kujali tena dai hilo kutokana na ushahidi uliokwishathibitishwa
kihistoria wenye kupinga maoni kama hayo. Wala sio haki au vyema
kudharau mawazo ya Uislam kwa kuyapendelea mawazo hafifu ya kijakazi ya
wanafalsafa wa Kiyunani.
Falsafa
ya Waarabu imeweza kuthibitishwa kuwepo kwake tangu karne ya mwanzo ya
zama za uislam kama ulivyoenezwa na Mtume Muhammad (S.A.W), ambayo
imehusishwa moja kwa moja na theolojia ya uislam. Kuwepo kwa Mwenyezi
Mungu mmoja, upekee wake, uwezo wake Mkuu, Mtenda Haki (asiyedhulumu),
Mwenye Huruma (kwa viumbe vyake), na sifa nyinginezo nyingi ni miongoni
mwa mada ambazo zilihitaji kutafakariwa kwa kina ili kuweza kuzielewa
kiusahihi. Mawazo mbalimbali yaliibuka wakati wa mijadala ambayo wakati
mwingine ilikuwa mikali kabisa. Makundi yenye mitizamo tofauti yaliibuka
kuhusu masuala ya hatima ya watu iliyokwisha kadiriwa (na Mwenyezi
Mungu), uhuru wa imani (kuabudu), ukombozi kwa njia ya vitendo au imani,
Khalifa wa Mtume kama kiongozi wa muda wa kuiongoza jamii ya Kiislam
mara baada ya Mtume kufariki na masuala mengine mengi.
Haya yalikuwa ni makundi ambayo yaliyojulikana kama Kharidji, Murdji na Kadari. Mwanzoni mwa karne ya 2 Hijria, lilizuka kundi la Mu’tazili. Yote haya yalisababisha zidurusiwe tarehe za tafsiri za Wagiriki, ambazo hazikuwa zimefanyika hadi wakati wa Ukhalifa wa AL-Mansur mnamo miaka ya 735 – 774, na pia ni ushahidi wa kuwepo kwa maendeleo tofauti ya uislam yaliyojitegemea.
Kwa
kuidurusu, kuisambaza na kuitumia elimu ya watu wa kale, Falsafa ya
Uislam ilitokea kuwa changamani (complex) na pambanuzi (subtle). Katika
karne ya 3, wakati wa utawala wa AL– Kindi, kundi la wasomi wenye
kushabikia somo la Falsafa lilianzishwa. Kundi hili lilichambua
mafundisho ya Kiyunani (Kigiriki) na ya Plato. Wasomi wengi wa Kiislam
walishughulika zaidi na kuoanisha mawazo ya Plato na Aristotle na
kuyahusisha na mafundisho ya Dini. Katika Falsafa, kama ilivyo katika
sayansi yoyote, wasomi wa Kiislam walionyesha kila aina ya shauku ya
kutaka kujiendeleza kielimu. Matatizo yote yenye kuhusu kiini cha mambo
kama yanavyotafakariwa na mwanadamu, aina zote za tafakari, kupitia
kwenye Nadharia ya Kushuku na Mantiki, yaliweza kuelezeka katika
mitizamo mbalimbali ya kifalsafa.
Tunaweza
kuuchunguza usomi wa Kiislam kwa undani zaidi kutokana na umuhimu wa
ushawishi (influence) wa wahubiri wake walivyokuwa makini na masuala ya
Dini, na pia kutokana na wasomi hawa kuwa misingi ya falsafa
iliyojengeka Ulaya kuanzia karne za zama za Kati. Avicenna (Ibn Sina) na
Averroes (Ibn Rushd), walisifika sana katika Ulimwengu wa Magharibi
kuliko Mashariki, ambako walijulikana tu kama madaktari au watabibu.
Umashuhuri
wa Ibn Sina, ambaye alifikiriwa na watu kuwa kigezo cha kilele cha
usomi wa karne za Kati, ni kutokana na kazi aliyoitoa katika seti ya
vitabu vyenye kuzungumzia mada mbalimbali. Tulishaelezea kazi zake
katika taaluma ya Tiba. Pia, alifanya mengi katika fani za Sayansi na
Falsafa. Anaheshimika kutokana na kuanzisha taratibu za kisayansi
zilizodumu kwa karne nyingi bila ya kubadilishwa. Kama msomi mkuu,
alianzisha somo la Falsafa na kulitolea mwelekeo wa siku hizo na za
baadae. Mawazo ya Aristotle na Plato pamoja na kuyasoma, hayakuathiri
asili ya mawazo yake mwenyewe. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kumjadili
Aristotle na pengine aliweza kumkosoa na kutoa hitimisho lenye mantiki.
Kazi zake kubwa zilizowekwa katika vitabu ni pamoja na: Kitab AL- Shifa (au
Taaluma ya Tiba), AL- Hidayat Fi’l Hikmat (au Mwongozo katika Hekima),
Hadithi ya Hayy Ibn Yagzan, Kitab AL-Isharat Wa’al Tanbihat (au Mwongozo
wa mafunzo ya Ishara na Tahadhari), n.k. Tafsiri ya kwanza ya Ibn Sina ilifanyika mwanzoni mwa karne ya 12.
Ushawishi wa Ibn Sina katika maendeleo ya somo la Falsafa kwa nchi za Magharibi ulikuwa mkubwa sana. "Hakuna Tasnifu ya msomi yoyote ambaye haikumnukuu Avicenna, kama anavyosema mamaA.M. Gorchon.. Na tafakari zaidi zinaonyesha wazi zaidi kwanba Avicenna alizivutia sana fikra za wanafalsafa wa Ulaya."
Albetus Magnus
alimchukulia kama mtu wa mfano mwema ingawa yeye mwenyewe alikuwa
msitari wa mbele katika kuishambulia falsafa ya Waarabu. Naye Renan,
katika kitabu chake chenye maana ya "Averos na Uaverosi", hakusita
kuthibitisha kwamba masomo yaliyotolewa katika Chuo cha Mtakatifu Thomas
yalitegemea kwa kiasi kikubwa elimu ya Ibn Sina. Mt. Thomas mwenyewe, ambaye alivutiwa sana na Ibn Sina, hakuwa mgeni wa fikra zake. Papa Yohana wa 21, kabla ya kusimikwa kwake, "alifundisha nadharia ya elimu ambayo aliihusisha na Aristotle badala ya mwenyewe Avicenna."
Hayo yamesemwa na wasomi kama akina William mwenyeji wa Auvergne,
Alexander wa Hales na wengineo wengi ambao walisoma hapo kwa Mt.Thomas.
Averroce,
jina ambalo limepotoshwa kutokana na Abdul Walid Mohammed Ibn Rushd,
alikuwa pia na mafanikio makubwa yaliyoonewa wivu na wasomi wa nchi za
Magharibi hata kumzidi Ibn Sina. Ni kutokana na Tahariri zake juu ya
Aristotle ambazo zilimfanya kuwa maarufu zaidi ya wasomi wenzake wa
Kiislam.
Azma
ya Averroes (Ibn Rushd) ilikuwa ni kujitwisha dhima ya kihistoria ya
kuzifundisha falsafa nchi za pande mbili za ulimwengu yaani Mashariki na
Magharibi. Alikubalika kama Mhariri Mkuu wa kazi za Aristotle, msomi
mkubwa kabisa, ingawa alishambuliwa na wengine kuwa hakuwa Mcha Mungu.
Hata kama Albertus Magnus mara chache sana alimnukuu, kadhia ya Mt.
Thomas Aquinas inakanganya. "Mt.Thomas", anasema Renan, "wakati
huohuo anaonyesha kuwa adui mkubwa kupita kiasi wa Mawazo ya Ibn Rushd,
na mtu anaweza kupata mshangao ulio wazi kuhusu mabadiliko ya ghafla ya
mfuasi huyu wa kwanza wa Mwanafalsafa huyo mkuu. Albertus Magnus
alitumia mawazo ya Ibn Sina wakati Mt. Thomas yeye alitumia sana mawazo
ya Ibn Rushd."
Padri Asin Palacio,
aliyesoma sana falsafa ya kidini itokanayo na mafundisho ya Ibn Rushd
yaliyofundishwa hapo kwa Mt. Thomas, aliyafananisha na mafundisho
yaliyotolewa katika nchi za Latin (Milki ya Kirumi), baada ya
kuyachunguza maandishi mbalimbali ya Wanafalsafa wa Cordova na
kuyalinganisha na yale ya Ibn Rushd. Kufanana kwa mawazo hayo
kunaonyeshwa na matumizi ya misemo inayofanana kiasi kwamba hakuna shaka
juu ya mchango (au ushawishi) wa Falsafa ya Mwislam huyu ulivyokuwa
mkubwa katika mafundisho ya Wakatoliki.
Karne
za 14 na 15 zilishuhudia kilele katika matumizi makubwa ya Falsafa ya
Ibn Rushd. Katika Vyuo Vikuu vya Magharibi, Mihutasari yake ilitumiwa
kama kiada badala ya makala za Aristotle. Yohana Baconthorp, aliyefariki
mwaka 1346, aliyekuwa Askofu wa Jimbo moja nchini Uingereza, na daktari
wa Mipango, aliamrisha yaingizwe mafundisho ya Averroes katika mfumo wa
elimu katika Chuo chake. Naye Paul mwenyeji wa Venice
aliyefariki mwaka 1429, alikiri waziwazi kuzipenda nadharia za Averroes
(Ibn Rushd). Alipoliandaa somo la Falsafa mwaka 1473, Louis wa 11
alizifanya nadharia za Aristotle pamoja na Tahariri za Averroes kuwa
somo la lazima kwa wanafunzi wake. Naye Vicomercato alilifundisha somo
hilo katika Chuo chake nchini Ufaransa toka mwaka 1543 hadi 1567.
Lakini
ni Chuo Kikuu cha Padua kilichokuja kuwa Kitovu cha elimu ya Kiarabu
kwa wakati huo. Ibn Rushd ndiye aliyeonekana kuwa bingwa wao. Mafunzo
yake yalidumu hadi karne ya 17. Bologna, Ferrara na Venice
zililazimishwa kufuata mafundisho ya Kirumi, ingawa hakukutokea
pingamizi juu ya Tahariri za Kiarabu juu ya Falsafa ya Aristotle.
Mwaka
1240, Askofu William kutoka mjini Paris aliamuru yaondolewe mawazo ya
Kiarabu katika baadhi ya maandishi na vitabu. Mwaka 1269 Etienne Tempier
aliyekuwa Askofu wa Paris wakati huo pia, alithibitisha kutekelezwa kwa
amri hiyo. Hatua zote hizi hata hivyo, hazikusaidia kuzima harakati za
maendeleo ya Falsafa ya Kiislam. Falsafa hii iliendelezwa na Warabu na
kuweza kuimarika zaidi. Ukweli Siger de Brabant, anayesemekana kuwa
muasisi wa harakati za (Ibn Rushd) Averroes, alikuwa mwalimu wa Falsafa
hii katika miaka ya 1266 na 1277 katika Chuo Kikuu cha hapo mjini Paris.
Huko kabla mnamo mwaka 1227, aliyekuwa Papa wakati huo, aliamuru
yapitiwe upya maandiko, na ndipo makala zipatazo 219 zilizoonekana kuwa
za uasi dhidi ya Kanisa zilipopigwa marufuku. Matokeo yake ilikuwa ni
kufukuzwa kazi kwa Bwana Siger, na baadaye alihukumiwa na Kanisa
kutumikia kifungo cha maisha jela. Pamoja na hatua zote hizi, Uaverosi
uliendelea kuimarika zaidi.
Kundi
lililokuwa mstari wa mbele katika kuipinga Falsafa ya Averroes ni lile
lililoamua kuanza kufuata mafundisho ya Kirumi na Kiyunani tu
(lililoitwa the Humanist). Kwa mtizamo wao, walimwona
Averroes kuwakilisha fikra za Waarabu, na kwa kuwa sasa walishaelewa
moja kwa moja asili ya elimu ya kale, Waarabu wakawa ni watu wa
kushambuliwa, tena kwa nguvu zote. Bila ya kujali wala ya kuthamini
mchango wao mkubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya mwanadamu
baada ya kuichambua na kuiendeleza elimu ya Wayunani (Wagiriki), badala
yake walishutumiwa kwa kuudumaza na kuupotosha utamaduni wa kale, jambo
ambalo kama tulivyokwishaona kuwa halikuwa la kweli.
Petrarch,
aliyedhaniwa, na kwa uhakika zaidi kuwa miongoni mwa watu walioasisi
ustaarabu unaoendelea sasa hivi duniani, aliandika katika mojawapo ya
barua zake kwa rafiki yake aliyeitwa Jean Dondi maneno yafuatayo: "Mimi
binafsi nalichukia sana kabila hili (la Waarabu). Kwani inaniwia vigumu
sana kwangu mimi kuamini kwamba Waarabu wanaweza kuleta jambo lolote la
manufaa (kwa watu)."
Hata
hivyo, pamoja na mashambulizi haya yaliyotoka katika sehemu zote mbili,
za walimu wa dini (theologists) na wasomi wa Kirumi na Kiyunani (the
humanists), Uaverosi (falsafa ya Ibn Rushd) uliendelea na kusambaa kwa
wasomi mbalimbali duniani hadi kufikia kwenye karne ya 17.
Harakati
za kuendeleza mawazo ya Averroes (Ibn Rushd) zilikuwa kubwa, na kuwepo
kwa uhakiki tofauti tofauti juu ya kazi zake ni ushahidi tosha wa jinsi
gani alivyokuwa mwana falsafa makini kabisa wa Kiislam. Kumekuwepo na
tofauti kubwa kati ya fikra sahihi za Ibn Rushd na mawazo ya wasomi
wengine ambayo amekuwa akihusishwa nayo. Falsafa ya Averroes ni kitu
kimoja na Uaverosi (Averroism) ni kitu kingine. Mambo hayo mawili hayana
budi kutofautishwa.
Si
jambo la kubabaisha tu katika kubainisha tofauti hizo. Tunatumai
kutokana na maelezo tuliyoyaona hapo nyuma kwamba Ibn Rushd alikuwa
amewazidi katika elimu ya Falsafa, wasomi wa Ulaya tena kwa karne nyingi
tu, kiasi kwamba nadharia na mafundisho yake, hata yale yaliyopotoshwa
ama kufichwa kwa makusudi, yalisaidia katika kujenga muamko wa kielimu
katika bara la Ulaya na pia yalichangia katika kuondoa dhana potofu
zilizokuwa zimedumaza na kukwaza uhuru wa watu kufanya tafiti na kutoa
fikra mbalimbali.
Somo la Fasihi na Lugha (Literature)
Huenda
mojawapo ya mafanikio ya Uislam ni katika mchango wake katika maendeleo
ya somo Falsafa. Ukilinganishwa, ushawishi wake katika maendeleo ya
somo la Fasihi ya Lugha bila shaka haukuwa mkubwa sana. Ila katika
baadhi ya sehemu za nyanja hii, uislam ulitoa mchango mkubwa na ulio
dhahiri kabisa.
Kama
mtu ana shaka na hilo, anaweza kufuatilia asili ya taaluma ya utunzi wa
nyimbo na mashairi katika nchi za Ulaya. Lini na wapi yalianza kutokea
haya ni jambo ambalo linaloweza kuthibitishwa kwa usahihi kabisa.
Yalianza kutokea katika nchi za Hispania na Ufaransa mwanzoni mwa karne
ya 12, halafu taaluma hii ilianza kusambaa kupitia Italia na baadaye
katika nchi nyingine za Ulaya. Fasihi juu ya mahaba na methali katika
nchi ya Hispania ni miongoni mwa vielelezo hivyo. Kipindi cha mwamko wa
Fasihi na Lugha katika nchi za Magharibi kilizidi historia ya maendeleo
ya usomi. Ni kipindi kilichotoa hatma ya maendeleo ya ustarabu katika
nchi za Magharibi.
"Ni vigumu kukosa kusisitiza", anaandika Gustave Cohen,
" kwamba ubunifu na thamani ya aina ya ushairi wa Kiislam hasa katika
kujenga hisia.. Hakika ni mama wa ushairi wa siku hizi, labda zaidi
kuliko ule wa KI-Latin. Bila ya ushairi huu hawezi mtu kuzungumzia tenzi
za Kitaliano, Kihispania, wala Kijerumani au Kifaransa."
Lakini,
ni zipi hasa tungo za washairi? Tofauti ya mashairi haya na mengine ya
kimapenzi yaliyojulikana tangu zamani, ni ulimbwende juu ya mwanamke.
Heshima yake kubwa kama mtu mtukufu, pamoja na kuyatukuza sana mapenzi
kama mambo ya kiroho. Hiyo ndiyo iliyokuwa dhamira ya mashairi ya watu
kama Mfalme William wa 9, mtawala wa Aquitaine, ya Marcabru, ya Jauffre
Rudel, Dante, Petrarch na wengine.
Mtu
anaweza kujiuliza nini chanzo cha mawazo haya ya ghafla juu ya
mwanamke, yaliyokuwa kinyume na utamaduni wa nchi hiyo yalipoanzia. Aina
ya mahadhi ya nyimbo hizi bila shaka hayakuwa na asili yake katika
jamii ya Wayunani wa kale, wala miongoni mwa Warumi.
Kazi za Julien, Ramon Menedez Pidal, na R. Nycle
zinaonyesha kuwepo kwa washairi waliokuwa wakitangatanga kutoka
Mashariki ya Kati na Hispania (nchi za Andalusi), waliosababisha kuletwa
kwa mabadiliko katika fikra na hisia za watu wa nchi za Magharibi.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo kimoja nchini Hispania
umeonyesha kuwepo kwa mashairi yenye mahadhi ya Ki-Andalusi, mifano ya
awali ilithibitisha kuwepo kwa mashairi hayo mwishoni mwa karne ya 19.
Mahaba
ya Plato, kama yalivyohusudiwa ya kunyenyekea sana matakwa ya mwanamke,
utumishi katika jina la mapenzi, uzito wa maumivu ya kimapenzi, yote
haya yalikuwa miongoni mwa vibwagizo katika tungo za Waarabu tangu karne
ya 8. Katika Andalusia, aina hii ya ushairi ilianza kuonekana katika
karne ya 19 na ilijulikana kwa jina la "zajal". Ni kielelezo cha mojawapo ya mafanikio yaliyotokana na makutano ya tamaduni mbili za Waarabu na Warumi.
Kosa la kusikitisha lililotokana na vita vya kidini (kuukomboa msalaba na ukristo), ni kule kuingilia na kuharibu usanisi
(muunganiko) huu uliokuwa umeanza kujitokeza wa kati ya tamaduni mbili
za eneo la Mediterani, usanisi ambao ulikuwa ni jambo la kawaida katika
maendeleo ambayo yangeleta faida isiyo na kifani katika fani za sanaa na
fasihi.
Lakini
hata wakati wa vita hii, mahusiano ya kiuchumi, kisayansi na kisanii,
hayakukatizwa kabisa. Maingiliano bado yaliendelea kati ya mataifa ya
Kiislam, Hispania na ya Kirumi. Katika maingiliano hayo, utunzi wa
mashairi na nyimbo yalikuwa miongoni mwa mambo yaliyochukuwa nafasi
kubwa. Miji ya Kiarabu iliendelea kuwa vitalu vya kuzalishia washairi,
wanamuziki na wacheza dansi ambao walitumbuiza sana katika nchi za
kusini mwa Ulaya.
Kazi kubwa ya Asin Palacios juu ya asili ya Tamthilia–chekeshi (comedy) za kiislam, imeonyesha ushawishi mkubwa kwa Dante wa Muhy Ad Din Ibn Arabi na wa mshairi aliyekuwa kipofu aliyeitwa Abul Ala Al-Maari, ambaye tungo zake mahiri zilijaa ndani yake falsafa ya kushuku au kutazamia mabaya.
Riwaya ya Kifalsafa ya Ibn Tofayl, Hay Ibn Yakzan, iliyotafsiriwa katika Ki-Latin na Edward Pococke mwaka 1671 na baadaye katika lugha nyingine, ilimhamasisha pia Daniel Defoe na kumsaidia katika utunzi wa riwaya yake maarufu ya "Robinson Crusoe."
Ibn Hazim,
ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi bora wa Kiislam kutoka Hispania,
aliathiri kwa kiasi kikubwa fasihi za Magharibi. Kama mwandishi mahiri
alitunga Hekaya na masimulizi mengi ambayo kuanzia karne ya 13
yalisambaa na kuzikumba nchi zote za Ulaya. Tungo za Hekaya zake
zilitafsiriwa katika Kispaniola na mtu aliyejulikana kama Alphonse
mwenye Busara, Mfalme wa Castille, na baadaye katika Ki-Latin, Kiyahudi,
Kiajemi na Kifaransa. Lafontaine alikiri pia kuwa hekaya hizo zilikuwa
ni miongoni mwa vyanzo muhimu katika tungo zake. Boccaccio, Chaucer na
wasimulizi wengine wa Kijerumani, kwa kiasi kikubwa walivutiwa na utunzi
wa hekaya hizo. Hapa hatuna budi kusisitiza mvuto wa Hekaya maarufu ya "Alfulela Ulela" (au The Thousand And One Nights), kwa watu wengi waliopata kuisoma huko Ulaya na hata hapa Afrika ya Mashariki.
Pia tunapaswa kuuelezea ubora wa tungo za mashairi ya Tennyson na Browning kuwa na asili ya Arabuni.
"Don Quixote", kazi ya Cervante
imejaa asili ya Kiarabu. Mtunzi wa kazi hii aliwahi kufungwa kwa muda
huko Algeria na aliwahi kuongea kiutani kwamba kitabu chake mwanzo
kiliandikwa katika lugha ya Kiarabu.
Hivyo, mtu anaweza kuhitimisha, kama asemavyo Phillip Hitti kwamba, "kwa
jumla mchango mkubwa wa Waarabu katika maendeleo ya fasihi na lugha
katika zama za kati huko Ulaya, ni katika ushawishi wake katika
utokezaji wa miundo ya lugha, kama ulivyoweza kubuniwa na wataalam wa
Magharibi na hivyo kuweza kujinasua katika matatizo ya sheria ngumu za
miundo ya lugha za awali."
Mtu
pia hawezi kuimalizia sura hii juu ya Fasihi ya Kiislam bila ya kutaja
ubora wa mashairi ya Waajemi (Wafursi). Mahadhi ya mashairi haya ndilo
jambo lililoyafanya kupendwa na hivyo kuweza kusambaa haraka sana.
Wataalam wa herufi za Kizungu, walielezea juu ya ushairi wa Waajemi kuwa
ulijaa hamasa na shauku. Goethe, akiongea na Chancellor von Mueller aliwahi kusema: "kwa
muda wa karne tano Waajemi walikuwa na washairi maarufu saba ambao
walidhaniwa kuwa mabingwa, ingawa hata hao wengine ambao hawakuhesabika
kuwa mabingwa, walikuwa ni bora zaidi kuliko mimi."
Mabingwa hao saba wa fasihi ya Kifursi ni Firdusi, Djelal Ed Din Rumi, ambaye alikuwa miongoni mwa washairi wakubwna wa ajabu Ulimwenguni kama si mbora wao wote, Sadi, mghani maarufu wa Kishirazi, Anwari, ambaye hakulinganishwa na yeyote katika utunzi wa wasifu, Hafiz, mtunzi mahiri wa mashairi yenye hisia za kimapenzi na ambaye alikuwa kipenzi cha Goethe. Wengine ni Nizami na Djami.
Hafiz
alikuwa mshairi wa kwanza wa Kifursi kupata umaarufu huko Ulaya.
Alikuwa ni Mjerumani aitwaye von Hammer Purgstall aliyepata heshima ya
kumtangaza bingwa huyu wa "ghazal", mashairi ya mahadhi nyororo kwa watu wa Magharibi. Tafsiri ya "Diwan", kitabu chenye tungo zote za Hafiz, ilianza kupatikana kati ya miaka ya 1812 na 1813.
Kama
ukweli ukitolewa mwanzo, ni watu wachache tu na labda wawe ni wasomi
ndio wenye kuupokea. Lakini lilikuwa ni jambo jingine pale Goethe
alipochapisha "West – Ostlicher Diwan" mwaka 1819. Tunaelewa kwamba kitabu hiki kina alama ya maandishi yenye maana kwamba: "Iwapo
mtu atataja neno Mke na Roho akaiita Mme, yule mwenye kumsifia Hafiz
atakuwa ameshuhudia ndoa ya maneno hayo mawili (mke na mme)." Pia mtu anaweza kusoma pale maneno yasemayo: "Mashariki
imekatiza kiajabu bahari ya Mediterranean. Yule tu amjuaye na kumpenda
Hafiz ndiye anayeweza kuuelewa wimbo wa Caldrenon."
Diwan
ya Hafiz ilitafsiriwa katika lugha zote za Wazungu. Lakini umaarufu
wote wa Hafiz, kama wa watunzi wengine wote wa Mashariki na Magharibi,
ulizidiwa na ule wa Omar Khayyam. Bila shaka huyu alikuwa miongoni mwa
watunzi waliosomwa sana tenzi zao na watu wa pande zote mbili za dunia.
Kuna
angalau mpaka leo tafsiri kumi na mbili katika lugha za Kifaransa,
Rubayat, Kiingereza, Kijerumani, Kirusi, Kitaliano, Kispaniola,
Kidanish, Kihungaria na Kituruki. Na baadhi ya beti zake zilitafsiriwa
katika lugha nyingine zaidi.
Klabu
ya Omar Khayyam iliyoanzishwa mjini London mwaka 1892, ilsababisha
kuanzishwa kwa taasisi nyingine kama hiyo katika nchi nyingi za Ulaya.
Mchango wa Uislam katika masomo ya Jiografia na Historia
"Hamu yao ya kupenda kusafiri", anasema Renan, "ni
mojawapo ya tabia za Waarabu, na mojawapo ya mambo yaliyowafanya kuweka
athari katika historia ya maendeleo ya ustaarabu wa aina mbalimbali
duniani. Hadi kufikia zama za mwanzo wa safari za upelelezi kwa njia za
baharini zilizofanywa na Wareno na Wahispania katika karne ya 15 na 16,
hakuna watu waliokuwa wametoa mchango mkubwa kama Waarabu katika kupanua
nadharia ya sura halisi ya ulimwengu na hivyo kuitolea maelezo sahihi
sayari yetu hii tuishimo ambayo ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya
kweli."
Mapema
katika karne ya 9, wafanyabiashara wa Kiarabu walikuwa watu wa mwanzo
kutembelea nchi mbalimbali, kama China, Afrika na nchi zilizoko
kaskazini mwao kama Urusi. Hekaya ya Safari ya Suleiman mmoja, iliyoanza
kutungwa mwaka 851 na kumalizika mwaka 880, na mtu aitwaye Abu Zayd, ilikuwa ni kazi ya kwanza kuchapishwa nchini China. Masudi (Hassan Ali Al-Masudi),
ambaye umaarufu wake katika masomo ya sayansi ulitambulika mwishoni mwa
karne ya 18, alifanya safari katika karne ya 10, ya kuizunguka na
kuimaliza Himaya yote ya Kiislam kuanzia pembe moja hadi nyingine. Pia
alitembelea nchi za visiwa kama Ceylon, Madagascar na Zanzibar. Katika
kitabu chake chenye maana ya "Mbuga za Dhahabu", anaelezea hali ya nchi
zote alizowahi kutembelea, milima yake, bahari, mabonde na hata tawala
zake, na pia tamaduni mila na mifumo ya ibada katika nchi hizo."
Ibn Haykal al- Biruni, Idrissi na Ibn Batuta
ni miongoni mwa wapelelezi na wasomi maarufu, na waandishi wa taarifa
muhimu za kijiografia, ambao walisaidia kuwapanua mawazo wenzao Wazungu.
Idrissi kwa mfano, aliyezaliwa hapo Palermo, alimtayarishia makala ya
kijiografia Mtawala wa Sicily aliyeitwa Roger wa II. Anasema Sellidot
kwamba; "Kwa miaka takriban mia moja na hamsini, wachora ramani wa
Kizungu hawakuwahi kufanya lolote ila kunakili tu makala hiyo bila ya
hata kuifanyia marekebisho makubwa."
Hebu
sasa tuitaje ramani ya Ulimwengu iliyotayarishwa na Ulug Beg, mjukuu wa
Timur (Tamburlaine), na muasisi wa Jedwali la Unajimu lijulikanalo kwa
jina lake. Katika kulitayarisha jedwali hili, alitegemea zaidi taarifa
za akina Nasr Ed Din Tusi na Al – Khoshadji, ambaye alilazimika kusafiri
hadi nchini China, ili kuhakiki kipimo cha digrii moja ya meridian,
pamoja na ukubwa wa Ulimwengu.
Hebu pia tuzungumzie chati (ramani) zilizotayarishwa na Waarabu. Sellidot anaripoti kwamba: "Vasco
de Gama alipata kuiona mojawapo ya ramani hizo mnamo mwaka 1497,
iliyotayarishwa na Malem Cana, Moor wa Gujarat na hivyo kuitumia katika
safari yake ya kuelekea Melinda. Nyingine, iliyotayarishwa na Mwarabu
aliyeitwa Omar, ilimsaidia Albuquerque wakati akisafiri katika bahari ya
Oman na Ghuba ya Uajemi."
Ni
kweli pia kwamba kazi za wasomi wa Kiislam zilisaidia katika ugunduzi
wa bara la Amerika. Katika barua aliyoiandika akiwa Haiti ya mwezi
Oktoba 1498, Christopher Columbus amemtaja Ibn Rushd (Averroes)
lakini kwa jina la Aventuez, kama mtu aliyemsaidia katika kufikia dhana
ya kuwepo kwa Nchi Mpya (yaani bara la Amerika).
Ukweli
ni kwamba idadi ya wasomi wa Kiislam walioacha kazi zao za Kihistoria
ni kubwa sana. Katika Kamusi ya Historia iliyotayarishwa na Katib
Tchelebi, ijulikanayo kama "Hadja Khalfa", imekusanya mamia ya majina ya wana-historia maarufu wa kiislam.
Maandishi
ya Kihistoria ya zamani zaidi ni yale yaliyofanyika wakati wa zama za
Utawala wa ukoo wa Umeyyad. Miongoni mwa waandishi wa kwanza bila shaka
ni pamoja na Abu Minaf, aliyenukuliwa na Masudi katika kitabu chenye maana ya "Mbuga za Dhahabu", au (Golden Pastures).
Huyu alifariki mwaka 747 A.D (130 A.H). Wasomi wengi wa Ulaya hupenda
kuwalaumu wanahistoria wa Kiislam kwamba walipenda zaidi kuandika ukweli
wa taarifa au mambo kama yalivyo, bila ya kuyafanyia uchambuzi na
kuyaacha mawazo ya jumla jumla bila ya kutafuta viunganishi vya matukio
ya kihistoria. Lawama hizi pengine zinaweza kukubalika lakini si katika
ujumla wake.
Bila
shaka wanahistoria wengi wa Kiislam hawakupata fursa ya kujenga dhana
kuu za lengo la somo la Historia, ambazo ndizo zilizoshughulisha zaidi
mawazo ya wasomi wa Magharibi na ambazo zimechukuliwa kama Sayansi ya
Historia ya siku hizi. Wasomi wa Kiislam, wao walijiona kuwa na jukumu
la ukusanyaji wa taarifa mbali mbali na kuziweka katika kumbu kumbu kwa
faida ya vizazi vya baadae. Wao walijizuia kutoa tafsiri na maamuzi juu
ya mambo ya kale (ya kihistoria).
Dhana
hii kuhusu somo la Historia, bila shaka ni kinyume na dhana ya watu wa
Magharibi. Lakini je ni jambo la busara ama baya? Ni suala linalohitaji
mjadala. Kwa vyovyote vile, mtu ambaye anahitaji kurithisha tamaduni na
taratibu ambazo na yeye alirithishwa, bila ya kuzitolea maoni au
uhakiki, anaonyesha uaminifu na kutoegemea upande wowote kuliko wale
watu watoao nyaraka zilizokwisha dodoswa dodoswa na kuhujumiwa kwa lengo
la kuzidhibiti kulingana na malengo ya imani zao.
Baada
ya kuyasema hayo, itakuwa si jambo la busara kuwalaumu wanahistoria wa
Kiislam eti walikuwa na mawazo finyu na kwamba hawakufanya maamuzi yao
kwa makini. Badala yake, wamepata umaarufu kutokana na uono wao mpana,
na walielezea hisia zao wazi wazi katika masuala ambayo kwa muda mrefu
yalikuwa nje ya upeo wa watu wa Magharibi. Hivyo, ndio maana historia ya
Fasihi na uandishi ilionekana sana katika kazi zao. Ndio maana pia,
tunashindwa kuwataja wote hapa, ila kwa mifano ya wawakilishi wa wana
historia wengi wa Kiislam.
Tabari (Abu Djafar Mohammad Ibn Djarir AL-Tabari)
Aliyezaliwa
mwaka 839 na kufariki dunia mwaka 922, kama mtaalam wa somo la
Historia, mwana sheria na mwalimu wa Dini, alipata mamlaka ya heshima ya
utoaji wa ushauri katika masuala hayo, heshima ambayo hakuwahi kuipata
mtu yeyote katika Ulimwengu wa Mashariki. Masudi namuelezea Tabari kama
mtu wa zamani lakini aliyekuwa amemzidi sana yeye, pale aliposema: "Kanuni
ya Abu Djafar Mohammad Ibn Djarir AL-Tabari, ni kazi bora kuliko
nyingine zote juu ya Historia. Ukweli wa taarifa na taratibu za
kisayansi katika ukusanyaji wa taarifa zake, vinakifanya kuwa kitabu cha
kufundishia."
Kitabu chake cha "Tarikh", ni
miongoni mwa kazi za msingi sana katika somo la Historia ya Waarabu.
Thamani yake inatokana na usahihi wa taarifa zake kuhusu mwanzo wa
Uislam. Kimejaa taarifa muhimu sana juu ya Lugha, mila na desturi za
watu wa enzi hizo. Simulizi ndani ya Tarikh ziliendelezwa hadi mwaka 914
A.D.
Masudi (Hassan Ali AL-Masudi),
aliyezaliwa mjini Baghdad mwishoni mwa karne ya 9 na kufariki mjini
Cairo mwaka 956, naye aliwafunika wengi kwa umaarufu kama alivyofanya
AL-Tabari, kutokana na upeo na ubora wa elimu yake kuhusu masuala
mbalimbali. Miongoni mwa mambo ya kumkumbukia ni historia ya utafiti
wake katika somo la Fasihi. Anasema Renan kwamba: "mtu anaweza kudai
kwamba Masudi, kama mtu aliyetarajia changamoto na uhakiki wa kileo,
alitambua mchango unaoweza kutolewa na somo la Fasihi katika historia ya
kisiasa na kijamii katika zama zozote husika."
Kazi kubwa za kihistoria za Masudi zimejumuishwa katika kitabu chake kiitwacho: "Akhbar Az-Zaman
(Habari za Kale)", ambacho kilitolewa katika juzuu ishirini (20). Kwa
bahati mbaya licha ya kupata taarifa juu ya vitabu hivyo, vyenyewe
hatukuweza kuvipata. Vitabu vyenye maana ya "Mbuga za Dhahabu" na
"Kitabu cha Mafunzo", ndivyo vitabu pekee vya mtaalam huyu ambavyo
vimeweza kupatikana.
Ibn Miskawayh,
mwanahistoria aliyefariki mwaka 1030, alikuwa miongoni mwa watu
waadilifu wa Kiislam. Kazi zake pekee zinatosha kuonyesha kwamba ni
lawama zitokanazo na mtizamo finyu zitolewazo kiholela na wasomi wa
Kimagharibi kwamba wanahistoria wa Kiislam hawakuwa makini. Kwa fikra
zake asilia, huru na zenye kuchukuwa tahadhari, Ibn Miskawayh ni
mwandishi wa kitabu kiitwacho: "Tadjarib AL-Ummah" (au Uzoefu wa
Mataifa), ambacho kinaelezea historia ya Arabuni na Ajemi ya kale hadi
wakati wa uhai wake. Alikuwa mtoaji wa mawazo yenye mantiki, na alikuwa
na msimamo wa wastani juu ya Uislam. Ingawa hakueleza Maisha ya Mtume,
lakini alionyesha kuwa Waarabu walianza sera za kujitanua kiutawala hata
kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W. Shauku yake kubwa ilikuwa
juu ya masuala ya siasa, falsafa na matatizo ya kiuchumi. Ameongelea
sana masuala ya miundo ya taasisi za kijamii na utawawa bora.
Katika mlolongo huo huo, kuna kazi zilizofanywa na Makkari (Ahmed Ibn Mohammad AL-Makkari),
mwanahistoria maarufu kutoka Hispania ilipokuwa chini ya utawala wa
Kiislam, alizaliwa mwishoni mwa karne ya 16 na kufariki mwaka1631.
Tasnifu yake iliyokuwa na kichwa chenye maana ya: "Jumuisho la dondoo za Historia na Fasihi za Waarabu katika Hispania",
ilichapishwa hapo mjini Leyden kati ya mwaka 1855 na 1859. Hiki ni
kisima chenye taarifa kutoka sehemu mbalimbali za nchi ya Hispania, juu
ya maisha, tamaduni na mila za wakazi wake. Humo, mwandishi ametoa picha
halisi ya maisha ya kila siku ya hapo Andalusia, inayoonyesha kuwa hata
hapo kulikuwa na harakati za kisomi, licha ya zile zilizoendeshwa
katika miji mikubwa kama Cordova, Granada na Seville. Maelezo ya kina
kuhusu hali ya wanasheria, madaktari, wanamuziki na wasomi wa kike
katika nyanja mablimbali, yalisaidia katika kuiunda upya jamii ya
Kiislam ya watu wa Hispania.
Rashi Ed Din (Fadhl A-Rashid Ed-Din AL-Mamdani)
ni miongoni mwa wataalam wakubwa sana wa somo la Historia kutoka Iran.
Hamadan, Kazvin na Tebriz ni sehemu zinazobishaniwa kuwa huenda ndiko
alikozaliwa bwana huyu. Kama mtaalm wa hali ya juu, alimwandikia
Historia ya watu wa Mongolia Mfalme Ghazan Khan baada ya kuombwa
kufanya hivyo. Humo aliongezea muhtasari juu ya historia ya makabila
mengine na sehemu mbalimbali za nchi ya Mongolia. Kazi yake iliyoko
katika juzuu nne (4) ijulikanayo kwa jina la: "Djami AL-Tawarth" (yaani
Mkusanyo wa Historia), ilikamilika mwaka 1130. Kazi hii ndio iliyokuja
kuwa msingi wa maarifa juu ya kuwepo kwa utawala wa Mongol na Turco.
Elimu ya Siasa na Sayansi ya Jamii (Sosiolojia)
Kazi
zilizoelekezwa kwenye Falsafa ya Siasa na sayansi ya Jamii, ni miongoni
mwa vito vyenye thamani sana vilivyotokana na wasomi wa Kiislam.
Waandishi, kwa kutumia lugha kuu za Uislam yaani Kiarabu, Kituruki na
Kiajemi, walielezea kinaga ubaga maoni tofauti juu ya muundo bora wa
serikali na namna bora ya kutatua matatizo mbalimbali ya jamii.
Al-Farabi,
mwanafalsafa mahiri wa Kiislam kabla ya Ibn Sina, aliandika Tasnifu
yake iliyojaa hisia za kiroho iliyoitwa kwa jina lenye maana ya: "Taifa au Jiji La Mfano (The Model City)."
Akianzia
kwenye kanuni ya Plato kwamba binadamu aliumbwa kuishi kijamii,
Al-Farabi alihitimisha kwa kusema kuwa muundo sahihi wa Taifa au Dola ni
ule utakaohusisha eneo lote lililokaliwa na watu wa aina zote.
Dhana
ya kuwa na Taifa moja mara nyingi huamsha hisia za Wazungu juu ya
iliyokuwa Dola ya Kirumi, msuguano uliokuwapo kati ya Mamlaka ya Papa na
Dola ile wakati wa zama za Kati, n.k. Hata hivyo, hilo halikuwa wazo
geni katika falsafa ya Kiislam. Vile vile ni jambo la kiroho lenye
kuhimizwa katika Theolojia ya Uislam. Jiji la Mfano, ni mojawapo ya
dalili za kuwepo kwa dhana hiyo katika fikra za wasomi wa Kiislam.
Kutokana na mwelekeo wa ajabu wa Falsafa yake, mtunzi analipatia Taifa
hilo na watawala wake jukumu la kutenda uadilifu. Al-Farabi aliamini
kwamba jukumu kubwa la Taifa kama hilo la Mfano ni kuwaundia Serikali
sahihi na kamili raia wake itakayowahakikishia amani na usalama katika
maisha yao ya hapa duniani na ya Akhera pia. Hivyo jiji kamili lilipaswa
kutawaliwa na kiongozi mmoja tu mkuu na mwenye sifa zifuatazo: "mwenye
busara na uwezo wa kutumia akili yake vizuri sana, mwenye kumbukumbu
sahihi ya mambo, mwenye uwezo mkubwa wa kueleza mambo, asiyerukia mambo
na kutoa maamuzi bila ya kwanza kuyatafiti, mwenye kujirudi na
kushaurika, mkarimu na mpole kwa raia wake, mpenda kutenda na kutendewa
Haki, mwenye msimamo na asiye dhaifu katika kutekeleza maamuzi au
maazimio yaliyokubalika." Kama akikosekana mtu mmoja mwenye sifa
hizo zote, hapo itabidi watafutwe watu wawili au watatu au wengi zaidi,
ambao kwa pamoja, kutokana na sifa za mmoja mmoja, wanaweza
kuzikamilisha na hivyo wapewe dhamana ya kuunda Serikali ya Taifa hilo.
AL-Farabi, kama Plato, anafikia dhana ya aidha kuwa na serikali adilifu
au Taifa la Kifalme (lenye kurithishana utawala).
Upeo wa mawazo ya AL-Farabi, unapingana na maadili ya Ibn Zahr, mwarabu aliyeishi Sicily katika karne ya 12 ambaye kazi yake iitwayo: "Salam AL-Mota", iliyolinganishwa na kitabu cha Machavelli kiitwacho "The Prince" yaani
Mtoto wa Mfalme. Ndani ya kitabu hiki kuna maneno ya hekima kama yale
yaliyoandikwa na Katibu wa Florentina, ingawa pia kimejaa ulaghai.
Msomi mwingine ni Al-Mawedi
aliyeishi katika miaka ya 972 na 1058. Huyu alikuwa mwanasheria mahiri
na Hakimu Mkuu hapo Ostowa, karibu na mji wa Nishapur. Alitunga kitabu
kiitwacho: "AL-Ahkam Es Sultaniah" (yaani Kitabu cha Hukumu au
Kanuni za Utawala bora). Kazi hii, ambayo mtu ataguswa na shauku ya
kutaka kuelewa dhana ya Ukhalifa, ilikusudiwa kuongelea masuala ya
taasisi za kisiasa, kijamii na kisheria katika dola ya Kiislam. AL-Ahkam
Es Sultaniah na kitabu kingine cha AL-Mawedi kilichomaanisha "Kanuni za
Serikali", baadaye vilitafsiriwa katika lugha ya Kifaransa.
Msomi mwingine aliitwa Ibn Khaldun. Huyu
aliishi mnamo miaka ya 1332 na 1406. Wale wote waliozoea kuushutumu
ustaarabu wa Kiislam, ambao huangalia yale yaliyochukuliwa toka kwa
Wayunani, na kukataa ubunifu wa Kiislam, wanalazimika kutambua deni la
Historia ya Falsafa ya kwanza kuandikwa, si Mwarabu au Mzungu, aliyepata
kuwa na maoni juu ya historia ambayo kwa mara moja yamekuwa kamilifu na
yaliyojaa Falsafa. Maoni ya watu wote hata ya wale waliomuelekezea
lawama Ibn Khaldun, wansaema kwamba bwana huyu alikuwa mwanahistoria
maarufu sana aliyepata kutolewa na Uislam na miongoni mwa walio bora na
katika zama zote. Hapo zamani kabla ya kuwepo kwa somo la Sosiolojia (sociology)
kama tulijuavyo hivi leo, kabla hata ya maelezo ya akina Comte, Vico,
Marx na Spengler, Ibn Khaldun alishaelezea historia na hatua za
maendeleo ya jamii ya wanadamu, na alijaribu kutoa maelezo ya kina
kuhusu umuhimu wa somo la Historia na maendeleo yake kwa siku zijazo.
Ibn Khaldun aliweza kuikusanya Historia ya Ulimwengu mzima katika kitabu chenye juzuu tatu, ambazo zina Utangulizi na Tawasifu (autobiographies). Juzuu ya kwanza ikiwa na utangulizi hufanya sehemu inayoitwa "Prolegomena",
(ambayo ilitafsiriwa katika lugha ya Kifaransa na mtaalam mmoja
aliyeitwa de Slane mwaka 1868). Sehemu hii ni jambo la kihistoria lenye
kudumu ambalo pia limempatia mwandishi, heshima na umaarufu duniani.
Humo kuna kumbukumbu ya mambo ya kihistoria, juu ya aina mbalimbali za
ustaarabu duniani uliotokana na athari za mazingira na hali ya hewa
tofauti, maisha ya makazi ya kibedui (ya kuhamahama) na ya kudumu pamoja
na tamaduni tofauti tofauti za jamii hizo na pia taasisi tofauti za
kijamii, sayansi na sanaa zao. Mwandishi pia anaongelea masuala ya
sayansi, hesabu, muziki na ala zake, kilimo na sanaa kwa mujibu wa
Qur’an. Kwa kweli, ni kazi yenye maelezo kuhusu mambo mengi na
yaliyoelezwa kifasaha ambapo historia yenyewe imeelezewa kuwa ni sehemu
ya somo la Falsafa kwa maneno yafuatayo: "Hebu tutazame undani wa
somo la Historia", anasema Ibn Khaldun kwamba, ni uchunguzi na
uthibitisho wa taarifa, uchunguzi makini wa sababu za kuwepo kwa mambo
(kama yalivyo) na uerevu wa kina wa jinsi mambo yalivyoweza kutokea.
Hivyo, Historia ni mojawapo ya sehemu za somo la Falsafa, na inapaswa
kutambuliwa kama mojawapo ya elimu ya sayansi." Hii kwa kweli ndiyo
dhana ya kileo juu ya somo la Historia, kutokana na kuuona umuhimu na
nafasi yake katika uchambuzi wa taarifa mbalimbali na kutafuta chanzo au
sababu za mambo. Historia inapaswa kuwa ni elimu ya kudumu katika
ustaarabu wa mwanadamu na saikolojia yake.
Ni
vigumu kuweza kuchambua kwa kina kazi kubwa aliyoifanya Ibn Khaldun.
Uchunguzi wake adilifu juu ya upoteaji na uharibifu wa staarabu
mbalimbali, katika mzunguko, na mchango mkuu wa wasomi katika uundaji wa
Mataifa mbalimbali, ambao amewanukuu katika jitihada za kuhami dhana
yake, ni mambo yenye kuvutia. Ibn Khaldun alipindukia pale alipoainisha
maisha ya Taifa lolote na ya watu au ya kiumbe kingine chochote, kwamba
hata mataifa yanazaliwa, yanakua na yanakufa. Pia kwamba mataifa yako
chini ya kanuni ya mabadiliko asilia. Ibn Khaldun amehusika na uvumbuzi
wa kanuni hii ya mabadiliko ya taifa lolote.
Mawazo
yake ya kiuchumi kama ya kisiasa, yameendelea kutumika hata leo.
Mwandishi huyu kutoka iliyokuwa ikiitwa Maghreb (Morocco) anasema: "Taifa
ni sawa na mfanyabiashara mkubwa, kwani ana jukumu la kuhakikisha kuwa
pesa azipatazo kutokana na kodi, zinarudi na kuwazungukia watu. Kodi za
wastani ni motisha tosha ili watu waweze kujituma katika kufanya kazi.
Kwa upande mwingine, kupandisha kodi yoyote tena kiholela holela,
kunaweza kusababisha yasipatikane mafanikio ya malengo ya kodi husika." Anachunguza
kwa makini sana masuala ya utaifishaji au ushikiliaji wa mali za watu,
ukiritimba, usimamizi na udhibiti wa biashara kabla ya kuhitimisha kwa
kusema kwamba rasilimali za Taifa, misingi yake mikuu ni watu, ari ya
makampuni yake ya kibiashara na tija katika ufanyaji wa shughuli zote za
kiuchumi.
Kujiingiza
kwa serikali katika utendaji wa shughuli za kiuchumi hupunguza uwezo wa
uzalishaji na utumiaji wa rasilimali za Taifa na hivyo huchelewesha
upatikanaji wa maendeleo katika jamii. Ukweli ni kwamba, taaluma ya siku
hizi katika dhana ya uchumi huria haikuongeza lolote katika mtizamo
kama huu, ambao ulishajengeka tangu karne ya 15.
Msomi mwingine ni yule aliyeitwa Abul FazL aliyeishi kati ya miaka ya 1551 na 1602. Huyu alikuwa mwanafalsafa, msomi, mwanasiasa na rafiki mkubwa wa Mfalme msomi pia, Mogul wa India. Kazi yake iitwayo "Akbar Nameh", bila
shaka ni miongoni mwa kazi muhimu za Kiislam kutoka bara Hindi. Kazi
hii imegawanyika katika sehemu tatu. Ya kwanza inaongelea historia ya
uvamizi wa Timur (Tamburlaine) wa nchi ya India, na pia ile ya mtoto wa
Mfalme Timuridh aliyeitawala nchi hiyo. Sehemu ya pili inaelezea utawala
wa muda mrefu na wa mafanikio wa Akbar, na sehemu ya tatu, inayoitwa Ayn I Akbari,
inatoa taarifa muhimu juu ya shughuli za taasisi za serikali, sheria na
utawala, juu ya hali ya maisha ya Wahindi na dini zao, falsafa na
sheria kwa jumla. Baadhi ya sura zinaelezea juu ya sanaa na ufundi wa
Wahindi, vyanzo vya pesa za kuendeshea serikali, takwimu na taarifa za
kiutawala na maendeleo yaliyofikiwa katika utengenezaji wa silaha
mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya majeshi na pia vitabu vilivyokuwa
vimekwishatafsiriwa.
Ayn I Akbari
pia ndani yake kina kiasi kikubwa cha maneno ya Hekima, maamuzi ya
busara na nukuu mbalimbali za kisiasa za Akbar, ambazo Waziri wake Mkuu
na rafiki yake wa karibu alizokuwa akiziandika kila siku.
"Hiyo ni kazi ya ajabu kabisa", anasema Carra de Vaux, "iliyojaa
uhai, mawazo na mafunzo, ambamo kila kipengele cha maisha
kimechunguzwa, kuorodheshwa na kupangiliwa, ambamo mlolongo wa maendeleo
ya mambo mbalimbali hufurahisha macho ya msomaji wake, ni hati ambayo
Ulimwengu wa Mashariki umeweza kujivunia. Watu ambao vipaji vyao
vimeongelewa katika kitabu hiki, walishapiga hatua za mbele zaidi kuliko
hali ya zama walizoishi, wazo katika masuala ya uundaji na uendeshaji
wa serikali, na pengine katika udodosi wao katika Falsafa ya Dini. Wale
washairi na wanafalsafa, huelewa vyema namna ya kushughulikia mambo ya
kidunia. Huchunguza, hupanga, hupima na kukadiria, kisha hutekeleza.
Mawazo yote ambayo huwajia hujaribiwa dhidi ya ushahidi uliopo. Kutoka
Magharibi tumshukuru Leibnitz, kwa kutuonyesha matumizi ya takwimu,
ambazo tunaziona kama ni somo jipya la sayansi, na msaada unaoweza
kutolewa na somo lenyewe (la takwimu). Serikali ya Akbar iliweza
kuzitumia takwimu kwa makini kabisa katika utawala wake, miaka zaidi ya
mia tatu iliyopita, pamoja na kanuni za ustahimilivu kisiasa, utendaji
wa Haki na kuthamini heshima na utu wa mwanadamu."
Usanifu wa Majengo na Sanaa za Plastiki
Kukua
kwa sanaa ya Kiislam ni mojawapo ya maendeleo yaliyopatikana kwa haraka
katika historia ya Ulimwengu. Mwanzoni mwa Hijria, Sanaa rasmi ya
Kiislam haikuwapo. Ilianzishwa baada ya Waarabu kuunganisha aina ya
mitindo waliyoikuta katika nchi walizoziteka za Mashariki mwa bahari ya
Kati. Baada ya kuimarika sanaa hii, upesi sana ilienezwa katika Himaya
yote ya Makhalifa. Kanuni ya sanaa hii mpya iliboreshwa zaidi na watu
waliokuwa katika jumuia ya Kiislam, kutokana na ubunifu wao asilia, nje
ya ushawishi wa watawala hao wapya.
Hivyo,
kumbukumbu ya mafanikio ya Cairo au ya Cordova, ni rahisi kuchanganywa
na ile ya mafanikio ya Samarkand au Delhi. Mlingano makini wa mipango,
uhuru wa kusanifu majengo wa hapo Aleppo na Damascus ni tofauti na ndoto
za anasa zilizozikumba kasri za Granada na Seville.
Fikra
za kiakili za watu wa jangwani ziliishia katika kubuni vipimo maalum
vya mistari ya jiometria, uchoraji kwenye vigae na enameli za kupambia
kuta za majengo, kama ilivyotokea hapo Ispahan, mambo ambayo yamekuwa
vielelezo vya tafsiri ya ndoto za wasanii wa Iran.
Lakini
tofauti hizi hazikuathiri umoja wa Kiislam. Fahari za Kiislam huonekana
dhahiri. Umoja huu unatokana na umoja wa kiimani au kiroho katika jamii
ya Kiislam na hasa kutokana na mafundisho ya Qur’an. Ni Dini hii
iliyowapa wasanii wa Kiislam himizo la kiroho na kuwajengea tabia ya
kufikiri au kutumia vyema akili kama tunavyofahamu. Matumizi ya fikra
yanajionyesha hasa pale tunapoona ubunifu wao katika sanaa za Kiislam
kwa sababu zimebaki kumbukumbu chache ambazo hazikutokana na mafundisho
ya dini hii. Kwa bahati mbaya, halikusalia jengo lolote la kale hapo
Baghdad, lakini yanapatikana maelezo mengi ya kihistoria kuhusu jiji
lililokuwa limejengwa wakati wa utawala wa ukoo wa Abbassid kwamba
lilitia fora kwa uzuri.
Uharibifu uliofanywa na Mtawala wa Kimongolia aliyeitwa Halagu katika
mwaka 1258, uliuteketeza kabisa mji wa Baghdad enzi hizo, kiasi kwamba
leo hawezi mtu kuonyesha hata ilipokuwa imejengwa Ikulu. Ni kutokana na
maelezo ya kihistoria tu juu ya kazi za usanii zilizokuwepo kwa wakati
huo, kama tunavyosimuliwa katika Alfu Lela U Lela (au Siku Elfu na Moja). Huenda maelezo hayo yangeonekana kuwa si ya kweli kama tusingekuwa na kumbukumbu ya majengo ya Alhambra na Alkazar ya hapo mjini Serville. Na bado hata Alhambra
ambayo mpaka leo ni kivutio cha macho (utalii), kwa fikra na maelezo tu
bila shaka haiwezi kulinganishwa na kasri au Ikulu nyingine ambazo
zimesahaulika kabisa, ingawa bado tuna kumbukumbu ya maelezo yake tu.
Mifano inapatikana katika Hispania yenyewe. Kuna jengo lililoitwa Madinat Az Zahar, ambalo Abdur Rahman An Nasir alilijenga kwa heshima ya mke wake alieitwa Zahra.
Sanaa
Tukufu zaidi ya Waislam ni usanifu na ujenzi wa Misikiti. Huu ni
ushahidi tosha wa aina ya usanifu bora wa majengo ya zamani yaliyoupa
sifa Uislam. Sanaa hii pia ilileta ushawishi katika ujenzi wa Makanisa
na boma za wakubwa na watawala wa enzi hizo. Hispania, zama hizo iliiga
tena bila ya kinyongo aina ya Sanaa iliyopatika hapo Andalusia, wakati
ilipokuwa bado chini ya utawala wa moja kwa moja wa Waarabu. Pia,
ushawishi wa sanaa hiyo ulijionyesha katika sanaa ya Wataliano kutokana
na ukaaji wa Waarabu hapo njini Sicily. Aina hii ya sanaa iliingia pia
nchini Ufaransa kupitia sehemu iliyoitwa Septimania. Maelezo ya Emile Male, mtaalam wa historia ya somo hili la sanaa ya ujenzi, yanaonyesha umuhimu wa sanaa hii ya Kiislam.
Male
ametoa mwanga juu ya ulingano kati ya usanifu wa Kiislam na ule wa
Kirumi. Kuna baadhi ya maumbo yenye nakshi za Kiislam katika fani ya
ujenzi, kwa mfano mihimili ya pembe tatu, na milango ya mfano wa maua
yaliyochanua na mengineyo. Bado majengo hayo tunayaona hapo Auvergne,
Notre Dame du Port na Clermont. Mpangilio wa nakshi za Kiislam bado
unaweza kuonekana katika Makanisa mengi ya hapo Auvergne.
Usanifu
na nakshi zilizoipamba Misikiti ni jambo ambalo pia limeigwa katika
ujenzi wa majumba mengi hapo Cordova na Notre du Puy. "Si kwa bahati
tu, kwamba usanifu kama huo kuonekana pia katika jengo la Cathedral hapo
Puy. Asili ya usanifu huu wa watu wa Mashariki ni katika utamaduni wa
Kiarabu katika kuyaremba milango ya majengo yao."
Katika
maelezo ya jumla, tulipata fursa ya kutaja ushawishi wa Uislam katika
maendeleo ya sanaa ya viwandani. Bidhaa adimu na vya anasa
vilivyotengenezwa kutokana na ubunifu wa wasanii wa Kiislam,
viliwashangaza sana watu wa Ulimwengu wa Magharibi. Bidhaa hizi bado
zimewekwa na kuhifadhiwa kama vito vya hazina kubwa katika majumba ya
Wafalme na Makanisa mbalimbali.
Mchango wa Uislam haukuwa kwenye maendeleo ya ubunifu wa bidhaa za viwandani tu. Angalia jinsi F. Diez,
katika matokeo ya utafiti wake juu ya sanaa ya Kiislam, anavyoelezea
ushawishi uliotokana na maumbo yaliyotokana na sanaa ya uchongaji wa
Seldjuk ulivyochukuliwa na kuigwa na watu wa Ulaya, pale alipoandika: "Umuhimu
wa sanaa hii ya uchongaji wa vitu vya kawaida kama vionekanavyo katika
mazingira ya mwanadamu, unatokana na tabia na uwezo wake katika
kujiingiza katika sanaa ya Wazungu hasa wa Ulaya ya Kaskazini. Maelezo
juu ya aina hii ya mapambo iliyoshamiri katika zama zakarne za Kati,
yanapatikana katika historia ya mabadiliko ya mwelekeo wa misafara ya
kibiashara kutoka kusini kuelekea Kaskazini, uliotokana na uhamiaji wa
Waturuki kuelekea katika nchi za Magharibi. Mojawapo ya misafara hiyo ya
kibiashara ni ule uliotoka Asia ndogo kuelekea Kaskazini, aidha kwa
kuzungukia Urals au kwa kukatiza, halafu kupitia Ujerumani ya Mashariki,
na Bahari ya Baltic hadi katika kisiwa cha Uingereza. Miji ya
kibiashara kama Hamburg, Lubeck, Riga na Novgorod ilianza kujengeka
kuanzia sehemu ya pili ya karne ya 12. Vladmir na Sudal, iliyoko
mashariki mwa Moscow ni miji iliyovuma sana kuliko hata Kiev katika
umaarufu. Maumbo ya milango ya Makanisa ya zamani katika miji hii miwili
bado ni ushahidi tosha hadi leo wa jinsi gani sanaa ya Kiislam
ilivyoweza kujipenyeza Ulaya."
Hebu tujikumbushe jukumu moja kubwa la Sanaa ya Kiislam katika maendeleo ya msamiati na taaluma ya utengenezaji na utumiaji wa Nembo (helaldry).
Mti
wa Uzima, alama au nembo yenye siri kubwa kwa watu wa Mashariki, mchoro
uonyeshao wanyama walioelekeana, pia sanaa hii imeweza kukutwa
imechongwa katika milango ya Makanisa mbalimbali kama ya watakatifu
Etienne de Beauvais, Brice de Chartres, Notre Dame de la Couture, Le
Mans na mengine mengi tu. Nembo hii pia ilichorwa katika vitambaa, vifaa
vilivyochongwa na kwenye makaratasi na nyaraka za kuandikia. Katika Biblia ya Charles the Bald, wameonyeshwa simba katika sehemu mbili za mti huu wa kiroho, na katika Injili ya Lothair,
wamewekwa chui, yote yakithibitisha zaidi asili ya sanaa ya Waislam
kama ilivyopokelewa tena kwa shauku na watu wa Magharibi. Na mahali
pengine wamewekwa wanyama bila ya kuwekwa mti huu unaoitwa wa Uzima:
kama La Trinite ya hapo Caen, St. Germain de Pre la mjini Paris na
kwingineko. Michoro ionyeshayo kundi la wanyama wanaotafunana, na ya
aina ya wanyama watokanao na fasihi simulizi za kale kama mnyama mwenye
mwili na kichwa cha simba na mbawa za tai, au ndege mwenye kichwa cha
binadamu, au tai mwenye vichwa viwili, wametokana na sanaa ya Kiislam.
Hizi
zote ni Sanaa zilizotokana na ubunifu na dhamira binafsi za wasanii na
hivyo ni rahisi hata kuzitambua. Lakini Sanaa ya Kiislam, kwa kawaida ni
ya kutumia mkusanyiko wa mistari. Hivyo, inakuwa vigumu wakati mwingine
kuamua kama nyingine zilichukuliwa na Wazungu baada ya kuzifanyia
marekebisho au la. Unakili wa Sanaa hiyo lazima ulitokea kwani mtu
atakuta kwamba katika uhandisi-ujenzi wa Kirumi kuna uchongaji wa herufi
za Kiarabu kiasi ambacho zingine zinaweza hata kusomeka kwa wenye kujua
kuzisoma. Mifano inapatikana hapo Voute Chillac, Haute Loire, Toulouse
na St. Guillaume la Desert na katika jumba la Makumbusho la mjini Lyons,
Ufaransa.
Katika miIango ya Cathedral hapo Puy kumechongwa herufi za Kiarabu zinazosomeka Maa’Sha Allah (yaani Kwa Mapenzi ya Mungu). Na
pia katika jumba la Makumbusho mjini London, kuna Msalaba uliohifadhiwa
tangu karne ya 9 ambao katikati yake kumechongwa maneno ya Kiarabu
yasomekayo: Bism Llah (yaani kwa Jina La Mwenyezi Mungu), na pia
katika milango ya Mt. Peter kwenye Cathedral moja mjini Milan, ambayo
alikabidhiwa Papa Eugene wa IV, kumechongwa herufi za Kiarabu kuzunguka
kichwa chote cha sanamu la Yesu, na katika kanzu za sanamu za Mt. Peter
na Paul.
Mchango katika Somo la Muziki
Katika
imani sahihi ya Kiislam, muziki ni jambo ambalo halikupendelewa. Mfumo
mzima wa ibada na sala katika Uislam umeepukana na matumizi ya nyimbo.
Mtazamo wa walimu wengi wa dini na hata waanzilishi wa madhehebu kuu nne
za Kiislam walipinga matumizi ya nyimbo na miziki katika ibada. Ni
katika amri za kushangaza zilzoitwa Law lewi (zilizojulikana Ulaya kama Amri za Whirling Dervishes, Derkawa huko Afrika Kaskazini), na nyigine za Kisufi zilizoupa umuhimu muziki na nyimbo.
Uimbaji
wa tenzi na michezo ya ngoma kwa kutumia Ala za muziki zimehusishwa
sana katika kufundishia hasa watoto masomo ya dini. Wasufi waliamini
kwamba katika muziki kuna mwangwi wa kudumu wa mambo yasioonekana.
Walikusudia kuutumia muziki katika kuitafakari Akhera.
Walimu
wa dini na madaktari wa sheria walihofia nguvu ya muziki katika
kuutikisa moyo wa mwanandamu na hata kuweza kumletea usumbufu na
hatimaye kumpotezea katika mambo ya kidunia na kumsahaulisha jukumu la
kujitayarishia Akhera.
Pamoja
na hadhari hii, hilo halikuweza kuzuia maendeleo katika fani hii ya
muziki katika jamii ya Kiislam. Tangu mwanzo wa Himaya ya Kiislam,
muziki ulipewa nafasi kubwa katika Kitala (boma) cha utawala wa Umeyyad
mjini Damascus na cha utawala wa Abbassid mjini Baghdad. Khalif Harun AL-Rashid na warithi wake waliupa muziki nafasi muhimu kama ilivyokuwa katika sayansi na sanaa nyingine.
Kuanzia
Mashariki, muziki uliingia Spain kupitia Morocco. Kwa maelezo ya
Averroes (Ibn Rushd), ni katika Seville ambapo muziki ulipata
kuendelezwa na kukuzwa kwa nguvu zaid. Wanafalsafa walijadili umuhimu wa
muziki, athari za sauti katika roho ya mwanadamu, na nguvu zake katika
kuwasilisha ujumbe au hisia. Historia imetukarimu kwa kutuhifadhia
kumbukumbu ya majina ya wanamuziki na waimbaji maarufu. Hapa tutawataja
tu Abul Hassan Ali Ibn Nafis, aliyeitwa pia Ziriyab,
ambaye alianzia shughuli zake hapo Baghdad na kujiendeleza hadi
kuzoeleka katika Kitala cha Abd Ur – Rahman wa II mjini Cordova.
" Katika muziki", anasema Levi – Provencal, "alionyesha
kuwa mtu mbunifu na mwenye kipaji cha hali ya juu. Alijenga kisima cha
muziki wa Andalusia, ambacho mwanzoni kilifanana na kile cha Chuo cha
Elimu ya Mashariki, ambayo baadaye iliendelezwa na Waislam katika nchi
za Magharibi."
Na
katika maendeleo ya nadharia, miongoni mwa waandishi wa Kiislam
kushughulikia taaluma ya muziki alikuwa si mwingine bali mwanafalsafa
aliyeitwa AL- Farabi. Kwake tunajivunia kitabu chake kiitwacho Kitab Al- Musiki (Kitabu
cha Muziki). Mtunzi, ambaye shauku yake katika muziki ilianzia katika
masomo ya Hesabu na Fizikia, alipoweza kuwa mtu wa kwanza kutoa maelezo
ya kina juu ya utoaji wa sauti na utengenezaji wa kanuni za utayarishaji
wa Ala za Muziki.
Wakianzia
kwenye mizania ya Wachina na Wa-Iran, Waarabu walitafiti na kuweza
kutengeneza mizania asilia na kupata mafanikio makubwa katika mbinu za
utengenezaji wa Ala za Muziki kama magitaa, zumari, ngoma, dufu n.k Pia
walitengeneza aina ya kwanza ya piano na kinanda. Ala zote hizi
ziliingizwa kwa mara ya kwanza huko Iberia na kisha Ulaya na Waislam
wenyewe.