![]() |
SEHEMU YA TATU |
FUNGA YA RAMADHANI, HUKUMU,
FADHILA NA ADABU ZAKE.
Ibrahim A. H. Ghulaam
(SEHEMU YA TATU)
YANAYO BATILISHA (KUHARIBU) FUNGA
1- Kula au kunywa kwa kukusudia.
2- Kila kinachoingia tumboni au kooni kwa kukusudia.
3- Tendo la ndoa.
4- Kusababisha kutokwa na manii (kwa kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana nakadhalika).
5- Kujitapisha kwa makusudi.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah ( رضي الله عنه ) amesema: amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم ): {...na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa.} (Wameipokea maimamu watano).
YASIO FUNGUZA
1- Kula au kunywa kwa kusahau.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه ) amesema, amesema Mtume ( صلى الله عليه وسلم ): {Mwenye kusahau nae amefunga, basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake….} (Al Bukhariy na Muslim).
2- Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa udhu (bila ya kubalighisha).
3- Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji katika kiwiliwili (hasa katika maeneo yenye joto kali).
4- Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti ya kutokumeza alichokionja).
5- Kutokwa na mbegu za uzazi (manii) katika usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.
6- Kuamka na janaba. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mamama `Aishah na Ummu Salamah (رضي الله عنها) kwamba Mtume (صلى الله عليه وسلم ) alikuwa akiamka na janaba, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy na Muslim).
7- Kupiga mswaki (wakati wowote).
8- Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.
9- Kung`oa jino na mfano wake.
10- Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au nifasi.
ADABU ZA FUNGA
BAADHI YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI
1- Kula daku. Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas ibn Maalik ( رضي الله عنه ) amesema: amesema Mtume ( صلى الله عليه وسلم ): {Kuleni daku kwani hakika chakula cha daku kina baraka ndani yake} (Al Bukhariy na Muslim).
*Na inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.
2-Kuharakisha kufutari (mara tu likizama jua). Imepokewa hadithi kutoka kwa Sahl ibn Saad ( رضي الله عنه ), Hakika Mjumbe wa Mungu (رضي الله عنه ) amesema: {Watu watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari}.
( Al Bukhariy na Muslim).
*Na inasuniwa (kuanza) kufutari kwa tende au maji.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Salmaan ibn`Aamir (رضي الله عنه ) kutoka kwa Mtume (s.a.w.) amesema: {Anapofutari mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi na afutari kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho).
(Wameipokea Maimamu watano).
*Na pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa kufutari, kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufutari ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (سبحانه وتعالى ).
Itaendelea inshaallah..