12/17/2017

11:45 PM

Ibrahim A. H. Ghulaam

(SEHEMU YA KWANZA)

بسم الله الرحمن الرحيم
 الحمد لله رب العالمين   و الصلا ة  و السلا م  علي نبينا  محمد  وعلى آله  وصحبه,  و بعد:

UTANGULIZI.

Baada ya kumshukuru  Allah [سبحانه وتعالى ] na kumtakia rehma na amani Mtume [صلى الله عليه وسلم ] pamoja na Ali zake na Maswahaba zake wote.

Basi kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu (سبحانه وتعالى ) amejaalia kwa waja wake  miongo [misimu] ya kuzidisha ndani yake matendo mema  na Mwenyezi Mungu (سبحانه وتعالى ) huzidisha pia malipo ya matendo 
hayo kwa waja wake , na miongoni mwa miongo hiyo ni huu  mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

Basi katika makala hii nitaelezea kwa ufupi  juu ya funga na yale yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na  hukumu, fadhila na adabu zake.

Ninamuomba Allah [سبحانه وتعالى ] awanufaishe Waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na aturuzuku ikh-laswi [kutaka radhi zake pekee] katika matendo yetu yote,  amiiin.

Na kwake pekee ndio kwenye mafanikio ya dunia na akhera.

Ndugu yenu katika imani:
IBRAHIM A.H.GHULAAM.
22  RAJABU  1426H,
SANA`A  YEMEN.


MAANA YA FUNGA
Neno swaumu ambalo ni funga katika lugha ya kiswahili,   kilugha lina maana ya kujizuilia. Ama katika sheria funga [swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu [سبحانه وتعالى ] kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia kudhihiri alfajiri [ya pili] mpaka kuchwa [kuzama] kwa jua na kwa kunuilia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu [سبحانه وتعالى ]. 

HISTORIA YA FUNGA
Kwa hakika funga si ibada ngeni, bali ni ibada iliyofaradhishwa kwa umati zilizotangulia na pia kufaradhishwa katika umati huu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: 
{{Enyi mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu] kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu}} (2:183).

Ama katika umati huu wa Muhammad [صلى الله عليه وسلم ] funga ilifaradhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya hijrah (2H).

HUKUMU  YA FUNGA.
Funga ya mwezi wa Ramadhani ni nguzo katika nguzo za Uislamu, nayo ni wajibu kwa dalili ya kitabu (Qur-an), Sunnah na Ijmai (makubaliano) ya Wanavyuoni wote wa Kiislamu.

1: Amesema Allah [سبحانه وتعالى ]: 
{{Enyi mlioamini mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha mungu.  Siku chache tu (kufunga huko)... (Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili) Atakae kuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. …} (2:183-185). 

2: Na imepokewa hadithi kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar (رضي الله عنه ) amesema: 
Nimemsikia Mtume (صلى الله عليه وسلم ) akisema: “Umejengwa Uislamu juu ya nguzo tano; kushuhudia ya kwamba hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (سبحانه وتعالى ) na kwamba hakika ya Muhammad (صلى الله عليه وسلم ) ni Mtume wa Allah (سبحانه وتعالى ) na usimamishaji Swalah na utoaji Zakah na kuhiji katika nyumba (tukufu) ya Alkaaba na funga ya Ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).

Na kuna hadithi nyingine nyingi zinazojulisha wajibu huo, na wanavyuoni wote wamewafikiana juu ya uwajibu huo.

Itaendelea Inshaallah