![]() |
SEHEMU YA PILI |
FUNGA YA RAMADHANI, HUKUMU,
FADHILA NA ADABU ZAKE.
Sheikh Ibrahim A. H. Ghulaam
(SEHEMU YA PILI)
INAE MUWAJIBIKIA FUNGA YA RAMADHANI.
Funga ya Ramadhani inamuwajibikia kila Muislamu, baleghe, mwenye akili, alie katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye siha (afya- asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga (kama hedhi na nifasi kwa wanawake).
*Na inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao wanapofikia umri wa miaka saba (7) na kuwalazimisha hadi ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi (10), na hili inabidi pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.
NYUDHURU ZA KUFUNGA
Nyudhuru za kuacha kufunga zinatofautiana na kila udhuru una hukumu yake, na hapa nitazielezea nyudhuru hizo kwa ufupi.
1- Hedhi na nifasi, huu ni udhuru ambao unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa haramu kwake funga na iwapo atafunga haitosihi (Haitokubaliwa) funga yake, na ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.
2- Maradhi au Safari. Na mwenye udhuru wa maradhi (yanayotibika kwa kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga na itawawajibikia kulipa baada ya Ramadhani. Amesema Allah (سبحانه وتعالى ): {{Atakaye kuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku alizoacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.. .}} (2:185).
Na kama maradhi yatazidi au kumletea madhara iwapo atafunga basi itakuwa lazima kwake kutokufunga.
*Ama safari ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake kutokufunga wanachuoni wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au kwa mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa takiribani kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa msafiri anayesafiri kwa kutumia chombo cha aina yoyote atakachosafiria, ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito wowote.
3- Vizee (vikongwe) na wenye maradhi sugu (yasiotarajiwa kupoa).
Na haya mawili iwapo yana msababishia madhara basi ni katika udhuru na ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa kumlisha masikini kibaba (mudi) cha chakula (ambacho ni sawa na na uzito wa gramu 600g takiribani)au chakula kinacho mshibisha masikini mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.
4- Waja wazito na wanyonyeshaji.
Nao ni katika wenye ruhusa ya kutokufunga, na inawabidi kulipa siku walizoshindwa kufunga kwa sababu ya udhuru huo. Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha ikiwa watakhofu Swawm itawadhuru watoto wao au wenyewe, hao sio lazima kufunga. Lakini ikiwa hawatafunga Ramadhaan basi ni lazima wafunge baada ya Ramadhaan kulipa siku zao. Na ikiwa waliacha kufunga kwa sababu tu ya kukhofia afya ya watoto wao, basi wanapaswa kulipa na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku moja iliyowapita katika Ramadhaan.
5- Iliemzidia njaa au kiu na akahofia kuangamia, huu pia ni katika udhuru wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni kwamba: yule mwenye kuhofia kuangamia inakuwa kwake ni wajibu kufungua, na itamuwajibikia kulipa kama mgonjwa.
NGUZO ZA FUNGA
1- Nia nayo ni kukusudia kufunga usiku wa kuamkia funga, kwa funga ya faradhi.
2- Kujizuilia na vyenye kufunguza (kufuturisha).
3- Muda wa kufunga (mchana kuanzia alfajiri mpaka kutwa (kuzama) kwa jua.
UNAVYOTHIBITI KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI
1- Kwa kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa shaabani.
2- Kwa kuonekana mwezi mwandamo siku ya 29 ya mwezi wa Shaabani, imepokewa hadithi na Abu Hurayrah ( رضي الله عنه ) kwamba Mtume (صلى الله عليه وسلم ) amesema:
{Fungeni kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake} (Al Bukhariy na Muslim).
*Na mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonekana na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonekane na Waislamu waadilifu wawili au zaidi.
Itaendelea InshaAllah